Ukatili wa Kijinsia ni Natija ya Sera ya Usawa wa Kijinsia ya Kimagharibi

Mnamo Jumatano, 30 Juni 2021, Rais Uhuru Kenyatta alikemea kukithiri kwa idadi kubwa ya ukatili wa kijinsia barani Afrika, kwa kusema kuwa viwango vimefikia vya dharura duniani. Alizungumza hivyo katika majadiliano ya jopo katika ufunguzi wa kikao cha Kongamano la Kizazi Sawa (GEF) huko Paris, Ufaransa. GEF ni mjumuiko wa kimataifa wa usawa wa kijinsia ulioitishwa na Wanawake wa Umoja wa Mataifa na mwenyeji wake wakiwa ni Mexico na Ufaransa. Suluhisho alisema ni kuweka sera na kanuni madhubuti zenye kupambana na janga hili pamoja na kuzidisha ufadhili katika kulitatua. (The Standard, 30/06/2021)

Rais alisema kwamba Cameroon ina asilimia 35, South Afrika asilimia 37, Jamhuri ya Afrika ya Kati asilimia 50, Liberia asilimia 50 na Kenya asilimia 50 za viwango vya ukatili wa kijinsia na kwamba zimerekodi idadi kubwa hususan katika miezi kumi na mbili iliyopita ndani ya hichi kipindi cha Covid-19. Itakuwa ni ukosefu wa akili kujadili natija au matunda ya mti pasina kuwekeza umakini kwa mizizi yake. Kwa maana nyingine ni muhimu kufahamu chanzo cha janga la hili la ukatili wa kijinsia na kujua ni njia ipi sahihi ya kutatua tatizo hili. Hivyo basi, ni vyema kudadisi historia ya mwito wa kijinsia ili tujue mwanzo wake na mpaka ilipofikia hivi sasa.

Christine de Pizan alizaliwa kama mtoto wa pekee 1364 M mjini Bologna, Italia na kukulia, kuishi na kufariki 1430 M mjini Paris, Ufaransa. Babake, Tommaso di Benvenuto da Pizzano aliyejulikana kama Thomas de Pizan alikuwa ni daktari, mtu wa kutabiri siku zijazo na mshauri katika baraza la Venice huko Italia.  Babake aliteuliwa kuwa mtabiri wa ziku zijazo wa mfalme Charles wa Tano wa Ufaransa na kuhamia Paris, Ufaransa. Mwaka 1368 M Christine alihamia Ufaransa na mwaka 1379 M akiwa na miaka 15 aliolewa na mthibitishaji na katibu wa ufalme Etienne du Castel.

Mwaka 1389 M mumewe Christine alifariki na mwaka kabla yake babake alikuwa amefariki. Kwa hiyo, Christine alilazimika kuwasimamia mamake pamoja na watoto wake watatu aliokuwa amewazaa. Aliisimamia familia yake kwa mali chache aliyoiwacha mumewe na kupitia malipo ya uandishi wake. Mwaka 1405 M aliandika kitabu kwa jina Kitabu cha Mji wa Wanawake kikiwa ni jibu kwa kitabu kilichoandikwa na kiongozi wa kanisa na mtunzi wa mashairi Mathieu wa Bologna kikiitwa Maombolezo ya Matheolus. Mathieu kupitia kitabu chake alidai kuwa ndoa / ‘wanawake’ wanawafanya wanaume kuishi maisha duni. Christine kupitia kitabu chake aliwatetea wanawake kwa kudai kuwa ndoa baina ya mwanamume na mwanamke ni ushirika wa usawa, na kuwataja wanawake kadhaa kama mfano wa kuigwa. Pia aliongezea kuwa wanawake wamekuwa nyuma katika kila nyanja ya maisha kutokana na mpangilio wa mujtama unaompa kipaumbele mwanamume na kumtelekeza mwanawamke.

Christine de Pizan alikuwa ni katika watu wa tabaka la juu katika mujtama zama zake. Baada ya kuchapishwa kitabu chake hicho na vinginevyo ndipo alipoanza kuingia katika mvutano na viongozi wa makanisa karne hizo. Viongozi wa makanisa walimpinga kwa kuwa walibeba imani kwamba lengo la ndoa ni kuendeleza kizazi na kwamba mujtama wao uliokuwa umetawaliwa na wanaume na kuwataka wanawake kujisalimisha. Tokea zama hizo Christine de Pizan amekuwa akirudiwa na kuwa kiigizo cha wanaharakati na kila anayedai kutetea haki sawa za wanawake katika zama hizi ambapo mwito wa usawa wa kijinsia umeshamiri duniani kote.

Usawa wa kijinsia unaopigiwa debe na wa Magharibi hivi sasa duniani kote na ambao eti unalenga kuwakomboa wanawake katika utumwa wa kisiasa, kiuchumi, kijamii na kielimu. Ukombozi huo unaolenga kuwapa wanawake uhuru usiokuwa na mipaka ili kufikia malengo yao kwa mujibu wa akili zao zinavyowatuma. Muasisi wa ukombozi wa wanawake leo karne ya ishirini ni Muamerika Betty Friedan, anayatambulika kwa kitabu chake kiitwacho Siri ya Uke. Kupitia kitabu chake anadai kwamba lau wanawake wa nyumbani wa Amerika watachangamkia taaluma za kudumu, watakuwa na furaha na afya zaidi, ndoa bora na watoto wao watastawi.

Madai yake hayo ni kinyume na hali halisi ilivyo kwa kuzingatia takwimu zenye kutamausha na zinazoendelea kuzidi. Takwimu zinafichua mporomoko wa maadili, kuvunjika kwa familia, kuzidi kwa uzinifu na maovu mengi yote yakisababishwa na miito ya ‘usawa wa kijinsia’ ulimwenguni. Wanadamu wamevuka mipaka na kuwa kama wanyama! Hakuna haya wala stara kwani kila mmoja anakwenda mbio kufikia usawa wa kijinsia. Kiasi kwamba wanawake wanatembea uchi wakidai miili yao chaguo lao!

 

Tukitoa mifano baadhi ya matukio nchini Kenya, tafiti za miaka ya karibuni zinaonesha vurugu za ndani ya majumba zinaendelea kuzidi kila uchao. (The Star, 06/04/2021) Katika Kaunti ya Kirinyaga mnamo Jumatatu, 28 Juni 2021 makasisi kutoka katika kanisa la Anglican waliweka wazi kwamba kuna ongezeko la visa vya mizozo ndani ya majumba huku wanaume wakidaiwa kupigwa na kufurushwa na wake zao. (k24tv.co.ke, 28/06/2021) Kwa kuongezea huko Kaunti ya Embu, wanaume ndani waliooa walipaza sauti zao kuwa wanadhulumiwa kimwili na kukosa haki zao za ndoa. Samuel Muturi ambaye ni mwenyekiti wa kikundi cha Inua Wazee alisema kwamba ‘Tunakabiliwa na wakati mgumu ndani ya familia zetu; hatufurahii ndoa. Tunaiomba serikali kuwawezesha wanaume na kuweka mpango sawa katika kuamiliana wanaume na wanawake ndani ya kaunti.” (The Star, 03/06/2021) Ama tukivuka na kwenda nchi jirani na ng’ambo hususan katika mataifa yanayodai kuwa zimeendelea katika kuwapa raia wake uhuru kama Amerika, Ufaransa, Uingereza, Ujerumani n.k. Mashaka na vilio vimeshamiri pasina kupatikana suluhisho msingi!

Hali hizo za mashaka na vilio zitaendelea kuwa hivyo kwa sababu wanadamu wamejitenga na muongozo wa Muumba wao (swt). ﴿ َمَنۡ أَعۡرَضَ عَن ذِڪۡرِى فَإِنَّ لَهُ ۥ مَعِيشَةً۬ ضَنكً۬ا وَنَحۡشُرُهُ ۥ يَوۡمَ ٱلۡقِيَـٰمَةِ أَعۡمَىٰ﴾ “Na atakaye jiepusha na mawaidha yangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na Siku ya Kiyama tutamfufua hali ya kuwa kipofu.” [20. Ta Ha: 124]. Katika mchakakato wa kupigia debe usawa wa kijinsia wa Magharibi pamoja na watawala vibaraka ulimwenguni wamefaulu kumakinisha fikra za mujtama huria. Wahanga wakubwa wakiwa ni Waislamu walioweza kuupiga vita Uislamu kwa kuitukuza itikadi ya kisekula yenye kutenganisha dini na maisha. Wakiona kwamba kufanya hivyo ndio kuendelea, kufaulu na kuwapatia umaarufu. Kinyume chake ni kuzama ndani ya makaa ya moto wa kihuria!

Leo imefikia kiasi cha wazee kwa vijana Waislamu kutekwa nyara kifikra na wa Magharibi kwa sura eti ya kuwakomboa kwa kuwapa elimu ya kisekula. Kisha hatimaye kuwapa tuzo za kimatiafa na dori ya kuwa mabalozi wa usawa wa kijinsia na elimu ya kisekula ulimwenguni. Ili kufikia malengo yao hutoa kauli hadaifu zenye kupiga vita taasisi ya ndoa. Kwani ndoa ni moja katika mawe msingi katika ujenzi wa mujtama na kizazi kwa ujumla. Lengo likiwa ni kuhakikisha watu wanabakia kuwa kama wanyama wanaoshiriki ufuska kwa shinikizo la usawa wa kijinsia na kufurahia uhuru wao.

Mfano ni kauli ya hivi majuzi ya mwanaharakati na mshindi wa tuzo ya Amani ya Nobel, Malala Yousafzai alisema, “Bado mimi sielewi kwa nini watu wanapaswa kuoana. Ikiwa unataka kuwa na mtu katika maisha yako, kwani yapasa muweke saini karatasi za ndoa, kwa nini isiwe tu ni ushirika?” Hayo yakiwa ni sehemu ya matamshi yake katika mahojiano na Jarida la Vogue Toleo la Julai 2021. (www.vogue.co.uk, 01/06/2021) Na kupitia matamshi kama hayo kutoka kwa wanaodaiwa ni watetezi wa ukombozi wa wanawake ambao wameandaliwa na kuwekewa mazingira ikiwemo pamoja na kupewa fursa na vyombo vya habari vya wa Magharibi ili kuendeleza fikra za mujtama huria.

Hakika vurugu za kijinsia hazikuwahi kushuhudiwa chini ya utawala wa Dola ya Kiislamu. Kwani Uislamu ukiwa ni mfumo kamili wa maisha unaotoka kwa Muumba wa ulimwengu, mwanadamu na uhai. Umepangilia kwa makini majukumu na haki za mwandamu katika uhai wake. Vile vile Muumba akawaumba wanadamu kwa jinsia ya kike na kiume ili iwe ni rehema kwa wanadamu na wala sio kwa ajili ya kusababisha vurugu kama inavyoshuhudiwa leo chini ya mfumo batili wa kirasilimali.﴿وَمِنۡ ءَايَـٰتِهِۦۤ أَنۡ خَلَقَ لَكُم مِّنۡ أَنفُسِكُمۡ أَزۡوَٲجً۬ا لِّتَسۡكُنُوٓاْ إِلَيۡهَا وَجَعَلَ بَيۡنَڪُم مَّوَدَّةً۬ وَرَحۡمَةً‌ۚ إِنَّ فِى ذَٲلِكَ لَأَيَـٰتٍ۬ لِّقَوۡمٍ۬ يَتَفَكَّرُونَ﴾ “Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao fikiri.” [30. Ar-Rum: 21] Kwa hiyo uumbaji wa jinsia ya kike na kiume sio kwa ajili ya kuleta ushindani na mizozo badala yake ni kuletea utulivu na amani katika mujtama kupitia mume na mke kuoana kwa mujibu wa Shari’ah ya Kiislamu.

Uislamu unawahesabu mwanamume na mwanamke kuwa wako sawa mbele ya Shari’ah. Zaidi ya hayo Uislamu ukawapa haki sawa mwanamume na mwanamke ikiwemo haki za kushiriki katika kumchagua mtawala, kumiliki mali, kuajiri, kuajiriwa, kufanya biashara n.k. Haki ambazo kiasili zimekuwepo kwa takribani zaidi ya karne 13 na zitabakia mpaka Siku ya Kiyama. Wakati wa Magharibi wamezama ndani ya kiza cha mporomoko wa kihadhara, mwanamke alikuwa ni mtumwa anayetumika kama chombo cha kujistarehesha asiyekuwa na haki ya kushiriki uchaguzi (kuchagua au kuchaguliwa), kumiliki mali, kuajiriwa, kuajiri n.k. Ilhali upande wa pili, wanawake katika Uislamu walikuwa wanashiriki kikamilifu katika siasa ya kiwango cha juu katika mfano ni kumpa mkono Mtume(saw) katika kiapo cha ahadi ya utiifu (Ba’yah al-Aqaba) kuwa mtawala wao. Miongoni mwa walioshiriki ni wanawake wawili ambao ni Umm Umara Nasiba na ambaye alikuwa akifanya kazi kama muuguzi na Umm Mani, Asma. Wanawake wengine wengi wamewapa Ba’yah makhalifah na kushiriki upiganaji ‘Jihad’ kuilinda Dola ya Kiislamu kwa karne nyingi mno.

Ama upande wa haki za kielimu, wanawake wengi akiwemo Umm al-Darda al-Kubra (ra). Alikuwa ni mwanachuoni bingwa katika Karne ya Saba huko Sham. Alifundisha katika sehemu ya wanaume msikitini na alikuwa mwalimu wa hadith na fiqh. Miongoni mwa wanafunzi wake alikuwa ni Khalifah Abd al-Malik ibn Marwan. Mwingine ni Hafsa bint Sirin (rh) miongoni mwa tabieen alikuwa mwanachuoni aliyeishi na kufunza huko Basra. Fatima bint Muhammad al-Fihriyya al-Qurashiya alikuwa ndiye muasisi wa Msikiti wa al-Qarawiyyin mnamo 859 M. Msikiti ambao baadaye ulikuwa ni taasisi ya masomo na inayotambulika kuwa chuo kikuu cha kwanza duniani.

Kiuchumi wanawake wameruhusiwa na Shari’ah kuajiriwa, kuajiri, kufunga mikataba, kuwakilisha/kuwakilishwa katika mikataba ya kibiashara, kushiriki kilimo n.k. Lakini suala zima la uchumaji kwa ajili ya kuisimamia familia ni jukumu la babake, mumewe au msimamizi wake na sio mwanamke mwenyewe. Kufanyakazi kwa mwanamke sio lazima japo ameruhusiwa na Shari’ah (mubah). Mshahara au malipo yake ni yeye ndiye anayeamua atakavyotumia kwa mujibu wa kipimo cha halali na haramu na hashurutishwi kufanya kazi wala kutoa matumizi. Mwanamke ni tunu inayostahiki, kuheshimiwa, kulindwa na kuhifadhiwa kutokana jukumu muhimu alilopewa na Muumba. Mwenyezi Mungu (swt) amempa jukumu la kuwa mke na mama. Ambaye kazi zake ni ndani ya nyumba yake ni kazi za nje zikiwa za mumewe.

Kinyume chake leo mwanamke ametolewa ndani ya nyumba yake na kufanywa mtumwa wa hawa’a za nafsi yake. Kwa kujisalimisha kwa mchoro wa Magharibi wamiliki wa makampuni na viwanda vinavyokwenda mbio kupatiliza idadi kubwa ya wanawake duniani. Eti naye mwanamke amekuwa anapigana vikumbo na wanaume katika uchumaji tonge la familia. Huku akili yake na mawazo yake ni kumpiku mumewe katika uchumaji ili awe ndiye mwenye usemi na kuendesha mambo ndani ya familia! Watoto na majumba yakitelekezwa kupindukia. Katika mchakato huo wanawake wanapigiwa debe na kusifiwa na vyombo vya habari na kupongezwa eti ni wanawake wachapakazi shupavu na mfano wa kuigwa. Na wakati huo huo vikidunisha umama kuwa ni mzigo na kikwazo kwa mwanamke kutofurahia maisha na uhuru wake. Si hayo tu, kila kukicha kunazuka mapya, kiasi kwamba leo imefikia hata mwanamke kuamua siku ya kukutana na mumewe na kinyume chake mara mwanamke anamshitaki mumewe kwa kosa la kumbaka! Ilhali ni haramu kwa mke kutoitikia ombi la mumewe anapomuhitaji katika malazi!

Natija yake ni maangamivu ya kupindukia yanayoendelea hadi sasa na yanayoshuhudiwa na kila mmoja duniani. Kusita kwa hali hii ni pale ambapo wanadamu na hususan Waislamu duniani watakapozinduka na kuona kuwa usawa wa kijinsia ni fikra potofu na hatari kwa mujtama. Hatimaye washikamane na kujiunga na harakati yenye kufanyakazi ya kuregesha tena maisha ya Kiislamu kwa kusimamisha Serikali ya Kiislamu ya Khilafah kwa njia ya Utume. Ni kupitia Khilafah ndipo mwanamke atakuwa ni tunu ya kweli yenye kustahili kuheshimiwa, kulindwa na kuhifadhi. Jukumu la umama litapewa cheo na kufanyiwakazi barabara ili kuandaa kizazi chenye utambulisho (shaksiyyah) madhubuti wa Kiislamu. Kizazi ambacho kitamtwii Mwenyezi Mungu (swt) na Mtume wake (saw) na kuwaheshimu na kuwaenzi wazazi wao kwa kwa kujisalimisha kwa maamrisho na makatazo ya Mwenyezi Mungu (swt).

Khilafah pekee ndio yenye uwezo wa kukomesha kimsingi ukatili wa kijinsia kwa kuwafurusha wa Magharibi wakoloni kutoka katika ardhi za Waislamu na kuitupilia mbali hadhara yao iliyojikita katika itikadi ya kutenganisha dini na maisha / serikali. Khilafah itakwenda mbio kuwaandaa na kuwajenga mabinti shupavu wenye kuthamini haki na kuridhika na majukumu msingi waliowekewa na Mwenyezi Mungu (swt). Napia kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika nyanja za maisha ikiwemo kuwa wavumbuzi na wanachuoni mahiri. Na wala sio kuwafanya kuwa kizazi cha Z kama kinavyojulikana hivi sasa. Kizazi kinachotambulika kwa sifa ya kuogolea ndani ya bahari ya uhuru wa kupindukia!

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir