Duniani kote wanadamu wanakabiliwa na ujasusi mpana, udhibiti na ufuatiliaji kutoka kwa tawala na makampuni. Ama tawala zinajaribu kulinda madaraka na uhalali wao dhidi ya kuhesabiwa kwao na watu kitaifa na kimataifa. Watu wanafichua kufeli kwa sera na sheria za tawala zilizojikita katika mfumo batili wa kirasilimali wa kisekula. Kwa upande mwingine, makampuni yanalenga kuzidisha mapato yao na kuwapiku washindani. Kila upande ima kwa kushirikiana au kila mmoja kivyake huweka mbinu na mipango ya kidijitali ili kuweza kushawishi upitishaji wa sera na sharia mpya au kuzikiuka zilizopo tayari ili kufikia malengo yao.
Natija yake ni kuwa idadi ya watu wanaojifunga na matumizi ya VPN inaendelea kuongezeka wakitafuta ulinzi dhidi ya hatari ya ujasusi, ukusanyaji wa taarifa zao na vitisho vya kiusalama. Kwa hiyo VPN inakuwezesha kuingia mtandaoni ukiwa na usalama na usiri zaidi. Kwa kuongezea, inakupa uwezo wa kuepuka udhibiti na kupata maudhui yaliyodhibitiwa. VPN ina uwezo wa kufanya yote hayo kwa kubuni kiunganishi kilicho na kodi baina ya kifaa/tarakilishi yako (desktop/ laptop/ tablet/ smartphone/ tv etc.) na sava ya VPN. Hivyo basi, unaingia mtandaoni kupitia kiunganishi kilicho na kodi na eneo lako ni kwa mujibu wa sava uliyojiunganisha nayo.
Ni muhimu kutambua kwamba unapoingia mtandaoni bila kutumia VPN kila unachofanya kinaweza kufuatiliwa hadi pale ulipo khaswa na kifaa unachotumia. Inawezekana kupitia anwani ya kifaa chako mtandaoni (IP). Inamaanisha kwamba unapotumia VPN eneo lako la kweli na anwani ya chombo chako hufichwa na badala yake kuchukua sava ya VPN unayotumia. Hata hivyo, wanaotoa huduma za mitandao (ISP) au yeyote anayefuatilia mtandao wako anaweza kuona kuwa umejiunganisha na sava ya VPN; lakini hawezi kurekodi taarifa zako (vitendo vyako mtandaoni). Pia, unapotumia VPN ni muhimu kutumia browser na kidhibiti matangazo imara. Daima ni bora kutumia VPN za kulipia na kuepuka za bure. Tafiti nyingi zinathibitisha kwamba VPN nyingi za bure zina rekodi, fichua na fanyia biashara taarifa za watumizi. Na VPN za kulipia zinakuwezesha kupangilia upya GPS yako na kuficha kuonekana kama umejiunganisha na sava ya VPN.
Kwa kufupisha VPN inatumika kwa sababu ya usiri, usalama na kuepuka udhibiti. Hususan VPN inakupa uwezo wa: 1- kutotambulika mtandaoni kwa kuficha anwani na eneo lako, 2- kuzuru tovuti na maudhui yaliyodhibitiwa, 3- ulinzi dhidi ya wadukuzi/majasusi unapotumia mitandao binafsi na ya ummah ya Wi-fi, 4- kulinda taarifa zako binafsi (neno la siri n.k).
Katika zama hizi ambapo mradi wa demokrasia unazama kutoka janga hadi janga, tawala zimeamua kutumia mbinu katili ili kuweza kuhifadhi mamlaka zao. Na katika kufanya hivyo wameweza kufichua uhadaifu ulipo wa kile kinachoitwa uhuru wa kibinafsi na uhuru wa maoni ambayo ni sehemu katika nguzo za demokrasia. Haishangazi kwani huko Amerika, wahudumu wa mitandao wanaweza kisheria kurekodi taarifa zako na kuziuza kwa watangazaji au kuzikabidhi vitengo vya ujasusi. Kwa kuongezea nchini Uingereza makampuni ya mitandao na simu yanatakiwa kisheria kurekodi taarifa zote za wateja wao (historia ya kubrowse, jumbe za simu na eneo walipo) na kisha kuzikabidhi vitengo vya Uingereza. Hilo linathibitisha mpango unaofuatwa na dola kuu ya zamani na ya sasa katika kiu chao cha kujilinda dhidi ya hasira za ummah kwa kuwatia hofu. Hali iliyoko kwa mataifa mengine ni ya kusikitisha!
Matumizi ya VPN yataendelea kuzidi kwani mizozo inaendelea kuzikumba serikali za kidemokrasia. Na kuwapelekea watu kutafuta njia na majukwaa mbadala ili kuweza kupaza sauti zao na kuwahesabu watawala wao.
Suluhisho la kimsingi ili kupatikane dunia salama inayotanua ikiwa ndani ya uhesabianaji na upataji taarifa za kweli unaweza kupatikana kupitia kusimamisha Dola ya Kiislamu ya Khilafah kwa njia ya Utume. Serikali ya Kiislamu ambayo haiwafanyii ujasusi raia wake isipokuwa pale itakapokuwa imeamrishwa na Shari’ah (Qur’an na Sunnah) kufanya hivyo tena katika dhurufu maalum kuhusiana na adui. Kwa kuongezea, itajizatiti kuwajenga raia wake kuwa na utambulisho wa Kiislamu. Hivyo basi raia wake watakuwa chini ya ushawishi wa utambulisho wa Kiislamu katika kuyaendea mambo yao ya kila siku.
Raia wanaoshawishiwa na utambulisho wa Kiislamu watajituma kuhakikisha kuwa kuna amani na utulivu ndani ya Khilafah. Kinyume chake yeyote atakayejihusisha na kuleta vurugu atahesabiwa kwa mujibu wa Shari’ah na wala sio kwa kutegemea hawaa za walioko madarakani kama inavyoshuhudiwa leo katika tawala hizi kandamizi duniani kote. Mtawala, Khalifah ni raia kama raia mwingine mbele ya Shari’ah na hana kinga kutokamana na vitendo vyake kama wanavyopewa watawala wa sasa (marais/wafalme/mawaziri wakuu n.k). Khilafah itachora na kutekeleza sera pana itakayowaelekeza raia namna ya kutumia mtandao na huduma zinazaohusiana na teknolojia. InshaAllah.
Imeandikwa kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Ali Nassoro Ali
Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir