Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Mnamo Jumatatu 27 Agosti 2018, Raisi Uhuru Kenyatta atafanya mazungumzo na mwenzake wa Amerika Donald Trump jijini Washington. Katika taarifa iliyotolewa na Waziri wa Habari wa Amerika Sarah Sanders, Raisi Trump amemkaribisha Raisi Kenyatta katika mkutano ikuluni White House ili kujadili ukuaji wa biashara baina ya nchi mbili hizi na kutafuta suluhisho la kudumu la utovu wa usalama katika nchi jirani za Somalia na Sudan Kusini.
Kuhusiana na ziara hii, sisi Hizb ut Tahrir / Kenya tunasema yafuatayo:
Majadiliano kati ya Kenyatta na mwenzake wa Amerika raisi Donald Trump juu ya ukuaji wa biashara na usalama si chochote isipokuwa ni kutia shinikizo kwa utawala wa Uhuru katika utekelezaji wa sera katili za kibepari zitakazo endelea kuidhuru Kenya. Ni kupitia mikataba ya kibiashara na dola kuu za Kimagharibi kama Amerika ndio iliyoiacha Kenya na Afrika kwa jumla kufazaika kwa viwango vibaya vya umasikini, njaa, na maradhi. Sera batili za kibiashara zinazopigiwa debe na Amerika mithili ya soko huru zimepelekea majanga ya kiuchumi yanayoshuhudiwa nchini leo, ambapo deni lake la umma limefikia kiwango cha shilingi trilioni 5. La dhahihiri, sera ya Trump ya Afrika ni mwendelezo wa juhudi za kibepari za kuitawala na kuinyanyasa nchi hii na bara zima la Afrika. Hivyo basi, tuionavyo ziara hii haitaiokoa Kenya kwani Amerika imekuwa katika upande mbaya wa historia dhidi ya maslahi ya wafanyi biashara wa Kiafrika.
Ama kuhusu madai ya kutafuta suluhisho la kudumu la utovu wa usalama, tunakariri kuwa Amerika haina mbinu za kupambana na utovu wa usalama na ugaidi kwani yeye mwenyewe ni mdhamini mkuu wa ugaidi duniani. Kama vile watangulizi wake, utawala wa Trump unaongeza uvamizi wa kibepari wa kijeshi barani Afrika kama ilivyo sehemu nyenginezo duniani. Ni dhahiri shahiri kuwa kwa miongo kadhaa hakuja kuweko na mipango kabambe inayohusiana na amani na usalama barani humu na ulimwenguni chini ya utawala wa Amerika, yaani, kuanzia serikali zilizopita mpaka serikali ya leo. Zaidi ya hayo, kwa kisingizio cha ugaidi Amerika imepatiliza fursa ya majeshi ya mataifa mengi barani Afrika na kuyatia mikononi mwake; na kuasisi kambi za kijeshi katika mikakati yake ya kuipiku Uingereza na Ufaransa ili iwe na mgao mkubwa katika uporaji wa Afrika.
Kwa kuwa ziara ya Kenyatta Amerika inajiri miezi minne tu baada ya ziara ya mwenzake wa Nigeria Muhammadu Buhari, tunaiona ziara hii kama uhakikishaji wa mkakati wa kujitolea wa kuzitongoza zilizokuwa koloni za Kiingereza ikizingatiwa kuwa wote Kenyatta na Buhari ni watumishi vipenzi wa Uingereza. Kenya na Nigeria zote zinacheza dori muhimu kama washirika changamfu wa Amerika katika kupigana vita vyake vya wakala kwa jina la usalama na mipango ya kupambana na ugaidi. Huku Nigeria ikipigana na ‘Boko Haram’ katika eneo lake la kaskazini na Sahel, Kenya nayo inapigana na ‘Al Shabab’ kifikra ndani na kijeshi nje ya mpaka wake na Somalia chini ya muongozo wa vyombo vya usalama vya Amerika. Tunaitahadharisha Kenya na nchi nyenginezo juu ya hatari ya vita vya wakala, ikiwemo kuigawanya nchi vipande vipande.
Kwa kutamatisha: Sisi katika Hizb ut Tahrir / Kenya tunaitazama ziara hii kama njia ya Amerika kuminyana na koloni za Kiingereza, kuzitumia rasilimali zao, na kuzitumbukiza nchi hizi katika ghasia na madeni zaidi! Fauka ya hayo, damu za raia wasiokuwa na hatia hususan Waislamu itaendelea kumwagwa kwa kisingizio cha kupambana na misimamo mikali na ugaidi kama inavyojitokeza katika mfumo batili na muovu wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake zilizovunda zinazochipuza kutokana na sera za usalama za Amerika kama ifanyavyo nchini Syria, Yemen, Iraq, Libya, Ardhi Tukufu ya Palestine nk.
Shabani Mwalimu
Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari wa Hizb ut Tahrir Kenya
KUMB: 13 / 1439 AH
Jumapili, 15 Dhul-Hijjah 1439 H /
26/08/2018 M
Simu: +254 707458907
Pepe: mediarep@hizb.or.ke