Mwenyezi Mungu (swt) alisema: (وَمَآ أَرۡسَلۡنَـٰكَ إِلَّا رَحۡمَةً۬ لِّلۡعَـٰلَمِينَ) “Nasi hatukukutuma [Muhammad] ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote.” [21. Al-Anbiya: 107] Uislamu ni mfumo kwa maana nyingine ni mwenendo kamili wa maisha unaochipuza kutoka kwa Muumba wa ulimwengu, mwanadamu na uhai, Mwenyezi Mungu (swt). Hivyo basi, Mwenyezi Mungu (swt) amempa mwandamu changamoto ili aweze kutambua uwepo Wake kwa kutumia akili yake. Ni kupitia kufikiria ndipo hukumu na maamuzi yanaweza kutolewa. Vilevile vitendo vinatendwa kama natija ya fahamu zinazochipuza kutoka katika fikra aliyobeba mtendaji. Kwa kuongezea mahitaji muhimu ya kiviungo na ghariza humuhitajia yeye kuweza kuyashibisha kwa kutegemea msingi ambao amejifunga nao kutokamana na fikra aliyoibeba. Kwa hiyo, kufikiria (akliyya) na kushibisha (nafsiyya) kwa mwanadamu kwa pamoja hujenga utambulisho (shaksiyya) wake. Ikimaanisha ima anaweza kuwa na utambulisho wa Kiislamu au kinyume chake.
Utambulisho wa Kiislamu ni ule ambao kwamba kufikiria na kushibisha kumethibitiwa na mipaka ya Shari’ah ya Kiislamu (Quran, Sunnah, Ijma’ Sahaba na Qiyas). Muislamu aliye na utambulisho wa Kiislamu ni mtumwa kwa Mwenyezi Mungu (swt) kwa maana anajisalimisha kwa maamrisho na makatazo Yake. Kwa upande mwingine, yeyote ambaye hana utambulisho wa Kiislamu daima atakuwa ni mtumwa kwa matakwa yake na atakuwa na utambulisho wa kirasilimali wa kisekula. Hiyo ndio dhati ya uhalisia leo ambapo watu ambao hawana utambulisho wa Kiislamu ima ni Waislamu au la wameiondoa dori kubwa ya Muumba katika kuweka sheria na kujipa wao. Hivi sasa ndio wanaotawala na kuwasimamia watu mambo yao kwa msingi wa matamanio yao. Na katika mchakato huo wakisababisha majanga yasiyokua na hesabu katika kila nyanja ya maisha kutokana na kujifunga na mfumo wa kirasilimali wa kisekula na kutekeleza nidhamu zake zenye sumu zinazojumuisha sio tu nidhamu ya kiuchumi ya kirasilimali. Nidhamu yenye kuangamiza ambayo inaendelea kukazanisha vitanzi vya kiuchumi katika shingo za watu na kuwasababishia tabu na kukata tamaa duniani kote!
Kila mchumi, mwanasiasa na msomi wa kirasilimali wa kisekula yupo katika hekaheka za kuwapa watu matumaini ya kesho ambayo kuja kwake hakuna dhamana! Kwa maana nyingine, nidhamu ya kiuchumi imevunjika na hairekebishiki kamwe. Kwani mzizi wa kufeli kwake ni msingi ambao umejengewa juu yake. Nidhamu ya kiuchumi ya kirasilimali imejikita katika uhadaifu wa uchache wa rasilimali hauwezi kukidhi mahitaji ya kuendelea ya mwandamu! Ikiwa imesimama juu ya msingi huo wa kimakosa ikaanza kuzalisha bidhaa na huduma nyingi kama suluhisho kwa tatizo linalodaiwa! Hivyo basi, tunashuhudia kiwango kikubwa cha utajiri kikiwa kinamilikiwa na watu binafsi wachache pamoja na makampuni yao mtawalia ilhali umma umetumbukia katika umasikini endelevu na usioingia akilini. Kwa mfano Amerika inadai kuwa ndio ardhi ya maziwa na asali, raia wake hawana makazi, wana njaa na afya yao imedorora! Je, hali ikoje katika sehemu nyingine duniani?
Ili kuzidisha unga maji nidhamu ya kiuchumi ya kirasilimali inazishajiisha tawala za kidemokrasia kuendeleza uporaji wa mchana wa mali za raia walizozichuma kwa dhiki. Inafaulisha malengo yake kupitia kuandikwa na kufanyiwa kazi sera na sheria za ushuru katili na zenye kukandamiza ambazo kwamba zinazidisha ugumu kwa raia ambao tayari wanataabika. Kwa kuongezea, serikali zinasonga mbele kubuni miradi hewa kwa ufadhili wa mikopo ambayo inatozwa riba ya juu yenye kuadhibu. Na ndio sababu pato la kitaifa (GDP) la mataifa yote ya kisekula imejikita katika uzalishaji, faida na hasara iliyopatikana katika makampuni na sio uwezo wa raia binafsi kuweza kukidhi mahitaji msingi na kuwawezesha na nyenzo za kuweza kukimu mahitaji ya ziada!
Uchumi wa mataifa ya kisekula duniani kote ni wa kudhaniwa! Naam, kwa kuwa thamani yake imetiwa mnyororo kwa dola! Kiudhati, thamani yake ndogo inaendelea kushuka kila imani juu ya mamlaka ya Amerika inavyo endelea kufifia! Na sio jambo la kushangaza kuona kila kosa linalofanywa na kampuni za Amerika linahisika duniani kote kupitia athari zake! Kila Amerika inapochapisha makaratasi (pesa zisizokua na thamani (dhamana) yoyote) uchumi wake na ule wa sehemu nyingine za dunia huporomoka na mfumuko wa bei huzidi! Yote haya ikiwa ni natija ya sera za Taasisi za Bretton Woods, Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa! Taasisi mbili ambazo zilibuniwa kutokamana na mkutano wa nchi 43 huko Bretton Woods, New Hampshire nchini Amerika mnamo Julai 1944. Lengo lao kuu lilikuwa ni kuujenga uchumi wa kiulimwengu uliokuwa umeporomoka baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Taasisi hizi zilikuwa ni natija ya mawazo ya wajuzi watatu – Waziri wa Fedha wa Amerika Henry Morganthau, mshauri wake mkuu wa kiuchumi Harry Dexter White na mchumi wa Kiengereza John Maynard Keynes. Uchumi wote wa ulimwengu ulikuwa juu ya mabega ya watu watatu ambao akili zao zina kikomo! Alas! Majanga yanaendelea pasi na kusita hadi leo. (Bretton Woods Project)
Kinyume chake katika nidhamu ya kiuchumi ya Kiislamu ambayo imechipuza kutoka kwa Mwenyezi Mungu (swt). Ni sehemu ya ukamilifu wa nidhamu ya Uislamu ambayo inatekelezwa na dola ya Kiislamu ya Khilafah. Nidhamu ya Kiislamu ilitekelezwa chini ya usimamizi wa Mtume Muhammad ibn Abdullah (saw) huko Madinah akiwa Rais wa Dola ya Kiislamu. Kisha akafuatiwa na Makhalifah ambao walikuwa idadi ya 101. Kwa takribani karne 13 dola ya Kiislamu ilitekeleza nidhamu ya kiuchumi ya Kiislamu. Nidhamu ambayo imefafanuliwa wazi na aya hiyo hapo juu, iliyonukuliwa mwanzoni wa makala haya. Ni nidhamu ya rehema na sio ya ukandamizaji, ukatili na kuwapatiliza watu na haitekelezwi juu yao kama inavyo shuhudiwa leo duniani kote.
