Marufuku ya Hijabu: Vita vya Kimfumo Dhidi ya Uislamu na Waislamu

بسم الله رحمنرحم

Alhamisi, 24 Januari 2019 Mahakama ya Upeo ya Kenya ilibatilisha uamuzi wa Mahakama ya Rufaa mnamo Septemba, 2016 uliosema kuwa sheria za shule haziwezi kuruhusiwa kukandamiza imani au haki ya mtu ya kuabudu na hivyo kuwaruhusu wanafunzi wakike Waislamu kuvaa hijabu shuleni. Baada ya Mahakama Kuu ya Kenya mnamo Jumanne, 23 Septemba 2014 kupiga marufuku mavazi ya hijabu kwa wanafunzi wakike Waislamu (The Standard, 28/09/2014). Mfano kama huo umetokea katika Jimbo la Oyo nchini Nigeria pale ambapo Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Ibadan kilipofungwa Jumatatu, 19 Novemba, 2018 kutokana na wanafunzi wakike Waislamu kuvaa hijabu (Premium Times Nigeria, 19/11/2018). Hivi majuzi Jumatatu, 14 Januari 2019 nchini Nigeria katika Jimbo la Oyo, wanafunzi wasiopungua 55 walinyimwa ruhusa ya kuingia ndani ya Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Ladoke Akintola kutokana na mavazi ya hijabu! (THISDAYLIVE, 15/01/2019)

Ni wazi kuwa tatizo sio hijabu bali ni “mfumo unaodhamini hijabu na wafuasi wake” ndio vinavyopigwa vita navyo ni Uislamu kama mfumo kamili wa maisha unaotoka kwa Mwenyezi Mungu na Waislamu wanaojizatiti kujifunga na Uislamu wao. Ni wazi kuwa ulimwengu wote unaendeshwa kwa mujibu wa mfumo batili wa kisekula wa kirasilimali unaotenganisha dini na maisha. Hivyo basi, binadamu amejipa mamlaka ya kutunga sheria na kupanga mambo katika maisha kwa mujibu wa matamanio ya nafsi na akili yake yenye kikomo! Chini ya mfumo huu binadamu ana mamlaka ya kuhalalisha na kuharamisha kwa mfano hivi sasa ni halali kunywa pombe na kutoza mikopo ya riba n.k! Mfumo wa kisekula wa kikoloni wa kirasilimali ambao hivi sasa umefika ukingoni ukitatapa ndiyo unaodhamini mashambulizi dhidi ya Uislamu, Waislamu na nembo muhimu za kuashiria kujifunga na Uislamu ikiwemo hijabu n.k.

Mtizamo wa kisekula wa kiliberali (uhuru) umejifunga kuwa hijabu ni “kitambaa kinachovaliwa kichwani na Waislamu wanawake!” Lakini ukweli ni kuwa Hijabu ni vazi ambalo hufunika uchi (awrah) wa mwanamke. Hijabu hujumuisha vipande viwili cha chini na cha juu. Kipande cha chini ni vazi pana (lisilokuwa jembamba) ambalo latiririka mpaka chini na kufunika nyayo zake, ambalo mwanamke lazima alivae juu ya nguo zake za kawaida kabla kutoka nje. Ama kipande cha juu (kitambara cha kichwa) au mfano wake au nguo yoyote itakayofanya kazi ya kufinika kichwa kizima, na shingo yote, na ufunuo wa kipande cha chini juu ya kifua.  Uislamu jumla umekitwa katika kujifunga na maamrisho na makatazo ikiwemo vazi la Hijabu. Mwenyezi Mungu (swt) Ametuamrisha: ﴿يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاء الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ“Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie nguo zao.” [Al-Ahzab: 59]. ﴿وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَى جُيُوبِهِنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاء بُعُولَتِهِنَّ… “Na waangushe shungi (vitambaa) zao juu ya vifua vyao, wala wasionyeshe uzuri wao ila kwa waume zao…”[An-Nur: 31].

Vita dhidi ya Uislamu na Waislamu vinalenga kuufanya Uislamu uwe kwa mtizamo wa kisekula wa kirasilimali na Waislamu walegeze misimamo yao ili wawe na utambulisho wa kisekula (Shaksiyyatul Ilmaniyya). Kwa maana nyingine ni kuwa Waislamu wajitoe katika utumwa wa Mwenyezi Mungu (swt) na kuwa watumwa wa wanadamu na kukubali kuhukumiwa na hukumu za wanadamu ambazo zinaathiriwa na maslahi/manufaa/mazingira! Ndiyo maana tukashuhudia kilele cha unafiki wa mfumo huu pale unapopigia debe wanawake kutembea uchi kama ilivyoshuhudiwa katika kampeni maarufu kwa kichwa “Mavazi Yangu, Chaguo Langu” #MyDressMyChoice iliyoanza katika mitandao ya kijamii Alhamisi, 4 Septemba, 2014 na kukamilika na maandamano yaliyofanyika mjini Nairobi, Kenya, Jumatatu, 17 Novemba 2014 eti wanawake waruhusiwe waendelea kutembea uchi! (World Bank Group, 03/16/2015). Hivi juzi Mahakama Kuu iliamurur mwanafunzi arudi shule baada ya kufukuzwa Shule ya Upili ya Olympic iliyoko Kibera asihudhurie kutokana na kuwa na rasta kwa mujibu wa imani ya rastafaria! (The Star, 30/01/2019). Lakini Waislmu wakitaka kujifunga kikamilifu na Uislamu wao wanabandikizwa kuwa ni wenye Misimamo Mikali au Magaidi wanaostahili kuwa chini ya uangalizi makini wa sheria za kupambana na misimamo mikali na ugaidi mfano: Sheria ya Kupambana na Ugaidi ya 2012 na Mikakati ya Kitaifa ya Kupambana na Misimamo Mikali ya 2016.

Suluhisho msingi dhidi ya vita vya kimfumo dhidi ya Uislamu na Waislamu ni kwa kurudisha tena maisha ya Kiislamu kwa kusimamisha Serikali ya Kiislamu ya Khilafah kwa njia ya Utume. Khilafaha pekee ndiyo itakayopambana kwa ukamilifu na kila ambaye anapinga Uislamu na kuwadhuru Waislamu wanapotaka kutekeleza Uislamu wao kwa mujibu wa Shari’ah (Qur’an na Sunnah). Ikiwemo Dola za Kisekula za Kimagharibi zikiongozwa na Marekani, Ufaransa, Uingereza, Ujerumani n.k ambao wanapigia debe mfumo huu batili na unaonuka wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake chafu zenye kumakinisha miito ya uhuru “liberali” na kuwapelekea watu kuwa duni zaidi kuliko hata wanyama eti kwa kuwa wanafurahia uhuru wao! Kwenda kutafuta haki katika mahakama za kitaifa au kimataifa hakutatusaidia sisi Waislamu wala Uislamu wetu; kwani tayari Uislamu na Waislamu wanatizamwa kwa sura ya “wenye makosa, mpaka wachunguzwe na kupatikana kuwa hawana makosa.” Kwa kuwa Uislamu ni tishio kwa mfumo ulioko mamlakani na uliofeli kusimamia wanadamu na kuwadhaminia utulivu kinyume chake unawakandamiza wanadamu na kuwakatisha tamaa na uhai kutokana na makucha ya sera zake za kinyama!

Hali hii tayari Mtume (saw) alikuwa ameshaizungumzia takribani karne 13 zilizopita: «يِأْتِي عَلَى النَّاسِ زَمَانٌ الْقَابِضُ عَلَى دينه كالقابض على الجمر» “Zitakuja zama ambapo kujifunga na dini yako itakuwa kama kushika kaa la moto.” [Sahihi Muslim]. Kwa hivyo, Waislamu ni muhimu wasirudi nyuma na waendelee kushikamana na Uislamu wao na wakati huo huo wajiunge na ulinganizi wa kurudi kwa Khilafah katika nchi iliyo na sifa mbili muhimu: 1.Ina hukumu kwa Shari’ah (Qur’an na Sunnah) kiukamilifu na 2.Usalama wa ndani na nje uko mikononi mwa Waislamu kiukamilifu. Huku wakiendelea na kazi hiyo wayakumbuke maneno ya Mwenyezi Mungu (swt): “فَإِنَّ مَعَ ٱلۡعُسۡرِ يُسۡرًا (٥) إِنَّ مَعَ ٱلۡعُسۡرِ يُسۡرً۬ا (٦) ” “Basi kwa hakika pamoja na uzito upo wepesi,. Hakika pamoja na uzito upo wepesi

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya