Sheikh. Ata Abu Rashta (Ameer)

Sheikh Abu Yaseen Ata ibn Khaleel Abu Rashtah, (alizaliwa mnamo 1943 kijiji cha Ra’na, Hebron, Palestina); ni msomi wa Fiqh ya Kiislamu, mwanachuoni na mwandishi. Yeye ndiye amiri wa sasa wa kiulimwengu wa chama cha kisiasa cha Kiislamu Hizb ut Tahrir.

Sheikh Ata ni mwanachuoni nadra sana wa Kiislamu. Alizaliwa katika familia iliyoshikamana na Uislamu mnamo 1943 katika kijiji kidogo cha Ra’na eneo la Hebron nchini Palestina. Alishuhudia uharibifu wa kwanza wa Israel wa Ra’na mnamo 1948 na baada ya hapo kuhama na familia yake kwenda katika kambi ya wakimbizi iliyoko karibu na Hebron.

Elimu yake ya msingi na ya upili alimalizia katika kambi ya wakimbizi. Kisha alipata shahada yake ya kwanza ya elimu ya upili mnamo 1960 kutoka katika shule ya Al Hussein Bin Ali mjini Hebron na baadaye kumaliza shahada yake jumla ya elimu ya upili katika shule ya Ibrahimiya jijini Jerusalem mnamo 1961.

Sheikh Ata Abu Rashtah kisha alijiunga na Kitengo cha Uhandisi katika Chuo Kikuu cha Cairo nchini Misri na kuhitimu na shahada ya uhandisi wa ujenzi mnamo 1966. Baada ya kuhitimu, Sheikh Ata Abu Rashtah alifanya kazi katika biladi kadhaa za Kiarabu kama mhandisi mjenzi na kuandika kitabu kuhusu hesabu za idadi kuhusiana na ujenzi wa majengo na barabara.

Kujiunga na Hizb ut Tahrir

Sheikh Ata Abu Rashtah alijiunga na Hizb ut Tahrir katikati mwa miaka ya hamsini na moja kwa moja akaanza kutekeleza harakati za chama katika ulimwengu wote wa Kiarabu. Alifanya kazi kwa karibu na Sheikh Taqiuddin an-Nabhani, muasisi wa Hizb ut Tahrir na Sheikh Abdul Qadeem Zallum aliyekuwa amiri wa Hizb ut Tahrir kufuatia kifo cha Sheikh Nabhani mnamo 1977. Mnamo miaka ya thamanini alikuwa mwanachama mstari wa mbele wa Hizb ut Tahrir nchini Jordan na kuteuliwa kama msemaji rasmi wa Hizb ut Tahrir.

Sheikh Ata Abu Rashtah alicheza dori kubwa nchini Jordan wakati wa vita vya ghuba la fursi alipoitisha mikutano ya waandishi wa habari, mihadhara na midahalo katika sehemu za umma kote nchini. Alijadili kuhusu uvamizi wa Iraq nchini Kuwait katika Msikiti wa Jerusalem jijini Amman ambako alitoa muhadhara kwa anwani Uvamizi Mpya wa Kimsalaba Katika Bara Arabu na Ghuba. Mara kwa mara alitiwa nguvuni na vyombo vya dola vya Jordan.

Mnamo 1994, katika mahojiano, Sheikh Ata Abu Rashtah alisema, “Kusimamisha Khilafah kwa sasa ni matakwa jumla miongoni mwa Waislamu, wanaotamani hili: ulinganizi wa serikali ya Kiislamu (Khilafah) umeenea nchini Misri, Syria, Uturuki, Pakistan, Algeria na kadhalika. Kabla ya Hizb ut Tahrir kuanza kazi yake kadhia ya Khilafah ilikuwa haijulikani. Lakini, chama hiki kimefaulu katika kumakinisha uongozi wake wa kifikra, na sasa kila mmoja anaimani na fikra zake, na anazungumzia kukihusu: hili liko wazi kupitia vyombo vya habari ulimwenguni kote”.

Uongozi Wake

Abu Rashtah alikuwa amiri wa kiulimwengu wa Hizb ut Tahrir mnamo 13 Aprili 2003 kufuatia kifo cha Sheikh Abdul Qadeem Zallum.

Tangu kuchukua uongozi wa Hizb ut Tahrir, amezungumza katika makongamano kote ulimwenguni ikiwemo Indonesia, Pakistan na Yemen.
Ya karibu zaidi, ni hotuba yake kwa Waislamu nchini Syria mnamo Januari 2013. Alifafanua mipango ya dola kuu za kiulimwengu, kwa upande mmoja, zinamsaidia Assad huku, upande mwengine, zikifanya kazi kuasisi serikali kibaraka; na kuwashajiisha Waislamu wa Syria kwa Quran na Sunnah kudumisha mapambano yao yenye ikhlasi dhidi ya serikali hiyo na kushikamana imara na Uislamu.

Yeye pia alitofautisha kwa kuwahi kuandika juu ya kadhia ya utekelezaji kivitendo wa suluhisho ya Kiislamu kwa matatizo mengi ya leo, kama vile maendeleo ya viwanda na elimu katika ulimwengu wa Kiislamu.

Sheikh Ata mara kwa mara huhutubia kuhusu kadhia zenye umuhimu wa kisiasa za kiulimwengu, kadhia za kiuchumi na kadhia za kifiqhi ya Kiislamu.

Vitabu Vyake

1. Migogoro ya Kiuchumi – uhakika wake na suluhisho lake kwa mtazamo wa Kiislamu [zamat Iqtisadiyya – waqi’uha wa mu’alajatuha min wijhat nadhar al-Islam]

Kitabu chenye kurasa 40 kilichoandikwa baada ya mgogoro wa kiuchumi wa mwaka 2008

PDF (English) |

2. Taysir fi Usul at-Tafsir – Surat al-Baqarah [Wepesi katika elimu ya tafsiri – Surah al-Baqarah]

Kitabu chenye kurasa 460 kinachojumuisha Makala mafupi juu ya misingi ya elimu ya tafsiri ikifuatiwa na utekelezaji wake kupitia tafsiri ya surah al-Baqara. Aliandika kazi hii safi akiwa gerezani nchini Jordan.

3. Wepesi wa kufikia elimu ya Usul [Taysir al-Wusool ila al-Usul]

Kitabu chenye kurasa 350 kinachowasilisha fani ngumu ya elimu ya Usul al-Fiqh kwa lugha na muundo mwepesi ili kiwe kama msingi wa somo hili.

4. Sera ya maendeleo ya viwanda na kuunda dola ya kiviwanda kwa mtazamo wa Kiislamu. [Siyasat al-tasni’ wa bina’ al-dawla sana’iyyan min wijhat nadhar al-Islam]