Kenya ilikuwa mwenyeji kwa mara ya kwanza wa Kongamano la Ngazi ya Juu kuhusu Uchumi Endelevu wa Buluu Duniani lililofanyika Nairobi kuanzia 26 hadi 28 Novemba 2018. Kauli mbiu ya kongamano hilo ilikuwa “Uchumi wa Buluu na Ajenda 2030 ya Maendeleo Endelevu.” Kongamano hilo lilifanyika kwa ushirikiano wa Canada na Japan. Lengo la kongamano lilikuwa ni kuweza kujifunza namna ya kujenga uchumi wa buluu ambao unaounganisha uwezo wa bahari na machimbuko ya maji duniani ili kuinua maisha ya watu wote. Uongozi wa Afrika uliwasilishwa vilivyo kwa kuhudhuria mwenyekiti wa AU Paul Kagame na mwenyekiti wa Tume ya AU Mousa Faki pamoja na wengine. (www.blueeconomyconference.go.ke)
Ni muhimu tutaje yafuatayo ili tuweze kufahamu yaliyoko nyuma ya kongamano hilo:
Kwanza: Jumuiya ya Madola mnamo 2013 ilitia saini Mkataba wa Buluu wa Jumuiya ya Madola ambao ulikuwa ni makubaliano ya nchi zote 53 za Jumuiya ya Madola ili kushirikiana kikamilifu kutatua matatizo yanayohusiana na bahari na kufikia ahadi za maendeleo endelevu ya bahari. Mkataba huo umeweka misingi ya Buluu, kuhakikisha kuwa Jumuiya ya Madola inachukua mtizamo wa kimakini, kiusawa na unaojumuisha maendeleo na ulinzi wa uchumi wa bahari. Zaidi ya hayo, wakati wa mkutano wa Jumuiya ya Madola wa Viongozi wa Serikali uliofanyika Aprili 2018 London, Uingereza, ulipelekea kuundwa kwa Makundi ya Utendaji ya Mkataba wa Buluu wa Jumuiya ya Madola ambayo yataendeshwa na wanachama, yakiongozwa na nchi “watetezi”. Nchi kumi na moja (11) zilijitokeza ili kuwa watetezi wa mada nane ambazo zilipendekezwa kuwa vipaombele. Makundi ya Utendaji yatahakikisha kuwa nguvu za mataifa 53 zimetumika vyema na kutoa muongozo katika maendeleo ya zana na mafunzo. (bluecharter.thecommonwealth.org)
Pili: Kenya, Canada na Fiji ni katika nchi tatu kati ya nchi 11 za Jumuiya ya Madola ambazo zilijitokeza kuwa watetezi wa vipaombele. Kenya itasimamia Kundi la Utendaji kuhusu kubuni mtizamo makini juu ya Uchumi wa Buluu, kusukuma matumizi endelevu ya rasilimali za bahari kwa ukuwaji wa kiuchumi, kuinua hali za maisha na afya ya mazingira ya bahari. Canada itasimamia Kundi la Utendaji juu ya Uangalizi wa Bahari. Fiji itasimamia Kundi la Utendaji juu ya Bahari na Mabadiliko ya tabianchi. (bluecharter.thecommonwealth.org)
Tatu: Umoja wa Mataifa (UN) wakati wa Mkutano wa Maendeleo Endelevu ya UN mnamo Septemba 2015 Mjini New York, USA; nchi 193 wanachama wa Baraza la UN walipitisha Ajenda 2030 ya Maendeleo kwa kichwa “Kuibadilisha dunia yetu: Ajenda 2030 ya Maendeleo Endelevu.” Ajenda hiyo ina Malengo 17, inayojumuisha Lengo Na.14: Maisha Chini ya Maji. Inalenga kuhifadhi na kutumia vyema bahari na rasilimali za baharini. Zaidi ya hayo, Umoja wa Mataifa iliandaa kwa mara ya kwanza “Kongamano la Bahari” kuanzia 5 hadi 9 Juni, 2017 Mjini New York, USA. Lililofuatiwa na kuchaguliwa kwa Peter Thomson wa Fiji kuwa Balozi Maalum wa UN kuhusiana na Bahari mnamo 12 Septemba 2017 ili kufuatilia matokeo ya Kongamano la Bahari la UN. (www.un.org/sustainabledevelopment)
Nne: Benki ya Dunia iliandaa kongamano juu ya “Ufadhili wa Uchumi Endelevu wa Bahari na Hali ya Hewa ndani ya Afrika” kuanzia 19 hadi 23 Februari 2018 katika Hoteli ya Savoy, Seychelles. Lengo la kongamano lilikuwa ni kuongeza maarifa na kutathmini suluhisho la kiubunifu juu ya namna gani Afrika inaweza kupatiliza fedha ili kusaidia mikakati endelevu ya uchumi wa buluu. Uendelezaji wa maendeleo ya uchumi wa buluu Afrika ni njia za kupanua uchumi huu na kuboresha ukomavu wao mbele ya tabianchi. (www.worldbank.org)
Tano: Uchumi wa buluu umeelezewa kuwa ni ‘Mpaka Mpya wa Mwamko wa Afrika.’ Uwezo wake juu ya bara ambalo takribani thuluthi mbili ya dola zake zina mkondo wa bahari, ambao biashara yake ni asilimia 90 inategemea bahari na maziwa yake yanajumuisha idadi kubwa ya maji safi duniani. Hakika uwezo wake ni trilioni nyingi za dola na unaashiria ukuwaji wa uchumi mkubwa pamoja na uhifadhi wa mazingira, lau utaelekezwa vyema. Mkakati wa Umoja wa Afrika Juu ya Bahari (AIMS 2050) unaotoa mpangilio kabambe wa kupatiliza kiukamilifu uwezo wa bahari na hivyo basi Kongamano la Uchumi Endelevu wa Buluu ni fursa adhimu kwa mataifa ya Afrika kufikia mkakati wake. (IPS, 21/11/2018)
Ni wazi kuwa kongamano hili liko chini ya usimamizi wa mataifa malafi ya ya kisekula ya kirasilimali hususan Uingereza na Marekani kwa ushirikiano wa marafiki na mashirika yanayoendeshwa kwa baraka zao duniani kote na hususan Afrika. Mataifa haya ya kimagharibi ya kikoloni hivi sasa yamo katika Vita vya Kiuchumi vya Karne ya 21 ambavyo vina watia hasara mabilioni ya fedha! Hivyo kila mmoja anatafuta njia ya kujiokoa na maaumivu ya kiuchumi na Afrika ni sehemu katika kufikia malengo yao maovu kwa sura ya kuijali na kuithamini Afrika! Lakusikitisha, Afrika kwa mara nyingine iko katikati ya mzozo wao wa kiuchumi na kwa kuwa Afrika na viongozi wake vibaraka wamedhibitiwa kati ya mabwana wakoloni wamagharibi; itatumika kama ngao ya kiuchumi na bwana mkoloni aliye mjanja zaidi! Miradi ya uchumi wa buluu itapatilizwa kwa ukamilifu na mataifa ya kimagharibi ya kisekula ili kuendeleza uporaji wa rasilimali za bara la Afrika ambalo tayari limo katika maumivu! Zaidi ya hayo, uchumi wa buluu utatishia jamii za wavuvi kuangamia, ufujaji wa ardhi miongoni mwa matatizo mengineyo yanayohusiana na mkondo wa bahari ya Afrika yatakayo sababishwa na kiu ya faida ya kimada kutoka kwa makampuni ya kisekula ya kikoloni! (VOA, 27/11/2018) Huku uongozi wake ukizawadiwa kwa dori muhimu wanayocheza kufikia mipango ya mabwana zao wakoloni kwa mfano Rais Uhuru Kenyatta alipokea zawadi maalum kutoka kwa Tume ya Umoja wa Afrika mnamo Jumanne, 27 Novemba 2018 kwa dori yake ya kuwa mwenyeji wa kongamano la kwanza la uchumi wa buluu! (The Star, 28/11/2018).
Uwezo na mwamko wa kweli wa Afrika utafikiwa chini ya ngao ya Khilafah. Khilafah iliyosimamishwa kwa njia ya Utume itadhamini ardhi ya Afrika kuwa huru kutoka kwa wakoloni wamagharibi kwa kuyakata mahusiano yao na mfumo wao batili wa kisekula wa kirasilimali ambao ndiyo chanzo cha Afrika kuwa katika utumwa wa kiakili na kuganda kijamii na kiuchumi! Zaidi ya hayo, Khilafah itaipa Afrika muongozo mbadala na muhimu wa mfumo wa Kiislamu ambao utaikomboa Afrika kutoka katika ufisadi wa utumwa wa kiakili hadi upeo wa juu wa utambulisho wa Kiislamu na ustawi. Ni Khilafah pekee itakayotoa urafiki wa kweli na kuwa kiigizo chema kwa Afrika ili kufikia utulivu wa kweli na maendeleo katika sekta zote za maisha.
Ali Nassoro Ali
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya