يْ لَا يَكُونَ دُولَةً بَيْنَ الْأَغْنِيَاءِ مِنْكُمْ
ili (mali) yasiwe yakizunguka baina ya matajiri tu miongoni mwenu
[Al Hashr: 7]
Mapinduzi ya kiviwanda yaliyotokea nchini Uingereza kati ya mwaka wa 1815 hadi mwaka wa 1848, yalitarajiwa kuwa mageuzi ya kuboresha sio tu, mbinu za uzalishaji bidhaa na huduma, bali hata mbinu ya usawa katika ugavi wa mali baina ya raia wa matabaka tofauti. Lakini, licha ya vivutio vyote hadaifu vya mapinduzi hayo, ulimwengu mzima ulio chini ya mfumo wa kibepari, umeshindwa kutatua tatizo la umasikini. Badala yake, hali inazidi kuwa mbaya kwa kasi mno. Hivyo basi kusababisha pengo kubwa baina ya matajiri na maskini, kinyume na matarajio ya wengi.
Uingereza, licha ya kuwa taifa la tano tajiri ulimwenguni, na ambalo linaaminika kuwa kilele cha mapinduzi ya kiviwanda, linakumbwa na tatizo la ugavi wa mali na utajiri kwa usawa miongoni mwa raia wake. Tatizo ambalo, ndio uti wa mgongo wa kupalilia shina la umasikini. Raia takriban milioni 7.8 wakiwemo watoto milioni 2.6 nchini Uingereza wanakumbwa na tatizo la umaskini. Kwa mujibu wa taasisi ya Joseph Rowntree Foundation (JRF) kila mtu 1 kati ya wafanyakazi 8, hii ni kusema, idadi ya watu milioni 3.8 milion, wanaishi katika hali mbaya ya uchochole. Asilimia 60% ya Waingereza, wanaishi na umasikini, huku mmoja wao akiwa na kazi na kutegewa na familia yote. Huku tishio la kudidimia kwenye matatizo ya kifedha likiwa juu, hasa miongoni mwa wapangaji nyumba za kibinafsi. Helen Barnard, kinara wa taasisi ya Joseph Rowntree Foundation asema,” Uchumi nchini Uingereza haulengi kunufaisha familia zenye mapato madogo. Licha ya kuwa uchumi waendelea kukua tangu mwaka wa 2010, lakini katika wakati huu, kumeongezeka kodi, mshahara kupungua, na kupunguzwa kwa malipo ya manufaa ya uzeeni, ikimaanisha kuwa familia nyingi, zikiwemo zenye kufanya kazi zimeshuhudia kuongezeka kwa tishio la umasikini.” Haya yanajiri, licha ya kuwepo hatua kama zile zilizo pigiwa upatu na Henry George kwenye kitabu chake “Maendeleo na Umasikini (Progress and Poverty)”, zilizo lengwa kupunguza angaa kwa uchache tatizo hili, hali hii inaendelea.
Miongoni mwa mapungufu makubwa yaliyomo katika mfumo wa kibepari, ni kushindwa kugawa mali kwa njia ya sawa baina ya raia katika usawa wa kiuchumi. Dosari hii, yatokamana na nidhamu mbaya ya kiuchumi ya kibepari ambayo imeufunga mzunguko wa mali kwa matajiri pekee na kuzuia wengine njia za kufikia umilikaji wa mali; na kuchanganyikiwa katika kutofautisha baina ya nidhamu ya kiuchumi na sayansi ya kiuchumi. Uislamu, umechukua hatua kabambe za kuhakikisha raia wote wa Khilafah wanapata nafasi ya kufikia njia za umilikaji mali na hivyo basi kuondoa tatizo la umasikini kabisa. Kama ilivyokuwa chini ya Khilafah ya Umar ibn Abdul-Aziz, ambapo kulikosekana hata maskini mmoja. Tofauti za kimaumbile na kiakili hutiliwa maanani miongoni mwa raia. Hivyo, hulazimisha matajiri kuwasaidia maskini na wahitaji. Huduma zote muhimu na zenye kuhitajiwa na jamii ni mali ya umma, hakuna ruhusa ya kubinafsishwa; kwa kuwa ni wajibu kwa serikali ya Khilafah kudhamini bidhaa na huduma kwa raia. Hizi zikiwa ni baadhi tu ya hatua zinazoweza kuweka usawa katika mzunguko wa mali na utajiri ndani ya serikali ya Khilafah.
Hussein Muhammad Hassan
Mwanachama wa Hizb ut Tahrir Kenya