Ili kuweza kufahamu kwa kina ukweli juu ya jibu la suala hili,kuna udharura wa kujua mafunzo, mila,desturi,tamaduni na mifumo mengine kando na Uislam,juu ya suala hili hili.
Ktk tamaduni na mila za kale.Kwa vile ni nyingi,tutagusia baadhi ya mifano ktk mila, desturi na mifumo ya maisha,ili kupata usafi wa jibu la suala hili
1)Wayunani(Greeks).Watu ambao jina la nidhamu ya utawala ya ubepari: Demokrasia limetoka kwao.Nidhamu ambayo,leo yapigiwa debe kuwa ndio yenye kudhaminia haki,uadilifu, usawa na kuwa,sehemu yoyote isotawala kwa nidhamu hio,basi kuna utawala wa kiimla, dhulma na ukandamizi.Wanawake wa Kiyunani,walikuwa wakipitia unyanyasaji sehemu kadhaa za maisha.
Upande wa Kiuchumi; Hawakuwa na haki ya kumiliki mali wala kufanya biashara au kuekeza na kwa upande wa Kisiasa wakawa hawana haki ya kushiriki katika maamuzi yoyote sawa iwe ni ktk utawala au uchaguzi. Ama katika upande wa Kijamii wakawa wakimilikiwa kama mali.Hata mahari ambayo ni haki yao,yalikuwa yakipangwa na kutwaliwa na jamaa zao wakiume pindi yanapotolewa.Baya zaidi,walinyimwa hata haki ya kuamua nani afaa kuwa mume wao.Yeyote atakae kuletwa na jamaa zake wakiume ndie mume.
2)Bara Arabu
Kabla ya kuchipuka nuru ya Dini ya Kiislam ulimwenguni;mtoto wa kike alikuwa akidharauliwa na Kupitishiwa mateso makubwa.Ikiwemo kuuliwa kwa kuzikwa akiwa ALlah ﷻ Atwambia namna ya hali ilivyokuwa:
“Na pale mtoto wa kike aliyezikwa hai atapo uliwa: Kwa dhambi gani aliuwawa?”
(Tak-wir: 8-9)
Mwanamke akiwa mja mzito,basi mume ambae ni babake mtoto alikuwa ashaingia kiwewe:Jee kutazaliwa mtoto wa kike?Ikiwa ni wa kike,basi huwa kama aloangukiwa na jabali kubwa kichwani.
“Na anapobashiriwa mmoja wao (kwa kuzaa) msichana, uso wake huwa mweusi (kwa hasira) na majonzi.Ajificha kwa watu kwa sababu ya ubaya wa alichobashiriwa. Jee,amshikilie kwa fedheha au amzike udongoni?Hakika ni maovu wanayo hukumu!”
( An-Nahl: 58-59)
Mfumo wa kibepari wenye kutawala ulimwengu kwa sasa;na ulobuniwa na Adams Smith na nidhamu yake ya utawala demokrasia,mwanamke ni chombo cha kujistarehesha(sexual toy).Kwa msingi huu mwanamke,ili apate kazi au kupandishwa cheo,humlazimu kunyanyaswa kingono na waajiri wake.Na hii hudhihirika leo jinsi matajiri wakuu ulimwenguni,hutumia mwili wake,ima ukiwa nuru au hata uchi wa mnyama, ktk matangazo ya biashara zao!Uko mbele kusambaza propaganda, kupinga na kuonyesha kama ni dhulma,unyanyasaji na kutomuheshimu mwanamke,kuoa zaidi ya mke mmoja! Lakini wakati ule ule,ni sawa na jambo la kuigwa na kulindwa kikatiba,kuwa na mahusiano ya kimwili na mahawara zaidi ya mmoja.Bali ni kutukuza uhuru wa kibinafsi.
Huku ukidai kuwa kumekuja kumkomboa mwanamke kwenye minyonyoro ya dhulma za kijinsia.Kwa kumtoa jikoni alikokiwa amefungiwa.Lakini mwisho wanamfungia afisini na mwanamume anaeutumia mwili wake atakavyo!Na mara nyingi wakisema hivi,huwa wakusudia Uislam.Kwa sababu, ndio mfumo pekee ambao ni tishio kwake.Fikra chafu ambazo zimeenezwa kupitia vyombo vya khabari vya kimagharibi,runinga na tawala za kidemokrasia ulimwenguni,zenye kwenda kinyume na hukmu za MwenyeziMungﷻ!
Masikitiko makubwa,ni kuwa fikra hizi zimepenyezwa mpaka ndani ya majumba ya Waislamu!Kwa kupitia taasisi za kielimu na mitaala yao.Na dada zetu,kwa kukosa malezi safi ya Uislamu na ulitima wa ilmu ya Dini yao tukufu ulokuja kuwakomboa na unyanyasaji,wamenywishwa sumu hizi! Bila kujua kuwa ujio wa Uislamu,ulikuwa pambazuko la kumpa heshima na kumpandisha cheo mtoto wa kike.Na kumtukuza kwa kumpa utu kamili!Tofauti na uhayawani uliopo kwenye mifumo,dini,mila na desturi nyingine kando na Uislamu!
Uislamu ulikuja na njia ya kipekee ya kumtukumza mwanamke na maanamume.Wote kama waja wa ALlah ﷻ.Hivyo kugawa majukumu baina ya jinsia hizi mbili: mume na mke.Na kila mmoja akipewa haki zake.Na kugawa majukumu haku,hakukuzingatia ubora wa jinsia.Bali kutatua tatizo kwa mujibu wa kila jinsia na mazingira yake,yalivyogawa na ALlah ﷻ.
Majukumu hayo,yako aina tatu:
Kwanza:Majukumu jumla: Haya huhusisha wote wawili bila kuzingatia au kujali jinsia.Kwa mfano:Ibada .ALlah ﷻAnasema wanawake na wanaume ni sawa mbele Za ALlahﷻ katika thawabu na adhabu:
“Mwenye kutenda mema mwanamume au mwanamke naye ni Muumini, tutamhuisha maisha mema…”
(An-Nahl:97)
Na katika ayah nyingine:
“Na Waumini wa kiume na Waumini wa kike,baadhi yao ni walezi wa wengine; wanaamrisha mema na wakataza mabaya, wanasimamisha Swalah na watoa Zakaat,na wamtii ALlah na Mtume Wake.Hao ndio watakaorehemewa na ALlah.Hakika ALlah ni Mwenye nguvu,Mwenye hikma.”
(Tawba: Aya 71)
B)Kupata elimu:Hii ni haki ya kila mtu.Bila kuangalia jinsi yake.Awe mume au mke ana haki ya kupata ilmu.Jjambo ambalo,lilikuwa hakuna nyuma kabla kudhihiri kwa Uislam. Mtume ﷺ atwambia:
Kutafuta ilimu ni fardh kwa kila Muislamu!
(Imepokewa na ibn Majah)
Jina ‘Muislamu’,lajumuisha jinsia zote mbili:ya kike au ya kiume.
Pili:Majukumu ya mwanamume
Uislamu ukamkalifisha mume kumuangalia mke upande wa chakula,mavazi,Makazi na vinywaji.Hili ni jukumu la mume na wala haijalishi mke ni bilionea hawajibiki ila akiridhia yy mwenyewe kuvua haki hii.MwenyeziMungu SWT anasema:
Na juu ya baba wa mtoto ni kuwapa riziki na mavazi yao kwa wema.
Tatu:Majukumu ya mke
Uislamu ukaamrisha mwanamke,awe ndie mlezi na msimamizi wa watoto.Haya ni baadhi ya majukumu ya mwanamke peke yake.Mume hafai kujitwika hata awe mahiri ktk kulea hafai, kumnyima mwanamke haki hio.Hivyo,dhulma na unyanyasaji zenye kubebwa na mila na desturi za watu binafs,hata wakidai kuwa Waislam,hazifai kurushiwa Uislamu.Bali lazima watu wapambanue tofauti kubwa baina ya :
1.Uislamu kama Dini (Mafundisho ya Qur’an na Sunnah).Ambao wafundisha kumtukuza na kumheshimu mwanamke.
2.Na baadhi ya mila au desturi za watu au jamii fulani zenye kujinasibisha na kuufuat Uislam, ambazo zinaweza kuwa kinyume na mafundisho ya Dini.
Uislamu Unawaheshimu Wanawake na kuwapa haki ya maamuzi ktk kila jambo lenye kuwahusu wao moja kwa moja.Kama kumpa mwanamke haki ya kuchegua mchumba.Jambo ambalo halikuwepo kabla wala kwa sasa ktk baadhi ya jamii
AbdaLlah bin Burayda (ra) amesimulia kutoka kwa babake kuwa:
“Msichana mmoja alikuja kwa Mtume ﷺ akasema:
“Hakika babangu ameniozesha kwa mtoto wa kaka yake ili kunyanyua hadhi yake ya chini.”
Mtume ﷺ akampa haki ya kuvunja ndoa hiyo. Msichana akasema: “Nimekubali yale aliyoyafanya babangu,lakini nilitaka kuwajulisha wanawake (wengine) kuwa kina baba hawana mamlaka ya kuwaozesha binti zao pasi na ridhaa zao!
(Imesimuliwa na Ibn Maja
Mafunzo haya yabainisha wazi kuwa,mwanamke ana haki ya kuolewa kwa hiari:
Ndoa ya kulazimishwa haikubaliki katika Uislamu.Sawa ulazimishaji uwe ni kwa:Kumletea mchumba ambae mschana hakumpenda au kumzuia kuolewa na mchumba aliempenda bora mchumba huyo awe ametimiza sifa tulizofundishwa Kisharia kustahiki kuoa.
MwenyeziMungu ﷻ Anasema:
“Basi msiwazuie kuolewa na waume zao ikiwa wamekubaliana kwa wema kati yao!
Mtume ﷺ alisema:
Haolewi mke mkuu bila maamuzi yake.Wala haolewi bikra mpaka kwa idhni (ruhusa) yake.”*
(- Bukhari na Muslim)
Haki ya kurithi: Uislamu,tofauti na mila,desturi na tamaduni nyingine,kumekuja kutambua haki ya kurithi na kumiliki mali kwa mwanamke.ALlah Atwambia:
“Wanaume wanayo sehemu katika yale waliyoacha wazazi na jamaa wa karibu,na wanawake wanayo sehemu katika yale waliyoacha wazazi na jamaa wa karibu, iwe kidogo au kingi ni sehemu iliyofaradhiwa!
Katika mafunzo ya Uislam,wanawake wanaruhusiwa kumiliki,kurithi, kufanya biashara, na kutumia mali yao bila ya kuingiliwa ndani ya mipaka ya Sharia kama mwanamume.
Haki ya kushiriki kijamii na kisiasa:
Katika taarikh ya Kiislam, wanawake walikuwa walimu, wafanyabiashara, na hata washiriki wa mashauriano ya kijamii,katika Baraza la Shura.
Chanzo cha Tuhuma kuwa Uislamu unanyanyasa Wanawake
1.Taasub ya kitamaduni:Baadhi ya jamii,licha kusilimu,badi hutekeleza mila na desturi kandamizi kwa wanawake kwa jina la Dini wakati si sehemu ya Uislamu.
2.Uelewa mdogo wa sheria za Kiislamu:Watu wengi wananyinwa makusudio fursa ya kusoma Uislam kama mfumo mbadala.Hivyo, huendekea kuchanganya mazoea ya jamii na Dini yenyewe.
3.Propaganda kutoka kwa vyombo vya habari vya Kimagharibi:Mara nyingi Uislamu huoneshwa kwa mtazamo hasi hasa kuhusu wanawake bila kuangalia muktadha au asili ya mafundisho yake.
Uislamu kwa asili yake unamtukuza mwanamke na kumpa heshima, haki,na nafasi ya kujitokeza katika maisha ya kidini, kijamii,na kiuchumi.Tatizo haliko kwenye Uislamu bali linatokana na uelewa mbaya au utekelezaji mbovu wa mila na desturi na watu ambao wajinasibisha na Uislamu.Ukiona mahali ambapo mwanamke anadhalilishwa kwa jina la Dini hakikisha unachunguza:
Jee,huu ni Uislamu wa kweli?Au ni mila na desturi zilizojificha nyuma ya dini?Wala si kukurupuka na kutupa tuhma dhidi ya Uislam
Hussein Muhammad.
Mwanachama wa Hizb-ut-Tahrir Kenya
16:Swafar 1447
11th August 2025