بسم الله الرحمن الرحيم
Swali na Jibu
(Imetafsiriwa)
[(Washington: Amerika inazuia kuipa Uturuki ndege za kivita aina ya F-35 stealth fighter … msemaji wa Pentagon alisema, “Huku ukisubiriwa uamuzi wa Uturuki wa kufutilia mbali utekelezaji wa (mkataba) S-400, upelekaji na amali zinazo husiana na kusimama kwa uwezo wa utendakazi wa F-35 wa Uturuki zimesimamishwa,” Akiongeza kuwa “mazungumzo yanaendelea pamoja na Uturuki juu ya kadhia hii muhimu” …) i24news.tv 1/4/2019]
Swali
Makubaliano ya Uturuki pamoja na Urusi juu ya mkataba wa S-400 yalianza tangu Septemba 2017. Wakati huo, Amerika haikupinga kwa nguvu makubaliano hayo, lakini msimamo wake sana ulikuwa ni kama wa kutoridhika. Ni kipi kilichoifanya kupinga kwa nguvu leo baada ya mwaka mmoja na nusu, na hata kukaribia kuitishia Uturuki endapo itapokea mkataba huu kutoka kwa Urusi? Mwenyezi Mungu akujazi kheri.
Jibu
Ili kutoa ufafanuzi wa jibu la swali hili, tutaregelea nukta hizi zifuatazo:
1- Uvamizi wa Urusi juu ya Syria ulianza mnamo 30/9/2015 baada ya makubaliano na Amerika [ulipuaji mabomu mara moja ukatanguliwa na mkutano kati ya Obama na Putin mnamo 29/9/2015 uliochukua dakika 90 … mgogoro wa Ukraine ulitawala sehemu ya kwanza ya mkutano huo huku marais hao wawili wakiangazia juu ya hali nchini syria katika sehemu iliyo bakia ya mkutano huo. Mara moja matokea ya mkutano huu yakajitokeza, na mnamo 30/9/2015 Baraza la Kifederali la Urusi kwa pamoja likaidhinisha matakwa ya Putin ya kutumia jeshi la anga la Urusi nchini Syria …” (Russia Today, 30/9/2015)]. Amerika ilijua kuwa Urusi huenda, endapo vita vitarefuka na “sokomoko” hii itaifazaisha, ikakimbilia vitendo ambavyo havijapigiwa hesabu na Amerika. Hivyo basi, ikataka kumfanya Erdogan wa Uturuki kama macho yake ili kudhibiti mwendo wa Urusi kwa mujibu wa mipaka ya Amerika. Hivyo iliiagiza Uturuki kuamiliana na Urusi katika muungano sawa na huo hadi Uturuki iweze kudhibiti kasi ya mashambulizi ya Urusi ili yasizidi mipaka inayo takikana, ambayo ni kutoumaliza upinzani uliokusanyika mjini Idlib kabla ya kumalizika kwa mradi wa Amerika wa suluhisho la mwisho la mgogoro wa Syria kwa sababu Amerika inataka kuubakisha upinzani ili kujadiliana pamoja na serikali katika suluhisho hilo la tamati.
2- Lakini tatizo lilikuwa kwamba Uturuki ilionekana kupingana waziwazi na Urusi na serikali hiyo, yaani, wao ni maadui. Kisha kadhia ikazidi kuwa mbaya wakati ndege ya Urusi ilipo tukunguliwa na marubani wa Kituruki mnamo 24/11/2015 na Erdogan akaendesha wimbi hilo! Na kukataa kuomba radhi. Kwa sababu Amerika ilivutiwa na maridhiano ya Uturuki pamoja na Urusi, rai yake ilikuwa kwamba Uturuki iombe msamaha na kuungana na Urusi, na hivyo hili likatokea. Baada ya Uturuki kusema kuwa ndege ya Urusi ilikiuka anga na hivyo haistahili msamaha, licha ya hayo iliomba msamaha mnamo 27/6/2016: [Dmitry Peskov, Katibu wa Habari wa Kremlin alisema: “Rais wa Uturuki ameonyesha masikitiko yake makubwa na rambirambi zake kwa familia ya rubani wa Urusi aliye uwawa na kuomba msamaha,” akiongeza: “Erdogan atafanya kila awezalo kurekebisha mahusiano ya jadi ya kirafiki kati ya Uturuki na Urusi,” (Al-Arabiya, 27/06/2016)]. Vile vile ilikuwa kama fidia [Meya wa eneo la Kremer nchini Uturuki ameitunuku familia ya rubani huyo aliye uwawa nyumba wakati wa mkutano pamoja na Balozi wa Urusi jijini Antalya, uliofanywa mapema mnamo Ijumaa … (Russia Today 07/01/2016)]. Baada ya Putin kuwa adui aliyewapiga mabomu watu, hususan katika Mlima Turkoman, mazungumzo naye yalifanyika katika mazingira ya kirafiki. Erdogan aliwasiliana kwa simu na Putin mnamo 29/6/2016 (kwa mujibu wa duru za afisi ya rais wa Uturuki, maongezi hayo ya simu yalifanyika katika mazingira ya kirafiki mno … (Al-Arabi Al Jadeed, 29/6/2016)). Na Uturuki na Urusi zikawa kama marafiki, na Erdogan anamwita Putin rafiki yake ingawa Urusi inaendelea kuwapiga mabomu Waislamu nchini Syria!
3- Hivyo basi, urafiki huu ukageuka kuwa usiri na Erdogan akaingia katika makubaliano na mikutano na Putin. Tulisema katika jibu la swali lililopita mnamo 5/2/2017: (Uturuki iliendelea kucheza dori hii katika kuihudumia Amerika kama msaidizi mtiifu hata baada ya tangazo la Rais mteule Trump mnamo 20/1/2017.
Kwa kuwa Trump ameonyesha ulaini kwa Urusi katika kampeni yake ya uchaguzi, Urusi ilidhani kuwa kupitia kufanya kongamano la Astana baada ya kutawazwa Trump kutaifanya Amerika kulikadiria kwa hali ya juu kongamano hilo na kulihudhuria kwa ujumbe wa kiwango cha juu. Urusi imekuwa ikimsubiri kwa hamu raisi Trump kuchukua hatamu kwa matarajio kuwa Waziri wa Kigeni wa Trump atahudhuria. Hii ndio sababu Urusi ilitarajia kongamano la Astana liwe ndio mwanzo wa majadiliano kwa ajili ya amani pana kati ya upinzani wa Syria na serikali ya Bashar kwa usaidizi wa Trump, kutokana na ubwege wake wa kisiasa wa kufikiria kuwa Trump inaiunga mkono Urusi! Hivyo basi, iliialika Washington kuhudhuria kongamano hilo, ikitaraji kuwa litahudhuriwa na ujumbe wa kiwango cha juu. Lilikuwa ni kofi usoni mwa Urusi pindi Washington ilipomtuma balozi wa Amerika jijini Astana badala yake kama mwangalizi! Hivyo basi, majadiliano ya Astana yalifanywa mnamo 23/1/2017 na kumalizika mnamo 24/01/2017 bila ya matokeo yoyote ya maana ya kusitisha vita; badala yake, ulipuaji mabomu uliongezeka katika Wadi Barada! Bila shaka, pasi na suluhisho lolote la kisiasa. Hivyo, mazungumzo ya Astana yalikuwa katika kiwango cha chini kuliko vile Urusi ilivyotaka, na yalimalizika kwa kukwama waziwazi kusitishwa vita.) Mwisho wa nukuu
4- Hali hii iliendelea hadi mwisho wa 2017. Hali ya Urusi ilizidi kuwa mbaya na Urusi ikaanza kutishia kuumaliza upinzani mjini Idlib. Hili lilikuwa na maslahi makubwa kwamba Amerika iliogopa Urusi kuwa kichwa maji na kutoka nje ya udhibiti wa Amerika, na kujitayarisha kwa shambulizi la mwisho juu ya Idlib kabla ya suluhisho la mwisho la Amerika kwa mgogoro wa Syria. Kufikia hapa, kulikuwa na udharura wa kuziunganisha imara Uturuki na Urusi kwa sura ya muungano ili kusitisha shambulizi kamili juu ya Idlib pasina ridhaa ya pande mbili hizo, na hivyo kupatikana mkataba wa S-400 pamoja na $2.5 bilioni, ambazo ni kivutio kwa Urusi, hususan wakati wa mgogoro wake wa kiuchumi. Erdogan alihalalisha hili kwa kusema kuwa zaidi ya nusu ya marubani wa Kituruki walikamatwa baada ya jaribio la mapinduzi lililo tibuka katikati mwa Julai 2016, na hivyo basi, Majeshi ya Anga ya Uturuki hayana marubani wa kutosha walio na uwezo wa kutumia ndege za kivita aina ya F-16 zinazo milikiwa na Uturuki, na hivyo inahitaji mkataba wa Urusi ulioendelea wa S-400 ili kufidia upungufu wa marubani wa ndege za kivita, ili Uturuki iwe salama katika upande wa ulinzi wa angani.
5- Urusi ilifurahi kuhusu mkataba huo, huku ikiangazia kupata mafanikio ya kimada. Mkataba wa S-400 pamoja na Uturuki uko katika kiwango cha $ 2.5 bilioni. Moscow inataka kujilipa hasara zake kutokana na vikwazo vya Ulaya na Amerika na kususia kwa wengi wao mafuta na gesi ya Urusi. Mkataba huu ndio fungamano jipya baina ya Urusi na Uturuki, na pindi Uturuki ilipoweka sharti la kukamilisha mkataba wa uzalishaji wa pamoja [Gazeti la Kituruki, Aksham, lilinukuu taarifa ya Waziri wa Kigeni wa Uturuki Mouloud Oglu mnamo 9/10/2017 kuwa nchi yake huenda ikatafuta makubaliano pamoja na nchi nyingine ili kuwa na mfumo wa ulinzi dhidi ya makombora endapo Urusi haitakubali uzalishaji wa pamoja wa mfumo wa makombora wa S-400. ((DW mnamo 9/10/2017)]. Urusi ilikataa uzalishaji wa pamoja, hivyo basi Uturuki ilijiondoa na kukubali mkataba huo ili kukomesha mashambulizi ya Urusi juu ya Idlib ambayo kwa hakika Urusi iliyaanzisha [AFP – kwa uchache raia 28 waliuwawa mnamo Ijumaa/Jumamosi usiku katika mashambulizi ya angani juu ya mji wa Armanaz katika mkoa wa Idlib, ambao ni miongoni mwa sehemu za kupunguza taharuki eneo la kaskazini magharibi mwa Syria, kwa mujibu wa Shirika la Uangalizi wa Haki za Kibinadamu la Syria maiti 12 zilitangazwa katika matokeo yaliyo tangulia yaliyo tangazwa na Shirika hilo mnamo Ijumaa jioni … mkoa wa Idlib ni eneo lililo tangazwa la kupunguza uhasama chini ya makubaliano ya Astana, lakini likashambuliwa na Urusi … Rami Abdul Rahman, mkurugenzi wa Shirika hilo alitaja: “Kutekelezwa kwa shambulizi la pili na ndege za kivita kulilenga mji wa Armanaz katika wilaya ya kaskazini magharibi mwa Idlib, ndege hizo zililipua mabomu maeneo ya shambulizi la kwanza, wakati wa mchakato wa kuwaokoa majeruhi na kuwabeba waliokwama katika vifusi vya majengo yaliyo vunjwa na ndege za kivita. Shirika hilo kwa upande mwengine lilisema kuwa raia 13 waliuwawa kutokana na mvua ya mabomu katika maeneo tofauti tofauti ya mkoa huo. Mkoa wa Idlib umekumbwa na mashambulizi ya Urusi ya wiki mbili na mashambulizi mengine makali dhidi ya Syria … (Gulf News mnamo 30/09/2017)] na hivyo mkataba huo ulifanywa bila ya uzalishaji wa pamoja! Erdogan alisema wakati alipokuwa anarudi kutoka katika ziara moja nchini Ukraine na Serbia, [“Hakutakuweko na uzalishaji wa pamoja wa awamu ya kwanza ya makombora aina ya S-400, ambayo yatanunuliwa na nchi yake”, lakini katika awamu ya pili, “tutachukua hatua juu ya uzalishaji wa pamoja …” na makombora ya S-400 ni makombora ya hali ya juu yaliyo na uwezo wa kuangamiza maeneo lengwa kutoka masafa ya mbali, na idadi ya maeneo lengwa yanayo weza kuandamwa mtawalia ni mia tatu, na uangamizaji wa ndege ni kati ya kilomita 3 na 240, na yaweza kuharibu aina zote za ndege za kivita na kuangusha makombora yenye mbawa … Mbali na uwezo wake wa kuangamiza, mfumo wa S-400 unahitaji dakika tano ili kuwa tayari kwa awamu ya A, jeshi la Urusi limepewa mfumo huu tangu 2007 … (Al Jazeera mnamo 29/12/2017)].
6- Kimaumbile, Amerika ilichukua msimamo tulivu juu ya makubaliano hayo, na ilikaribia kutoridhika, licha ya Uturuki kuwa mwanachama wa NATO. Na upangaji silaha katika muungano huo ni upangaji wa Magharibi na hauwiani na silaha za Urusi, hususan S-400, ambazo zaweza kupenya mfumo huo wa Kimagharibi katika muungano huo. Lakini Amerika na Muungano huo wameonyesha msimamo laini kwa mambo mawili: La kwanza ni kuwa Amerika yazihitaji Urusi na Uturuki kubakia kuwa na ukuruba ili kuizuia Urusi kutokana na kuishambulia Idlib kabla ya kukamilika kwa suluhisho la mwisho la Kiamerika la mgogoro wa Syria. Na la pili ni kuwa imeondoa uwezekano wa kutekelezwa mkataba huu maadamu Uturuki imo ndani ya NATO. Amerika hairuhusu Uturuki kuanzisha mfumo wa Urusi ndani ya mfumo wa Kimagharibi katika NATO. Kwa mazingatio haya mawili, Amerika ilitulia na kuwa karibu na msimamo wa baridi! [… Washington inaendelea kusisitiza kutoridhika kwake kwa ununuzi wa Uturuki wa makombora haya, na NATO inaamini kuwa Uturuki ina haki ya kujipatia silaha zinazoisaidia kudumisha usalama wake baada ya Ankara kutangaza kuwa mfumo mkuu hautaoanishwa katika mifumo ya NATO … (Asharq Al-Awsat 28 /12/2017)].
7- Kutokana na matokeo ya mkataba huu, mahusiano kati ya Urusi na Uturuki yamenoga waziwazi na Harakati ya Idlib kwa kiasi fulani imekuwa kimya. Urusi iliamini kuwa urafiki huu na mazungumzo ya pamoja na Uturuki yange harakisha suluhisho ambalo lingeitoa Urusi kutoka katika tatizo lake. Lakini hali hii ilibakia kwa karibu mwaka mmoja hadi mwishoni mwa 2018. Na hakuna lolote lililo badilika katika tatizo la Urusi. Amerika haikutilia maanani sana mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea hususan mjini Astana, lakini iliyahudhuria kama mwangalizi tu, kama vile Jordan, au kuwakilishwa na balozi wake nchini Kazakhstan! Urusi inatambua kuwa hakuna suluhisho endapo Amerika haitashiriki kwa umakinifu.
Inaonekana kana kwamba Urusi imeutambua mchezo wa Amerika na kuamua kushambulia Idlib. Kutokana na ubwege wake wa kutafakari, ilidhani kuwa Uturuki itasimama nayo, lakini ikashangazwa na kukataa kwake na kisha ikarudisha majeshi yake kambini! Tulifafanua hili katika jibu lililopita mnamo 22/9/2018: [Pindi mapinduzi ya kisilaha ya Syria yalipo zimwa mjini Idlib, Urusi ilitaka kuendelea na oparesheni zake za kijeshi; hivyo, ilipeleka majeshi, na kutekeleza mazoezi ya kijeshi eneo la Mediterrania, pamoja na manuari kubwa na vianzilishi mashambulizi angani vya kistratejia, na kufunga anga katika eneo la mashariki mwa Mediterrania kwa mara ya kwanza katika historia yake. Ilijipata katika utata mkubwa; Urusi iligundua vitu ambavyo haikuvitajarajia, ikiwemo:
A- Uturuki haikuafiki vita vipana juu ya Idlib. (Waziri wa Uturuki alikadiria kuwa “magaidi” wanapaswa kutambuliwa na kupigwa vita, na sio haki kuanzisha vita kamili juu ya Idlib na kuibwagia mabomu kila mahali) I’nab Baladi 14/8/2018. Upinzani wa Uturuki kwa vita hivyo ulionyeshwa waziwazi wakati wa kongamano la Tehran baina ya maraisi wa Urusi, Uturuki na Iran. Uturuki, kwa njia iliyoishangaza Urusi, iliangazia hofu yake ya vita hivyo dhidi ya Idlib na kufurika kwa wakimbizi ndani yake. Iliifedhehesha Urusi kupitia kuvichukulia vita hivyo kama ala ya kuondoa suluhisho la kisiasa nchini Syria. [Recep Tayyip Erdogan, Rais wa Uturuki alisema mnamo Ijumaa kuwa mashambulizi yanayo endelea juu ya mkoa wa Idlib, yakidhibitiwa na upinzani, yatapelekea kuanguka kwa mchakato wa kisiasa nchini Syria … (Al-Youm As-Sabi’ 7/9/2018)]. Na kisha kwa kupaa kwa sauti ya Amerika dhidi ya juhudi za Urusi kwa vita juu ya Idlib, Uturuki imevijaza vituo vya udhibiti mjini Idlib kwa silaha; vituo hivyo viliasisiwa ndani ya makubaliano hayo ili kupunguza joto la Urusi na Iran, [duru za uwanjani na mashahidi waliliambia shirika la habari la News Arabia, Jumapili, msafara wa kijeshi wa Uturuki ulielekea mjini Idlib, karibu na mpaka wa Uturuki, unaodhibitiwa na makundi ya upinzani ya Syria na makundi mengineo. Duru hizo zilisema kuwa msafara huo wa kijeshi wa Uturuki uliingia eneo la Syria kutoka kivuko cha Kafr Lusin na viungani mwake, kaskazini mwa Syria, ulijumuisha vifaru, vifaa vya kijeshi na ulikuwa umebeba silaha … (Sky News Arabia 09/09/2018)].
Hivyo basi, Uturuki imekuwa kizingiti kwa matarajio ya Urusi ya kuyamaliza makundi ya kijeshi mjini Idlib. Kutokana na hili, ilifanya mkutano wa pili baina ya Erdogan na Putin mnamo 16/9/2018 mjini Sochi, yaani, kwa siku tisa pekee baada ya mkutano wao jijini Tehran.
B- Hivyo basi, Amerika inaitaka Urusi kubakia imekwama ndani ya Syria, ikishindwa kujitoa hadi Amerika ikamilishe utekelezaji wa suluhisho la kisiasa kwa mujibu wa mipango yake.
Urusi sasa inaijua sera hii ya Amerika, na pengine imetambua athari ya kuhusishwa kwake na Amerika nchini Syria. Imekwama kikweli kweli ndani yake na haiwezi kutoka isipokuwa kwa ruhusa ya Amerika ambayo ina ala zote za ushawishi nchini Syria. Hii ndio sababu haikuweza kukamilisha shambulizi ililolitayarisha kwa ajili ya kumaliza mgogoro mjini Idlib kwa njia yake kwa sababu Uturuki ilipinga (ikisukumwa na Amerika) na Iran ikasalia kimya. Hivyo basi, mkutano wa Iran mnamo 7/9/2018 ulifeli kuidhinisha mpango wa Urusi ili kushambulia Idlib na kumaliza mgogoro huo kwa njia ya Urusi. Ni siku chache tu sasa tangu mkutano wa Erdogan na Putin na shambulizi hilo lilibadilishwa kwa kupitia kuasisiwa eneo la kusitisha vita!
Hili lilikuwa kupitia baraka za Amerika. Shirika la habari la Novosti lilimnukuu afisa wa Amerika mnamo 18/9/2018 akiliambia shirika hilo: [“Tunazikaribisha na kuzishajiisha Urusi na Uturuki kuchukua hatua za kivitendo kuzuia shambulizi la kijeshi kutoka katika serikali ya Assad na washirika wake juu ya mkoa wa Idlib …” Rais wa Urusi alisema wakati wa kutamatisha mkutano wake na mwenzake wa Uturuki katika eneo la Sochi: “Tumekubaliana kuasisi “eneo la kusitisha vita” lenye kina cha kilomita 15 na 20 kando kando ya laini ya mawasiliano, kuanzia Oktoba 15 mwaka huu”. Waziri wa Ulinzi wa Urusi, Sergei Shweigo, aliyaambia mashirika ya Urusi kuwa makubaliano haya yatazuia shambulizi hilo lililo tarajiwa kwa siku kadhaa juu ya ngome ya mwisho ya makundi nchini Syria. Katika kujibu swali juu ya je, makubaliano haya yanamaanisha kuwa hakutakuwepo na shambulizi la kijeshi juu ya Idlib, waziri huyo alijibu “ndio”, kwa mujibu wa mashirika ya Interfax na Tass. Kinyume chake, Erdogan alisema katika mkutano wa waandishi habari baada ya mkutano baina ya marais hao wawili: “Urusi itachukua hatua zinazo hitajika ili kuhakikisha kuwa hakuna shambulizi juu ya eneo la kusitisha vita mjini Idlib.” (France 24 / AFP 17/09/2018)]. Hivyo basi, Urusi ilisitisha ubwagaji mabomu wake mjini Idlib na kurudisha manuari zake, zilizokuwa zikifanya mazoezi ya kijeshi katika eneo la Meditterania. Yaani, hamu ya Uturuki na Amerika nyuma yake ya kusitisha shambulizi la Urusi juu ya Idlib kimsingi ilikuwa kwa manufaa ya Amerika na wala sio kuizuia serikali kutokana na kuifikia Idlib au kulinda raia, bali katika wakati ambao Amerika italazimisha suluhisho inalolitaka na kuilazimisha Urusi kwalo. Hapo, hawatajali damu ya Idlib, raia au wasiokuwa raia, kusitisha vita au kutositisha vita, na historia yao inazungumzia hili katika maeneo tofauti tofauti ya Syria, na uhalifu wao unajulika vyema …] Mwisho wa nukuu.
8- Na hivyo, Amerika ilijihakikishia upya mafanikio ya mpango wake na kwamba Uturuki inaweza kutibua shambulizi lolote la Urusi juu ya Idlib kabla ya kukamilisha suluhisho la Amerika kwa mgogoro wa Syria; litakalomfanya Amerika kupata kibaraka mpya ili kumrithi wa sasa na ambaye atakubaliwa na upinzani ulioko sasa na hili kimaumbile lahitaji kuubakisha upinzani mjini Idlib ili kujadiliana na serikali kuidhinisha utawala mpya kwa mujibu wa mpango wa Amerika, Kwa hayo, Amerika haina haja na ushirikiano wa Uturuki pamoja na Urusi. Urusi haina uwezo tena wa kupeleka watu na kushambulia Idlib, na hivyo, hii ndio sababu kwa nini Amerika imebakia kimya juu ya mkataba wa Uturuki na Urusi wa S-400. Hivyo, msimamo mkali wa Amerika na tabia za vitisho kwa Uturuki endapo itaidhinisha mkataba huo kama mfumo wa makombora wa Urusi ndani ya mfumo wa NATO wa Kimagharibi, na misimamo ya Amerika dhidi ya mkataba huu ikawa mikali. Wakati ambapo ilikuwa laini mwanzoni, ili badilika kwa sababu Amerika ilihitaji maridhiano kati ya Uturuki na Urusi wakati makubaliano ya mkataba huo yalipo fanyika mnamo 2017, lakini hitajio hili limemalizika mnamo 2019.
9- Miongoni mwa misimamo hii mikali iliyo tangazwa:
A- (Maafisa wa Amerika na NATO waliionya Ankara kuwa mfumo wa Urusi hauwezi kuoanishwa katika mfumo wa makombora wa muungano huo na kwamba ununuzi wa S-400 utadhoofisha uwezekano wa Uturuki kupata ndege za kivita za F-35 kutoka Amerika, “Lockheed Martin’, na huenda ikapelekea vikwazo kutoka upande wa Washington … Sky News Arabia 26/2/2019)
B- (Msemaji wa Wizara ya Ulinzi Charles Summers alitangaza mnamo Ijumaa 8/3/2019 kuwa Uturuki huenda ikakumbwa na matokea mabaya endapo itanunua mfumo wa usalama wa Urusi, na kuongeza kusema katika mkutano wa habari katika Pentagon: [“Endapo Uturuki itachukua makombora aina ya S400 kutakuweko na matokeo mabaya sana katika upande wa uhusiano wetu wa kijeshi pamoja nao na pamoja na mradi wa Patriots na F-35” (DW 8/3/2019.)]
C- (Afisa mmoja wa Wizara ya Kigeni ya Amerika alisema mnamo Jumanne kuwa Amerika imeiambia Uturuki kuwa endapo itaendelea na mkataba wa S-400, itahatarisha kushiriki kwake katika mradi wa F-35 na itahatarisha mkataba wowote wa silaha wa mustakbali pamoja na Washington. Katika kitendo cha kwanza cha Amerika kuzuia usafirishaji wa F-35 hadi Uturuki, msemaji mmoja wa Pentagon alisema mnamo Jumatatu kuwa Amerika imesitisha usafirishaji wa vipuri vinavyo husiana na ndege hizi hadi Ankara … Duru mbili ziliwaambia wanahabari wa Reuters kuwa maafisa wa Amerika waliwaambia wenzao wa Uturuki katika siku chache zilizopita kuwa hawatapokea shehena nyenginezo za vipuri vinavyo husiana na F-35 ambavyo kuwasili kwake ni muhimu na ambavyo vinahitajika ili kujitayarisha kwa kuwasili kwa ndege aina ya Stealth iliyo tengezwa na Lockheed Martin. Msemaji mmoja wa Pentagon, Luteni Kanali Mike Andrews, alisema katika taarifa: “Uamuzi wa wazi unaosubiri wa Uturuki wa kuachana na upokezi wa S-400, mapokezi na amali zinazo husiana na kusimama kwa uwezo wa Uturuki wa uendeshaji F-35 zimehairishwa,” Al-Arabiya Net 2/4/2019)
D- (Waziri Msaidizi wa Kigeni wa Amerika Robert Paladino alisema kuwa Washington ilikuwa na wasiwasi sana kuhusu mkataba huo, na akasisitiza kuwa kuna uwezekano wa kufikiria upya kuhusu uzalishaji wa pamoja wa F-35 kwa ushirikiano na Uturuki pamoja na mikataba yoyote ya silaha ya siku za mbeleni. Pia alitaja kuwa taasisi za Dola hiyo na taasisi za kibinafsi na watu binafsi watakao husika katika ununuzi wa S400 huenda wakakabiliwa na uwezekano wa vikwazo chini ya kifungu cha sheria cha CAATSA. Kurdstreet mnamo 11/3/2019).
10- Matarajio ya kuidhinisha mkataba huo yamo ndani ya mipaka ya uwezekano ifuatayo:
A- Ikiwa Uturuki itaamua kutoendelea na mkataba huu kwa sababu ya mafungamano yake ya karibu ya kisiasa na kiuchumi na Amerika, na kuufidia kwa ununuzi wa silaha za kimikakati, kama vile helikopta, kutoka Urusi badala ya mkataba wa S-400. Silaha kama hizo za kimikakati hazitapokea majibu makali kutoka NATO au Amerika. Hivyo Uturuki itapokea zana za kujihami kwa ajili ya usalama wake. Kaimu Waziri wa Ulinzi wa Amerika Patrick Shanahan aliwaambia maripota katika Pentagon mnamo Jumanne: [“Nataraji tutatatua tatizo hilo ili wawe na haki ya kuwa na zana za kujihami ikikusudiwa Patriots na F-35.” (Al Arabiya Net mnamo 2/4/2019)].
B- Ombi la Waamerika ni “Suluhisho la Kigiriki,” yaani, kuyaweka ghalani makombora ya Urusi na kuyawacha yashike kutu kwa badali ya ununuzi wa silaha za kivita aina ya Patriot kutoka Amerika, zinazo gharimu bilioni $ 3.5.
Uhalisia wa hadithi ya makombora ya Urusi nchini Ugiriki ni kuwa Moscow kiasili iliyauza kwa Cyprus, ambayo iliyalipia, lakini upinzani mkali wa Ankara uliilazimisha Athens kubaki nayo ili kuepusha mgogoro mbaya na Uturuki. Inayo maanisha kuwa Waturuki watalipa kiwango hiki ikiongezewa na dolari bilioni mbili na nusu kwa ajili ya makombora ya Urusi! Kwa yakini hili linamfaa Donald Trump, lakini gharama yake kubwa itaiweka serikali ya Uturuki usoni mwa shambulizi la upinzani wa Uturuki, ambao utakuwa na haki ya kuituhumu serikali kufuja pesa za watu wa Uturuki kutokana na makosa ya sera ya kigeni ya serikali hiyo.
C- Mfumo huu huenda ukatumwa hadi nchi ya tatu kama vile India ili kuepuka hasira za Urusi, ambayo pia iko sambamba na mkakati wa Amerika wa kuizingira China.
Inaonekana kana kwamba uwezekano mkubwa zaidi ni wa kwanza (nukta A), kwa kuwa imegunduliwa kuwa taarifa za sasa kutoka pande zote za kesi hiyo zinatoa njia kwa jambo hilo, kwa mfano taarifa iliyo tajwa juu ya Shanahan ya mnamo 2/4/2019, pamoja na taarifa ya Naibu Waziri Mkuu wa Urusi juu ya uboreshaji wa kijeshi: [“Hakuna hofu kuwa Uturuki huenda ikatupilia mbali mkataba wake wa S-400. (Al Jazeera mnamo 3/4/2019)]. Na pia yale yaliyo ripotiwa na Al Jazeera siku hiyo hiyo 3/4/2019: [Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi ya Duma Urusi, Vladimir Shamanov, hakukataa uwezekano wa Uturuki kuachana na mkataba wa mfumo wa S-400 pamoja na Urusi … (Al Jazeera Net mnamo 3/4/2019)], na pia yale yalio nukuliwa na Al Arabiya Al Hadath Al Youm 4/4/2019: (Uturuki inatoa wito wa kuweko na kikundi kitakacho fanya kazi na Washington ili kujadili hatari za mfumo wa makombora wa Urusi wa S400). Yote haya yanaufanya uwezekano wa kwanza kuwa ndio mkubwa zaidi, wa kutoidhinisha mkataba wa makombora na Urusi, yaani, kufutilia mbali mkataba huo.
28 Rajab 1440 H
4/4/2019 M