Habari:
Uchunguzi uliofichua dori ya Cambridge Analytica – kampuni ya takwimu ya Kiingereza katika uchaguzi wa Kenya imeibua hisia mseto kutoka kwa Wakenya katika mitandao wa kijamii. Uchunguzi huo, uliopeperusha na runinga ya umma ya Kiingereza ya Channel 4 News, ulionesha kuwa mmoja wa wakubwa wa kampuni hiyo, Alexandar Nix, akijigamba namna gani walivyo endesha kampeni za mwaka 2013 na 2017, namna gani walivyo viunda upya vyama vya TNA na Jubilee, kuandika hotuba na manifesto, kufanya tafiti mbili kwa niaba ya vyama hivyo, “kupangilia kila kitu” na “kuendesha kila nukta ya kampeni yake [ya Kenyatta]”.
Maoni:
Kashfa hii mpya imefichua umbile halisi la uhadaifu wa inayoitwa ‘Demokrasia’, ambayo imekuwa ikipigiwa upatu kama nidhamu ya matumaini na ukombozi na warasilimali masekula. Lakini, kiuhalisia Demokrasia ni nidhamu ya kiutawala ya kijambazi inayotumiwa na kipote cha matajiri kuwanyanyasa walala hoi walio wengi kwa kuwatumia kama mashini za upigaji kura ili kuhalalisha kuwepo kwao afisini. Kipote hicho cha matajiri hutumia njia zote zilizoko mikononi mwao kuhakikisha wanashinda mashindano ya kisiasa kwa gharama zote. Kwa kuwa aliyeko madarakani ndiye mfalme, wengine wote ni wafuasi tu wa utawala wake, na hutekeleza sera zilizo undwa kuhakikisha walala hoi wanabakia katika hali hiyo hiyo yao ya umasikini na matajiri kuendelea kulimbikiza na kufuja mali ya umma pasi na hofu yoyote ya kuchukuliwa hatua. Kamwe haihusiani na suala la kuleta mageuzi msingi ya kweli yanayo dhamini kuimarisha maisha ya wapiga kura. Kutokana na kuwa wengi wa wapiga kura hukitazama kipindi cha upigaji kura kama fursa ya uhai na kifo ya kuwachagua wawakilishi wao watakao wahudumia kwa bidii na kuleta sera zitakazo inua hali zao za kimaisha kutoka kuwa mbaya hadi kuwa nzuri lakini matokeo yake daima huwa kinyume ya hivyo ni kutoka kuwa mbaya hadi kuwa mbaya zaidi!
Wapiga kura wenye papatiko wanaotambulika na matajiri kuwa mashini zao za upigaji kura hutumiwa wakati wa kampeni za uchaguzi kwa kuwa wanasiasa wengi hujihusisha na kinyang’anyiro kikali cha kupigania viti ima kuingia au kubakia mamlakani. Utumiaji huu unajumuisha pakubwa hongo kwa wapiga kura, vita vya kiuvumi vya moja kwa moja au visivyo vya moja kwa moja vinavyo lenga wafuasi wa wanasiasa kwa kutumia urongo au lugha chafu. Yote haya yanatokea kwa sababu, lengo huhalalisha njia; hivyo basi kila njia itatumiwa maadamu itahakikisha kuingia au kubakia mamlakani. Kuendelea kuimarika kwa teknolojia kumepelekea kuinuka kwa makampuni ya kisekula ya kirasilimali yanayo pata pesa kwa kukusanya na kuuza rekodi za maisha ya watu binafsi kwa wagombezi wakuu bila ya kujali lengo la matumizi yake, na mwenye kuzitumia, namna na wakati wa kutumiwa rekodi hizo. Kwa kuwa mtazamo wa kisekula wa kirasilimali wa vitendo umejengwa juu ya manufaa na maadamu kuna faida hakuna kinacho weza kuwa kizingiti. Kampuni hizo zilizo julikana kama kampuni za ujasusi hatimaye zilibadilishwa na kuwa mitandao ya kijamii na tangu wakati huo zimewavutia mamilioni ya watumizi katika majukwaa yao, ambayo yanajumuisha mitandao ya Facebook, Twitter, Instagram, WhatsApp, nk. Kupitia majukwaa haya, mawazo huru na uhuru vimeenea mithili ya moto katika nyasi kavu. Lakini, majaribio yoyote ya kutumia majukwaa haya kuuamsha Umma wa Kiislamu kufikiri kimfumo na kuukumbatia mfumo wa Kiislamu chini ya mradi wa Khilafah huvurugwa na kupigwa marufuku kudaiwa kuwa jumbe za chuki na wale wanao husika nazo hubandikwa majina ya kuwa wenye misimamo mikali au magaidi kwa mfano nchini Uzbekistan, Urusi, na Syria nk.
Huku mamilioni wakijiunga na huduma zao, hufungua pia mwanya kwa watumizi wake kutumiwa hususan na makampuni, yanayo fanya kazi kwa kula njama na wamiliki wa majukwaa haya waliopewa kandarasi na mfano wanasiasa kuhakikisha wananyakua mamlaka sio kwa kupitia kuendesha kampeni zao kwa msingi wa sera na ukweli bali kwa msingi wa urongo na kuhadaa hamasa za wapiga kura wanao tapatapa. Kama ilivyo thibitishwa na mfanyikazi wa Cambridge Analytica (CA) aliyesema, “Hakuna maana ya kugombania kampeni ya uchaguzi kwa msingi wa ukweli kwa sababu kiuhalisia, zinazo husika ni hamasa pekee”. Katika muktadha wa Kenya ambapo ukabila ndio injini ya siasa ilipelekea kampuni kama CA kupatiliza fursa ya hisia za kikabila za wapiga kura wanao tapatapa kwa manufaa yao kuamsha hisia za kikabila kumsaidia mteja wao dhidi ya mpinzani wake. Hili lilifanya kazi barabara ikizingatiwa kuwa matumizi ya simu za rununu za smartphones na mtandao wa intaneti yako katika viwango vya juu ikilinganishwa na majirani zake eneo la Afrika Mashariki yakifikia takriban asilimia 80%.
Kwa hivyo, kelele hazipaswi kuwa juu ya CA kuwa imeshawishi ushindi wa wagombezi katika uchaguzi au la bali zilipaswa kuwa juu ya kubadilisha ‘nidhamu ya kijambazi iitwayo demokrasia na mfumo wake wa kisekula wa kirasilimali’ ambazo ndizo mzizi wa migogoro ya kisarakasi inayo wakabili wanadamu leo. Kuwepo kwa CA na makampuni mengine mfano wake kumejengwa juu ya msingi wa mfumo wa kisekula wa kirasilimali na hivyo basi kuyafunga kikamilifu kwahitaji kulingania mabadiliko kamilifu ya mfumo huu muovu unao yapa hadhi uwepo wayo. Ni kwa kutekelezwa Uislamu pekee kama mfumo badali ulioshuka kwa wahyi kutoka kwa Muumba ndio utakao karibisha mmuliko sahihi wa matokeo ya uchaguzi yanayo simamiwa kwa kutafuta radhi za Allah (swt). Wakaliaji viti vya utawala watashajiishwa kwa kupewa mabustani ya juu ya Pepo kutokana na uaminifu wao na kuhisabiwa kwao katika kutekeleza sera zinazo imarisha maisha ya wanadamu na kulenga kushibisha kiu yao ya kudumu ya mali.
Ali Nassoro Ali
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya