Kuzidi kwa Gharama za Maisha: Uislamu Ndio Tiba

Kila kukicha wanadamu duniani wanaoishi chini ya kivuli cha nidhamu fisadi ya kiuchumi wa kirasilimali wanaendelea kutamka kauli chungu “afadhali jana,” ilhali Wakenya matamshi haya yalianza takribani miaka 56 tokea 1963 Kenya ilipopata “Uhuru Bandia” na kabla yake wakati wa ukoloni kutoka kwa Uingereza! Ripoti ya hivi majuzi ya Benki ya Dunia (WB) ilisema kuwa eneo la Afrika Mashariki, Tanzania inaongoza kwa watu walio katika umasikini wa kupindukia takribani watu milioni 21.9, ikifuatiwa na Kenya ikiwa na watu milioni 17.6 na Uganda ikiwa na watu milioni 15.8! Kwa mujibu wa kipimo cha Benki ya Dunia (WB) mtu yeyote ambaye matumizi yake ni chini ya dola 1.90 (Ksh200) kwa siku ni masikini wa kupindukia! Watu milioni 368 ambao ni nusu ya jumla ya watu duniani walio katika umasikini wa kupindukia wanatoka katika nchi 5 pekee: India, Nigeria, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, Ethiopia na Bangladesh. Ambazo pia zina sifa ya kuwa nchi zenye watu wengi kutoka Asia Kusini na Jangwa la Sahara Afrika. WB ilitangaza kuwa Nigeria itaipita India na kuwa nchi ya kwanza duniani inayoongoza kwa idadi kubwa ya masikini wa kupindukia! Kufikia mwaka 2030 mgao wa masikini wengi duniani watakaokuwa wakiishi katika Jangwa la Sahara Afrika inakadiriwa kuwa ni asilimia 87, “lau ukuwaji wa uchumi ndani ya miaka 12 utakuwa sawa na ukuwaji wa uchumi kihistoria.” (theeastafrican.co.ke, 06/02/2019)

Kwa mujibu wa ripoti ya Wealth-X, nchi ambazo zinatarajiwa kutoa mamilionea wapya kwa idadi kubwa ndani ya miaka mitano ijayo ndani ya Afrika ya kwanza ni Nigeria ya pili ni Misri na ya tatu ni Kenya! Kasi ya ukuwaji wa mamilionea nchini Kenya inatarajiwa kuwa sawa na ile ya nchi ya pili duniani yenye uchumi mkubwa, China ambazo pamoja na Kenya zimeshikilia namba sita duniani! Fauka ya hayo, ripoti iliyochapishwa na Realtor Knight Frank ilionyesha kuwa Kenya ilizalisha mamilionea wapya 180 ndani ya mwaka 2017, ikiongeza idadi ya watu walio na utajiri wa zaidi ya milioni Sh500 na kuwa 1,290! (africabriefing.org, 22/01/2019)

Kwa mujibu wa shirika la msaada la Oxfam, matajiri 26 wanamiliki mali za watu bilioni 3.8 ambao wanajumuisha nusu ya watu masikini duniani. Utajiri wa asilimia 1 ya matajiri ni sawa na jumla ya utajiri asilimia 99 iliyobakia. Ndani ya miaka 10 tangu kuweko kwa janga la kiuchumi, idadi ya mabilionea imekuwa mara dufu. Utajiri wa mabilionea umezidi kwa dola za marekani bilioni 900 mnamo 2018. Mtu tajiri duniani, Jeff Bezos, mmiliki wa Amazon, utajiri wake ulizidi hadi dola za marekani bilioni 112. Asilimia 1 ya utajiri wake ni sawa na bajeti ya afya ya Ethiopia nchi iliyo na watu milioni 105. Masikini wanalipa ushuru wa juu kuliko matajiri. Takribani watu 10,000 kwa siku wanakufa kutokana na ukosefu wa huduma ya afya na milioni 262 ya watoto hawako shule kwa sababu wazazi wao hawawezi kumudu ada, sare na vitabu. Wanawake wanafariki kutokana na ukosefu wa huduma za uzazi na watoto wananyimwa elimu ambayo inaweza kuwa ndiyo njia yao ya kujikwamua kutoka katika umasikini. Mkurugenzi wa Oxfam wa kampeni na sera: Matthew Spencer, alisema: “Namna uchumi wetu ulivyopangiliwa inaamisha kuwa utajiri unazidi na unafungika kwa watu binafsi wachache ilhali mamilioni ya watu wanajitahidi tu kuishi. (theguardian.com, 21/02/2019)

Ripoti hizo zinadhihirisha kwa hakika kuwa wanadamu wamefungwa katika muundo wa mtumwa na bwana unaopigiwa debe na mfumo batili wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu yake ya kichumi ya ukandamizaji iliyokitwa katika uhuru wa kumiliki. Nidhamu ovu ya kiuchumi ambayo imeundwa kuhakikisha kuwa ina wakamua walala hoi vishilingi vyao mpaka tope la mwisho la damu zao kupitia ushuru na sera za kuwapendelea wakuu watawala!

Kwa upande mwingine tunao Uislamu kama mfumo unaotoka kwa Muumba wa binadamu na ambao umetekelezwa kikamilifu na kudhihirisha kivitendo pasi na shaka yoyote ndani ya takriban karne 13 kwamba una uwezo wa kutatua matatizo ya wanadamu. Uislamu chini ya Khilafah iliyosimamishwa kwa njia ya Utume, sera yake ya kiuchumi imekitwa kuhakikisha kuwa usambazaji wa mali unafanyika kwa njia ya haki na kwa raia wake wote. Kwa kudhamini watu binafsi mahitaji yao msingi: maji, chakula, makaazi na mavazi kwa kuweka mazingira mazuri ya watu/wanaume (wasimamizi wa familia) kufanya kazi ili wapate riziki. Ikiwa kufanya kazi/kutofanya kazi hakupelekei kukidhi mahitaji msingi basi ndugu zake wanabeba jukumu hilo la kumpa mahitaji msingi na ikiwa nao hawana uwezo basi Khilafah inaingilia kati na kumpa mahitati yake na hata kumuwezesha kukidh mahitaji ya ziada na wakati huo huo kusimamia mahitaji ya mujtama: usalama, elimu na afya n.k. Khilafah itaweza kumkidhia kutokana na Zaka iliyokusanywa ambayo imefungwa kwa watu aina nane pekee. Pia ikiwa Zaka haikutosha, basi itatumia mali iliyoko ndani ya Baitul Mal na kama haitoshi, basi matajiri Waislamu wataombwa kulipa ushuru kwa muda kutoka katika mali yao ya ziada ili kuweza kutatua dharura iliyopo na pale dharura hiyo ikiondoka basi ushuru huo nao unasitishwa mara moja. Zaidi ya hayo, Uislamu umejifunga na dhahabu na fedha kama sarafu ya matumizi ndani ya mzunguko wake wa kiuchumi na wakati huo huo umeharamisha utozwaji ushuru na riba kwa aina zake zote, upangaji wa bei, uhalifu, uhadaifu na ukiritimba katika biashara na urundikaji wa utajiri miongoni mwa maovu mengineyo. Ndani ya Khilafah inayoendesha sera ya kiuchumi aina hiyo, raia watawezeshwa kufurahia baraka za Muumba wao kwa kuwa riziki zao zitakuwa zimewekwa salama na hivyo kupelekea kupata utulivu, maendeleo na ustawi wa kweli.

Hivyo basi, maswali msingi ni kwa nini wewe unaendelea kuwa mtumwa wa mfumo huu wa kisekula wa kirasilimali uliofeli na nidhamu zake zinazonuka ambazo ndio chanzo cha wewe kuwa katika maisha duni na kuzidi kwa gharama za maisha?  Wataka kuhisi ukombozi wa kweli na kutoka katika utumwa na kuganda kisiasa-kijamii-kiuchumi unaoendelezwa na nidhamu ya kiuchumi ya kirasilimali; ambayo inajali tu ukuwaji wa kisanii wa pato la taifa (GDP) ukiashiriwa na pesa za makaratasi zisizokuwa na thamani yoyote. Jibu ni wewe kujiunga na ulinganizi wa kurudisha tena maisha ya Kiislamu kwa kusimamisha Khilafah kwa njia ya Utume. Na kuutekeleza Uislamu na Shari’ah (Qur’an na Sunnah) yake kwa ukamilifu kama mfumo ulioletwa kwa wanadamu kama muokozi. Mpaka wakati huo maisha duni na yaliyojaa majanga yataendelea kuukumba ulimwengu! Lakini lazima tuendelee kuifanyia kazi kwa bidi Khilafah inayokuja licha ya uzito na vikwazo vilivyoko mbele. Mwenyezi Mungu (swt) ametuahidi kuwa:

(فَإِنَّ مَعَ ٱلۡعُسۡرِ يُسۡرًا* إِنَّ مَعَ ٱلۡعُسۡرِ يُسۡرً۬ا)

“Basi kwa hakika pamoja na uzito upo wepesi. Hakika pamoja na uzito upo wepesi.

[Ash-Sharh: 5-6]

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya