Janga la uvamizi wa Nzige: Njia ya Uislamu ya kukabaliana nalo.

Jimbo la Afrika Mashariki linakabiliwa na janga la uvamizi wa nzige linaloendelea kuwa kero kubwa kwa wakulima.  Mataifa mengine yaliyoathiriwa na janga hili ni kama vile Yemen, Oman na Pakistan. Kwa hapa Kenya, kero hili ambalo limekumba majimbo 17 ndio baya zaidi kwa kipindi cha miaka sabini iliopita. Shirika la chakula na kilimo duniani linakaridia kwamba eka 55,000 za mashamba zimevamiwa na nzige. Kwa mujibu wa shirika la utangazaji la BBC, ni kwamba kuna hofu ya kuongezeka zaidi kwa wadudu hawa hatari ambao tayari wamefikia mabilioni.

Licha ya matumizi ya mbinu za unyunyuizaji dawa miongoni mwa mbinu nyengine,mataifa ya ukanda wa Afrika mashariki hadi sasa hayajafaulu katika kudhibiti wadudu hawa. Kwa upande wa serikali ya Kenya tayari ishasema  kuwa itachukua takriban miezi sita kudhibiti suala la nzige jambo ambalo moja kwa moja linaathiri pakubwa uzalishaji wa chakula. Tayari  zaidi ya watu milioni kumi wanakabiliwa na uhaba wa chakula kutokana na uvamizi wa nzige, hili ni kwa mujibu wa ripoti ya shirika la chakula na kilimo dunia (FAO.) Inakisiwa kwamba nzige wanaweza kusafiri umbali wa kilomita 150 (maili 93) kwa siku, na kila nzige mkubwa anaweza kula kiasi kikubwa cha chakula kwa siku.

Janga hili ni miongoni mwa majanga ya hali ya kimaumbile (natural) yaani mara nyingi kutokea kwake kuko kinyume na matakwa ya wanadamu hivyo katu mwanadamu hawezi kuyazuia. Pamoja na hivyo,Mwenyezi Mungu (swt) amewaonya wanadamu kufanya mambo ambayo huhatarisha maisha ya mwanadamu. Aidha, wanadamu wametunukiwa akili ambazo zapaswa zitumike katika kuweka mipango na matayarisho  kabambe kama njia ya kupunguza athari ya mikasa itakayotokea. Kwa bahati mbaya, ndani ya tawala za Kibepari yote hayo hukosekanwa, yaani twaona jinsi gani uchafuzi wa mazingira ukiendelezwa kwa kasi sambamba na kupuuzwa kwa tahadhari kabla ya kutokea majanga. Kwa mfano, katibu mkuu wa umoja wa mataifa amasema sababu kuu ya kuenea kwa nzige kwa kasi kubwa ni mabadiliko ya tabia nchi. Wataalamu wa hali ya anga wanataja kwamba kiwango kikubwa cha moshi viwandani huchangia pakubwa kuongeza kiwango cha joto duniani hatimaye kusababisha mvua nyingi zinazoleta mafuriko. Mvua zilizoshuhudiwa kwa hivi karibuni katika maeneo mengi duniani zinatajwa kama mazingira yanayochochea nzige wazalikane kwa wingi. Mataifa mengi hasa ya kimagharibi licha ya kuwa kila mara huzungumzia athari ya mabadiliko ya tabia za nchi, na kuweka kanuni za kudhibiti hali hii, kanuni hizi hubana mataifa madogo tu huku mataifa makubwa bado yakiwa bado yanashindana kuwa na viwanda vya uzalishaji silaha, ambavyo huchangia pakubwa kuzalisha hewa chafu. Kulingana na utafiti wa shirika la Mazingira nchini Uholanzi liliorodhesha Uchina, Marekani, India na Russia kuwa ni yenye kuongoza katika uzalishaji wa hewa chafu duniani. Kwa hivyo ni wazi kwamba Ubepari umesahilishia dunia kutokea janga hili la nzige na majanga mengineyo mengi.

Mbali na haya, janga hili limekuwa kubwa kwa sababu ya dharau za tawala za kibepari ambazo kikawaida husubiria majanga kutokea licha ya kutolewa kwa tahadhari za mapema. Shirika la Chakula na Kilimo duniani lilitoa tahadhari uvamizi wa nzige mapema katika mwezi Juni mwaka jana yaani miezi takriban saba kabla, lakini hakuna hatua yoyote iliochukuliwa! Na hii kwa kuwa mashamba mengi yaliyovamiwa na nzige ni ya wakulima wa kawaida wala sio kwenye mashamba ya mabwenyenye.Ni wazi kuwa mfumo kibepari hujenga utabaka katika kila kitu hivyo mashamba ya matajiri huangaliwa kwa mbinu zote huku ya walalahoi yakipuziliwa mbali.  Serikali ya Kenya, kupitia waziri wake wa kilimo Peter Munya ilikiri kutochukua kwake hatua za mapema za kutatua tatizo la nzige na hata baada ya uvamizi wa wadudu hao ikaonekana kuligeuza kama uwanja wa majaribio ya mbinu za kukabiliana nalo. Ikaanza kwa kutumia vitoa machozi, hatimaye unyunyuizaji wa dawa kutumia ndege lakini pamoja na mbinu zote hizo maji yalizidi unga. Lakini cha kusikitisha zaidi ni kusikia matamshi ya baadhi ya viongozi wakitaka raia kuondosha wasiwasi kwa madai kwamba nzinge waliovamia Kenya wemezeeka watakufa hivi karibuni!

Janga hili kiuwazi linaonyesha namna tawala za kirasilimali na serikali zake jinsi zinavyo puuza maslahi ya umma. Wakati huohuo kwenye kinyang’anyiro cha kutafuta uongozi utawaona viongozi wake wakizurura nchi yote kwa ndege wakitafuta kura huku wakati wa majanga hutoa tu matamshi matupu! Hiyo ndiyo sura kamili ya urasilimali na viongozi wake ambao wanathamini tu maisha yao na hawayapi umuhimu maisha ya walalahoi.

Kama mfumo kamili, Uislamu unaliweka jukumu la kusimamia mambo ya umma kwa serikali na sio watu binafsi. Mtume (saw) alisema:

«الإِمَامُ رَاعٍ وَهُوَ مَسْئُولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ»

“Kiongozi wa watu ni mchungaji na atahesabiwa juu ya raia wake.”

Hadithi hii haibebi tu kazi ya kiongozi bali kuna ufahamu mzito ndani unaotafautisha uongozi wa Kiislamu na ule wa kidemokrasia. Uongozi ni amana yaani MwenyeziMungu atamuuliza kila aliyekuwa na mamlaka ya usimamizi wa watu. Kwa hisia ndio Uislamu umezingatia kuwa ni khiyana kubwa sana kwa mtawala kupuuza maslahi yoyote yale ya kiraia.Kwa haya serikali ya Kiislamu (Al-Khilafah) imepewa jukumu la kuhifadhi maisha ya raia wake wakati wotewote iwe kuna majanga ama hakuna majanga.Ama kuhusiana na mikasa kama hili ya uvamizi wa nzige, ukame na mfano wake , Khilafah huwajibika kwanza ya kufanya mikakati mapema endapo kuna ishara za kutokea kwa majanga. Na yanapotokea serikali huwajibika, kuchukua  fedha zilizoko katika hazina (Baitul Mal) ili kuwasimamia walioathirika na jukumu lake juu kwa umma sio fadhla. Lau itakuwa hakuna fedha katika hazina, basi Khalifah atalazimika kuwatoza matajiri kiwango maalumu cha kodi ili kutatua tatizo hilo. Hivi ndivyo Khilafah inavyotarajiwa kukabiliana na majanga na mikasa bi idhni llah Taala.

Shabani Mwalimu

Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari

Hizb ut-Tahrir Kenya.