Afrika yalazwa njaa kikatili na wakoloni wa kibepari chini ya uangalizi wa viongozi wake wafisidifu

Habari&Maoni

Habari:

Onyo la Mashirika ya  FAO –WFP  juu ya  maeneo yanayokabiliwa na ukame kuhusu ripoti ya tahadhari ya mapema kuhusu uhaba wa chakula iliyotolewa na mashirika haya mawili ya kimataifa(Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) inatoa mwito wa kuchukuliwa hatua za haraka za kibinadamu ili kuokoa maisha na kuzuia njaa katika nchi zenye uhaba mkubwa wa chakula ambapo unatarajiwa kuwa mbaya zaidi kuanzia Oktoba 2022 hadi Januari 2023. Tayari katika eneo la Pembe ya Afrika, zaidi ya watu milioni 37 katika eneo hilo wanatarajiwa kufikia kiwango cha juu zaidi cha Kiwango cha Uainishaji cha Awamu ya Usalama wa Chakula (IPC3). )

Maoni:

Madhara ya ukame ni makubwa hasa maeneo ya mashariki na kusini mwa Ethiopia, mashariki na kaskazini mwa Kenya, na kusini na kati ya Somalia. Hii ina maana kwamba idadi kubwa ya watu iko katika hali mbaya, na ina uwezo mdogo wa kupata mahitaji ya kiwango cha chini ya chakula na hilo hufikiwa ima kwa kukatiza pakubwa zile bidhaa msingi au kwa kile kiitwacho mikakati ya kukabiliana na mgogoro.

Kwa miongo kadhaa,eneo la pembe ya Afrika bali bara lote limekabiliwa na majanga chini ya mnyororo wa ukoloni wa kibepari. Afrika imesibiwa na Mauaji ya halaiki, kuharibiwa kwa miundo mbinu, uporaji wa rasilimali,ukame na umasikini. Tawala za kibepari pamoja na mashirika ya kimataifa ya kutoa misaada yako mbali mno kuweza kufikia kwenye suluhisho la kweli juu ya majanga na maafa haya!

Sababu msingi hasa kwa nini watu wana njaa katika sehemu hii ya bara ambayo kiujumla haina mahusiano na uhaba wa mvua au mabadiliko ya hali ya hewa na migogoro kama inavyodaiwa na vyombo vya habari na taasisi za chakula na utafiti duniani; badala yake, inahusiana kwa pakubwa na sera mbovu za kiuchumi za mfumo wa Kibepari pamoja na tawala mbovu na wanasiasa ambao hawajali chochote isipokuwa matakwa yao ya uchoyo. Afrika ambayo inajumuisha sehemu ya pembe yake ina utajiri mkubwa wa asili yakiwemo madini, mito, ardhi kubwa yenye rutuba, lakini, rasilimali hizi zinatumiwa na mabwenyenye wa makampuni pekee wanaojinufaisha huku raia wakiishia mikono mitupu! Bara hili tajiri limenyanyaswa kinyama, na watu wake wanakufa njaa kikatili chini ya uangalizi wa viongozi wake. Hili limefafanuliwa vyema na mwandishi Torm Burgis katika kitabu chake ‘The Looting Machine’ ambapo anaeleza jinsi wingi wa malighafi unavyopelekea baadhi ya mabwenyenye wa Kiafrika, wafadhili wa nchi za Magharibi, waekezaji waovu Wachina, na hata Benki ya Dunia  kupora na kunyonya Afrika.

Afrika kamwe haitoweza kujinasua na hali mbaya ila kwa kuyaondoa mashirika ya wamagharibi yanayonyakua na kufukarisha ardhi kuchimba lindi la umasikini,ujinga na maradhi. Njia ya Afrika kujitoa hakuna ila waachiliwe kulima ardhi zao zenye rutuba na kula mazao yake waachane kabisa na kuchukua suluhisho za mataifa ya kigeni ambayo ndiyo yanayofukarisha nchi na watu wake. Lakini hili nalo haliwezekani ispokuwa kwa kuangalia na kutatua tatizo la utawala na mfumo unaotakikana hapa duniani kutekelezwa.

Ni muhimu kufahamu kwamba ndwele hii inayokumba pembe ya Afrika yapaswa itie chachu Afrika kufanya kazi kwa haraka pamoja na harakati ya kiulimwengu ya Hizb ut-Tahrir kusimamisha utawala wa Khilafah chini ya mfumo wa Utume kwani pekee ndio utakaolinda Afrika na ulimwengu kwa ujumla dhidi ya majanga haya, kusitisha kabisa uingiliaji wa kikoloni katika ardhi zetu na hapa  kuhakikishia kila raia ndani yake ya anapata  usalama wa chakula.

Kwa ukumbusho, ni chini ya Khilafah ya Umar Ibn Khattab pindi Madina iligubikwa na baa la njaa akawaandikia Mawalii kuwataka wapeleke nafaka ya chakula Arabuni. Ngamia waliobea shehena ya nafaka ya chakula na mahitaji mengine yalikuja kutoka Syria, Iraqi, na Misri. Milo ilipikwa katika ngazi ya Jimbo na watu wote waliokimbilia Madina walilishwa kila siku kwa gharama za serikali. Kulingana na akaunti moja, watu takriban watu 40,000 walilishwa kila siku. Umar (ra) alikataa kula nyama au siagi wakati wa kipindi cha njaa. Tumbo lake lilikuwa likiunguruma, lakini akasema: “Ewe tumbo unaweza kunguruma upendavyo, lakini maadamu njaa inaendelea, siwezi kukuruhusu kitu chochote kitambo.”.

Imeandikwa kwa niaba ya Ofisi kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Shaban Mwalimu

Mwakilishi kwa Vyombo Vya Habari Hizb ut Tahrir Kenya