Taifa la Kenya hivi sasa limekumbwa na sintofahamu kutokana na kauli kinzani za viongozi wa kuu katika serikali wakiwemo wabunge na wengineo. Sintofahamu hiyo imesababishwa na kauli ya Rais Uhuru Kenyatta kuhusiana na ukaguzi wa maisha ya wafanyikazi wa serikali aliyoitoa tarehe 14 Juni 2018 akisema, “Lazima uweze kueleza namna ulivyoipata gari yako, nyumba yako na ardhi tukizingatia mshahara unaopata…”. Na ili kutoa mfano bora ukaguzi huo alipendekeza uanze kufanyiwa yeye kama mfanyikazi wa kwanza katika serikali kisha ufuatie Makamu wa Rais na walioko chini yao.
Hali inabainisha wazi kuwa kuna mirengo miwili tofauti; kuna wale wanaounga mkono na wale wanaopinga pendekezo hilo la Rais. Kila mrengo ukitoa sababu zake mfano wanaounga mkono wanasema ni hatua muafaka Rais aliyoichukua na inatarajiwa kuliangamiza jinamizi la ufisadi nchini. Upande mwingine wanapinga wakisema kuwa hakuna sheria zinazoweza kutumika ili kufaulisha pendekezo hilo na pia kuna uwezekano pendekezo hilo likatumika kisiasa. La msingi ni kuwa utata huu unadhihirisha kuwa wasiwasi ndani ya serikali kuhusiana na kufaulu au kufeli kwa zoezi hilo lau litafanyika.
Tatizo msingi ambalo linaloikumba Kenya, Afrika na Ulimwengu jumla ni serikali kuasisiwa juu ya itikadi ya usekula na mfumo wa urasilimali. Itikadi ya Usekula imeasisiwa na akili finyu ya mwanadamu na lengo lake ni kuyatenganisha maisha na Mwenyezi Mungu. Kwa maana nyingine ni kuwa Sheria za Muumba zisiwe na usemi na zisitumike katika kuendesha maisha jumla ya wanadamu. Ama kuhusu mfumo wa urasilimali umetokamana na Itikadi ya Usekula na umeupa kipao mbele nidhamu ya uchumi kwa kipimo cha manufaa na hasara; na ndio maana ukaitwa mfumo wa urasilimali kwa sifa ya uchumi.
Hivyo basi, raia jumla wamebeba Itikadi ya usekula na fikra za Kirasilimali na kumfanya mwanadamu kuwa bwana aliye huru na kujitungia sheria mwenyewe. Kiasi kwamba hakuna utambulisho wa uchajiMungu (Shaksiyatul Ilmaniyah) ndani ya wanadamu ambao pia baadhi yao ni wafanyikazi wa serikali. Kila mmoja ana pima vitendo kwa mujibu wa faida na hasara; huku ulafi na uchu wa kulimbikiza mali kila mmoja ukiwa umemjaa na ndio lengo lake kuu la kuishi hapa duniani ili astareheshe viungo vyake kwa kipimo cha juu. Ufahamu huo ndio chanzo cha kashfa zinazoshuhudiwa nchini Kenya ziwe ni za kiuchumi/fedha, kijamii, kiutawala n.k zote chimbuko lake ni utelezaji wa mfumo batili na uliofeli wa Usekula wa Kirasilimali.
Kinyume chake Uislamu umemfanya mwanadamu ni mtumwa anayetakiwa kujisalimisha kwa Sheria za Mwenyezi Mungu. Maisha yake jumla lazima vitendo vyake vyote avipime kwa msingi wa halali na haramu na ajilazimishe na kwamba kuchukia na kupenda kwake kuwe ni kwa ajili ya Mola wake. Lengo la uhai wake ni kwa ajili ya Uislamu na Jukumu lake ni kumcha Mola wake. Hivyo basi, Itikadi ya Uislamu inamfanya mwanadamu kuwa na utambulisho wa uchajiMungu (Shaksiyatul Islamiyah). Kupitia utambulisho huo ndio wanadamu jumla wanaongoka na ufisadi jumla.
Ili tuweze kufikia katika hali ya uchajiMungu hatuna buda ila kuyarudisha maisha ya Kiislamu. Haiwezikani kuishi katika maisha ya Kiislamu isipokuwa chini ya kivuli kinacho washajiisha raia wake kuwa na uchajiMungu. Kivuli hicho si chengine bali ni Serikali ya Kiislamu ya Khilafah. Khilafah kwa sasa haipo ulimwenguni kote na ndio maana wanadamu jumla wanateseka kwa majanga tofauti tofauti mfano vita vya kuendelea, uzorotaji wa nidhamu ya kijamii iliyoasisiwa juu ya uhuru, sera hadaifu za kiuchumi zilizoasisiwa juu ya mtizamo wa uporaji n.k; yote hayo yakiwa yanaendelea chini ya Serikali za Kisekula za Kirasilimali ikiwemo Kenya.
Ili wanadamu waepuke na majanga ya ufisadi n.k hawana budi kujiunga na mwito wa Kiislamu wa kuleta mageuzi msingi juu ya mgongo wa ardhi. Mwito huu unalenga hatimaye kusimamisha Serikali ya Kiislamu ya Khilafah kwa njia ya Utume ndani ya nchi yenye vigezo vya kuwa Dola ya Khilafah ikiwa ni pamoja na iwe na Waislamu wengi. Serikali hii ndio itakuwa nishati kuu ya kuweza kumakinisha fikra na mazingira yanayopelekea mwanadamu kupata uchajiMungu. Kwa kuwa mwanadamu atajisalimisha kwa Sheria za Muumba wake na kufahamu kuwa anahitaji kuchuma na kutafuta mali na hatimaye akifariki atakuja kuhesabiwa kuhusu vitendo vyake vyote ikiwemo njia aliyoitumia kuchuma na alivyoitumia mali.
Hapa ndio kuna jukumu kubwa na zito kwa kila Muislamu nalo ni kurudisha maisha ya Kiislamu juu ya mgongo wa ardhi ili Sheria za Allah (swt) zitumike katika kuhukumu wanadamu. Jukumu hili tayari Hizb ut-Tahrir imetangulia kulibeba lakini kwa kutambua uzito wake ni muhimu kila mwenye kupenda mageuzi msingi naye asiachwe nyuma bali ajiunge.
Ni muhimu kwa wasomi na wanafikra watumie fursa yao kuusoma Uislamu na kuufahamu kuwa ni mfumo mbadala ulio na suluhisho ya matatizo ya wanadamu wote leo duniani. Kwa ukweli mfumo ulioko leo wenyewe umefeli hivyo kuonyesha aibu zake ni kama jeraha kwa maiti.
Imeandikwa kwa Ajili ya Tovuti ya Radio Rahma
Ali Nassoro Ali
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya
Makala Na.1 Tarehe: Ijumaa, 22 Shawwal 1439 | 2018/07/06