Zaka na Madeni ya Baba na Mtoto

بسم الله الرحمن الرحيم

Jibu la Swali

Kwa: Abu Khaled

Swali:

As Salaam Alaikum Wa Rahmatullah Wa Barakatuhu our honourable Sheikh, and warm greetings to you.

Nina swali kuhusu Zaka na madeni, nataraji utakuwa na muda wa kujibu maswali yangu.

Babangu ana madeni mengi. Kwa sasa ni katika desturi zetu kutotafautisha baina ya pesa na madeni ya baba na mtoto. Hii yamaanisha moja kwa moja madeni yake pia ni madeni yangu na sote tunafanya kazi kwa ajili ya kuyalipa. Vipi ufafanuzi wa hili katika sheria ya Kiislamu, hususan kwa mtazamo wa Zaka? Je, deni hili liko juu ya babangu pekee na amewekwa huru kutokana na utoaji Zaka au sote twalazimika kulipa deni hili?

Baraka za Allah ziwe kwenu, Allah awahifadhi na pokeeni maamkuzi bora kutoka kwa Mashabab nchini Ujerumani

Jibu:

Wa Alaikum Assalam Wa Rahmatullah Wa Barakatuhu

1- Pesa za baba kwa mujibu wa sheria si pesa za mtoto, na deni la baba sio deni la mtoto, kwa hivyo sharia imemfanya baba kuwa msimamizi wa pesa zake na mtoto kuwa msimamizi wa pesa zake. Sharia imeweka katika pesa za baba haki na majukumu kando na pesa za mtoto. Na ikaweka majukumu katika pesa za mtoto kando na pesa za baba kwa sababu kila mmoja wao ana jukumu huru na mwengine. Kwa mfano, sharia inamuamrisha baba kulipa Zaka katika pesa zake zinapofikia Nisab na kuzungukiwa na mwaka kando na pesa za mtoto. Kwa mtoto pia ni vivyo hivyo. Kwa mfano, mtoto anaruhusiwa kuchuma pesa kama malipo ya juhudi kando na pesa za babake. Kwa hivyo, kila mtu katika Uislamu ana jukumu la kipekee kwa mujibu wa sharia ya Kiislamu.

2- Miongoni mwa dalili zinazo onesha kuwa pesa za mtoto si pesa za baba, na pesa za baba ni tofauti na pesa za mtoto:

  1. A) Mtoto harithi pes azote za baba lakini anashirikiana na wengine katika hilo, Allah (swt) asema: يُوصِيكُمُ اللهُ فِي أَوْلَادِكُمْ لِلذَّكَرِ مِثْلُ حَظِّ الْأُنْثَيَيْن)) “Allah anawahusia kuhusiana na watoto wenu: kwa wa kiume mafungu mawili ya wa kike” [An-Nisa: 11]

Na Yeye (swt) asema: وَلِأَبَوَيْهِ لِكُلِّ وَاحِدٍ مِنْهُمَا السُّدُسُ مِمَّا تَرَكَ)) “Na kwa wazazi wake, kwa kila mmoja wao ni sudusi moja katika mali aliyo iwacha” [An-Nisa: 11]

Allah (swt) amewapa wengine haki ya kushirikiana na baba katika urithi wa mtoto. Hivyo basi, haimkiniki kuwa pesa hizo ziwe milki ya baba wakati wa uhai mtoto wake na kisha baadaye baadhi yake ziwe milki ya mwengine kando na baba huyo. Allah asema katika ayah ya mirathi: وَلِأَبَوَيْهِ لِكُلِّ وَاحِدٍ مِنْهُمَا السُّدُسُ “Na kwa wazazi wake, kwa kila mmoja wao ni sudusi moja katika mali aliyo iwacha” [An-Nisa: 11]. Kwa hivyo, Yeye (swt) amempa mamake hisa katika urithi wa mtoto wake baada ya kifo chake. Hivyo basi, kwa kuwa sharia imempa mama hisa katika urithi wa mwanawe, haimkiniki sharia ikadirie pesa za mtoto ziwe mali ya babake.

  1. B) Kabla ya urithi kugawanywa, baba au mtoto aweza kupendekeza na kutekeleza matakwa yanayo mridhisha au yasiyo mridhisha mtoto au baba, na kabla ya hilo deni lake ni lazima lilipwe kabla ya urithi kugawanywa, ishara kuwa mali ya maiti ni yake yeye na wala si pesa za babake au mtoto wake. Allah Azza Wa Jal asema: (مِنْ بَعْدِ وَصِيَّةٍ يُوصِي بِهَا أَوْ دَيْن) “Baada ya wasia (alioacha) au deni” [An-Nisa: 11]

Hivyo basi, kwa kuwa ni wajib kulipa madeni ya mtu kabla ya kugawanya urithi wake, haimkiniki kukadiria kuwa pesa za mtu ni mali ya babake. Zaidi ya hayo, kwa kuwa inaruhusiwa kwa Muislamu kuweka wasia kabla ya kifo chake, haimkiniki kuzikadiria pesa zake kama mali ya babake.