Nidhamu ya kiuchumi ya Kiislamu imejengwa juu ya msingi kwamba tatizo lipo katika usambazaji wa utajiri na sio uchache wa rasilimali kama inavyodaiwa na nidhamu ya kiuchumi ya kirasilimali. Mwenyezi Mungu (swt) alisema, (كَيْ لَا يَكُونَ دُولَةً بَيْنَ الْأَغْنِيَاءِ مِنْكُمْ) “ili yasiwe yakizunguka baina ya matajiri tu miongoni mwenu.” [Al-59. Hashr: 7]. Kwa kuongezea, nidhamu ya kiuchumi ya Kiislamu inatambua kwamba mahitaji ya wanadamu yana kikomo na sio kuwa hayana kikomo kama inavyodaiwa na nidhamu ya kiuchumi ya kirasilimali. Kwa hiyo, nidhamu ya kiuchumi ya Kiislamu inakwenda mbio kutatua usambazaji wa rasilimali kwa watu binafsi na kuwawezesha kukidhi mahitaji yao msingi ambayo ni mavazi, chakula na makazi; na mahitaji ya kijamii ambayo ni elimu, usalama na matibabu na kuwawezesha nyenzo za kufikia mahitaji yao ya ziada. Zifuatazo ni baadhi ya ushahidi wa ustawi wa kiuchumi chini ya Khilafah ilipokuweko kabla kuvunjwa kwake mnamo 28 Rajab 1342 H sawia na 3 Machi 1924 M:
Kwanza: Ilikuwa ni katika utawala wa Khalifah wa pili, Umar ibn Khattab, Fursi ili kombolewa na kiwango kikubwa cha mali kikapatikana kama ngawira ya vita na kugawanywa kwa Waislamu na nyingine kutumika katika kusimamia asasi muhimu za Khilafah kama jeshi. Khalifah mwenyewe alikuwa akihakikisha kuwa raia wanalishwa kutoka katika Bait ul-Mal. Wakati mwingine alikuwa akiziondosha sera ambazo zilionekana kuwakandamiza raia kama kuwakata wezi mikono katika kipindi cha ukame mpaka ulipoondoka. Fauka ya hayo, aliagiza wanaume wazee wasiokuwa Waislamu ambao hawawezi kulipa Jizya wasitozwe na badala yake wakimiwe kutoka katika Bait ul-Mal. Hayo ni kinyume na mipango na mikakati ya utozaji ushuru wenye kukandamiza kutoka kwa tawala za kidemokrasia za kisekula duniani kote, haziwajali wazee au vijana, wanaume au wanawake; wanaochokiona ni kuwa mwanadamu ni kigezo cha uzalishaji!
Pili: Katika kipindi cha utawala Khalifah, Umar ibn Abdul Aziz, ndani ya kipindi cha muda wa miaka 2 na miezi 5, Khalifah aliweza kurekodi idadi kubwa ya wasiokuwa Waislamu wakisilimu kutokana na kutekelezwa Uislamu katika nyanja zote za maisha hususan katika nyanja ya kiuchumi. Khalifah mwenyewe alikuwa mbioni kuongoza kwa mfano kwa kujiepusha na kuwafanyia dhuluma za kiuchumi raia wake. Na ikapelekea hali ambapo hakukuwepo na watu wakupewa Zaka. Hata hivyo, mali ya Zaka iliendelea kuzidi kwa kupungua idadi ya wale wanaohitajia mgao kutoka humo.
Tatu: Zama za utawala wa Khilafah ya Abbasiyya iliyoanza katikati ya karne ya 7 hadi katikati ya karne ya 13. Hujulikana kama Enzi ya Dhahabu ya Kiislamu. Ni katika kipindi hicho ndipo Uislamu na Waislamu walistawi. Mchango mkubwa wa kustawi huko ulipatikana kwa kupanuka maarifa baada ya Waislamu kuushinda kivita Ufalme wa Tang kutoka Uchina katika Vita vya Talas mnamo 751 M. Waislamu walipata mateka waliokuwa na elimu ya kutengeneza karatasi ambao waliwafunza Waislamu ujuzi huo wakutengeneza karatasi. Na kisha kupelekea upanuzi wa maarifa kutokana na kuweko kwa viwanda vingi vya kutengeneza karatasi na watu waliweza kuandika na kufunzana maarifa. Na wakati huo huo, viwanda vya karatasi vilileta mapinduzi katika uchumi kwa kuwa wanachuoni walijishughulisha kufanya utafiti mpana na kuleta mapinduzi katika nyanja za matibabu, hesabu nk. Hilo likapelekea kukuza uchumi wa dola ya Kiislamu, Khilafah.
Hayo matatu ni baadhi tu ya vidokezo vya natija ya utekelezaji wa nidhamu ya kiuchumi ya Kiislamu chini ya Khilafah. Khilafah haitowapora raia wake pesa zao walizo zichuma kwa jasho lao kwa kisingizio eti kwa ajili ya kuimakinisha au kusimamia mambo ya Dola. Kwa kuwa Shari’ahimeweka wazi vyanzo vyake vya mapato na matumizi. Hivyo basi, kufutilia mbali usomaji wa bajeti kila mwaka ambao huchosha na aghalabu hubadilika viwango kutokana na vipaumbele vya kilafi vya walioko madarakani. Miradi hewa haitoruhusiwa kwa kuwa kila shilingi itakayo tumika lazima ihesabiwe na raia wa Khilafah, bali kazi nzito inamsubiri Khalifah Siku ya Kiyama ili kuelezea juu ya uongozi wake mbele ya Mwenyezi Mungu (swt).
Dalili hizo tatu ni sehemu tu ya taswira inayolinganisha hali halisi ya sasa hivi ambapo Waislamu ni takribani bilioni 2 waliotapakaa duniani. Lau wataunganishwa chini ya kiongozi mmoja, bendera moja na dola moja huku Uislamu uwe ndio fungamano na kigezo cha kuwaunganisha kwao. Hautokuwa tu ndio Ummah wa Waislamu bali utakuwa ni nguvu isiyokuwa na mshindani kisiasa, kijamii, kiuchumi na kijeshi. Hata hivyo, tangu kuvunjwa kwa Khilafah, Ummah wa Waislamu umegawanyika na kujazwa
sumu ya fahamu za utaifa na kuwatia upofu machoni mwao ili wasione uporaji endelevu wa ardhi na rasilimali zao kama mafuta, aradhi zenye rutuba na nguvu kazi nk.
Kukosekana kwa Khilafah kunaendelea kukaba maisha ya watu pasi na kuzingatia umri, jinsia, rangi, dini, hali zao za kijamii, kiuchumi au kisiasa hadi leo miaka 101. Suluhisho pekee lililowahi kujaribiwa na kufaulu ni kusimamisha tena dola ya Kiislamu, Khilafah kwa njia ya Utume. Katika hii Rajab ya 1443 H ni wakati muhimu mno kuupatiliza na kuchukua fursa za mahangaiko yanayo shuhudiwa duniani na kubadilisha mpangilio uliopo kwa mpangilio Mpya wa Kiislamu ambao ni rehema kwa wanadamu.
Huu ni wakati wakujitenga mbali na mawazo ya kuridhika na hali iliyoko sasa ya kuwa hakuna linaloweza kufanywa. Alas! Tunatakiwa kunyanyuka na kuitikia mwito wa Mwenyezi Mungu (swt) kwa waumini. Huu ndio wakati wa kunadi kuwa imetosha na hatuwezi kamwe kubakia katika nidhamu hii ya utawala wa patapotea. Nidhamu iliyofeli ambayo inasubiri tu kuchipuza kwa Khilafah kwa njia ya Utume ili itangazwe kuwa imekufa na kuzikwa punde tu.
Ali Nassoro Ali
Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir