Imesalia miezi miwili tu kuingia kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu 2017. Huu utakuwa ni uchaguzi wa bunge la kumi na mbili na kama ilivyo ada miungano ya kikabila chini ya mwavuli wa vyama vya kisiasa imebuniwa huku vigogo wa miungano hiyo wakimwaya pesa wakidanganya watu kwa kuwasihi kushiriki kwenye uchaguzi. Kabla hata ya uchaguzi huu tayari uchafu wa Demokrasia ulihisika kwenye mchakato wa uteuzi uliokumbwa na uhuni,ghasia na mauaji! Bila shaka hii ilikuwa ni chachu ya Demokrasia ambayo kiuhalisia imeshindwa kuunganisha jamii bali ni siasa ya ulafi,ukabila na ufisadi.
Kwa jamii ya Kiislamu, uchaguzi huu unakuja baada ya miaka kadhaa ya oparesheni kadhaa za polisi dhidi ya Waislamu na kupotea kwa vijana wengi wa Kiislamu mikononi mwa jeshi la polisi katika maeneo yenye idadi kubwa ya Waislamu kama vile Pwani na kaskazini Mashariki. Jijini Nairobi, wakaazi wa Eastleigh wanakumbuka kwa machungu dhulma ya kutolewa majumbani mwao na kuwekwa katika uwanja wa Kasarani huku wakipigwa na baridi kali kwenye operesheni ‘Usalama Watch’. Licha ya hayo, mikakati kadhaa ya kiserikali kwa msukumo wa dola kuu za kimagharibi ya kuwalazimisha Waislamu kuachana na Uislamu wao imeshika kasi katika kile kiitwacho vita dhidi ya misimamo mikali na itikadi kali.
Kwa hivyo uchaguzi huu unakuja katika kipindi ambacho Waislamu wanajiuliza maswali mengi juu ya mustakabala wao. Licha ya kuweko baadhi ya viongozi wa Kiislamu wakihimiza watu haja ya kupiga kura lakini kihakika mwito wao huu unakabiliwa na upinzani mkubwa kwa Waislamu ambao kwa sasa ni waathiriwa wakubwa kwenye vita dhidi ya ugaidi. Sio hilo, hata ahadi za Wabunge Wakiislamu na vyama vyao walivyoegemea zote zimefeli katika kutetea maslahi ya Waislamu kikweli hivyo basi Waislamu wamejipata hali mbaya zaidi.
Japo kuwa uchaguzi wenyewe bado miezi kadha lakini tayari joto lake twalihisi. Hali hii ikiingia basi kila kilichobaki hakina umuhimu au kina chukua nafasi ya nyuma ya suala zima la uchaguzi. Wakati huu masuala kama ya Uchumi, Elimu, Matibabu, Usalama na hata majanga kama ya Ukame, mafuriko na migomo kama ya madaktari huchukua nafasi ya nyuma, yakitanguliwa na suala la uchaguzi. Na yakiangaziwa basi huwa kwa mazingira ya kutafuta umaarufu kwa lengo la kushinda uchaguzi huo.
Basi kwa nini hatujifunzi kutokana na yale yanaojirudia kila misimu ya uchaguzi? Bali swali la kuulizwa ni kwa nini tunga’ng’anie nidhamu hii ya kisiasa ya kidemokrasia inayotutia kitanzi cha koo kabla ya uchaguzi, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi? Kwani hatuoni kadri siku zinavyosonga hali yazidi kudorora kwa mwananchi wa kawaida ilihali twashiriki katika uchaguzi tukiwa na tamaa ya kuleta mabadiliko?
Kila wakati wa uchaguzi twashiriki kwa kisingizio imma kwa khofu kuwa kutoshiriki kwetu hali itakua mbaya zaidi (kuliko hii!?) au twatiwa tamaa kushiriki kutapatikana mabadiliko, (tamaa ya mazagizagi!?).
أَفَحُكْمَ الْجَاهِلِيَّةِ يَبْغُونَ وَمَنْ أَحْسَنُ مِنْ اللَّهِ حُكْمًا لِقَوْمٍ يُوقِنُونَ
Je, wao wanataka hukumu za Kijahiliya? Na nani aliye mwema zaidi katika kuhukumu kuliko Mwenyezi Mungu kwa watu wenye yakini?
[Al Maida:50]
Hizb ut-Tahrir Kenya imebainisiha mara kwa mara hukumu ya kisheria juu ya kushiriki kwenye chaguzi za Kidemokrasia. Kwa kuwa huu ni wajibu wa kila muislamu basi hatutochoka kurudia kuweka wazi hukmu hii licha ya baadhi kujitia uziwi na upofu mbele ya haki. Suala la uharamu wa kushiriki katika uchaguzi wa kidemokrasia uko wazi katika Muongozo wa Allah swt. Lakini kwanza twataka tuweke suala hili la uharamu wa kura wazi, tukisema kura ni haramu katika nidhamu ya kidemokrasia ni kwa sababu ya lile lengo lililowafanya watu washiriki katika uchaguzi huo nalo nikumchagua kiongozi atakaehukumu na ukafiri au kuwachagua watu watakao kwenda kutunga sharia. Kwetu sisi Waislamu ni jambo linalojulikana kuwa sheria ni za Mwenyezi Mungu SWT pekee na kuwa wanadamu wanapaswa kupeleka maisha yao kwa mujibu wa sheria hizo.
إِنِ الْحُكْمُ إِلَّا لِلَّهِ
Hapana hukumu ila ya Mwenyezi Mungu tu.
[Yusuf:40]
Uchaguzi/kura katika Uislamu ni mubah lakini inapokua uchaguzi unafanywa kwa misingi inaogongana na Itikadi yake au Sheria zake basi Allah swt ametukataza kushiriki. Nidhamu ya kidemokrasia ni nidhamu ya kisiasa katika mfumo wa kirasilimali uliochipuka kutoka katika itikadii ya ki’ilmani- kutenganisha dini na maisha na kwa kuwa Muumba na Sheria zake ametengwa kutoka katika maisha ya mwanadamu, jukumu la kutunga sheria zitakazo muongoza katika maisha yake hapa ulimwenguni limepewa mwanadamu mwenyewe na akili yake finyo. Mwanadamu kwa mujibu wa akili yake atachagua kipi kizuri na kipi kibaya na hubadilika haya kwa mujibu ya maeneo, mazingira, wakati, dhurufu na hali… Kwa hivyo jambo laweza kusemwa kuwa ni zuri kisha likabadilika kuwa baya na kinyume chake kwa kuathiriwa na maeneo, wakati… ukizingatia kuwa maslahi ndio kipimo cha maisha ndani ya mfumo huu. Amma katika Uislamu kizuri na kibaya ni kwa mujibu wa sheria za Allah, kwa hivyo haibadiliki wala kuathiriwa na humtatulia mwanadamu matatizo yake popote alipo na nyakati zote. Huku kumpa mwanadamu uweza wa kutunga sharia ni athari ya fikra ya kutenganisha dini na duniya ambayo inagongana moja kwa moja na fikra ya kumpwekesha Allah swt. Isitoshe itikadi hii ya ki’ilmani ndio iliompa huyu mwanadamu ubwana wa kujitungia sharia ambao ni ukafiri. Basi vipi Muislamu atashiriki katika uchaguzi huo wakuwapeleka watu imma kuhukumu kinyume na sheria za Allah au kutunga sharia kinyume na Allah swt? Kushiriki huku kwa kisingizio chochote ni kutambua ubwana wa mwanadamu kinyume na Allah swt na hili ni haramu hakuna shaka ndani yake.
Enyi Waislamu: Jee hamuridhiki na kile kilichomteremkia mtukufu wa viumbe Mtume saw na kuwafikishieni na kilicho kamilika na kutimia katika neema zake Allah swt nao ni Uislamu!? Basi kwa nini mutake upotofu unaotokamana na akili finyu za wanaadamu wachache wasokuwa na maadili? Ni wajibu juu yetu kama Waislamu kuuamini na kuubeba Uislamu kama mfumo kamili wa kimaisha ulio na suluhisho zote za kimaisha na kuwalingania wasio kuwa Waislamu ili kuwakomboa walimwengu na madhila haya! Hili ni sahali ikiwa tutawalingania Uislamu kwa usafi wake kama mstari ulionyoka na kuonyesha kombo ya mfumo, unaotawala leo ulimwenguni, wa kirasilimali na nidhamu yake ya kidemokrasia kwani watu wamechoshwa nao illa hawana mbadala. Hakuna pahala hili hudhihiri wazi kama Bara Afrika na haswa hapa kwetu Kenya, kwani urasilimali umeifukarisha kiuchumi juu ya kuwa na utajiri mkubwa, kuangamiza kwa migawanyiko ya kikabila na vita visivyokwisha, kuendeleza ubepari kwa maslahi ya Marekani na Ulaya. Hakika jamii zimechoshwa na hali zilivyo illa hawaoni badala nyengine kwa kuenezewa sumu dhidi ya Mfumo safi wa Uislamu, basi ni juu yetu kuwalingania usafi huu kwao na kuwasimamishia hoja. Basi huwaje Waislamu wakawacha kheri hii na kujiingiza kwenye machafu ya kidemokrasia? Imma kwa kugombea, kulingania au kushiriki katika chaguzi hizi na kuutia nguvu kinyume na Uislamu, hatuoni tuna majibu ya kujibu mbele ya Allah swt siku haitomfaa mtu mali wala wana?
Mfumo wa kirasilimali na nidhamu yake ya kiutawala ya kidemokrasia haijaleta kheri yoyote tangu mwanzo kuingia kwake bara Afrika na haswa nchi ya Kenya ilipoletwa kimabavu na wakoloni wakiingereza kwa malengo ya kuwatenza nguvu wenyeji na kufyonza rasilimali zao. Na hali haijabadilika hata baada ya kuondoka kwa wakoloni hawa na kuwapa wenyeji uhuru bandia wa bendera lakini hali halisi ikabakia kuwa wao ndio waendeshaji wa nchi kwa kupanga siasa kwa maslahi yao. Illa walifaulu kuwafunga watu macho kwa kuwaonyesha kuwa sasa nchi ipo katika mikono ya watawala ambao ni wenyeji na maraia wana haki ya kuwachagua kila baada ya miaka kadha. Hadaa hii imefaulu kuwapa watu tamaa ya kirongo kiasi ya kuwa hawaoni kuwa ukoloni unaendelea kwa sura nyengine na wala hayo mabadiliko wanayoyatarajia hayatokuja ndani ya mfumo huu, bali ni danganya toto tu.
Enyi Waislamu: Mfumo huu wa kibepari wa kirasilimali umefeli ulimwengu mzima, hata katika ulimwengu wa kwanza na wanaofaidika nao ni wachache walioko mamlakani. Kinachoibakisha kutotoweka kwake ni nidhamu yake ya utawala ya kidemokrasia inayowapa watu tamaa ya kushiriki kuleta mabadiliko na mwanzo mpya ilhali ukweli unabakia kuwa huu mfumo hauwafai hata kuwasimamia wanyama licha ya mwanadamu! Sisi Waislamu tuna mfumo badala wa Uislamu na nidhamu yake ya utawala wa Khilafah inayo tokamana na wahyi kutoka kwa Allah swt. Mfumo wa haki utakao leta uadilifu kwa kumpangia mwanadamu mahusiano yake na wengine kwa mujibu ya maamrisho na makatazo yanayotoka kutoka kwa Yule alietuumba na kutujua udhaifu wetu na mahitaji yetu. Ni juu yetu kuufahamu Uislamu wetu kama mfumo wa maisha ulio na suluhisho kamilifu kwa mwanadamu na utakao leta utulivu katika mgongo wa ardhi na kuondoa ufisadi ulioenezwa na mfumo mpotovu wa urasilimali. Ni juu yetu sisi kuwafikishia wasio kuwa Waislamu mfumo wa Uislamu kuwa ni suluhisho kwa mwanadamu na kumuondolea takataka masikioni alojazwa nazo na propaganda za mabepari wanaotishiwa na Uislamu. Urasilimali umekufa lakini yahitajika Uislamu ukitangaze kifo chake watu wabumburike kutoka katika usingizi mnono uliowagubika. Hatuna tena sababu za kunyamaza tukitarajia mambo yatakwenda kubadilika bali ni juu yetu kuleta haya mabadiliko kwa njia aliotuonesha Mtume saaw, laa sivyo tutaendelea kudhalilika na siku ya qiyamah tukutane na adhabu ilio kali.
Hizb ut tahrir Kenya inawakumbusha Waislamu kutembea nayo katika kuleta mageuzi ya kihakika yatakayo wakomboa wanadamu na madhila ya ukoloni unougubika ulimwengu. Pia tuna walingania kila mwenye akili kuuangalia Uislamu kama mfumo badala utakao wapa suluhisho za kudumu na kuleta utulivu kwa mwanadamu badala ya kila muhula kubahatisha katika uchaguzi wa pata potea ukijua ndani ya moyo wako kitendo chako hakitoleta mabadiliko ya kweli.
Allah swt asema:
وَمَنْ أَعْرَضَ عَنْ ذِكْرِي فَإِنَّ لَهُ مَعِيشَةً ضَنكًا وَنَحْشُرُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ أَعْمَى
Na atakaye jiepusha na mawaidha yangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na Siku ya Kiyama tutamfufua hali ya kuwa kipofu. [Taha:124]
Hizb ut-Tahrir Kenya
1 Shawwal 1438 Hijri
25/26 Juni, 2017 Miladi