Mauaji ya Samuel Paty, Mwalimu wa shule moja ya Kifaransa yamepokelewa kwa hisia kali ndani na nje ya Ufaransa. Paty aliuwawa kwa kukatwa kichwa na kijana mwenye umri wa miaka 18 mzawa wa Russia. Sababu ya mauaji haya inaaminika kwamba mwalimu huyo alikuwa akifundisha somo la uhuru wa kimaoni/kuzungumza na akawaonyesha wanafunzi darasani kibonzo cha mtu aliyeuchi wa mnyama na kusema kwamba huyo ni Mtume Muhammad!
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alitaja mauaji haya kuwa ni “kitendo hiki ni ugaidi wa Kiislamu” akaongeza kuwa ” Mwandani wetu aliuwawa kwa kuwasomesha watoto uhuru wa maoni. Waziri wa elimu wa Ufaransa Jean-Michel Blanquer aliyaita mauaji hayo ” mashambulizi dhidi ya wafaransa”. Naye mwakilishi mkuu wa Muungano wa Kimataifa wa ushirikiano wa hadhara (United Nation Alliance of Civilizations) Miguel Moratinos alikashifu mauaji hayo. Mbali na hayo kumekuweko na maandamo katika miji mbalimbali ya Ufaransa ambapo waandamanaji walionekanwa wakipaza sauti wakisema “uhuru wa maoni unapaswa kuheshimiwa’
Kupitia mwito wa uhuru wa maoni, vyombo vya habari vya kimataifa hususan vya kimagharibi vimekuwa vikikejeli na kuutusi Uislamu na matukufu yake. Ufaransa imekua msitari wa mbele katika kutusi Sheria za Hijab, Mtume Muhammad (SAAW) na pia kudharau raia wake wenye asili ya nchi za Kiislamu. Mwaka 2012 jarida la Charlie Hebdo lilichapisha vibonzo ilivyodai ni Mtume Muhammad S.A.W) kitendo kilicholeta mhemko mkubwa kwa Waislamu duniani ambapo mwaka 2015 ofisi zake zilishambuliwa na kupelekea kuuwawa watu 12. Tayari wanawake wa Kiislamu nchini humo wamekuwa wakinyanyapaliwa kwa kuvaa niqab.
Tukichunguza kwa makini tutakuta kutukanwa Uislamu hakuishii tu kwa vyombo vya habari vya kimagharibi bali hata wanasiasa wake wamekua wakifuata nyayo hizohizo. Waziri mkuu wa Uingereza ashawai kuwaita wanawake wa Kiislamu majambazi wa kibenki (bank robbers)! Kwa hakika yote haya yanatokea katika mataifa yanayojigamba kuwa na ustaarabu. Ni wazi kabisa kwamba mataifa ya Kimagharibi yanachukia Uislamu na yamejijengea sera kuunda misamiati ambayo kwayo ndio huitumia kuwa majukwaa ya kuhubiri chuki zao dhidi ya Waislamu.
Allah asema:
قَدْ بَدَتِ ٱلْبَغْضَآءُ مِنْ أَفْوَٰهِهِمْ وَمَا تُخْفِى صُدُورُهُمْ أَكْبَرُ ۚ
Bughudha zao juu yenu inadhihirika katika midomo yao. Na yanayoficha vifua vyao ni makubwa zaidi.
Pamoja na haya, mwito wa uhuru wa maoni unaolazimishiwa ulimwengu mzima leo unatokamana na imani ya kwamba Mwanadamu kupitia akili yake hana haja ya kuchukua sheria za MwenyeziMungu kumuongoza maishani. Imani hii ndio huitwa ilmaaniya( secularism). Hivyo masecular wamejipa pia uwezo wa kuwawekea watu viwango vya maoni! Sio ajabu watu wenye kuamini imani hii kuwaona wakikejeli sheria za MwenyeziMungu Swt na wakati huo utawaona wakitukuza kanuni za kibinadamu. Kwa madai ya mwito huu viongozi wa kimagharibi hushajiisha raia wao kuufanyia shere Uislamu. Na hii ni dalili ya kufilisika kwao kifikra hivyo wameshindwa kujadaliana kifikra na Waislamu. Uislamu hauna shida katika kufungua mlango wa mjadala wenye tija na watu wa dini na mifumo nyengine lakini inaonekana wazi kuwa wamagharibi wanaogopa jinsi fahamu za Uislamu zinavyokua na nguvu dhidi ya fahamu zao za kimatata. Kikawaida, serikali inayoegemea mfumo uliofilisika huibua semi za chuki zinazolenga mifarakano ya Kidini baina ya raia na ati huo ndio ustaraabu!
Wamagharibi wanadai kutukuza fikra ya uhuru wa kuzungumza chochote na kumhusu yeyote yule hata kama ni Kumtusi Mtume Muhammad SAAW na wakaunda kanuni na sera za kikatili ili kuwanyamazisha Waislamu na harakati zinazopinga dhulma za kisiasa, kiuchumi na kijamii ndani ya serikali za kibepari. Tunaona mwenye kulingania sheria za Kiislamu kama vile Khilafah, Hijab, Jihad na sheria nyenginezo basi hushikwa na kutiwa korokoni na wala hakuna serikali inayosema waacheni(hao walinganizi) wanapaza maoni yao! Huu ndio undumakuwili wa viongozi wa kibepari na itikadi yao ya uhuru wa maoni.
Uislamu unaruhusu Muislamu kutoa maoni juu ya jambo lolote lile almuradi liwe ndani ya mipaka inayoruhusiwa na Uislamu. Kwa hapa ndio Uislamu ukaruhusu kumwajibisha kiongozi kwa kumkosoa pale anapokwenda mrama. Hata hivyo jambo lolote ambalo linagongana na Uislamu inakua haifai kwa mtu kutoa maoni yake. Kwa mfano kulingania fikra za kiubaguzi, ukabila, usawa wa kijinsia na utabaka, yote haya ni mambo yaliyoharamishwa kwa uislamu, hivyo hakuna nafasi ya kuyalingania kwa hoja ya uhuru wa maoni.
Mtume Muhammad (S.A.W) anachukua sehemu kubwa katika imani ya Waislamu kiasi cha kwamba Uislamu wa mtu haukubaliki ila baada ya Kumuamini MwenyeziMungu pamoja na kuamini utume wa Mtume Muhammad (Saaw). Ni kosa kubwa kihakika kuivunja heshima ya mtume Muhammad Saw kwani MwenyeziMungu mwenyewe ametangaza kuwa Mtume SAAW yupo katika tabia njema. Kwa maana haya, Waislamu huwajibishwa kumpenda zaidi Mtume (S.aw) kuliko watu wote.
Mtume Muhammad Rehema na Amani za MwenyeziMungu zimshukie yeye na aali zake alisema:
( (لا يؤمن أحدكم حتى أكون أحبَّ إليه من ولده ووالده والناس أجمعين
Hawi muumini mmoja wenu hadi niwe kwake yeye ni kipenzi zaidi kwake kuliko watoto wake, wazazi wake na watu wote.
Shabani Mwalimu
Mwakilishi kwa vyombo vya Habari
Makala No: 106