Mwenyezi Mungu (swt) ametupa ahadi na kusema:
(وَعَدَ ٱللَّهُ ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ مِنكُمۡ وَعَمِلُواْ ٱلصَّـٰلِحَـٰتِ لَيَسۡتَخۡلِفَنَّهُمۡ فِى ٱلۡأَرۡضِ ڪَمَا ٱسۡتَخۡلَفَ ٱلَّذِينَ مِن قَبۡلِهِمۡ)
“Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walio amini miongoni mwenu na wakatenda mema, ya kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyo wafanya kabla yao.” [An-Nur: 55]
Mtume (saw) ametupa bishara na kusema:
“Kutakuwepo na Utume kwa muda atakao Mwenyezi Mungu, kisha Atauondoa Atakapotaka, kisha kutakuwepo na Khilafah kwa Njia ya Utume nayo itakuwepo kwa muda Atakao Mwenyezi Mungu, kisha Ataiondosha Atakapotaka, kisha kutakuwepo na Ufalme usiojali kwa muda Atakao Mwenyezi Mungu, kisha Atauondosha Atakapotaka, kisha kutakuwepo na Ufalme dhalimu kwa muda Atakao Mwenyezi Mungu, kisha Atauondosha Atakapotaka, na kisha kutakuwepo Khilafah kwa Njia ya Utume” na kisha akanyamaza kimya. [Ahmad]
Na Mtume (saw) akatuelezea ubora wa kuishi chini ya au kutawaliwa na Khilafah:
“Mtume alisema: ‘Banu Israel walitawaliwa na Mitume; kila anapofariki Mtume basi Mtume mwengine alichukua nafasi yake; lakini hakutakuwepo na mtume baada yangu mimi. Bali kutakuwepo na Makhalifah na watakuwa wengi.’ Wakamuuliza (maswahaba): ‘watuamrisha nini?’ Mtume alisema: ‘Wapeni bayah (ahadi ya utiifu) mmoja baada ya mwengine na wapeni haki zao; hakika Mwenyezi Mungu atawauliza juu ya yale Aliyoyaweka mabegani mwao.” [Muslim na Bukhari)
“Yeyote anayefariki pasina kuwa na ahadi ya utiifu kwa Khalifah katika shingo yake amekufa kifo cha kijahiliya.” [Muslim]
“Siku moja chini ya mtawala muadilifu (Khalifah) ni bora kuliko miaka 60 ya ibadah.” [Bayhaqi/Tabarani]
Tokea mnamo 28 Rajab 1342 H sawa na 3 Machi 1924 hadi hivi sasa ni takribani miaka 98H sawa na 95M hatuna Serikali ya Kiislamu ya Khilafah. Tangu wakati huo majanga yanayosibu Uislamu, Waislamu na Wanadamu jumla yanafahamika mpaka kwa wasiokuwa na macho na masikio na ni mengi kattu hayamaliziki yakianza kuorodheshwa na yanaendelea mpaka hivi sasa.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyoko hapo juu ni wazi kwamba kila Muislamu popote alipo ana jukumu la kuitekeleza ibada (kadhia) nyeti nayo ni kurudisha maisha ya Kiislamu kwa kusimamisha serikali ya Kiislamu ya Khilafah kwa njia ya Utume. Kwani ndiyo mama wa faradhi zote na haingii akilini kumuona mtu anapiga hesabu za kufaulu kesho akhera pasina na kupatiliza ibada nyeti ya kusimamisha Khilafah kwa njia ya Utume.
Enyi Waislamu jueni ya kwamba tupo ndani ya Ramadhani tukiingia katika kumi la tatu la kuachwa huru na moto. Kumbukeni kuridhia kutawaliwa na ukafiri (mfumo wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake ovu ikiwemo demomrasia n.k) na makafiri (Amerika, Uingereza, washirika wao na vibaraka wao ndani ya ardhi zetu) ni katika madhambi makubwa yanayomkasirisha Mwenyezi Mungu (swt) na hupelekea kukosa radhi zake na kutiwa motoni. Kinyume chake kufanya kazi/ibada kwa yakini ya kusimamisha Khilafah kwa njia ya Utume ni katika kheri kubwa zinazomridhisha Mwenyezi Mungu (swt) na hupelekea kuepushwa na moto na kwa rehema zake kutiwa peponi. Hima tupatilizeni fursa hii ya kutekeleza ibada ya Kusimamisha Khilafah kwa njia ya Utume.
Ali Nassoro Ali
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya
Makala Na.46: Ijumaa, 19 Ramadhani 1440 | 2019/05/24