Kumekuwa na vilio vya kudai ‘mabadiliko katika sekta ya elimu’ ndani ya Kenya tangu Fred Matiang’i alipochukua hatamu katika Wizara ya Elimu mwaka jana. Amejitahidi kwa kiasi fulani kujaribu kuondosha muozo uliokuwa unaikumba nidhamu ya mitihani nchini. Ama kuwa amefaulu au la hilo ni suala la kujadiliwa siku nyingine. La muhimu ni ndani ya muhula huu kunatarajiwa kuanza rasmi kwa mtaala mpya wa elimu; ambao unatarajiwa kuchukua nafasi ya ule unao kashifiwa wa 8-4-4. Mpangilio huu ambao umetumika kwa miongo mitatu uliweka miaka minane kwa elimu ya msingi, miaka mine kwa elimu ya shule ya upili na kwa miaka mine kwa elimu ya chuo kikuu. Kwa sababu hiyo mtaala huo ukachukua mahala pa mtaala wa 7-4-2-3 ambao ulikuwa unashtumiwa kuwa ni wa kikoloni na unaochangia kuwepo kwa matabaka. Ripoti kutoka kwa Taasisi ya Mitaala ya Elimu Kenya (KICD) inaashiria kuwa mtaala mpya umepangilia ngazi tatu; Elimu ya Miaka ya Mwanzo, Elimu ya Katikati na Elimu ya Wakuu. Hata hivyo imependekeza kuwepo mpangilio wa 2-6-3-3-3 wa elimu ambao wanasema utahakikisha wasomi wanapata uwezo na taaluma ya kuweza kufikia matarajio ya uajiri ndani ya Ruwaza 2030. Mkurugenzi wa KICD Juliua Jwan alisema kuwa “mtaala huo utapunguza mzigo na utabadilisha mpangilio wa kusoma na kuwafanya wasomi waweze kujitambua kwa misingi ya Demokrasia ya taifa hili, kitu ambacho mtaala uliopo sasa haujatatua” (Daily Nation ya 1 January, 2017)
Lawama na vilio vilishamiri punde tu baada ya kutangazwa matokeo ya Mtihani wa Shule za Upili ya Kitaifa (KCSE) ya Mwaka 2016. Hii inaashiria hali mbili yawezekana kuwa ni ukweli kutoka kwa washika dau wanaoijali sekta ya elimu au ikawa ni magenge ya wezi wa mitihani wakijaribu kulipiza kisasi. Kama ilivyoripotiwa na gazeti la Daily Nation la 3 Januari, 2017, kuwa Muungano wa Walimu wa Baada ya Shule za Msingi (KUPPET) kupitia Katibu Mkuu – Akello Misori ameyakosoa matokeo ya KCSE yaliyotolewa Disemba. Alisema kuwa; “hali ya kawaida ilitarajiwa kuonyesha waliopita wachache na idadi kama hiyo ikiwa chini, na wengi wakiwa katikati. Hali isiyokuwa ya kawaida imeashiria kuwa matokeo ya 2016 sio ya kutegemewa.” Akaongezea kusema kuwa walimu watataka uchunguzi ufanywe juu ya kutayarishwa mitihani na hali ya ilivyo ilivyomakiwa/alama zilivyopeanwa. Hii ni baada ya malalamishi kutolewa kuwa mitihani ilimakiwa haraka haraka.
Muhanga mwingine katika matoleo hayo ni mpango wa shahada za sambamba (Parallel Degree Programmes) ambao unapatikana katika vyuo vikuu. Fred Matiang’I alitangaza kuwa vyuo vikuu vya umma vitachukua moja kwa moja wanafunzi wote 88,929 waliopata alama ya C+ na zaidi katika KCSE. Zaidi ya wanafunzi 44,000 waliopata C na walitarajia kujiunga na vyuo vikuu kupitia mpango wa shahada za sambamba au kujiunga katika taasisi za kibinafsi wametupwa nje ya mipango ya shahada baada ya ishara za mapema kuwa alama za kuchaguliwa kusomea kozi tofauti tofauti hazitapunguzwa. Kozi hizi zimetumika na vyuo vikuu kupata mabilioni ya fedha kutokana na wanafunzi wengi kutopata nafasi za kujiunga na vyuo vikuu vya umma kupitia mpango wa kawaida wa usajili. Vyuo vikuu vimetumia rasilimali nyingi idadi kubwa ikiwa zimekopwa ili kubuni matawi ya vyuo hivyo ili kuweza kutosheleza mahitaji ya elimu ya juu yanayoongezeka kila mwaka kutoka na kujisajili maelfu ya watu kwa masomo ya jioni.Kwa mfano katika mtihani wa KCSE wa 2015 wanafunzi 165,766 walipata alama ya CT na zaidi zilizo watosheleza kujiunga chuo kikuu. Hata hivyo ni wanafunzi 74,384 pekee waliochaguliwa kujiunga na vyuo vikuu vya umma kutokana na uhaba wa nafasi hivyo kupelekea wanafunzi 91,377 kujiunga katika vyuo vya kibinafsi. Ikiwa idadi kubwa ya taasisi za elimu ya juu, hususan zile zinazojulikana kama matawi yaliyobuniwa na vyuo vya umma na kibinafsi; ni wazi kuwa yako ili kutapeli maanake yako hapo kwa msingi wa kufanya biashara tu na si kama taasisi za kusomesha.
Ni wazi kuwa kwa muda mrefu sasa tumekuwa na nidhamu ya kiujanja ya mitihani ambapo uizi wa mitihani umekuwa ni jambo la kawaida. Shule, wazazi na walimu wamekuwa wakishirikiana na maofisaa wa Baraza la Mitihani la Kitaifa (KNEC) kuiba mitihani. Ambayo hatima yake ni kupatikana kwa alama nyingi za juu ambazo haziwezi kuhimili vipimo. Ushahidi ulikuwa umeanza kuwa mwingi ukiashiria kuwa watahiniwa wengi waliopata alama nyingi wanaanguka wanapofika chuo kikuu. Nusu ya wanafunzi zaidi ya 50,000 ya wanaohitimu shahada kila mwaka ndio wanaotimiza viwango vya ajira. Na nusu ya wanaotimiza viwango hivyo haviambatani vigezo hivyo haviambatani na taaluma walizosomea. Baraza la Baina ya Vyuo Vikuu la Afrika Mashariki (IUCEA) ilibainisha kuwa katika utafiti uliofanyika 2014. Matokeo ya utafiti huo yalionyesha kuwa idadi kubwa ya wanaohitimu hawawezi kupata au watapata changamoto katika kupata ajira ya kudumu katika sekta walizosomea. Prof Kubasu, amabye ni mwanaelimu alisema kuwa “Hiyo ni sehemu moja ya shida. Nidhamu nzima ya elimu inatakiwa kufikiriwa tena. Hatuna tena motisha ya kutafuta elimu isipokuwa ni uchu wa kutafuta makaratasi ili tupate ajira. Kwa walimu, ni jambo lakutengeneza fedha nyingi kutoka kwa vyuo vikuu wawezavyo.”https://www.standardmedia.co.ke/article/2000123982/only-half-of-university-graduates-in-kenya-are-ready-for-job-market-study-says.
Suali msingi kwetu kujiuliza ni malengo ya elimu yanatimizwa? Twaona mabadiliko au ni mbinu tu zinatumika kuutuliza umma unahangaika kwa kuuliza masuali? Fikra ya kina inaonyesha kuwa hakuna malengo maalumu yanayofikiwa zaidi ya kutoa waliohitimu kwa viwango vya chini. Mabadiliko pia hayawezikani kutokea katika nidhamu fisadi mpaka mpaka nidhamu yenyewe ifanyiwe mabadiliko. Mabadiliko ya Elimu katika mfumo wa Urasilimali ni vigumu kufanyika kwa hiyo ni vigumu kuyanasibisha na matokeo. Waweza kuwekeza katika elimu bora kwa madaktari lakini haimaanishi kuwa utapata nidhamu nzuri ya huduma ya afya.
Kwa mujibu wa Serikali ya Kiislamu inayotarajiwa kusimamishwa kwa njia ya Utume; sera yake ya elimu kipengele 166 ndani ya kielelezo cha katiba yake kinasema, “ Lengo la elimu ni kujenga muonekano wa kiislamu kifikra na kitabia. Hivyo masomo yote ndani ya mtaala yatakuwa juu ya msingi huu”
Na katika nidhamu ya elimu imeandikwa “Elimu ndio njia ya kuhifadhi tamaduni ya umma ndani ya mioyo ya watoto wake na katika kurasa za vitabu vyake, ima ni katika yaliyomo au yasiyokuwemo ndani ya mtaala. Mtaala wa elimu unamaanisha elimu itapangiliwa kwa mujibu wa sera na kanuni za serikali; na serikali ikiwajibika katika kuitekeleza mfano kuweka umri wa kuanza, masomo na njia ya kusomesha. Ilhali elimu isiyokuwa lazima inawachiwa Waislamu kufunza katika majumba, misikiti, vilabu, kupitia vyombo vya habari na majarida n.k bila kulazimishwa kufuata mpangilio au kanuni zinazofungamana na mtaala wa elimu. Kwa hali zote mbili, hata hivyo Serikali ina jukumu la kuhakikisha kuwa fikra na maarifa yanayofundishwa ima yanatokana na Fikra Msingi ya Uislamu au yamejengwa juu yake.”
Haya ndiyo mabadiliko ya kina yanayoweza kuchukuliwa ili kubadilisha nidhamu ya elimu kutoka katika mfumo wa Urasilimali ambao hauna madhumuni wala maadili bali una tegemea zaidi hisia za kizalendo za serikali. Ni hadi pale umma utakapokubali kuwa mabadiliko makubwa wanayoweza kuyafurahia matunda yake ni kupitia elimu ya kweli ambao mwanzo kabisa ni iwafunze kumtambua Muumba wao. Kisha imfunze mwanadamu lengo la kuumbwa kwake, wapi ametoka, yuko wapi na mwisho kabisa yuwaenda wapi. Haya ndiyo mabadiliko tunayotakiwa tuyatamani.
Kassim Aggesa – Mwanachama Katika Kamati ya Mawasiliano
Hizb ut-Tahrir Kenya
Kutoka Jarida la UQAB Toleo 1