Alhamisi, 20 Septemba 2018; Wakenya walishuhudia kwa mara nyingine tena namna wabunge wao walivyopitisha mapendekezo ya Serikali ya kuzidisha utozwaji ushuru. Wanasiasa wakuu katika Jubilee wote waliwashinikiza wafuasi wao wapitishe mapendekezo ya Serikali na kweli wakapitisha. Walala hoi wamekwama wasijue la kufanya na wapi pakuelekea! Kwa kifupi wengi wao wamekata tamaa! Ilhali wachache katika mabwenyenye na walafi wanashangilia kimya kimya huku mate yakiwatoka kutokana na uchu wao wakupora fedha zitakazopatikana kutokana na kuzidi kwa utozwaji ushuru huo!
Ulimwenguni mataifa yote yameasisiwa juu ya itikadi ya usekula (kutenganisha dini na maisha) na mfumo wa urasilimali (kipao mbele ni uchumi kwa sura ya maslahi/manufaa). Kwa kuwa itikadi ya usekula imemtenga Mwenyezi Mungu katika upangiliaji na uendeshaji wa maisha na badala yake kumpa mwanadamu uwezo wa kujitungia sheria kwa kutegemea kichwa chake finyu! Nidhamu ya kiuchumi kwa mujibu wa urasilimali imejikita katika kuhakikisha uzalishaji wa taifa unakuwa kwa kiwango cha juu huku ikiwajali wachache kwa sura ya wamiliki wa viwanda/wawekezaji na kuwakandamiza wengi walala hoi. Na tatizo la kiuchumi katika urasilimali eti ni uhaba wa rasilimali tukilinganisha na idadi ya watu ambao si kweli. Mataifa yote ya kisekula ya kirasilimali yanaendeshwa kwa kutegemea ushuru na mikopo ya riba!
Hicho ndicho chanzo cha maangamivu na kukosekana kwa amani kwa wanadamu wote ulimwenguni leo. Wanadamu wanakwenda mbio usiku mchana si tajiri si masikini, si serikali si raia kila mmoja anamvizia mwenzake amnyoe! Mali/utajiri umebakia na kuzunguka kati ya watu wachache na ilhali idadi kubwa ya watu ulimwenguni hususan Afrika wamebakia kuwa watumwa ndani ya mataifa yao na huku mataifa yao yakiwa watumwa kwa wakoloni wamagharibi kupitia uporaji wa mali za Afrika na badala yake kuwapa sera fisadi za kiuchumi.
Kinyume na mfumo wa Uislamu kupitia Serikali ya Kiislamu ya Khilafah iliyosimamishwa kwa njia ya Utume. Khilafah inaendeshwa kwa mujibu wa Mwenyezi Mungu anavyotaka kupitia Qur’an na Sunnah. Nidhamu zinazochipuza kutoka katika mfumo wa Uislamu ikiwemo ya kiuchumi daima zinazingatia kuwafanyia wepesi raia (Waislamu na wasiokuwa Waislamu) wanaoishi chini ya Khilafah. Ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa haiwatozi ushuru wa aina yoyote raia wake isipokuwa kunapotokea dharura ambayo iko nje ya uwezo wa Khilafah. Hivyo basi kutatozwa ushuru kukimu dharura hiyo kwa wakati huo; lakini pia watakaotozwa ushuru huo watakuwa ni matajiri waliokuwa na mali ya ziada baada ya kukidhi mahitaji yao. Mikopo itakopwa ikiwa kuna dharura ya kukopa kinyume na ilivyo sasa mataifa yanakopa ili kufuja mali kwa sura ya udhamini wa miradi mikubwa ambayo kiasili siyo katika mahitaji msingi ya raia. Kattu hakutakuwepo na riba ya aina yoyote kwa kuwa riba imekatazwa na Mwenyezi Mungu.
Kwa sababu hiyo Wakenya na wanadamu jumla hawana budi kuupinga usekula urasilimali na nidhamu zake za kidhulma na badala yake kujiunga na ulinganizi wa kurudisha tena Dola adilifu ya Khilafah katika miongoni mwa nchi za Waislamu. Ili waweze kupata utulivu, amani na ustawi unaotokana na usimamizi mzuri chini ya kiongozi mchajimungi Khalifah kama ilivyoshuhudiwa takribani karne 14 mpaka mwisho ikiwa ni kuangushwa kwa Khilafah mnamo 3 Machi 1924. Khilafah haitakuwa mtumwa kwa wakoloni na mashirika yao ya fedha mfano IMF au WB n.k itajizatiti kukidhi mahitaji yake kwa kutegemea kuzipatiliza vyema mali nyingi iliyoruzukiwa na Mwenyezi Mungu kwa kuwasimamia raia wake. Kinyume chake Wakenya na walimwengu kwa ujumla wataendelea kusononeka na kuangamia kutokana na makucha ya usekula urasilimali.
Ali Nassoro Ali
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya