Mnamo Jumatatu, 28 Septemba 2020 Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kufunguliwa kwa baa na mikahawa na kuruhusiwa kuuza pombe (The Standard, 28/09/2020)! Hivi sasa wazazi nchini wako mbioni kutimiza masharti muhimu ya kuhakikisha kuwa watoto wao wamerudi shule kwa kuitikia agizo la serikali la kufunguliwa kwa shule kwa awamu kuanzia mnamo Jumatatu, 12 Oktoba 2020 (The Star, 06/10/2020). Kwa kuongezea, viongozi wa kisiasa wanavutana katika kampeni za kisiasa ambazo zinatishia usalama wa taifa kiasi kwamba mnamo Jumamosi; Rais Uhuru aliongoza Maombi ya Kitaifa eti kuliombea taifa liweze kuhimili changamoto za kisiasa, kiuchumi na kijamii zinazolikumba taifa!
Inatia wasiwasi kuona kwamba madrasa zinataabika na hazina anayeangazia matatizo yao tangu kufungwa kwao mnamo Machi 2020 kwa kisingizio cha kupambana na janga la Covid-19. Wanafunzi, walimu na wazazi Waislamu wanapata shida kwa sababu kusoma kumesitishwa kabisa na wamebakia njia panda wasijue la kufanya kusuluhisha janga hilo. Wale wanaoitwa viongozi wa kidini na kisiasa Waislamu wamenyamaza kimya na wanafuata na kujifunga na maagizo ya serikali kama ambaye ni bendera zinaelekezwa na upepo!
Hali hii sio ya sadfa badala yake ndio ukweli wa uhalisia wa namna tawala za kisekula za kirasilimali zinavyoendesha mambo yake. Kiuhakika, Kenya ni dola ya kisekula na vipaombele vyake vinasukumwa na usekula. Kwa hiyo, madrasa ni taasisi za Waislamu ambazo zinadaiwa na tawala za kisekula ikiwemo Kenya kuwa ndio vituo vya ‘upenyezaji wa misimamo mikali.’ Hivyo basi, Covid-19 imetoa fursa kwa tawala hizi kuzidhibiti uwepo wake na ndio sababu serikali ya Kenya imenyamazia kimakusudi suala la kufunguliwa kwa madrasa ilhali inakwenda mbio kuhakikisha baa, mikahawa na shule zinafunguliwa!
Ni unafiki kwa serikali hiyo hiyo kuwaita viongozi wa dini wakijumuisha wale wanaodai ni viongozi wa Waislamu katika yale yanayoitwa ‘Maombi ya Kitaifa’ na kisha rais anaomba msamaha pasi na kuelezea khaswa ni nani aliyemkosea. Uislamu na Waislamu wanabaguliwa na kukandamizwa kwa kisingizio cha vita dhidi ya ugaidi na misimamo mikali. Na ukimya huu wa kimakusudi katika kutofunguliwa kwa madrasa ni sehemu ya muendelezo wa ubaguzi wa dola ya kisekula ya Kenya dhidi ya Uislamu na Waislamu. Kwa kuongezea, wale wanaodai kuwa ni watetezi wa haki za kibinadamu wameungana na asasi za serikali juu ya hili!
Uislamu na Waislamu wanajipata katika hali hii kwa sababu wao ni mayatima wasiokuwa na mlinzi na ngao ya kuwalinda kutoka kwa maadui wa Uislamu na Waislamu. Kukosekana kwa Dola ya Kiislamu ya Khilafah ndio chanzo cha hali hii ya kutamausha ya Uislamu na Waislamu sio tu nchini Kenya bali duniani kote. Kuvunjwa kwa Khilafah mnamo 28 Rajab 1342 H sawia na 3 Machi 1924 M kwa mikono ya usaliti ya Mustafa Kamal aliyelaaniwa akiongozwa na dola kuu duniani wakati huo Wamagharibi wakoloni, Uingereza na Ufaransa ndio mwanzo wa matatizo yetu. Hivyo basi, tunaongozwa na muongozo wa Ukafiri (itikadi ya kisekula/ilmaniyya) na Makafiri (wakati huo Uingereza na sasa Amerika na washirika wake). Ama kuhusu njia ya kutatua suala la madrasa; ni kuchukua hatua mbili muhimu:
Kwanza, mchakato wa muda mfupi – Waislamu nchini Kenya lazima waungane na kudai kufunguliwa kwa madrasa zao pasi na masharti. Ili kufaulisha mchakato huu lazima wawe imara na kuepuka sintofahamu zao duni za muda mrefu ambazo zimekuzwa kimakusudi na maadui wa Uislamu na Waislamu ili kuwagawanya na kuwakoloni daima. Katika kipindi chote cha mchakato huu lazima waunganishwe na ‘La Ilaha Ila Allah’ pekee na wajiepushe na aina yoyote ya vurugu au nguvu. Hatimaye ni kuchua hatua ifuatayo.
Pili, mchakato msingi na mpana – Waislamu nchini Kenya lazima waunge juhudi zinazoongozwa na chama cha Kiislamu cha Hizb ut Tahrir ‘chama cha ukombozi.’ Chama cha Kiislamu kinachosimama juu ya ukweli, hakiudanganyi Ummah wa Waislamu na wanadamu kwa ujumla na HAKITUMII vurugu wala nguvu katika kufikia lengo lake la kurudisha maisha ya Kiislamu kupitia kusimamisha Dola ya Kiislamu ya Khilafah kwa njia ya Utume. Ni kupitia mchakato huu PEKEE ndipo wanadamu watakombolewa kiukamilifu kutoka katika minyororo ya mfumo batili wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake zenye sumu ambazo zinaleta maangamivu duniani kote. Waislamu na wasiokuwa Waislamu watafurahi na kupata ustawi, amani na utulivu wa kweli ambao wameukosa na badala yake wamekuwa wakizama ndani ya moto wa kudumu wa kisekula! Mwenyezi Mungu (swt) asema: يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن تَنصُرُوا اللَّهَ يَنصُرْكُمْ وَيُثَبِّتْ أَقْدَامَكُمْ “Enyi mlio amini! Mkimnusuru Mwenyezi Mungu naye atakunusuruni na ataithibitisha miguu yenu.” (Muhammad 47: 7).
Ali Nassoro Ali
Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir