Idadi ya Watu hugeuzwa na kuwa idadi za kisiasa huku walalahoi wakiendelea kusota kwa hali ngumu.

Habari Na Maoni

Habari:

Ijumaa tarehe 21 Februari, shirika la kitaifa la takwimu ilitoa ripoti tatu za matokeo ya mwisho ya hesabu ya watu ya mwaka 2019 (kwenye mijeledi mitatu; II, III and IV) iliochapishwa na taasisi kuu ya Kenya ya watu na makaazi (KPHC) inayoonyesha kwamba idadi ya wakenya kwa sasa ni 47.5 Million.  Matokeo hayo yalikuja na tarakimu za kutamausha juu ya uhalisia wa hali ya maisha ya wakenya wengi- hali ya nyumba wanazoishi, vyanzo vya maji ya kunywa na mafuta ya majiko ya kupikia. Twakimu hizo zinaonesha kwamba asilimia  41 ya nyumba zilizoko mashambani kuta zake  zimejengwa kwa matope na kinyezi cha ng’ombe. Kiwango hiki kinaanza kati ya asilimia 50 na 80 ya kaunti nyingi katika maeneo ya pwani, Bonde la ufa, Magharibi na Nyanza. Sawa na viwango hivyo,imebainika kwamba vifaa vya ujenzi vinavyotumiwa sana kujenga nyumba ni matope, mchanga na mavi ya ng’ombe kwa asilimia 43 miongoni mwa vifaa vyengine. Asilimia 14 pekee ndio walio na uwezo wa kupata maji ya mifereji. Kulingana na tarakimu hizo, ukosefu wa ajira kwa vijana upo kwa asilimia 39 huku watu milioni 5.2 wenye umri katika ya 18 na 34 hawana kazi za kufanya.

Maoni:

Takwimu hizi za kushtusha zinazoonesha msoto mkubwa wa kimaisha wa watu ni dhihirisho kwamba tarakimu za zoezi la idadi ya watu hadi sasa hazijasaidia serikali kikweli kuondosha matatizo yanayokumba jamii. Imebainika wazi urongo wa ile nadharia ya Malthuniasm ndani ya mfumo wa kibepari inayodai kwamba kuhesabu watu ni mchakato unaoipa serikali  fursa ya kupangilia vyema mipango yake na kusambaza huduma zake kwa raia. Lau kujua idadi ya watu kunasaidia kikweli mipangalio ya serikali basi watu waishio kwenye ardhi kame na maeneo yanayokaribia kuwa kame wasingeliishi katika hali mbaya wakikosa hata mahitaji msingi bali wesingelikufa njaa kutokamana na uhaba wa chakula.

Kwenye ulingo wa Kisiasa,matokeo ya idadi ya watu yameibua hisia mseto miongoni mwa wanasiasa huku athari ya kisiasa ikianza kujitokeza kama ilivyo kwenye mijadala juu ya ripoti ya BBI ilioshika kasi  na kampeni za uchaguzi ambazo tayari zikiwa zimeng’oa nanga.Tarakimu za idadi ya watu tayari zimekua zikiibua mazungumzo ya jinsi gani zitakavyoathiri mustakabala wa siasa. Tokea kutolewa kwa matokeo ya awali ya Censa mwezi Novemba mwaka jana, baadhi ya wanasiasa, kwa hofu ya kupoteza nafasi na nguvu zao za kisiasa, walikataa  matokeo hayo kwa kuwa yalionesha mapungufu makubwa ya idadi halisi ya watu katika kaunti zao. Kiongozi wa waliowengi bungeni Adan Duale, aliiongoza mkao pamoja na viongozi wa Kaskazini mashariki kutaka kutolewa kwa matokeo ya kwanza ya nyanjani yaliyoegemewa na maofisaa wa sensa. Baadhi ya viongozi wa bonde la ufa na kutoka Nyanza na eneo la mashariki mwa nchi pia wametaka maelezo ya kina juu yaa idadi ndogo ambazo usahihi wake umetetewa na shirika la kitaifa la takwimu. Kwa kuwa Demokrasia ni siasa inayojulikana katika kuleta migawanyiko ndani ya jamii hivyo kadri nchi ya ilivyogawanyika hivyohivyo suala la kuhesabu watu hugeuka kuwa la mzozo. Kwa kuwa siasa za Kenya hupelekwa katika misingi ya kikabila idadi ya watu,sensa imekua ikigubikwa na utata. Hii ni kwa kuwa tarakimu zinazohusishwa na baadhi ya kabila fulani hutajwa kuwa ni yenye kuathiri matokeo ya uchaguzi. Nchi ya pili kwa idadi kubwa ya watu barani Afrika –Ethiopia imekua ikihairisha zoezi la sensa kwa mara mbili tokea mwaka 2017 kutokana na kuibuka kwa maandamano makali na vurugu za kikabila. Na litakapo fanyika zoezi hilo,matokeo yatakuwa yana umuhimu mkubwa kwa makundi yanayopigania mamlaka ya kisiasa  hivyo kabila kubwa zaidi ndio linatarajiwa kuwa na nguvu zaidi na huenda likapatiliza nafasi hiyo ya kutaka kujitawala chini ya mfumo wa kimajimbo. Kwa mfano kwenye kura ya maoni, Kabila la Sidama kusini mwa Ethiopia lilipiga kura kusukuma kupata jimbo lake. Hali ni hivyohivyo Nigeria ambayo ina historia ya kuwa sensa zenye utata.

Zoezi la kitaifa la kuhesabu watu la mwaka jana ni tofauti na yale miaka mingine iliopita kwani serikali kwa wakati huo imekuja na kitendo cha kuwafanyia raia wake ujasusi ambapo walitakikana kutoa maelezo yanayohusu maisha yao ya kibinafsi. Kwa mwongo mmoja sasa Serikali imekua ikionekana kuwa na hamu kubwa ya kuwafanyia ujasusi raia. Chini ya kibandiko cha kupambana na mashambulizi ya kigaidi, Serikali ikaja na hatua inayojulikana kama mpango wa nyumba kumi unaowataka raia kuchunguzana na kila mmoja aweze kutoa maelezo ya mwenzake kwa wasimamizi wa mitaa na vyombo vya usalama. Katika historia serikali kadhaa duniani zimekua zikitumia data binafsi za watu ili kusukuma ajenda zake hatari. Mwanasiasa wa Kiamereika Michele Bachmann aliwahi kusema:”Tukiangalia historia ya Amerika katika ya mwaka 1942 na 1947 data za watu zilikusanywa na taasisi ya tume ya kuhesabu watu na kukabidhiwa maofisaa wa shirika la kijasusi na mashirika mengine hatua hiyo ilikuwa ni kuitikia agizo la rais Roosevelt. Na hivyo ndivyo raia wa Kiamerika wenye asili ya Kijapani walivyodhalilishwa kwa kuwekwa kwenye kambi maalumu”

Suala zima la kuhesabu watu linazunguka kwenye nadharia ya kimakosa ijulikanayo kama “mlipuko wa idadi ya watu” (Population Explosion). Mwaka 1798 aliekuwa Reverent Thomas Malthus alichapisha kitabu chake alichokiita An Essay on the Principle of Population akisema kwamba uwezo wa idadi ya watu kihakika ni kubwa sana kushina uwezo wa dunia kuweza kusimamia maisha ya watu. Nadharia hii potofu ndio imechochea kuweko kwa sera za kudhibiti idadi ya watu zinazopigiwa debe na mashirika ya kirasilimali kama Ford Foundation, Rockefelller na baraza la idadi ya watu.

Uislamu kwa upande wake hatakama haupingi suala la kuhesabu watu lakini unabeba mtazamo kwamba kile anayezaliwa hapa duniani anakuja huku mgao wake wa riziki tayari umewekwa na MwenyeziMungu SWT,ikiwemo suala zima la chakula. Kwa kuwa lengo msingi la mfumo wa kiuchumi wa Kiislamu ni kusambaza rasilimali ili kuhakikisha kuwa kila nafsi ilio hai inapata kukimu mahitaji yake, hivyo Serikali ya Al-Khilafah huhitajika kuwasimamia na kuwahakikishia raia wake mahitaji ya dharura ikiwemo chakula, mavazi na makaazi. Kwa muktadha huu Khilafah haitonekana kupoteza mabilioni ya pesa za umma kama zifanyazo serikali za kibepari kufanya sensa huku raia wanahitaji pesa kuwasimamia. Isitoshe, ongezeko la idadi ya watu kwa hakika sio tishio kwa uchumi bali utekelezwa wa sera mbovu za mfumo muovu wa kiuchumi wa kibepari ndio tatizo. Ubepari umejengwa katika misingi ya kudhalilisha walalahoi huku ukielemea katika kujali  na kukuza zaidi maslahi ya tabaka dogo la mabepari ambao uchu wao wa kung’ang’ania utajiri huongezeka siku hadi siku.

 

Makala haya yemeandikwa kwa niaba ya Ofisi kuu ya Habari ya Hizb ut-Tahrir

na Shabani Mwalimu

                                                  Mwakilishi kwa vyombo vya Habari Hizb ut-Tahrir Kenya.