Mpango Mpya wa Marekani wa Kuzidisha Kuipora Afrika

Mnamo Jumamosi 20 Oktoba 2018, Mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AU), Moussa Faki Mahamat, alimchagua aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga kuwa Balozi Mkuu wa Maendeleo ya Miundo Mbinu Barani Afrika (africa.cgtn.com, 20/10/2018). Raila amekuwa wa kwanza kupewa cheo hicho ambacho kimebuniwa hivi majuzi. Kuchaguliwa kwake kama balozi wa AU kumekuja siku mbili tu baada ya Raila na Uhuru wote wawili kutambuliwa katika sherehe za kila mwaka za Mwezi wa Watu Weusi na kupewa Tuzo la Amani Afrika 2018 kwa sababu ya mapatano yao ya Machi 9. Sherehe hizo zilifanyika katika Bunge la Uingereza katika Kasri la Westminister mnamo 18 Oktoba 2018 (The Star, 18/10/2018).

Ili kufahamu muktadha wa mpango mpya wa Marekani tunabainisha yafuatayo:

Kwanza: Shirika la Umoja wa Afrika (OAU) lilianzishwa mnamo 25 Mei 1963 na hatimaye kuvunjiliwa mbali na badala yake kuwekwa Muungano wa Afrika (AU) huku Thabo Mbeki (Afrika Kusini) akiwa Mwenyekiti wake wa kwanza kuanzia 9 Julai 2002 hadi 10 Julai 2003. Tokea mwanzo OAU na hivi sasa AU ni chombo tu cha mabwana Wamagharibi wakoloni hususani Uingereza na Marekani ambao wanawatumia viongozi watumwa wa AU kuendeleza ukoloni mamboleo barani Afrika na katika mataifa yao binafsi ndani ya Afrika. Hivi sasa Baraza la AU liko chini ya mwenyekiti wake Rais wa Rwanda Paul Kagame – 28 Januari 2018 na mwenyekiti wa Tume ya AU Balozi wa Chad Moussa Faki Mahamat – 14 Machi 2017; wote wanatoka katika mrengo wa Marekani ikimaanisha kuwa Marekani ndiyo yenye udhibiti kamilifu wa uongozi wa juu wa AU kwa sasa.

Pili: Vipaombele vya AU hivi sasa chini ya Kagame na Moussa ni amani na usalama vikitokana na sera ya kiujanja ya Marekani barani Afrika. Wiki ya kwanza alipoingia afisini Mousa Faki alizuru Somalia, ambapo jeshi la AU linapigana na Al-Shabaab. Wiki ya pili alizuru Sudani Kusini na mnamo Aprili 2017 akatilia shime kutiwa saini kwa mpango wa Muungano wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika (UN-AU) ulioazimia kuboresha ushirikiano juu ya Amani na Usalama (ICG, 17/01/2018) Kagame alipochukua uongozi wa AU, aliyekuwa Waziri wa Kigeni Rex Tillerson wa Marekani aliuzuru uongozi wa AU mnamo 8 Machi 2018 na kufanya mkutano na Moussa Faki juu ya usalama na kupambana na ugaidi, biashara na maendeleo, ufisadi na mizozo ndani ya Afrika (Capital News, 08/03/2018)

Tatu: Wakenya mnamo 9 Machi 2018 walipata mshangao pindi walipowatizama Kenyatta na Odinga wakipeana mikono nje ya Jumba la Harambee jijini Nairobi. Hii ni baada ya mkutano wao ambapo waliamua kufanya kazi pamoja na kuunganisha nchi baada ya uchaguzi uliochukua muda mrefu! Hili halikuingia akilini kamwe; lakini lililoingia akilini ni muda uliotengwa kwa ajili ya uamuzi wao, ambao ulichukua takriban saa 5 kabla ya ziara ya Waziri wa Kigeni wa Marekani Rex Tillerson jijini Nairobi. Uamuzi wao na ziara ya balozi mkuu wa kigeni wa Marekani inathibitisha kwamba kwa hakika kulikuwepo na ulegezaji msimamo baina ya Marekani na Uingereza kupitia watawala wao vibaraka.  Kaimu Waziri Msaidizi wa masuala ya Afrika Donald Yamamoto aliungama kuwa Marekani ilijadili kwa kina na Odinga juu ya haja ya kuwepo maridhiano kwa matayarisho ya ziara ya Waziri wa Kigeni wa Marekani Rex Tillerson. Akizungumza na Jarida la Wallstreet, alithibitisha majadiliano hayo, akisema kuwa “tulimwambia … kwamba uko na fursa kubwa sana ya kihistoria kusukuma kikweli mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi”. [Pulse, 10/03/2018]

Nne: Ziara ya Raila ya 24 Mei 2017 kwenda Sudan Kusini kama mjumbe maalumu kuwakilisha Muungano wa Afrika (AU) na kufanya mkutano wa saa 7 na Raisi wa Sudan Kusini Salva Kiir na baadaye kusafiri hadi Afrika Kusini kukutana na aliyekuwa makamu wa raisi wa Sudan Kusini Riek Machar kujadili uwezekano wa suluhisho la mzozo nchini Sudan Kusini [Daily Nation, 27/05/2018]. Hatimaye mahasimu hao wawili walitia saini mkataba wa serikali ya muungano mnamo Jumapili 5 Agosti 2018 jijini Khartoum, uliongozwa na Raisi Omar Bashir (Sudan) pamoja na Raisi Uhuru Kenyatta [The Star, 05/08/2018].

Tano: Uchumi wa China kiulimwengu uliupita ule wa Marekani mnamo 2016. China ndiyo mshirika wa kibiashara Nambari 1 duniani akishirikiana na nchi 138 kati ya mataifa 200 duniani. Mnamo 2014, takwimu rasmi zinaonyesha kuwa China inakiwango kikubwa cha dola bilioni 220 za mikataba ya kibiashara barani Afrika. Hilo likiifanya China kuwa mshirika mkubwa wa kibishara kwa Afrika ambamo imewekeza mabilioni ya fedha katika miradi ya maendeleo ya miundo mbinu. Mnamo 2013, Rais wa China Xi Jinping alizindua mradi wa Mkakati wa Mkanda Mmoja, Barabara Moja ambao umejikita katika kumwaga mamia ya mabilioni ya dola katika ujenzi wa bandari, reli na miradi mingine ndani ya Asia, Ulaya na Afrika.

Hivyo basi, kuchaguliwa Raila ni dhihirisho kuwa uongozi wa juu wa AU unaongozwa na Marekani nyuma ya pazia umebuni afisi hiyo mpya ili kuweza kumjumuisha na kumzawadia rafiki wa bwana wao ili aweze kuendeleza ajenda fiche ya bwana wao ndani ya bara. Ajenda yenyewe ni kuidhibiti hatua za China katika mbio zake za miundo mbinu barani Afrika kama ilivyodhihirishwa na kauli ya Rex Tillerson alipozuru Afrika “Uwekezaji wa China una uwezo wa kutatua pengo la miundo mbinu Afrika, lakini mtizamo wake umepelekea kukuwa kwa madeni na kuwepo kwa ajira chache lau zipo ndani ya nchi nyingi. Unapojumuishwa na mihemko ya kisiasa na kifedha, una hatarisha rasilimali asili na uchumi wa muda mrefu na umakini wa kisiasa wa Afrika”. (CNN, 10/03/2018)

Kimsingi, Marekani inataka kumtumia Raila kama “mjumbe wa bara” ambaye jukumu lake linajumuisha kutafuta uungwaji mkono wa kisiasa kutoka kwa Mataifa Wanachama wa AU na Jamii za Kiuchumi za Eneo (RECs) na kusaidia katika umilikaji wa juu wa kila mshikadau barani humo. Pia ataisaidia Tume na miradi ya NEPAD ili kuishajiisha kupata dhamana kutoka kwa washirika wa maendeleo. Kwa maana nyingine anatakiwa kucheza dori ya ushawishi ya kuweza kuiharibia China katika udhamini wake kifedha wa miundo mbinu ya Afrika ili kwamba miradi ya  miundo mbinu ikipitishwa na AU idhaminiwe na taasisi za fedha za mrengo wa Marekani. Raila pia atawahusisha “washirika katika maendeleo na wakopeshaji wakijumuisha Benki ya Dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa na wadhamini wakimikataba ili kuigharamia miradi ya bara (The Star, 25/10/2018) Kwani mnamo 2016 China ilitumia dola bilioni 6.413 dhidi ya taasisi za zinazoegemea Marekani Benki ya Dunia – dola bilioni 3.642 na Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) – dola milioni 413 (ICA, 2016)

Kwa kumalizia, Marekani inawatumia viongozi wake vibaraka Afrika ili kuzidisha uporaji wa rasilimali za Afrika kwa kuziteka serikali kupitia miradi ya mabilioni ya madeni kwa jina eti ni fedha za maendeleo ya miundo mbinu. Marekani haijali kuhusu masuala ya Afrika bali macho yake yamekita tu katika maslahi yake, ambayo hivi sasa inahisi kupata ushindani baadhi kutokana na mipango ya China ya kiuchumi kwa sura ya “miradi ya maendeleo ya miundo mbinu.”

Mwamko wa Afrika upo katika kujiunga kwake na mradi wa dhahabu wa Khilafah. Khilafah iliyosimamishwa kwa njia ya Mtume (saw) itahakikisha kuwa Afrika inafikia uwezo wake wa kweli kwa kuwafurusha Wamagharibi wakoloni kutoka ardhini mwake. Licha ya hilo, utekelezwaji wa Nidhamu ya Kiuchumi ya Uislamu chini ya Dola ya Kiislamu ya Khilafah itadhamini amani na utulivu kwa kuzitumia vyema rasilimali za Afrika kwa ukuwaji na maendeleo ya kweli ya Afrika. Hivyo basi, Afrika itaibuka kama moja ya vitovu vya uchumi bora ulimwenguni chini ya usimamizi wa Khalifah bora anayehukumu kwa Qur’an na Sunnah.

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya