Habari:
Mapendekezo ya ushuru yaliyowasilishwa kupitia Mswada wa Fedha wa 2018 yameandaliwa kuzalisha ongezeko la mapato ya ushuru la shilingi bilioni 27.5 la mwaka wa matumizi ya serikali wa 2018/2019. Bajeti ya mwaka 2018/2019 ina upungufu wa shilingi bilioni 558.9 (sawia na asilimia 5.7 za uzalishaji jumla wa nchi (GDP) utakaofadhiliwa na mikopo ya nje ya gharama ya shilingi bilioni 287.0 (sawia na asilimia 3.0 ya uzalishaji jumla wa nchi (GDP) huku mikopo mengine ya ndani ya nchi ikigharimu shilingi bilioni 271.9 (sawia na asilimia 2.8 ya uzalishaji jumla wa nchi (GDP). Takwimu rasmi zaonyesha kuwa mfumko mpya katika mrundiko wa deni umetokana pakubwa na ukopaji nje, ulioisukuma idadi jumla ya deni la kigeni kufikia shilingi trilioni 2.563 kufikia mwishoni mwa mwezi Februari. Deni la ndani, ambalo kwa sasa ni kubwa kwa kujumuishwa pia takwimu za mwezi uliopita, limefikia shilingi trilioni 2.448, iikifanya idadi jumla ya madeni yote (ndani na nje) kufikia shilingi trilioni 5.011!
Maoni:
Wakenya walifuatilia kusomwa kwa bajeti ya mwaka wa 2018/2019 mnamo Alhamisi 14 Juni 2018, huku wakiangika pumzi na wakijawa na wasiwasi wakijitayarisha kuendelea na mauvimu ya wizi wa hadharani wa pesa zao chache kutoka mifukoni mwao kwa mwaka mwengine tena mfululizo kupitia majambazi wa kisekula wa kirasilimali kufadhili kiu yao isokwisha huku wakitazamia ukuaji wa kinadharia katika uzalishaji jumla wa nchi (GDP)! Kama kawaida, Wakenya walikwama huku wakiwa hawana jinsi ya kuokoa maisha yao ya umasikini yalojaa mateso chini ya serikali ya sasa ya Jubilee ambayo ni maarufu kwa ujambazi wa kuwatoza ushuru raia mpaka senti yao ya mwisho na kuziba upungufu huu katika bajeti kupitia ukopaji uliopitiliza ambapo zaidi ya thuluthi moja ya bajeti hiyo hupotea kupitia uporaji!
Kenya kama dola nyengine yoyote ya kisekula matakwa ya nidhamu yake ya kiuchumi ya kirasilimali ni kuwa utozaji ushuru na ukopaji ndio yawe machimbuko ya kimsingi ya mapato ya serikali. Kupitia utozaji ushuru na mikopo ya riba, serikali inaweza kuendesha mambo yake kwa kukimu matumizi yake. Kinachoshangaza ni kuwa Kenya imebarikiwa na rasilimali nyingi k.m. madini, ardhi ya ukulima, vyanzo vingi vya maji na hivi karibuni kugunduliwa kwa mafuta nk. ambayo yangeweza kuisukuma Kenya katika ukombozi wa kiuchumi wa kiulimwengu lau kama yangetumiwa vizuri! Lakini, kwa sasa karibu rasilimali zote hizi zimebinafsishwa na kukabidhiwa kampuni za kimagharibi ambazo hulipa malipo duni kwa serikali ya Kenya huku kiwango kikubwa cha mapato kikisafirishwa ng’ambo na kunufaisha uchumi wa nchi za kimagharibi kwa gharama ya uchumi wa Kenya!
Kiini cha tatizo nchini Kenya ni utabikishwaji mfumo wa kikoloni wa kisekula wa kirasilimali ambao ndio unaochipuza nidhamu ya kiuchumi ya kirasilimali. Mtazamo wake kwa nchi za kikoloni kama Kenya; ni ule wa bwawa la maji ambamo wakoloni huja na kila aina ya vyombo vya uchotaji na kuchota kiwango wawezacho kuchota, kama ifanyavyo Uingereza na Amerika mpaka leo, na sasa China imeunga bogi kupitia kile inachokiita mikopo ‘iso dhamana’. Huku wakoloni wakisafirisha rasilimali hizi, upande mwengine wanatupa mikopo ya muda mrefu yenye viwango vya riba ya hali ya juu ili kuhakikisha kuwa hatutaweza kuilipa ndani ya muda wake na hivyo basi kuwageukia tena kwa mikopo mengine ili kukimu uchumi! Maadamu nidhamu ya kiuchumi ya kirasilimali inatabikishwa nchini kenya, ukombozi wa kiuchumi wa Kenya hauwezi kupatikana!
Uislamu chini ya Khilafah (Dola ya Kiislamu) iliyosimamishwa kwa njia ya Mtume (saw), utatekelezwa kwa ukamilifu ikiwemo nidhamu ya kiuchumi ya Kiislamu ichipuzayo kutokana nayo. Sera ya kiuchumi ya Kiislamu itakuwa kudhamini ushibishaji wa mahitaji yote msingi ya kila mtu binafsi kikamilifu, na kisha kumwezesha kushibisha mahitaji yake ya ziada kwa kadri awezavyo kama mtu anayeishi katika jamii maalumu iliyo na mfumo fulani wa kimaisha. Hii yamaanisha Khilafah itayatatua matatizo yote msingi ya kila mmoja kama mwanadamu, anayeishi kwa mujibu wa mahusiano maalumu, kisha kuwawezesha kuinua kiwango cha maisha yao na kufikia utulivu wao kwa mujibu wa mtindo fulani wa kimaisha. Hivyo basi, nidhamu ya kiuchumi ya Kiislamu ni ya kipekee na tofauti na sera zote za kiuchumi ziliopo leo duniani.
Katika Khilafah (Dola ya Kiislamu) Hazina ya Dola (Bait ul-Mal) itajumuisha machimbuko ya mapato yafuatayo: Ngawira (Fai’), Ghanima, Kharaj, Jizya, aina tofauti tofauti za mapato ya mali ya Ummah, mapato ya mali ya Dola, Ushr, Khumus kutokana na Rikaz, madini na pesa za Zakat. Tanbihi: ushuru uliotajwa hapa (Ushuru wa ardhi na Jizya) haupaswi kufahamika kimakosa kama huu unaotozwa leo juu ya watu na serikali za kisekula. Utozaji ushuru na mikopo ya riba imeharamishwa katika Uislamu. Khilafah haitatoza ushuru juu ya raia wake isipokuwa katika baadhi ya hali kama ukame na Jihad. Lakini, ushuru huo, utatozwa juu ya utajiri uliozidi kiwango cha kawaida ambacho mtu hutumia kushibisha mahitaji yake msingi na ya ziada. Hivyo basi, hufikia haki ya thamani ya maisha kwa kila mmoja kibinafsi, na kusahilisha kupatikana kwa mahitaji ya ziada. Wakati huo huo Uislamu umeweka mipaka ambayo mtu aweza kuchuma ili kushibisha mahitaji yake msingi na ya ziada na kupanga mahusiano yake na wengine kwa mujibu wa nidhamu maalumu.
Mwamko wa Kenya na Afrika kwa ujumla uko katika kubadilisha mfumo wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake chafu zitokanazo nao ikiwemo ile ya kijambazi ya demokrasia, nidhamu dhalimu ya kiuchumi na uhuru wa kijamii nk, ambazo ndio chimbuko la mateso na majanga yanayoikumba. Badala yake, kukumbatia mradi wa Khilafah chini ya ulinganizi wa mwamko wa Kiislamu, ambao kwa sasa umeenea ulimwengu mzima na ambayo kusimamishwa kwake tena kwa njia ya Mtume (saw) itaipeleka Kenya na Afrika katika hadhara kuu iliyojaa utulivu, amani na ufanisi ambayo kamwe hayajawahi kushuhudiwa mbeleni katika enzi zote za ukandamizaji wa kisekula wa kikoloni!
Imeandikwa kwa Ajili ya Jarida la Ar-Rayah Toleo Na.190 na
Ali Nassoro Ali
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya
- https://www.businessdailyafrica.com/news/Anxiety-as-Kenya-s-public-debt-load-hits-Sh5trn-mark/539546-4611208-hnvm86z/index.html
- https://www.standardmedia.co.ke/article/2001284223/kenya-s-most-painful-budget-speech-in-full