Makongamano yanayodhaminiwa na Wamagharibi kattu hayatomuokoa Mwanamke na makucha ya Ubepari

Hivi majuzi, Nairobi ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa kuhusu idadi ya watu na maendeleo (ICPD 25). Kongamano hilo liliwaleta pamoja zaidi ya washiriki 9,500 wakiwemo viongozi wa dunia, wanaharakati, viongozi wa kidini na wadau wengine kwa lengo moja; kutoa wito wa kuchukua hatua ya kutokomeza vifo vya kina mama wakati wa kujifungua, ukatili wa kijinsia na kukidhi mahitaji ya uzazi wa mpango katika kipindi cha miaka 10. Akihutubia wahudhuriaji, mkurugenzi mtendaji wa shirika la idadi ya watu duniani UNFPA, Dkt. Natalia Kanem, alisema: “Miaka 25 iliyopita, dunia iliweka ahadi ya kuhakikisha afya ya uzazi kwa wanawake na wasichana. Mambo hayo yanakuwa miongoni mwa haki ya msingi ya kuwawezesha kuwa huru na kufanya maamuzi ya maisha yao. Sasa umewadia wakati wa kutimiza ahadi hiyo.”

Mkutano wa Nairobi ulikuwa ni kuadhimisha miaka 25 tokea ule wa Qairo ambapo serikali 179 zilikubaliana kwa pamoja juu ya haki za binadamu ikiwemo haki za uzazi, ziwe ni msingi wa maendeleo na masuala ya idadi ya watu. Mpango wa hatua ya pamoja ulichukuliwa wa kuwahakikishia watu wote duniani wana haki ya kupata huduma jumla za afya ya uzazi ambayo pia hujumuisha  mpango wa uzazi wa kikhiyari/mbinu za kuzuia mimba na mimba salama. Wadau kwenye mkutano huo walitaja ili kufikia maendeleo endelevu  lazima dunia ilinde haki za kibindamu,afya ya uzazi na usawa wa kijinsia. Kongamano hilo lilihitimika kwa mashirika ya kibinafsi,mashirika ya kimataifa na wafadhili yakitoa ahadi ya kukusanya kima cha $ 8 bilioni kwa muda wa miaka kama juhudi ya kuungana mkono haki za kijinsia na za afya ya uzazi katika mataifa masikini.

Kongamano hili ni sehemu ya majukwaa yanayotumiwa na Malebarali wa kimagharibi katika kueneza maadili hatari  yenye sumu kiliberali dhidi ya mwanamke chini ya mwamvuli wa “kumkomboa mwanamke”.Katika kuendeleza harakati za “kumkomboa” wakatenga siku maalum duniani inayojulikana kama siku ya wanawake duniani inayosherehekewa kila mwaka tarehe 8 March. Maadhimisho ya siku hiyo hufanywa kwa kuandaliwa msururu wa matukio kote duniani kuangazia matatizo jumla yanayokumba wanawake duniani.Wanasiasa na watetezi wa wanawake hutoa hotuba za kuvutia wakiahidi ahadi chungu nzima kuhusu kulinda haki za wanawake ambazo karne nyingi zimepita hadi sasa zimekuwa kizungumkuti. Kinaya ni kuwa mashirika mengi ya kutetea haki za wanawake yanadhaminiwa na serikali zenye rekodi ya ukatili dhidi ya kina mama na watoto kupitia mashambulizi ya angani na nchi kavu katika mataifa kama vile Syria na Yemen na Somalia.

Wamagharibi wanaendelea kujenga dhana kwamba wanawake ili kupata haki na maendeleo, ni sharti afungamane na itikadi ya Kisekular yakutenganisha MwenyeziMungu na maisha na kumpa mwanadamu kazi ya kutunga kanuni huku akidharau sheria za Muumba wake. Wanashikilia kwamba pale mwanamke akishikamana na sheria za Kidini ndio anaendelea kujikwaza zaidi kimaendeleo. Hii ndio ajenda kuu ya mikutano yote inayofanywa na mashirika ya kimagharibi kuhusiana na wanawake. Hivyo, kwa mfano Uislamu bali dini zote zimekataza zinaa na uzinzi na kuusifu kuwa uchafu, lakini katika ulimwengu wa Kisekula  kuzuiliwa uovu ni dhulma na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Uzazi wa mpango imejengwa juu ya nadharia ya kimakosa ya Malthusian (Malthusian theory) inayodai kuwa ongezeko la idadi ya watu ni tishio kwa rasilimali. Wamezusha urongo kwamba dunia ina rasilimali chache hivyo kuna ulazima wa kupanga mikakati ya kudhibiti idadi ya watu. Huu ni uzushi wa wazi kwani uhalisia ni kwamba utajiri ulioko duniani ni zaidi ya wakaazi wake ispokua rasilimi nyingi huporwa na kipote cha warasilimali huku mamilioni wakiishia kwenye umasikini. Hivyo, tatizo si idadi ya watu bali ni mfumo wa kikoloni wa rasilimali uliokosa sera za usimamizi wa na ugavi wa rasilimali. Ama kuhusu afya ya uzazi, mwito huu haulengi kuimarisha afya kikweli za wanawake bali ni kushajiisha zinaa chini ya vazi la ‘ngono salama’. Wasomi wa kimagharibi wanashikilia msimamo kwamba ngono ni jambo la kimaumbile hivyo hakuna budi ila mtu kulifanya maadamu tu kuna vidonge na mbinu zitakazo hakikisha kwamba zinaa haina madhara! Hali hii ndio imeondosha haya kwa mwanamke wa kileo kiasi cha kuonekanwa kuwa ni mtumwa wa ngono jambo lililomtweza mwanamke. Kuhusu suala vifo vya kina mama wakati wa uzazi, hili limetokamana na uzembe wa serikali za kirasilimali jinsi ya kuhudumikia huduma afya za raia wao hasa ikizingatiwa kuwa hospitali nyingi za umma zina uhaba wa madaktari pamoja ukosefu wa dawa za kutosha hali inazozigeuza kuwa mitego ya vifo kwa mamilioni mwa kina mama.

Mikutano na makongamano ya kuzungumzia haki za wanawake ni ishara ya kufeli kwa serikali za kibepari katika  kudhaminia kikweli maslahi ya mwanamke. Hata kama ni kweli kuwa wanawake leo wanapitia dhulma nyingi lakini hii haimaanishi kwamba wamagharibi ndio wanaomiliki suluhu ya matatizo. Kwa maana hii, wanaharakati wa Wanawake kattu hawatoweza kuondoa matatizo hayo kwani wenyewe ni wahudumu wa serikali za kibepari zina rekodi ya ukatili sio dhidi ya wanawake tu bali kwa raia wote. Miito inayotukuzwa katika tawala za leo za Kidemokrasia kama vile haki za binadamu, uhuru wa kibinafsi, na fikra ya usawa wa kijinsia yote hiyo imemuondoshea mwanamke wa kileo haya na heshima yake aliyowekea na MwenyeziMungu. Uislamu pekee ndio utakaolinda heshima na haki za mwanamke kwani una sheria kamili zinafungamana na kila kipengele anachohitaji mwanadamu.

أَلَا يَعْلَمُ مَنْ خَلَقَ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ

Oh! Asiejua aliyeumba! Naye ndiye avijuaye visivyojulikana na vinavyojulikana

(Al-mulk 67:14)

Sheria hizi zitatekelezwa kupitia Khilafah ambayo baada ya kuangushwa kwake mwaka 1924 imekuwa ni faradhi kwa waislamu wote kuisamamisha tena.Ni kupitia kuisimamisha kwake ndio itadhamini sio tu haki za wanawake bali za rai wote.

Shabani Mwalimu

Mwakilishi kwa Vyombo Vya Habari Hizb ut-Tahrir Kenya.