Tunaweza kuugawanya Uislamu kwa misingi miwili; Itikadi (Imani) na Matendo. Itikadi mahala pake ni moyoni kwani ndio huamini. Kinachomsukuma mtu kujifunga na maamrisho na kujieupusha na makatazo ya MwenyeziMungu (swt) ni Imani. Amali au Matendo mema huwa ni natija ya Imani. Itikadi ya Kiislamu ni fikra jumla (Fikra Kulliyyah) inayo angazia ulimwengu, mwanadamu na uhai. Na kuwa nyuma ya vitatu hivi kuna MwenyeziMungu (swt) naye ndiye muumbaji wake. Na MwenyeziMungu (swt) ndiye aliyeleta mpangilio wa jinsi ya kupeleka maisha ya mwanadamu. Hapa ndio kuna kuja ufaradhi wa kujua hukumu ya kila kitu na kitendo kabla hajatenda mwanadamu.
Nini hukumu ya kiSheria?
Wanavyuoni wa Kiusuli wanaeleza Hukmu ya Kisheria kuwa ni maelezo ya Mwenye kuileta sheria yanayofungamana na vitendo vya waja.
خطاب الشارع المتعلق بأفعال العباد
Wanavyuoni wa kiusuli walitumia neno ‘mleta sheria’ الشارع)) ikasemwa maelezo ya mleta sheria badili ya maelezo ya MwenyeziMungu (swt) (خطاب الله) ili isije watu wakafahamu kuwa chimbuko pekee la sheria za Kiislamu ni Kitabu cha MwenyeziMungu (swt) tu yaani Quran. Ni jambo linalojulikana kwa Waislamu kuwa Sunna kwa maana ya Hadithi za bwana Mtume (saw) pia ni chimbuko la sheria kwa kuwa pia ni Wahyi. Katika hadithi Sahihi Mtume (saw) alisema:
ألا إني أوتيت القرآن ومثله معه
Zindukeni nilipewa Quran na mfano wake pamoja nayo. Maana ya ‘mfano wake’ ni Sunnah.
Kwa hivyo hukumu ya kisheria ni maelezo ya MwenyeziMungu (swt) aliyowahutubia waja wake. Maelezo hayo ni kuhusu kitendo au kitu basi hiyo ndiyo hukumu ya MwenyeziMungu (swt) yaani ndiyo hukumu ya kisheria. Kulingana na tafsiri hiyo Inabainika kuwa hukumu ya kisheria huchukuliwa kutokana na maelezo yatokayo kwa MwenyeziMungu (swt) (Wahyi). Basi lau kusingekuwa na Wahyi (Maelezo yatokayo kwa MwenyeziMungu (swt)) kwa Mtume wake Muhammad (saw) basi kusingekuweko na hukumu ya kisheria. Aidha lau usinge shuka wahyi basi matendo ya watu yasingegawanywa kwa misingi ya halali na haramu, uzuri na ubaya au wema na uovu. Kwa kifupi hukumu ya kisheria asili yake ni maelezo ya MwenyeziMungu (swt) ima Quran au Hadithi. Kulingana na ufafanuzi huu kanuni zitungwazo kwenye Bunge, Seneti na kamati za kutoa fatwa zisizokuwa na mashiko ya dalili za kisheria hazizingatiwi kuwa hukumu za kisheria kwani hazitokamani na wahyi. MwenyeziMungu (swt) anasema:
وَلَا تَقُولُوا لِمَا تَصِفُ أَلْسِنَتُكُمُ الْكَذِبَ هَٰذَا حَلَالٌ وَهَٰذَا حَرَامٌ لِّتَفْتَرُوا عَلَى اللَّهِ الْكَذِبَ ۚ إِنَّ الَّذِينَ يَفْتَرُونَ عَلَى اللَّهِ الْكَذِبَ لَا يُفْلِحُون
Wala msiseme uwongo, kwa kuropokwa na ndimi zenu: Hichi halali,na hichi haramu – mkimzulia uwongo Mwenyezi Mungu. Hakika wanao mzulia uwongo Mwenyezi Mungu hawatafanikiwa.
[An-Nahl: 116]
Ama maana ya ibara; ‘Yanayofungamana na matendo ya waja’ (المتعلق بأفعال العباد) hapa inakusudiwa maelezo ya Mwenyezi Mungu (swt) yanayofungamana na matendo ya waja. Ama maelezo yasiyofungamana na vitendo huwekwa katika fungu la itikadi ambayo asili kama tulivyo ashiria hapo nyuma hutakikana kusadikikishwa moyoni.
Aina ngapi za hukumu za Kisheria?
Ukiachilia mbali kauli ya Abu Hanifa kwamba hukmu za kisheria ni saba, jamhuri ya wanavyuoni wanataja kwamba hukumu za kisheria ni tano na huu ndio msimamo wenye nguvu. Hukumu hizi tano ndizo ambazo MwenyeziMungu (swt) amewakalifisha waja wake na ndio maana pia huitwa hukumu tano za kukalifishwa التكليف الخمسة) أحكام):
1-Faradhi ama wajibu
2-Mandoub- Sunna/Nafila/mustahabu
3-Haramu ama Mahdhur
4-Makruhu
5-Mubah
Ufafanuzi wa hukumu hizi ni kama ifuatavyo:
Faradhi/Wajibu:
Ni tendo ambalo sheria imeliamrisha kwa amri ya kilazima na alifanyapo mtu huandikiwa thawabu na akiliacha huandikiwa Dhambi. Hivyo lolote lile liloamrishwa kwa njia ya ulazima ndio huitwa faradhi au wajibu mfano kama Swala tano, funga ya Ramadhani, Jihad na kuwafanyia wema wazazi. Ili tendo liwe ni faradhi ni sharti kuweko na maelezo yakuashiria kuwa kutofanywa kwake kunapelekea adhabu kali. Ufaradhi wa swala kwa mfano umeashiriwa kwenye aya:
ما سلككم في سقر *قَالُوا لَمْ نَكُ مِنَ الْمُصَلِّين
Ni nini kilicho kupelekeni katika (Moto wa) Saqar? Watasema hatukuwa miongoni waliokuwa wakisali.
[Al-Muddaththir: 42-43]
Mandoub/ Sunna/ Mustahabu:
Ni kila jambo liloamrishwa na sheria lakini amri hiyo ikawa si ya ulazima kwa namna lau analifanya mtu jambo hilo hupata thawabu na wala haandikiwi dhambi kwa kuliacha kwake. Hivyo amri yoyote iliyo amrishwa lakini ikawa hakuna dalili inayo ashiria kuwa kuacha amri hiyo kunapelekea adhabu basi ndio huitwa sunna. Imamu Suyuti katika kitabu chake Al-Kaukab Saatiy amefafanua matamshi haya (Mandoub, Sunna na Mustahabu) kama ifuatavyo: Sunna ni kile kitendo alichokuwa akidumu nacho Mtume (saw) na kukihimiza kwa Waislamu mfano rakaa za Sunna baada ya swala za faradhi (Rawaatib). Ama kile kitendo alichokifanya (saw) mara moja moja na wala hakuwa ni mwenye kukidumisha ndio huitwa mandoub kama vile swala ya dhuha. Ama Mustahabu ni kile kitendo ambacho Mtume (saw) amekihimiza kufanywa lakini yeye mwenyewe hakufanya kama swaum ya Tasua’. Ama Naafila wanavyuoni huitaja kama ibada yoyote zaidi ya ile ya faradhi mfano kuhiji mara ya pili….swaumu kinyume na Ramadhani….swadaka, swala za usiku na kadhalika.
Haramu/Mahdhur:
Ni lile jambo ambalo sheria imelikataza tena kwa katazo la kukatikiwa kiasi cha kuwa anayefanya jambo hilo anapata dhambi na mwenye kuliacha huandikiwa thawabu. Mambo ya haramu ni mengi kama Riba, Zinaa, kuasi wazazi wawili na kuua.
Makruhu:
Ni hukumu ya nne ambayo huja Baada ya haramu. Nayo huelezwa kuwa ni lile jambo ambalo sheria imelikataza lakini katazo lenyewe halifungamani na adhabu. Yaani hakuna adhabu iliowekewa kwa kufanya jambo hilo. Mtu akifanya jambo hilo haandikiwi dhambi na anaye jieupusha huandikiwa thawabu. Wanavyuoni wakisheria hupiga mfano wa makruhu wa mtu kusahau alichohifadhi katika Quran. Mtume (saw) alikataza Waislamu waliohifadhi chochote katika Quran kusahau walichohifadhi. Hivyo Mtume (saw) anataka watu wasisahau na kutokwa na walichohifadhi katika Quran lakini hakuna adhabu ya atakaye sahau.
Mubah:
Ni jambo ambalo sheria imelikhiyarisha baina ya kulifanya na kuliacha. Alifanyaye haindikiwi thawabu wala anayeliacha hapati dhambi. Na hapa ni muhimu kuzindusha kuwa yale madai ya kuwa mtu akifanya mubah hupata thawabu ni madai yasokuwa na mashiko yoyote ya kisheria. Aidha, Mubah haifasiriwi kuwa ni jambo ambalo sheria imelinyamazia na kuwa halikupewa hukumu. Wanavyuoni wa kutegemewa wamekubaliana kuwa hakuna hukmu ya kitendo kabla ya kuweko kwa sheria; yaani, kabla ya sheria hakuwezekani kitendo kupewa hukumu. Hii ina maanisha matendo yote yamepewa hukumu ya kisheria. Hivyo, Mubah kama hukumu ya kisheria imejengwa juu ya dalili za kisheria.
هُوَ الَّذِي خَلَقَ لَكُم مَّا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا
Yeye ndiye aliye kuumbieni vyote vilivyomo katika ardhi.
[Al-Baqarah: 29]
Na hapa ndio ile qaida isemayo ‘Asili ya vitu ni Mubah isipokuwa vile vilivyoharamishwa’ inapo chipuza. Ama Hadithi ya Mtume (saw) isemayo “Na akanyamazia vitu iwe ni rahma kwenu nyinyi pasina na kusahau…” وسكت عن أشياء رحمة لكم غير نسيان)) maana yake ni kwamba ni kitendo kilichofanywa mbele ya Mtume (saw) kisha asikikataze kumaanisha kuwa amekikubali yaani ni halali. Hizi ndizo hukumu tano za kisheria ambazo Waislamu wanapojifunga nazo kwenye maisha yao ya kila siku ndio huambiwa kuna mujtamaa wa Kiislamu. La muhimu zaidi kutambua ni kuwa mahusiano yetu na baada ya maisha haya ya dunia ni kuwa tutahesabiwa kwa kila tulicho kitenda. Kwa Muislamu ni lazima ajifunge na sheria kabla ya kutenda matendo yake. Ndio ikasemwa kwamba ‘asili ya matendo ni kujifunga na sheria’ na kuwa MwenyeziMungu (swt) atatuuliza sote kwa yale tuliyoyatenda.
فَوَرَبِّكَ لَنَسْأَلَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ * عَمَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ
Basi Naapa kwa Mola wako Mlezi! Tutawahoji wote. Kwa waliyokuwa wakiyatenda.
[Al-Hijri: 92-93]
Shabani Mwalimu
Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari Hizb ut Tahrir Kenya