Namna Khilafah Ilivyo Vunjwa kwa Kifupi

Ni miaka 100 tangu Khilafah ilipovunjwa mnamo Rajab 1342 Hijria kwa mikono ya wakoloni na watawala vibaraka ndani ya ulimwengu wa Waislamu. Ni muhimu kuangazia yale yaliyojiri ili Ummah wa Waislamu uweze kufahamu tukio chungu katika historia yao. Inatarajiwa kupitia ufupisho huu kwamba Ummah wa Waislamu utaweza kupata nishati na kusonga mbele katika kazi ya kurudisha mlinzi na ngao yao, Dola ya Khilafah.  Kukosekana kwake kumeufanya Ummah wa Waislamu kuwa yatima ilhali wauaji wa mama yao ‘Khilafah’ wanatembea huru ilhali wamebeba kisu mkononi kwa miaka 100 sasa!

Kuvunjwa kwa Dola ya Kiislamu hakukuanza mwaka 1342 H. Badala yake ni kuwa katika mwaka huo ndio kilele cha njama ovu zilizokuwa zimepangwa na maadui wa Uislamu kwa karne. Jaribio la mwanzo lilikuwa la kuiangamiza Dola ya Kiislamu ndani ya Madinah ikiwa chini ya uongozi wa Mtume (saw) kwa uvamizi wa jeshi la washirikina likiongozwa na Abu Sufyan ibn Harb kabla kuwa Muislamu. Jaribio lao hilo ambalo halikufaulu liliungwa mkono na vibaraka wa ndani miongoni mwa Mayahudi ndani ya Madinah.

Chuki za maadui wa Uislamu zilizidi baada ya ukombozi wa kwanza wa al-Quds katika utawala wa Khalifah Umar al-Faruq (ra) chini ya kamanda Abu Ubaidah ibn Al-Jarrah (ra) mnamo 638 M. Hili liliwafanya maadui wa Uislamu kuwa na machungu zaidi. Hasira zao ziliwapelekea kupanga na kuzindua vita vya msalaba chini ya uongozi wa Papa II katika karne ya 11 M iliyopelekea mauaji ya Waislamu na kutekwa kwa al-Quds. Baada ya miaka 200 chini ya kamanda Salahuddin al-Ayyubi (rahimahullah) akasimama na kupambana dhidi ya watu wa msalaba na kuwashinda mnamo 4 Julai 1187 M katika Vita vya Hattin. Hivyo basi kuikomboa al-Quds kwa mara ya pili.

Khilafah chini ya uongozi wa Muhammad al-Fateh ikaishinda Ufalme wa Baizantini na kuikomboa Konstantinopli mnamo karne ya 15 M. Hivyo basi, kutimiza bishara kutoka kwa Rasulullah (saw): لَتُفْتَحَنَّ الْقُسْطَنْطِينِيَّةُ فَلَنِعْمَ الْأَمِيرُ أَمِيرُهَا وَلَنِعْمَ الْجَيْشُ ذَلِكَ الْجَيْشُ “Mutaifungua Konstantinopli, Amiri wake ndiye Amiri bora, na jeshi bora ni jeshi hilo.” (Ahmad). Kisha Uislamu ukaenea na kubisha milango ya Ulaya kusini na mashariki. Makundi ya watu kutoka Albania, Bulgaria, Yugoslavia miongoni mwa nchi nyingine yaliingia katika Uislamu kwa hiyari.  Kisha Khilafah chini ya Khalifah Sultan Sulaiman ikazindua kampeni ya Kuizunguka Vienna mnamo Septemba – Oktoba 1592 M.

Baada ya tukio la Kuizunguka Vienna watu wa Ulaya wakahisi hofu kubwa. Kwa hiyo waliamua kuungana na kuunda muungano ili kuweza kusitisha upanuzi wa Khilafah na kuivunja kabisa kwa maana Uislamu. Watu wa Ulaya kwa maana watu wa msalaba walitambua kwamba Waislamu hawashindiki kwa kuwa wamejifunga na aqeedah ya Kiislamu. Kwa maana nyingine ikiwa wataifuata kiukamilifu Qur’an na Sunnah.Hivyo basi, lau wanataka kufaulu katika mkakati wao huo mpana basi lazima waweke Waislamu mbali sana na Uislamu wa kweli kwa kuwalea na thaqafa isiyokuwa ya Kiislamu kwa kubuni vituo vya ‘kimishenari’ mwishoni mwa karne ya 16 M.

Wakabuni vituo vya kwanza vya kimishenari ndani ya Malta na kuvifanya kuwa ndio makao makuu ya mashambulizi ya kimishenari dhidi ya Uislamu. Vituo hivyo vilifanyakazi kwa sura ya taasisi za kielimu na kisayansi. Mwanzoni athari yake kwa Waislamu ilikuwa chache kwa kuwa Khilafah japo kidogo ilikuwa madhubuti licha ya kwamba ilikuwa inaporomoka. Lakini, ndani ya karne za 18 na 19 M, dola ya Khilafah iliporomoka kwa kasi na wamishenari wakapatiliza udhaifu  na kueneza fikra na ufahamu wao muovu kwa watu. Kwa hiyo, wakaifanya Beirut kuwa ndio kituo cha vitendo vya kimishenari katika karne ya 19.

 

Kazi za kimishenari ziliendelea ilhali wakati huo huo Uingereza, Ufaransa na Urusi kwa pamoja wakazindua mashambulizi kila mmoja upande wake dhidi ya Khilafah ya Uthmani. Urusi iliiteka Crimea, Ukraine Kusini na Caucasus Kaskazini. Uingereza ikaichukua Misri, Sudan na India. Ufaransa ikaikalia Afrika Kaskazini.  Ulikuwa mchoro wenye sura mbili ambao maadui wa Uislamu wameuchora kiasi kwamba mwishoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia  ilikuwa imebakia Uturuki pekee nayo ilikuwa chini ya majeshi ya washirika.

Wamishenari walikuwa na malengo mawili makuu kupitia kuwepo kwao: kwanza- kuwatenga Waarabu kutoka kwa Khilafah ya Uthmani na pili- kuwatenga Waislamu na fungamano la Kiislamu. Walikuwa wakiongozwa na Uingereza na Ufaransa miongoni mwa washirika wengine. Walisonga mbele na kubuni ‘Miungano ya Siri’ mnamo 1875 M ndani ya Beirut na kuchochea utaifa wa Kiarabu miongoni mwa watu kupitia kutoa matangazo ya kisiasa ya uhuru na matoleo hususan kwa wale wanaoishi nchini Syria na Lebanon. Kwa upande mwingine walishajiisha chuki dhidi ya Waturuki kwa kudai kuwa wamewapokonya mamlaka Waarabu na kukiuka Sharia’h ya Kiislamu.

Wakati huo huo walichochea utaifa wa Kituruki miongoni mwa Waturuki. Hivyo basi, walibuni harakati ya Waturuki Vijana mnamo 1889 na kuingia uongozini mnamo 1908 na kisha baadaye kumfurusha Khalifah, Abdul-Hamid II. Kwa kuongezea, ulinganizi kwa Waarabu ulifaulu pale ambapo Sharif Hussein kibaraka wa Uingereza kutoka Makkah aliwaongoza Waarabu kuiasi Khilafah ya Uthmani mnamo 1916. Uasi uliopelekea kugawanywa kwa ardhi za Khilafah ya Uthmani na baadaye kuwekwa chini ya mamlaka ya Uingereza na Ufaransa.

Uingereza ilimlea Mustafa Kemal, msaliti na aliyelaaniwa na Mwenyezi Mungu (swt). Mnamo 1922, Waziri wa Kigeni, Bwana Curzon aliratibu Kongamano la Lausanne kujadili kuhusu masharti ya uhuru wa Uturuki.  Masharti yalikuwa: kwanza- kuvunjwa kwa Khilafah kiukamilifu, pili- kumfurusha Khalifah nje ya mipaka ya Uturuki, tatu- kuzitaisha rasilimali za Khilafah nan ne- kutangaza kuwa Uturuki imekuwa dola ya kisekula. Waislamu nchini Uturuki walikataa kutimiza masharti hayo manne. Hivyo basi, ikamlazimisha Mustafa Kemal mnamo 3 Machi 1923 M kutumia nguvu na kuwatishia watu na kupitisha mswada wa Kupiga marufuku na kupelekea Khilafah kuvunjwa rasmi!

Uingereza na washirika wake waliipa Uturuki uhuru na kwa pamoja wakayaondosha majeshi yao yaliyokuwa nchini Uturuki. Wanachama wa Bunge la Uingereza walipinga hatua hiyo na Bwana Curzon akajibu kwa kusema: “Hali iliyoko sasa ni kuwa Uturuki imekufa na haitonyanyuka tena, kwa sababu tumevunjilia mbali nguvu zake msingi, Khilafah na Uislamu.” Akaongezea, “Lazima tuhitimishe kila kitu ambacho kitaleta umoja wa Uislamu baina ya watoto wa Waislamu. Kwa kuwa tumefaulu kuivunjilia mbali Khilafah, kwa hiyo lazima tuhakikishe kwamba hakutachipuza tena umoja wa Waislamu, ima uwe ni wa kifikra au kithaqafa.” Kwa hivyo, mpaka sasa mashambulizi ya Kimagharibi yanaendelea.

Uingereza na Ufaransa zikiwakilishwa na mabalozi wao Mark Sykes na Francois Georges Picot waliigawanya iliyokuwa Dola Moja Iliyoungana ya Khilafah na kuwa vijidola na kuvipa vibaraka wao ndani ya ulimwengu wa Waislamu. Ramani ya sasa ya Mashariki ya Kati imetokana na hawaa za mabalozi hao wakikoloni na kubakia kuwa ni zawadi yao kwa Khilafah ya zamani! Tangu wakati huo Ummah wa Waislamu umebakia yatima na unazama ndani ya majanga! Ufupisho huu wa matukio uwe ni chachu ya kuzidisha bidii na kufanyakazi ya kusimamisha Khilafah kwa njia ya Utume.

#أقيموا_الخلافة               #خلافت_کو_قائم_کرو

#ReturnTheKhilafah          #YenidenHilafet          #TurudisheniKhilafah

Imeandikwa kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir