Habari:
Kenya inalipa shilingi bilioni 658.2 dhidi ya shilingi trilioni 1.4 katika mapato tarajiwa ya ushuru hii ikimaanisha kuwa nusu ya pesa zote zilizo kusanywa na Halmashauri ya Ukusanyaji Ushuru ya Kenya (KRA) zinatumika katika ulipaji deni. Ikiwa mtu ataongezea matumizi katika gharama za ziada kama malipo ya mishahara na mafao ambazo hukatwa kabla ya kufika katika akaunti zetu za matumizi, mwaka huu Wakenya watalipa shilingi bilioni 735.6, huku zikisalia shilingi bilioni 700 pekee kama mgao baina kaunti na serikali ya kitaifa kwa ajili ya maendeleo. “Matumizi mengi ya serikali ni ya ziada ukiyaondoa yote hayo utapata kiwango kichache kinacho salia kwa matumizi ya mambo mengine,” Dkt. Kamau Thugge alisema haya wakati wa uwasilishaji wa kielelezo cha bajeti cha mwaka 2018. Ukijumuisha mikopo ya siri, deni la Kenya litafikia shilingi trilioni 5.4 mwaka huu kutoka kiwango cha chini cha shilingi trilioni 2.5 mnamo Disemba 2014 ambacho kimekuwa kwa asilimia 116 kwa miaka minne. [Chanzo: Gazeti la The Standard]
Maoni:
Janga lililoko sasa la deni la Kenya limetokana na ufisadi na ubinafsi katika uongozi wake na ulafi wake wa hali ya juu wa kuchukua mikopo kwa usuhuba na wakopeshaji waovu na matapeli wa humu nchini na wa kimataifa wanaokopesha fedha kwa msingi wa riba. Usuhuba wao huu umeundwa kutokana na mtazamo wa nidhamu ya kiuchumi ya kirasilimali ambapo taasisi za kifedha zenye msingi wa riba ndio uti wa mgongo wa uchumi wa dola yoyote ya kisekula ya kirasilimali ikiwemo Kenya. Ili nchi ijikadirie kukua kiuchumi huzingatia utajiri wake jumla (GDP) dhidi ya mrundiko wake wa deni, hivyo ikiwa kiwango cha utajiri wake jumla kitakuwa kikubwa kuliko mrundiko wa deni kwa mfano 4:1 itamaanisha kuwa uchumi uko imara na unaweza kufadhili madeni yake! Hivyo basi, nidhamu ya kiuchumi ya kirasilimali haitilii maanani kuhusu ugavi wa mali bali inatilia maanani uzalishaji wa mali pekee.
Utajiri jumla wa nchi (GDP) ukiwa juu humaanisha mabwenyenye wachache hutia mifukoni mamilioni au mabilioni dhidi ya idadi kubwa ya wananchi walala hoi. Shabaha za ukusanyaji mapato hazifikiwi kutokana na serikali kuondolea ushuru bidhaa na huduma fulani na mabwenyenye wakuu kukwepa ulipaji ushuru. Hii imepelekea kufichuka kwa umbile hadaifu la miito inayopigiwa debe hadharani ya ‘kulipa ushuru, ni kujitegemea’ na ‘wawekezaji ni lazima wapewe kipaumbele’. Miito kama hii imekusanya uhalisia aina mbili unaogongana; wa kwanza ni ule wa ufukara wa wananchi ambao daima hunyonywa na watoza ushuru na upande mwengine ni matajiri wakuu wanaohudumu kwa ukwepaji ushuru au kwa ushirikiano na maafisa wa utozaji ushuru. Mbinu za uwekezaji zinadhibitiwa na wakoloni kiasi ya kuwa sekta muhimu zilizo na uwezo wa kuleta mageuzi ya kimsingi katika uchumi, kwa mfano sekta ya madini, serikali imefanywa kuwa mtazamaji pekee ndani ya nchi yake ilhali wanaoitwa wawekezaji wakitumia makampuni yao makubwa ya kimataifa kuvinjari na kuendesha biashara zenye faida kubwa za madini humu nchini, kieneo na kiulimwengu na badali yake hutoa malipo duni kwa serikali kwa jina la jukumu la huduma kwa jamii na ada ya uzalishaji huku wakiishia kutia mabilioni ya faida mifukoni! Serikali inabakia pasi na khiari nyengine isipokuwa kuchukua mikopo iliyo na viwango vya riba vya hali ya juu ili kufadhili ile inayoitwa miradi ya maendeleo ambayo kiuhalisia ni mipango ya kukamua na kupora mali ya umma kwa ajili ya kujinufaisha kibinafsi na ili kuingia au kubakia mamlakani.
Suluhisho liko katika kutabikisha mfumo wa Kiislamu kama badali ya mfumo batili wa kisekula wa kirasilimali. Mfumo wa Kiislamu uliteremshwa kwa wahyi na Allah (swt); Aliye sema:
وَأَحَلَّ اللَّهُ الْبَيْعَ وَحَرَّمَ الرِّبَا
Na Allah amehalalisha biashara na akaharamisha riba
[Al-Baqara: 275]
Nchi yoyote au dola yoyote inayo endesha uchumi wake kwa msingi wa mikopo ya riba inayo tolewa na majambazi wa kirasilimali ambao wamejitolea kuhakikisha wanawafunga minyororo na kuwafanya watumwa viongozi na raia wa nchi hizo kwa majanga ya madeni yasiyo malizika, nchi kama hiyo itaporomoka na raia wake watateseka vibaya kinyume na taarifa za kindoto zinazotolewa kwa sasa na baadhi ya wasomi wa kiuchumi nchini Kenya ambao wanaeneza urongo na kuzisifu Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia kwamba kila kitu kiko shuari hatimaye wanatukaba kwa mapendekezo magumu ambayo yanazidisha majanga zaidi kama ilivyo shuhudiwa kwa mfano nchini Indonesia mnamo 1976, Jamaica mnamo 1978, Urusi mnamo 1997 na Argentina mnamo 2001!
Nidhamu ya kiuchumi ya Kiislamu inatambua kwamba ugavi mbaya wa mali ni kizingiti msingi kwa uchumi kunawiri. Hivyo basi, inalingania kuwepo kwa ugavi wake na pia kutoa njia za kushajiisha watu katika uchumaji mali. Zaidi ya hayo, siasa ya kiuchumi katika Uislamu ni kudhamini ushibishaji wa mahitaji yote msingi ya kila mtu kikamilifu, na kisha kumwezesha kushibisha mahitaji yake ya ziada kwa kadiri awezavyo, kama mtu aishiye ndani ya jamii maalumu, iliyo na mfumo fulani wa kimaisha. Kwa hivyo Uislamu humtazama kila mtu kipeke yake kuliko kama watu jumla ndani ya nchi. Kinyume na nidhamu ya kiuchumi ya kirasilimali inayojali tu watu wachache wanao endesha makampuni na hivyo ongezeko au upungufu wa uzalishaji wake ndio inayo amua utajiri jumla wa nchi (GDP) inayo tafsiriwa ima kudidimia au kukua kwa uchumi. Ambapo hamu kubwa ya serikali ni kudumisha hali halisi kwa mbinu yoyote ile ili kuhakikisha wanazisaidia kampuni zao pindi zinapokaribia kuporomoka! Kwa upande mwengine wanapuuza idadi kubwa ya raia wengine ambao daima wanateseka na kuendelea kuwanyanyasa kwa kuwaweka rehani wakati wanapochora mipango ya kuomba mikopo kama ilivyo hali sasa hivi nchini Kenya ambapo takriban kila raia ana deni la shilingi 100,000 kichwani mwake!
Ali Nassoro
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya