Sheria ya Kupambana na Siasa Kali Ndani ya Shule za Kenya: Njama ya Wamagharibi Wakoloni Kunyamazisha na Kushambulia Uislamu na Waislamu kwa Kisingizio cha Kupambana na Ugaidi na Siasa Kali!

Gazeti la The Star mnamo tarehe 4 Juni 2019 liliripoti kuwa Seneti inajadili sheria mpya ambayo itapelekea majasusi kutumwa katika mashule ili kupambana na siasa kali kutoka kwa wanafunzi na kupigana na ugaidi. Kwa mujibu wa sheria inayopendekezwa na Seneta Naomi Waqo kutoka Marsabit, walimu wakuu watasimamia mikakati ya kupambana na ugaidi. Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi wa 2018 unalenga kuwafunza walimu na wafanyikazi wengine ili kuwa makini kuweza kujua ishara za kuegemea misimamo mikali. Mswada unasema kwamba wasimamizi wa shule watafanya uchunguzi juu ya walimu pia. Kwa ushirikiano na washikadau wengine, mameneja wa shule watabuni njia za kuweza kugundua, kuondosha siasa kali na kuwarudisha tena wanafunzi watakaopatikana kuhusika na siasa kali au misimamo mikali. “Idara za usimamizi kwa mara moja zitaripoti kwa kituo cha polisi, taasisi ya kiusimamizi kesi yoyote inayohusiana na mwanafunzi kupotea pale ambapo kuna sababu ya kuaminika kuwa mwanafunzi huyo ana uwezekano wa kujihusisha na vitendo vya kigaidi au ametiwa siasa kali,” Mswada unasema. [The Star, 4 June 2019: https://www.the-star.co.ke/news/2019-06-04-senate-wants-spies-deployed-in-schools-to-fight-terrorism/]

Ni wazi kwa mujibu wa ripoti hiyo kuwa Kenya kwa mara nyingine iko kifua mbele kupigia debe utekelezaji wa njama ovu iliyochorwa na mabwana zake Wamagharibi wakoloni wakiongozwa na Uingereza, Amerika na Ufaransa katika kupambana na Uislamu na Waislamu kwa kisingizio cha kupigana na ugaidi na siasa kali! Kenya inajiunga na nchi kama Uingereza, Ufaransa, Amerika, Uchina n.k ambazo zimejitokeza wazi na kutangaza chuki zao dhidi ya Uislamu safi walioupachika jina la “Uislamu wa Siasa kali au Misimamo Mikali” na kuunga mkono chapa ya Uislamu wa kimakosa na kuutambua kama “Uislamu Poa.” Fauka ya hayo, uadui wao ukasonga mbele zaidi kiasi cha kuzindua mikakati miovu kama Mkakati wa Kuzuia wa Uingereza mnamo 2007, Mkakati wa Kujitoa katika Ugaidi na Siasa kali wa Amerika mnamo 2016 na Mkakati wa Kuzuia Uhalifu na Siasa Kali wa Ufaransa mnamo 2016. Hivyo basi, haya mabadiliko mapya yanayolengwa kujumuishwa katika Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi wa 2018 ni muendelezo wa Mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na Misimamo Mikali uliozinduliwa na Rais Uhuru Kenyatta mnamo 7 Septemba 2016.

Zaidi ya hayo, mabadiliko haya mapya yanalenga kuendeleza kuwapa thaqafa wanafunzi na kuwalazimisha kuwa na utambulisho wa kisekula unaolenga kupigia debe usekula katika kila nyanja ya maisha kiasi kwamba mtu atabakia tu kuwa Muislamu kwa jina lakini ni msekula kifikra na kivitendo! Kenya kama nchi zote za kisekula za kirasilimali duniani; sera na sheria zake zinachorwa na kupitishwa na mabwana zao Wamagharibi wakoloni; kisha zinapelekwa katika mabunge na mabaraza yao ili zikatiwe muhuri tu! Hivyo basi, Kenya inchojali zaidi ni maslahi yake tu itakayopata kutokana na utekelezwaji wa sera na sheria hizo ovu dhidi ya raia wake hususan Waislamu. Kwa kuwa kuna manufaa basi hakuna kitakachowafanya wasitishe utekelezwaji wa mikakati hiyo hatari.

Lakusikitisha, Kenya iko tayari kutekeleza kipofu sera aina hiyo pasina na kufikiria mzizi wa kile kinachoitwa ni vita dhidi ya ugaidi na siasa kali. Hakika lau Kenya ingelikuwa taifa huru na uongozi wake ukiwa ni wenye kujali mambo ya raia wake kiukweli; ingeligundua kwamba vita dhidi ya ugaidi na siasa kali ni vita dhidi ya Waislamu na Uislamu. Hii ikiwa ni natija ya kufeli kwa mataifa ya Kimagharibi ya kikoloni katika kuweka amani, usalama, utulivu na ufanisi duniani na badala yake yamesababisha na yanaendeleza majanga katika kila nyanja ya maisha. Kutokana na utekelezaji wa mfumo wao wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake za sumu kama nidhamu ya utawala ya kidemokrasia, nidhamu huru ya kijamii, nidhamu ya kiuchumi wa kirasilimali iliyochorwa kuwanufaisha wachache matajiri na kuwakandamiza wengi masikini na sera ya kigeni ya kikoloni. Sera ya kigeni ambayo imeipelekea nchi kama Kenya kuwalazimisha wanajeshi wake kupigana vita vya kiwakala vya Kimagharibi ndani ya Somalia kwa jina la kupambana na ugaidi; vita ambavyo Wamagharibi wenyewe wamefeli kuvishinda!

Hakika lau Kenya inataka kucheza dori kuu ndani ya Afrika au hata kimataifa basi kwanza ni lazima ikate mahusiano yake ya kikoloni na kukumbatia ulinganizi wa kurudisha tena maisha ya Kiislamu kupitia kusimamisha Khilafah kwa njia ya Utume. Khilafah itahakikisha kuwa inalinda akili za raia wake kutokana na thaqafa ya Kimagharibi ambayo inapigia debe usekula (kutenganisha dini na maisha/serikali). Zaidi ya hayo, itawajenga raia wake wawe na utambulisho wa Kiislamu uliokitwa katika kipimo cha Halali na Haramu na kwamba lengo kuu maishani ni kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu (swt). Khilafah itaikomboa Kenya na Afrika kwa ujumla kutoka katika makucha ya Wamagharibi wakoloni ambao ndio chanzo cha kuganda kiuchumi, kijamii, kisiasa na kielimu tangu kupata uhuru bandia. Khilafah itawaondosha mamlakani watawala vibaraka wa wakoloni ambao wanakwenda mbio usiku na mchana kutekeleza sera zilizochorwa na Wamagharibi na zinazolenga kuharibu maisha na mustakbali wa raia wao! Khilafah itadhamini amani, usalama, utulivu, maendeleo na ufanisi wa kikweli kwa raia wake wote walioko chini yake pasina na kuzingatia rangi, makabila au dini zao.

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya

Makala Na.48: Ijumaa, 4 Shawwal 1440 | 2019/06/07