بسم الله الرحمن الرحيم
Jibu la Swali
Kwa Mohammad Ibrahim
(Imetafsiriwa)
Swali:
Assalamu Alaykum Wa Rahmatullah Wa Barakatuhu,
Ndugu yetu mpendwa na mwanachuoni mheshimiwa, nataraji utalijibu swali hili lifuatalo:
Msemo kuwa hali asili (asl) kuhusiana na miamala ni ruhusa (mubah) na ibaha yahitaji kuzingatiwa na kuitegemeza na madhehebu manne yahitaji uhakika na utafiti…
Msingi huu (asl) umekuwa maarufu na kusemwa na wanachuoni wa sasa, lakini hatukuiona asl hii katika vitabu vya wanachuoni wa zamani. Ibn Najim al-Hanafi, ambaye ni mwana usuli wa Kihanafi (na inasemekana kuwa hukmu (qa’ida) hii ilitumiwa sana na wao) ametaja hukmu mbili pekee:
Asl katika vitu ni mubah maadamu hakuna andiko la kuharamisha.
Na asl katika kutangamana kijinsia ni haramu.
Swali ni ikiwa Mtunzi wa Shariah ameyahifadhi matangamano ya kijinsia kupitia kuweka hukmu yake asili kuwa haramu ili kuhifadhi kizazi! Je, hilo halionekani kuwa sambamba pia katika upande wa miamala ya mali na pesa, au angaa kusema kuwa asl kuhusiana nayo sio mubah…
Hivyo basi, ni muhimu kuzichunguza kadhia na miamala ndani ya vidhibiti vyake jumla ili kutoa uamuzi, kwa sababu kama ambavyo Mtunzi wa Shariah amekihifadhi kizazi, Yeye pia amezihifadhi mali…
Huenda ikawa nimekosea, hususan kwa kuwa sikuyafanyia utafiti yale yote ambayo wanachuoni na wana usuli wamesema juu ya kadhia hii…
Kwa sababu hatari ni kuwa tunaruhusu kila aina ya miamala ya kileo kwa mujibu wa msingi (qa’ida) “asili katika miamala ni mubah”, pasi na kuchunguza uhalisia wa kadhia hii na umbile la dalili inayo husiana nayo.
Hivyo je hukmu hii ina usahihi kiasi gani? Na je, wanachuoni wa fiqh (Fuqahaa) wameizungumzia?
Limetumwa na Abu Zakariyah kutoka Lebanon
Jibu:
Wa Alaikum Assalam Wa Rahmatullah Wa Baraktuhu,
Ndugu, kuna misingi (qa’ida) ambayo imetabanniwa na baadhi ya Mujtahidina ambayo ni hafifu (Marjouh) kwa mujibu wetu sisi, miongoni mwayo ni qa’ida uliyoitaja: “Asli katika miamala ni mubah”, ama yale tuliotabanni kutokana na uzito wa dalili zake ni: “Asli katika vitu ni mubah maadamu hakuna andiko lenye kuharamisha” na “asli katika vitendo ni kufungwa na hukmu ya Mwenyezi Mungu”. Na tumezungumzia qai’da kadhaa nyInginezo, na kuonyesha udhaifu wake, haya hapa ni maelezo:
Kwanza: imetajwa katika kitabu Shakhsiya ya Kiislamu Juzuu ya 3, chini ya mlango “Hakuna Hukmu Kabla ya Kuja kwa Wahyi”:
[Basi haIpaswi kusemwa kuwa asili ya vitu na vitendo ni uharamu (tahrim) kwa hoja kuwa ni utumizi (tasarruf) huru ndani ya mamlaka ya Mwenyezi Mungu Mtukufu pasi na ruhusa yake hivyo ni haramu, kwa kuvua qiyas juu ya viumbe, kwa sababu maana dhahiri ya ayah ni kuwa Mwenyezi Mungu haadhibu hadi amtumilize Mtume, hivyo Yeye hahisabu mpaka afafanue hukm. Fauka ya hayo viumbe vinaweza kudhuriwa, lakini Mwenyezi Mungu Mtukufu yuko juu ya uwezo wa kunufaishwa au kudhuriwa.
Vilevile haipaswi kusemwa kuwa asili ya vitendo na vitu ni mubah, kwa hoja kuwa ni utumizi ulio huru kutokana na alama yoyote ya ufisadi au madhara kwa mmiliki wake na hivyo ni mubah. Hili halipaswi kusemwa kwa sababu maana fiche (mafhoum) ya ayah hiyo ni kuwa mwanadamu amewajibishwa kwa yale anayo kuja nayo mtume; huadhibiwa kwa kuhalifu hili; hivyo asili inakuwa ni kumfuata [ittibā’] mtume na kufungika na hukmu za risala yake; asili sio mubah, ambayo ni kukosekana kujifunga huku. Kwani ujumla wa aya za hukmu waashiria juu yake wajibu wa maregeleo kwa sheria na wajibu wa kufungwa na hukmu zake; Mwenyezi Mungu Mtukufu asema,
(وَمَا اخْتَلَفْتُمْ فِيهِ مِن شَيْءٍ فَحُكْمُهُ إِلَى اللَّه)
“Na mkikhitalifiana katika jambo lolote, basi hukumu yake iko kwa Mwenyezi Mungu.” [al-Shūra: 10];
na
(فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللّهِ وَالرَّسُولِ)
“Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume” [al-Nisā’: 59];
na
(وَنَزَّلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ تِبْيَاناً لِّكُلِّ شَيْء)
“Na tumekuteremshia Kitabu hiki kinacho bainisha kila kitu” [al-Nahl: 89];
na Mtume (saw) amesema katika riwaya iliyo simuliwa na al-Daraqutni, “Jambo lolote ambalo si katika amri yetu, basi hukataliwa”, hii yaashiria kuwa asili ni kufuata sheria na kufungika nayo, na utumizi zaidi ambao uko huru kutokana na alama yoyote ya ufisadi au kuleta madhara kwa mmiliki wake sio dalili ya kuruhusiwa (ibaha)…
Vilevile haipaswi kusemwa kuwa asili ya vitu ni kusitisha [tawaqquf] na kukosekana kwa hukmu. Kwani kusitisha yamaanisha kutupilia mbali kitendo au hukmu na hili haliruhusiwi, kwa sababu (hukmu) iliyo thibitishwa katika Qur’an na Hadith kwa ukosefu wa elimu ni kuulizia kuhusu hukmu hiyo na sio kusitisha na kukosekana kwa hukmu. Mwenyezi Mungu Mtukufu asema,
(فَاسْأَلُواْ أَهْلَ الذِّكْرِ إِن كُنتُمْ لاَ تَعْلَمُونَ)
“Basi waulizeni wenye ilimu ikiwa nyinyi hamjui.” [al-Anbiyā’: 7];
na kauli ya Mtume (saw) katika Hadith ya tayammum, iliyo simuliwa na Abu Dawud kutoka kwa Jabir, “Basi, hawaulizi ikiwa hawajui, kwa tiba ya ujinga pekee ni kuuliza”; hii yaashiria kuwa asili sio kusitisha na kukosekana kwa hukmu.
Hivyo basi ni baada ya kuwasili Mtume ndio hukmu inakuwa sheria na hakuna hukmu kabla ya kuja sheria, hivyo hukmu hutegemea juu ya kuja kwa sheria, yaani, juu ya kuwepo dalili ya sheria kwa kila kadhia. Hivyo basi hakuna hukmu inayo weza kutolewa isipokuwa kwa msingi wa dalili, kama ambavyo hakuna hukmu yaweza kutolewa ila baada ya kuja sheria. Kwa hivyo basi asili, ni kutafuta hukmu ndani ya sheria, yaani, asili ni kutafuta dalili ya kisheria kwa hukmu ya sheria kutoka katika sheria …
Kutokana na haya, qa’ida ya kisheria, “Hukmu asili ya vitendo vya mwanadamu vimefungika na hukmu ya Mwenyezi Mungu” imethibitika. Hivyo si ruhusa kwa Muislamu kutenda kitendo isipokuwa baada ya kujua hukmu ya Mwenyezi Mungu kuhusiana na kitendo hicho, kutoka katika hotuba ya Mtunzi wa Sheria. Ruhusa (ibaha) ni hukmu miongoni mwa hukmu za shariah, ambayo kimsingi yahitaji dalili…
Hii ni kuhusiana na vitendo. Ama kuhusu vitu, ambavyo vinahusiana na vitendo, asili yake ni mubah maadamu hakuna andiko linalo haramisha. Hivyo basi hukmu asili ya kitu ni mubah; hakiharamishwi ila ikiwa kuna dalili ya kisheria ya uharamu wake. Hii ni kwa sababu nususi za kisheria zimetangaza kuwa vitu vyote ni mubah, na nususi hizi zimekuja kwa ujumla, zikijumuisha vitu vyote; Mwenyezi Mungu Mtukufu asema,
(أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّهَ سَخَّرَ لَكُم مَّا فِي الْأَرْضِ)
“Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu amevidhalilisha kwenu viliomo katika ardhi” [al-Hajj: 65];
maana ya kuvidhalilisha [taskhīr] Mwenyezi Mungu kwa mwanadamu vitu vyote duniani ni ibaha kwa vyote vilivyomo duniani. Yeye (swt) asema,
(يَا أَيُّهَا النَّاسُ كُلُواْ مِمَّا فِي الأَرْضِ حَلاَلاً طَيِّباً)
“Enyi watu! Kuleni vilivyomo katika ardhi, halali na vizuri” [al-Baqarah: 168];
na Yeye asema,
(يَا بَنِي آدَمَ خُذُواْ زِينَتَكُمْ عِندَ كُلِّ مَسْجِدٍ وكُلُواْ وَاشْرَبُواْ)
“Enyi wanadamu! Chukueni pambo lenu kwenye kila pahala wakati wa ibada, na kuleni, na kunyweni…” [al-A’rāf: 31]; na Yeye asema,
(هُوَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ ذَلُولاً فَامْشُوا فِي مَنَاكِبِهَا وَكُلُوا مِن رِّزْقِهِ)
“Yeye ndiye aliye idhalilisha ardhi kwa faida yenu, basi tembeeni katika pande zake, na kuleni katika riziki zake.” [al-Mulk: 15].
Hivyo basi ayah zote zinazo ruhusu vitu zimekuja kwa muundo wa jumla, ujumla wake unaashiria ibaha kwa vitu vyote. Hivyo basi ikiwa kitu kimeharamishwa ni lazima kuwepo na andiko la kubainisha ujumla huu, ikiashiria kuwa kitu hiki kiko nje ya ibaha ya vitu vyote. Kufikia hapa, asili ya vitu ni ibaha. Kutokana na haya tunapata katika wahyi, pindi vitu vinapo haramishwa, nususi maalumu kuhusiana na vitu vilivyobainishwa kuwa havimo kwa mujibu wa nususi jumla; hivyo Mwenyezi Mungu Mtukufu asema:
(حُرِّمَتْ عَلَيْكُمُ الْمَيْتَةُ وَالْدَّمُ وَلَحْمُ الْخِنْزِيرِ)
“Mmeharamishiwa nyamafu, na damu, na nyama ya nguruwe..” [al-Ma’idah: 3];
na yeye (saw) amesema, “Pombe (Khamr) imeharamishwa kwa nafsi yake”, imetajwa katika al- al-Mabsūt kutoka kwa Ibn ‘Abbas; hivyo kile ambacho wahyi unakiharamisha ni kubainishwa kutoka kwa nususi jumla na ni kinyume na asili, ambayo ni ibaha…]
Kutokana na haya, inadhihirika kuwa qa’ida hizo, ima zile ulizozitaja “asili ya miamala ni ibaha”, au nyinginezo kama tulivyo taja juu ni qa’ida hafifu (marjouh) kwa mujibu wetu sisi, na rai sahihi ni ile inayo husiana na vitendo na vitu kama tulivyo taja, yaani, “asili ya vitendo ni kushikamana na hukmu ya sheria” na “asili ya vitu ni mubah maadamu hakuna andiko la kuharamisha”
Nataraji kuwa jibu hili limetosheleza, na Mwenyezi Mungu (swt) ni Mjuzi zaidi na mwingi wa hekima.
Ndugu yenu,
Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
29 Jumada Al-Akhirah 1441 H
23/02/2020 M