Habari:
Kwa uchache watu 15 wameuwawa kufikia sasa tangu kuanza kwa mvua kubwa kote nchini. Shirika la Msalaba Mwekundu limewashauri watu katika maeneo ya Mashariki na Kati kusongea sehemu za juu kutokana na tishio la mafuriko. Mabwawa mawili nchini Kenya yakaribia kufurika kutokana na mvua hii kubwa, ikihatarisha maisha ya maelfu ya watu. Kwa mujibu wa ripoti yake, watu 200,000 tayari hawana makao kutokana na mafuriko na kwa sasa wanaishi katika mashule na sehemu za wazi. Wakati huo huo baadhi ya barabara kuu nchini Kenya zimefinikwa na maji na kutoweza kupitika. Video iliyo chukuliwa angani na kusambazwa na kituo kimoja cha runinga cha humu nchini ilionesha sehemu iliyo haribiwa ya Mai-Mahiu eneo la Kusini Magharibi ambapo ufa mkubwa sana umejitokeza unaoweza siku moja kuigawanya Afrika kuwa sehemu mbili. Katika Kaunti ya Tana River, watu 50,000 wamelazimika kuhama makaazi yao huku Mto Tana ukivunja kingo zake.
Maoni:
Matukio ya mafuriko kila msimu wa mvua ndefu (Machi-Mei) yanayo sababisha kupoteza maisha na mali inayo gharimu mamilioni ya shilingi yamekuwa ni matukio ya kujirudia rudia. Hali ni hii hii hata katika msimu wa mvua fupi (Oktoba-Disemba). Licha ya tahadhari kutoka kwa idara ya hali ya anga kuwa nchi ingekumbwa na mvua kubwa ya kuendelea, desturi ya serikali ni ile ile ya kutowajibika ila tu kuhisabu hasara za mali na maisha!
Kwa kinaya katika kongamano la tano linaloendea la kila mwaka la Ugatuzi, maseneta na magavana ni miongoni mwa wajumbe 6,000, wanaojadili ajenda ya Raisi Uhuru Kenyatta ya Mambo Manne Makuu miongoni mwao ikiwa ni miundo mbinu, Uboreshaji Miji, Ardhi na Makao. La kinaya zaidi, inasemwa kuwa tangu kuanzishwa kwake miaka mitano iliyo pita, mfumo wa ugatuzi umenakili vizingiti kadhaa vya kihakika katika nyanja zake nyingi kama maji na barabara. Lakini licha ya mvua kubwa; mgao wa maji utaendelea kuwepo kama ilivyo tangazwa hadharani na kampuni ya maji ya jiji la Nairobi (NCWSC). Barabara zimegeuka kuwa vidimbwi vya kuogelea hata kwa mvua chache tu!
Inafahamika hadharani kuwa kabla ya kutaja majanga ya kimaumbile na ukosefu wa matayarisho ya kukabiliana na majanga haya kutoka kwa maafisa wa serikali, tayari yapo majanga mengi ya kutengenezwa na binadamu. Manispaa zimeidhinisha ujenzi wa nyumba chini ya nyaya za stima au karibu na mabomba ya mafuta mijini. Serikali haichukui hatua yoyote isipokuwa inasubiri majanga yatokee ndipo ianze kulia na kulalamika, na kuwatuhumu watu kwa uzembe na kuleta hoja dhaifu kuliko nyumba ya buibui, ikibwaga majukumu yake kwa raia.
Aghlabu maafa haya yakitokea, hufichua umbile halisi la mfumo tata wa kirasilimali na nidhamu zake za utawala la kutoyapa kipaumbele maslahi ya raia. La dhahiri ni kuwa serikali ndani ya mfumo fisidifu wa kirasilimali kamwe hazijali raia wake wala kuchunga maslahi yao. Uislamu kama mfumo kamili umefafanua jukumu la kuchunga mambo ya raia kuwa la serikali na wala si la watu binafsi au mashirika ya kibinafsi. Hivyo basi, dola ya Kiislamu, al-Khilafah inajitolea kikamilifu katika kuchunga mambo ya watu. Ama kuhusu majanga kama mafuriko na mitetemeko ya ardhi, Khalifah anaruhusiwa kutumia mali kutoka kwa hazina ya dola (Bait ul-Maal) kuwahudumia walioathiriwa na hili ni jukumu lake kwa raia na wala sio fadhila. Ikitokea hakuna mali katika hazina ya dola, hapo Khalifah atalazimika kutoza kodi matajiri kwa kiwango maalumu kufidia hali hiyo. Hivi ndivyo namna Khilafah inavyo tarajiwa kuchunga maslahi ya raia wake pasi na kuzingatia dini, rangi wala eneo.
Imeandikwa na Shabani Mwalimu
Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari wa Hizb ut Tahrir Kenya
Kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut-Tahrir