  1. C) Katika Hadith ya kuchinja iliyo pokewa na Ahmad katika Musnad yake kutoka kwa Abdullah Bin Amr aliye sema: mtu mmoja alikuja kwa Mtume wa Allah (saw) na kumwambia: “Nifundishe nami Ewe Mtume wa Allah… naapa kwa yule aliye kutumiliza kwa haki, sitaongeza chochote kwacho, kisha akaondoka, Mtume wa Allah (saw) akasema:

«أَفْلَحَ الرُّوَيْجِلُ، أَفْلَحَ الرُّوَيْجِلُ»، ثُمَّ قَالَ: عَلَيَّ بِهِ، فَجَاءَهُ، فَقَالَ لَهُ: «أُمِرْتُ بِيَوْمِ الْأَضْحَى، جَعَلَهُ اللَّهُ عِيدًا لِهَذِهِ الْأُمَّةِ»، فَقَالَ الرَّجُلُ: أَرَأَيْتَ إِنْ لَمْ أَجِدْ إِلَّا مَنِيحَةَ ابْنِي، أَفَأُضَحِّي بِهَا؟ قَالَ: «لَا، وَلَكِنْ تَأْخُذُ مِنْ شَعْرِكَ، وَتُقَلِّمُ أَظْفَارَكَ، وَتَقُصُّ شَارِبَكَ، وَتَحْلِقُ عَانَتَكَ، فَذَلِكَ تَمَامُ أُضْحِيَّتِكَ عِنْدَ اللَّهِ

“Amefaulu mtu huyu, amefaulu mtu huyu” kisha akasema (saw): mleteni kwangu, mtu huyo alipokuja, yeye (saw) akamwambia: “nimeamrishwa kuadhimisha Siku ya Adh’ha, Allah ameijaalia kuwa sherehe (Idd) kwa Umma huu” mtu huyo akasema: ikiwa sina chochote cha kuchinja isipokuwa mtoto wa ngamia je nimchinje? Yeye (saw) akasema: “La, lakini nyoa nywele zako, na kata kucha zako, na punguza masharubu yako, na nyoa sehemu nyeti zao, hio itakamilisha udh’hiya yako mbele ya Allah.”  Abu Dawud amepokea riwaya sawia na hii na pia katika Sharh Maany Al Athar. Ad-Darqutny amepokea katika Sunnan yake katika riwaya: (Mtu huyo akasema: ikiwa sitapata chochote isipokuwa ngamia au kondoo wa babangu na familia yangu na kisha nimchinje? Yeye (saw) akasema: «لَا وَلَكِنْ قَلِّمْ أَظْفَارَكَ وَقُصَّ شَارِبَكَ وَاحْلِقَ عَانَتَكَ فَذَلِكَ تَمَامُ أُضْحِيَّتِكَ عِنْدَ اللَّهِ» “La, kata kucha zako, na kata masharubu yako, na nyoa sehemu nyeti zako, hii itakamilisha udh’hiya yako mbele ya Allah.”

Na kwa kuwa si ruhusa kwa baba kuchinja (udh’hiya) ngamia wa mwanawe au mwana kuchinja ngamia wa babake, hii inamaanisha kuwa pesa za baba si pesa za mtoto,

  1. D) Katika Mawahib Al-Galileel Fi Sharh Mukhtasar Khalil (2/505), kilicho andikwa na: Shams Ad-Din Abu Abdullah Muhammad Bin Muhammad Bin Abdul Rahman At-Tarabolsi Al-Maghribi, anaye julikana kama Hattab Al-Ru’ini Al-Maliki (aliye kufa: 954 AH):

“(tisa) Ikiwa ana deni basi hili litapewa kipaumbele kuliko Hajj pasi na ikhtilafu bali ataipa kipaumbele Hajj juu ya deni la babake, ima tukisema: Hajj moja kwa moja au kwa kasi yake, na ima ulipaji deni utacheleweshwa au litalipwa mara moja. Hili limetajwa katika At-Tiraz na nasi yenyewe ni: ‘ikiwa ana deni na pesa, ni bora kulipa deni kuliko Hajj, Malik amesema katika Al Muwaziyah. Aliambiwa: ‘Ikiwa babake ana deni, alipe deni hilo au aende Hajj’. Akajibu: ‘Afanye Hajj na hili liko wazi kwa sababu Hajj ni deni lake, moja kwa moja au kwa kasi yake mwenyewe, na deni la babake sio jukumu lake, si moja kwa moja wala kwa kuakhirishwa. Ubebaji jukumu unapiku lile ambalo si jukumu’ (mwisho wa nukuu).

3- Kwa hivyo Hadith ya (wewe na pesa zako) imeeleweka:

Katika Sharh Mushkil Al-Athar: (Kutoka kwa Jabir Bin Abdullah kwamba mtu mmoja alikuja kwa Mtume (saw) na kusema: nina pesa na watoto, na babangu ana pesa na watoto, na anataka kuchanganya pesa zetu, hapo Mtume (saw) akasema: «أَنْتَ وَمَالُكَ لِأَبِيكَ»“Wewe na mali yako ni vya babako”

Nilimuuliza Bin Abi Imran kuhusu Hadith hii, akasema: maneno katika Hadith hii ya Mtume (saw): «أَنْتَ وَمَالُكَ لِأَبِيكَ»“Wewe na mali yako ni vya babako” ni kama maneno ya Abu Bakar (ra) kwa Mtume (saw): “Lakini pesa zangu na mimi mwenyewe ni milki yako, Ewe Mtume wa Allah.” Ambapo Mtume alimwambia, «مَا نَفَعَنِي مَالٌ مَا نَفَعَنِي مَالُ أَبِي بَكْرٍ» “Nimenufaika pakubwa kutokana na mali ya Abu Bakar” Inarudi kwa Hadith ya Abu Huraira ambapo amesema: Mtume (saw) amesema: «مَا نَفَعَنِي مَالٌ قَطُّ مَا نَفَعَنِي مَالُ أَبِي بَكْرٍ» “Nimenufaika pakubwa kutokana na mali ya Abu Bakar”

Amesema: Abu Baker, (ra) alisema: “Lakini pesa zangu na mimi mwenyewe ni milki yako, Ewe Mtume wa Allah.” Kwamba Abu Bakar atatekeleza maagizo na maamrisho yote ya Mtume kwake mwenyewe na kwa mali yake kama ilivyo kwa wamiliki wa vitu ambapo wana mamlaka kamili juu ya wanavyo vimiliki. Na haya yalikuwa ndio maneno ya mtu yule aliye uliza katika Hadith ya hapo juu na yanabeba maana sawa, na Allah ni mjuzi Zaidi.

Vile vile, imepokewa na Ibn Habban katika Sahih yake: (Kutoka kwa ‘Aisha (ra) kwamba mtu mmoja alikuja kwa Mtume wa Allah (saw) ambaye alikuwa na ugomvi na babake kuhusu deni la babake. Mtume (saw) akamwambia: «أنت ومالك لأبيك» “Wewe na mali yako ni vya babako”. Abu Hatim asema maana yake ni kuwa Mtume alimkemea mtu huyo kutokana na kumchukulia babake kama mgeni kwake, na kumuagiza kuonyesha ulaini na upole kwa maneno na vitendo mpaka apate pesa zake, na akamwambia kwamba yeye na pesa zake ni vya babake, sio kwamba pesa za mtoto ni milki ya baba huyo maishani mwake pasi na ridhaa yake. Ibn Raslan asema: (Herufi ‘Lam’ ni ya kuruhusu na wala si ya mali, lakini pesa za mtoto ni mali yake na ni lazima azilipie Zaka na zinarithiwa kutoka kwake.)

4 – Hivyo basi, unalipa Zaka juu ya pesa zako, na babako atalipa Zaka juu ya pesa zake ikiwa itafikia Nisab na kuzungukiwa na mwaka ikiwa hakuna deni juu ya pesa hizo. Ikiwa atalipa deni, aweza kulipa Zaka kwa pesa zitakazo bakia ikiwa zitakuwa zaidi ya Nisab kwa sababu rai yenye nguvu tunayo fuata ni kuwa deni humueka huru mtu kutokana na Zaka ikiwa pesa zote zimetumika au zinazo bakia zitakuwa kidogo kuliko Nisab. Katika kitabu chetu “Mali Katika Dola ya Khilafah”, tunapo zungumzia kuhusu Zaka ukurasa 150, yafuatayo yametajwa:

(Yeyote aliye na mali, ambayo imefika Nisab na kuzungukiwa na mwaka, na ana deni linalo kula Nisab yote au linalo pelekea mali inayo bakia baada ya kulipa deni kuwa kidogo kuliko Nisab halipi Zaka yoyote. Kwa mfano, ikiwa mtu atamiliki Dinar 1,000 na kudaiwa Dinar 1,000, au ikiwa mtu anamiliki Dinar za dhahabu 40 na ana deni la Dinar za dhahabu 30, hakuna Zaka juu yake katika hali mbili hizi kwa kuwa hamiliki Nisab. Kutoka kwa Nafi kutoka kwa ibn ‘Umar aliye sema: Mtume wa Allah (saw) amesema: «إذا كان لرجل ألف درهم، وعليه ألف درهم، فلا زكاة عليه» “Ikiwa mtu ana Dirham elfu moja, na juu yake ana deni la Dirham elfu moja, basi hakuna Zaka juu yake.” Imetajwa na Ibn Qudama katika Al Mughni.

Pindi mali, baada ya kulipa deni, itafikia Nisab, basi Zaka itawajibika juu yake kutokana na yale yaliyo simuliwa na As-Saib b. Yazid aliye sema: Nilimsikia Uthman b. Affan akisema: “Huu ni mwezi wa Zaka yenu. Yeyote aliye na deni alilipe ili ulipe Zaka juu ya mali yako.” Katika riwaya nyengine, iliyotajwa na Ibn Qudama katika Al Mughni: “Yeyote aliye na deni alilipe na kisha kulipa Zaka juu ya mali iliyo bakia.” Alisema haya mbele ya Maswahaba ambao hawakulipinga hili; hivyo, hii inaashiria makubaliano yao ya pamoja (Ijma’a). Huo ndio mwisho wa nukuu kutoka kwa kitabu Mali katika Dola ya Khilafah.

Kwa hivyo, ikiwa baba au muulizaji ana pesa zilizo fikia nisab na kuzungukiwa na mwaka na ana deni, basi atoe deni hilo kutokana na pesa zake. Ikiwa deni hilo litachukua pesa zote, au ikiwa kiwango kitakacho bakia ni kidogo kuliko Nisab, atakuwa huru kutokana na kulipa Zaka. Ikiwa pesa zake zinazo bakia ni zaidi ya Nisab, basi atalipa Zaka juu ya pesa zile zitakazo bakia baada ya kuondoa deni.

Ama kuhusu watoto wa mwenye deni “baba”, hawawajibiki kulipa deni hilo kama ilivyo fahamika kutokana na swali hili, bali ni deni juu ya baba yao na ni wajibu wake sio wao. Wanachokifanya ni kumsaidia baba yao kulipa deni lake ambalo ni jambo la wema kwa wazazi (Bir al-walidain). Jambo ambalo Uislamu unalishajiisha kwa uzito, (وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا) “… na kuwatendea wema wazazi wawili” [Al-Isra’: 23]

Al-Bukhari amepokea

عن عَبْدُ اللَّهِ بْنُ مَسْعُودٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ: سَأَلْتُ رَسُولَ اللَّهِ (ص) قُلْتُ: يَا رَسُولَ اللَّهِ، أَيُّ العَمَلِ أَفْضَلُ؟ قَالَ: «الصَّلاَةُ عَلَى مِيقَاتِهَا»، قُلْتُ: ثُمَّ أَيٌّ؟ قَالَ: «ثُمَّ بِرُّ الوَالِدَيْنِ»، قُلْتُ: ثُمَّ أَيٌّ؟ قَالَ: «الجِهَادُ فِي سَبِيلِ اللَّهِ

Kutoka kwa Abdullah bin Masood (ra): Nilimuuliza Mtume wa Allah (saw): Ewe Mtume wa Allah, ni kitendo gani bora? Akasema: “kuswali kwa wakati wake”, nikasema: Kisha ni kipi? Akasema: «Kisha kuwatendea wema wazazi wawili », nikasema: Kisha ni kipi? Akasema: Jihad katika njia ya Allah.”

Hivyo basi, usaidizi wa watoto kwa baba yao ni jambo la wema kwa wazazi, lakini watoto wana jukumu la Zaka juu ya pesa zao baada ya kulipa deni lao. Ikiwa pesa zao zitafikia Nisab na kuzungukiwa na mwaka, ni lazima walipe zaka juu ya pesa zao. Ikiwa watamlipia deni baba yao kutokana na pesa zao kabla ya mwaka kukamilika, basi hawatalipa Zaka juu ya pesa hizo kwa sababu lilitolewa kutoka kwa pesa zao kabla ya jukumu la Zaka juu yake, na watawajibika kulipa Zaka juu ya pesa zilizo bakia baada ya kulipa deni hilo ikiwa pesa zinazo bakia zitafikia Nisab au zaidi yake na kuzungukiwa na mwaka.

Ndugu yenu,

Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah