Mwenyezi Mungu (swt) ameumba ulimwengu, mwanadamu na uhai. Mwanadamu ana utambulisho uliokusanya sehemu mbili: 1-aqliyyah -uwezo wa kuvitambua na kuvihukumu vitu na vitendo kwa mujibu wa kipimo anacho kiamini. 2-nafsiyyah -njia ya kufanyiakazi utambuzi na hukumu aliyoipata katika kukidhi ghariza zake na mahitaji yake ya kiviungo. Hivyo basi uhai na utambulisho ni masuala nyeti kwa mwanadamu. Ama uhai unachukua dori kubwa kwa mwanadamu. Kwani kupitia uhai ndio mwanadamu anayaendea maisha yake duniani na kinyume ni kifo chake.
Uhai umefungika na umri/muda/wakati alioukadiria Mwenyezi Mungu (swt). ﴿وَٱلۡعَصۡرِ* إِنَّ ٱلۡإِنسَـٰنَ لَفِى خُسۡرٍ* إِلَّا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ وَعَمِلُواْ ٱلصَّـٰلِحَـٰتِ وَتَوَاصَوۡاْ بِٱلۡحَقِّ وَتَوَاصَوۡاْ بِٱلصَّبۡر﴾ “Naapa kwa muda/wakati. Hakika mwanadamu bila ya shaka yumo katika hasara. Isipokuwa wale walio amini, na wakatenda mema, na wanaohusiana kwa haki na wakahusiana kusubiri.” [103. Al-Asr: 1 – 3]. Kwa hiyo mwanadamu anatakiwa kuupatiliza uhai wake kwa kujisalimisha kikamilifu na kuwa mtumwa wa Mwenyezi Mungu (swt). Kwa Maana nyingine mwanadamu anatakiwa kuwa Muislamu kamili aliyejisalimishe kwa maamrisho na makatazo ya Mwenyezi Mungu (swt). ﴿يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ ٱدۡخُلُواْ فِى ٱلسِّلۡمِ ڪَآفَّةً۬ وَلَا تَتَّبِعُواْ خُطُوَٲتِ ٱلشَّيۡطَـٰنِۚ إِنَّهُ ۥ لَڪُمۡ عَدُوٌّ۬ مُّبِينٌ۬﴾ “Enyi mlio amini! Ingieni katika Uislamu kwa ukamilifu, wala msifuate nyayo za Shetani; hakika yeye kwenu ni adui aliye wazi.” [2. Al-Baqarah: 208]
Kwa kuongezea Mtume (saw) alisema: «نِعْمَتَانِ مَغْبُونٌ فِيهِمَا كَثِيرٌ مِنَ النَّاسِ، الصِّحَّةُ وَالْفَرَاغُ»“Zipo neema mbili ambazo watu wengi wamezipoteza: afya na muda/wakati wa kufanya kheri.” [Sahih al-Bukhari]. Napia Rasulullah (saw) alisema: «لاَ تَزُولُ قَدَمَا ابْنِ آدَمَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ مِنْ عِنْدِ رَبِّهِ حَتَّى يُسْأَلَ عَنْ خَمْسٍ عَنْ عُمْرِهِ فِيمَا أَفْنَاهُ وَعَنْ شَبَابِهِ فِيمَا أَبْلاَهُ وَمَالِهِ مِنْ أَيْنَ اكْتَسَبَهُ وَفِيمَ أَنْفَقَهُ وَمَاذَا عَمِلَ فِيمَا عَلِمَ» “Miguu ya wanadamu haitoondoka mbele ya Mola wake Siku ya Kiyama, mpaka atakapoulizwa mambo matano: kuhusu uhai/umri wake na aliufanyia nini, kuhusu ujana wake na aliutumia katika nini, kuhusu mali yake na namna alivyoichuma na kuitumia na alikifanyia nini alichokuwa anakijua.” [Tirmidhi]
Mwanachuoni Muḥammad ibn Muḥammad aṭ-Ṭūsī al-Ġaz(z)ālī maarufu Imam Ghazali alisema yafuatayo: “Muda wako usiwe bila mpangilio wowote, kiasi kwamba unajihusisha na kila kinachokupitilia. Bali lazima ujihesabu na kupangilia ibadah zako kipindi cha mchana na usiku, kila kipindi ukitengee shughuli ambazo lazima usizitelekeze wala kuzibadilisha kwa nyingine. Kwa kuupangilia wakati, baraka ya wakati itajidhihirisha. Mtu ambaye hana mpangilio kama wanavyofanya wanyama, kutojua anachokifanya wakati fulani, atatumia muda wake mwingi pasi na faida yoyote. Muda wako ni uhai wako, na uhai wako ndio mtaji wako: kupitia huo ndio unafanya biashara yako, na kupitia huo ndio utafikia mafanikio ya milele kwa kuwa karibu na Mwenyezi Mungu. Kila pumzi yako moja ina thamani kubwa, kwa sababu haibadilishiki; ikisha toka, hairudi tena. Kwa hiyo usiwe kama wapumbavu ambao wanafurahi kila kukicha kwa kuongezeka utajiri wao ilhali uhai wao unapungua. Kuna kheri gani katika utajiri unaozidi ilhali uhai unapungua? Usifurahi isipokuwa katika kuzidisha maarifa au kuzidisha kazi zenye kheri. Kiuhakika vitu viwili hivyo ndio marafiki zako ambao watakuwa pamoja nawe hadi kaburini, wakati ambao mkeo/mumeo, utajiri wako, watoto wako na marafiki zako watabakia nyuma.” [Bidayat al-Hidayah]. Kwa hiyo ni lipi linatakiwa kukufurahisha na kuumaliza wakati wako: kuongeza maarifa na kulingania kurudi kwa Khilafah au kuridhika na kubakia katika kutawaliwa na ukafiri?!
Kwa kumalizia kuupatiliza wakati ni jambo la dharura mno hususan zama hizi za kutawaliwa na ukafiri wa mfumo wa kisekula wa kirasilimali. Hivyo basi, kila Muislamu anatakiwa kuwekeza juhudi zake zote katika kufanyakazi ya kurudisha tena maisha ya Kiislamu kupitia kusimamisha Khilafah kwa njia ya Utume. Kuutumia wakati katika njia ya ulinganizi wa kusimamisha Khilafah ni haki juu ya wakati tulio nao na kinyume chake ni kuudhulumu wakati wako. Kwani wakati wako ni amana utakayokwenda kuulizwa Siku ya Kiyama kuhusu namna ulivyoutumia. Basi hatuna budi kushindana Waumini katika yale yanayomridhisha Mwenyezi Mungu (swt) kupitia kuitikia mwito Wake: ﴿يَـٰٓأَيُّہَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ ٱسۡتَجِيبُواْ لِلَّهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمۡ لِمَا يُحۡيِيڪُمۡ﴾ “Enyi mlio amini! Muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapo kuitieni jambo la kukupeni uzima wa milele.” [8. Al-Anfal: 24]. Tuupatilizeni mtaji wetu mkuu kwa kuufanyia biashara ya ulinganizi wa Mwenyezi Mungu (swt). Na siku hiyo itakaposimama Khilafah tutafurahi kama alivyotuambia: ﴿وَيَوۡمَٮِٕذٍ۬ يَفۡرَحُ ٱلۡمُؤۡمِنُونَ﴾ “Na siku hiyo waumini watafurahi.” [30. Ar-Rum: 4]
Ali Nassoro Ali
Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir