Hotuba ya Rais 2019: Hewa Tupu Isiyojali Maisha ya Raia!

بسم الله الرحمن الرحيم

Alhamisi, 4 Aprili 2019, Rais Uhuru Kenyatta kwa mujibu wa Kipengee 132 cha Katiba ya Kenya alitoa hotuba yake kwa taifa huku raia jumla wakitarajia angalau afueni katika maisha yao magumu. Lakini hakuna lolote lililopatikana isipokuwa ni muendelezo wa uporaji na ukandamizaji wa raia! Raia wataendelea kutaabika pasina na kuwepo yeyote wa kuwanusuru kutokana na matatizo yanayo wakumba yakiwa kama kitanzi shingoni mwao kila kukicha kinakazwa na serikali ya kisekula ya kiraslimali!

Hotuba hii imetolewa siku moja tu baada ya kutolewa kwa ripoti ya mwaka 2019 ya Utafiti wa Matumizi ya Fedha Nyumbani iliyosimamiwa na Benki Kuu ya Kenya (CBK) pamoja na Sekta ya Kuimarisha Fedha (FSD) iliyosema kuwa takribani Wakenya asilimia 51 wanaishi kwa njia ya mkono kwa mdomo (hali ngumu)! Hii ikiwa ni ongezeko kutoka asilimia 34.3 mwaka 2016! (the-star.co.ke, 03/04/2019) Hotuba hii pia imekuja wiki chache baada ya ripoti ya Wakenya takribani milioni 1.2 wamo hatarini kufa njaa kutokana na ukame. Na jumla zaidi ya Wakenya takribani milioni 14.7 hawana chakula kwa msimu huu wa kiangazi unaoendelea. (the-star.co.ke, 18/03/2019).  Kenya imetajwa katika ripoti ya Benki ya Dunia (WB) kuwa ina watu milioni 17.6 katika umasikini wa kupindukia! Kwa mujibu wa kipimo cha Benki ya Dunia (WB) mtu yeyote ambaye matumizi yake ni chini ya dola 1.90 (Ksh200) kwa siku ni masikini wa kupindukia! (theeastafrican.co.ke, 06/02/2019). Hotuba hii haikuelezea namna taifa litakavyo jikwamua kutoka katika minyororo ya madeni ya riba ambayo hivi sasa yamefikia trilioni Sh.5.4 huku hazina ya kitaifa ikichukua mkopo kila siku wa bilioni Sh2!  (nation.co.ke, 02/04/2019) Madeni hayo yatarajiwa kuzidi hususan kutokana na ziara inayo tarajiwa ya Rais Uhuru Kenyatta kuzuru Uchina katika Kongamano la Mkakati wa Mkanda na Barabara (BRI) ambapo inatarajiwa atatia saini mkopo wa bilioni Sh368 kwa ujenzi wa SGR kutoka Naivasha – Kisumu. (mediamaxnetwork.co.ke, 02/04/2019)!

Kinyume ni kuwa hotuba hii iliangazia tu kukuwa kwa uchumi wa mwaka 2018 kwa asilimia 6.1 na inatarajiwa mwaka 2019 kufikia asilimia 6.3! Zaidi ya hayo, ili zungumzia kuhusu muendelezo wa kisanii wa vita dhidi ya ufisadi, usawazishaji wa makovu ya mizozo ya kihistoria kwa kutenga bilioni Sh10 ili kuboresha uwiano na amani, kumakinisha na kupigia debe “mkono wa heri” baina yake Rais na Raila na kuboresha usalama wa taifa kwa maana nyingine kuendeleza vita dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa kisingizo cha vita dhidi ya misimamo mikali na ugaidi! Hakuna mahali Mkenya mlala hoi ametajwa moja kwa moja kuhusiana na namna serikali itakavyo mtatulia moja kwa moja matatizo yake msingi ya kisiasa-kiuchumi-kijamii-kielimu!

Serikali ya Kenya kama zilivyo serikali zote duniani ambazo zimesimama juu ya msingi wa kisekula (kutenganisha dini na maisha/serikali) na mfumo wake wa kikoloni wa kirasilimali (unawapa kipaombele matajiri) na kuwakandamiza jumla ya raia na kuwabakisha kuwa majukumu yao msingi ni: kupiga kura ili kuwahalalisha matajiri kuingia au kubakia madarakani, kuendelea kuwa watumwa katika viwanda na majumba ya matajiri na kulipa ushuru ambao kila kukicha unazidi kwa kasi mno! Na baya zaidi ni kuwa Kenya ni shamba la bwana mkoloni Muingereza na viongozi wake ni vibaraka waliojisalimisha kwake! Kwa hivyo, ni jambo la kutarajiwa kuona kuwa hotuba hiyo ilikuwa ni Hewa Tupu Isiyojali Maisha ya Raia, kwa sababu serikali za kisekula zipo kwa ajili ya kuwawekea mazingira mazuri Wamagharibi warasilimali au vibaraka wao kwa sura za “wawekezaji” ambao wanaendeleza uporaji wa rasilimali za Kenya na Afrika na kuwafanya watumwa watu wake!

Kenya na Afrika kwa ujumla ili kujikomboa kutoka katika hotuba zilizojaa hewa tupu mfano wa hii; lazima waunge mkono mwito wa kurudisha Maisha ya Kiislamu kwa kurudisha Serikali ya Kiislamu ya Khilafah kwa njia ya Utume. Khilafah itahakikisha kuwa Shari’ah (Qur’an na Sunnah) inayotoka kwa Mwenyezi Mungu (swt) zinatekelezwa kwa ukamilifu wake pasina na kujali au kupiga hesabu za Wamagharibi warasilimali. Kwani Khalifah atakuwa anakwenda mbio kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu (swt) huku akihofia Siku ya Hukumu na akizingatia kwa makini maneno ya Mtume (saw):

«الإِمَامُ رَاعٍ وَمَسْؤولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ»

“Imamu (Khalifah) ni msimamizi /mchungaji na ataulizwa juu ya anaowachunga”

Kwa sababu hiyo Dola ya Khilafah itakuwepo kuwahudumia na kuwatatulia raia wake matatizo wanayo kumbana nayo na wala sio kuyapatiliza ili kuwakamua na kuwafanya biashara raia wake kama inavyo shuhudiwa katika tawala hizi za kidemokrasia za kirasilimali. Matatizo yote ya kiwemo ya kiuchumi yatatatuliwa kwa kutekeleza sera yake ya kiuchumi ya kuhakikisha usambazaji wa mali kwa raia wote na kuhakikisha mahitaji msingi yanakidhiwa kikamilifu na kuwezesha kupata mahitaji ya ziada. Kijamii kuhakikisha kuwa mujtama unahifadhika na fahamu ovu za uhuru (kiliberali) ambazo zimewapelekea wanadamu chini ya urasilimali kuwa kiwango cha chini kuliko hata wanyama eti kwa hoja ya uhuru wa kibinafsi! Kielimu kwa kuwajenga wanafunzi na raia jumla kuwa na utambulisho (shaksiyya) wa Kiislamu. Kisiasa kuwajenga na kuwapa nafasi kushiriki kikamilifu katika uendeshaji wa Dola yao adhimu ya Khilafah kwa mujibu wa Shari’ah. Hakika hivi karibuni kwa idhini na baraka za Mwenyezi Mungu (swt) tutapata mlinzi na ngao yetu Khilafah Rashidah na hapo ndipo tutakapo pata utulivu, ustawi na ufanisi wa kweli.

(فَإِنَّ مَعَ ٱلۡعُسۡرِ يُسۡرًا* إِنَّ مَعَ ٱلۡعُسۡرِ يُسۡرً۬ا)

“Basi kwa hakika pamoja na uzito upo wepesi. Hakika pamoja na uzito upo wepesi”

[Ash-Sharh: 5-6]

 

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya

Makala Na.39: Ijumaa, 29 Rajab 1440 | 2019/04/05