بسم الله الرحمن الرحيم
Mnamo 12 Disemba 2017 katika Uwanja wa Kasarani wakati wa sherehe za siku ya Jamhuri, Rais Uhuru Kenyatta katika hotuba yake alitangaza kwa taifa, mpango wake unaoitwa Ajenda 4 Kuu. Ajenda hizo nne zinajumuisha Ukuaji wa Viwanda, Utoshelezo wa Chakula, Makazi Bora na Afya kwa Wote. Ajenda 4 Kuu sio jambo geni kwani Ukuaji wa Viwanda na Utoeshelezo wa Chakula ni sekta kutoka Nguzo ya Uchumi ya Ruwaza ya 2030 na Makazi Bora na Afya kwa Wote ni sekta kutoka katika Nguzo ya Kijamii ya Ruwaza ya 2030.
Baada ya machafuko ya uchaguzi wa 2007 – 2008, serikali kuu ya muungano iliundwa na kujumuisha vyama vikubwa vya ODM kikiongozwa na Raila Odinga, cha PNU kikiongozwa na Mwai Kibaki na cha ODM-Kenya kikiongozwa na Kalonzo Musyoka. Viongozi hawa watatu kutoka katika vyama tofauti walikuwa Waziri Mkuu, Rais na Makamu wa Rais mtawalia baada ya janga la kisiasa mnamo Aprili 2008! Serikali kuu ya muungano ilibuni mchakato wa kuziunganisha manifesto zao za kabla uchaguzi na kuwasilisha Ruwaza ya 2030 ambayo ili zinduliwa rasmi mnamo Juni 2008!
Kwa uchanganuzi makini, Ajenda 4 Kuu sio chochote isipokuwa ni njama ya kukazanisha kitanzi shingoni mwa Wakenya kama inavyo fichuliwa zaidi ifuatavyo:
Kwanza, hakutarajiwi lolote jipya kutokana na viongozi walioko sasa ambao wamekumbatia nidhamu ya kiuchumi ya kisekula ya kirasilimali na sera zake ambazo hazina lolote zaidi ya kuwatajarisha warasilimali wachache (mataifa makubwa ya Kimagharibi) na vibaraka wao (kipote cha wanasiasa waliomo nchini). Lakutamausha zaidi ni kuwa wanaopigia debe Ajenda 4 Kuu ni watu wale wale kutoka 2008 hadi wa leo tofauti yao ni nafasi za vyeo walivyomo. Rais Uhuru Kenyatta – ambaye alihudumu katika serikali kuu ya muungano kama Naibu wa Waziri Mkuu na Waziri wa Fedha, Naibu wa Rais William Ruto – alihudumu katika serikali kuu ya muungano kama Waziri wa Kilimo. Zaidi ni kuwa, hivi sasa Raila Odinga amejiunga kama mshirika wa Uhuru Kenyatta kwa mujibu wa mkono wa kheri!
Pili, chini ya uongozo huu huu kulishuhudiwa na kunaendelea kushuhudiwa kashfa za ufisadi katika Mahindi, Kazi kwa Vijana, NYS 1 na 2, Anglo Leasing, Ardhi ya Ruaraka, Eurobond, SGR 1, NHIF, vifo vya raia kutokana na ukame, kuzidi kwa madeni makubwa kiasi cha trilioni Sh5.4 miongoni mwa nyingine!
Tatu, hivi sasa mchakato wa serikali wa kutimiza ajenda ya makazi bora unaelekea kusambaratika kwa kuwa unalenga kukazanisha vitanzi vilivyoko katika shingo za raia kupitia ushuru wa asilimia 1.5 usioingia akilini unaotarajiwa kutozwa wafanyikazi wanaopata mshahara ili kuweza kupata makazi ambayo umiliki wake utategemea njia ya bahati nasibu! Serikali itaweza vipi kujenga nyumba 500,000 kufikia 2022? Hili linakuwaja wakati ambapo Wakenya tayari wamesakamwa na ushuru wa mafuta wa asilimia 8 uliopitishwa Septemba 2018!
Nne, ajenda ya utoshelezo wa chakula inaelekea kusambaratika, kwani mpango wa shamba la kuzingatiwa linaloitwa Galana Kulalu la unyunyizaji maji haukuisha vyema kama ilivyo tarajiwa kutokana na kutupiana lawama baina ya serikali ya Kenya na Kampuni ya Israel, Green Arava ambao walipewa mkataba wa kufaulisha mradi huo. Zaidi ya hayo kuna tuhuma nyingi kuhusu matuzi mabaya ya mabilioni ya fedha yaliyo tengewa mradi huo!
Tano, ajenda ya afya kwa wote inaelekea kusambaratika kwani NHIF na Sekta ya Afya kwa ujumla imezama katika kashfa kubwa za ufisadi wa fedha!
Sita, ajenda ya ukuaji wa viwanda hivi sasa inafanya kazi japo kwa uchache kwa kuwa sekta ya nguo imo katika mchakato wa kutengeneza sare za polisi miongoni mwa majukumu mengine. Zaidi ya hayo, bado ni mapema kusema kuwa itaishilia kwa kufaulu kwani hivi sasa vikundi vya kimaslahi kutoka kila nyanja vinakwenda mbio kutafauta nafasi vikilenga kuwauzia serikali sare za polisi kutoka ng’ambo miongoni mwa bidhaa nyinginezo!
Kwa kuwa serikali ya Kenya imesimama juu ya mfumo wa kisekula wa kirasilimali ambao kipaombele chake ni manufaa/maslahi na uongozi wake upo kuhakikisha una watumikia wakoloni mabwana zao. Hivyo basi, Wakenya lazima wasitarajie lolote kutoka kwa hali iliyoko sasa ya gharama kubwa ya maisha na ambayo inaongeza pengo baina ya matajiri na masikini!
Kwa upande mwingine tunao Uislamu kama mfumo unaotoka kwa Muumba wa binadamu na ambao umetekelezwa kikamilifu na kudhihirisha kivitendo pasi na shaka yoyote ndani ya takriban karne 13 kwamba una uwezo wa kutatua matatizo ya wanadamu. Uislamu chini ya Khilafah iliyosimamishwa kwa njia ya Utume, sera yake ya kiuchumi imekitwa kuhakikisha kuwa usambazaji wa mali unafanyika kwa njia ya haki na kwa raia wake wote. Kwa kudhamini watu binafsi mahitaji yao msingi: maji, chakula, makaazi na mavazi kwa kuweka mazingira mazuri ya watu/wanaume (wasimamizi wa familia) kufanya kazi ili wapate riziki. Ikiwa kufanya kazi/kutofanya kazi hakupelekei kukidhi mahitaji msingi basi ndugu zake wanabeba jukumu hilo la kumpa mahitaji msingi na ikiwa nao hawana uwezo basi Khilafah inaingilia kati na kumpa mahitati yake na hata kumuwezesha kukidh mahitaji ya ziada na wakati huo huo kusimamia mahitaji ya mujtama: usalama, elimu na afya n.k. Khilafah itaweza kumkidhia kutokana na Zaka iliyokusanywa ambayo imefungwa kwa watu aina nane pekee. Pia ikiwa Zaka haikutosha, basi itatumia mali iliyoko ndani ya Baitul Mal na kama haitoshi, basi matajiri Waislamu wataombwa kulipa ushuru kwa muda kutoka katika mali yao ya ziada ili kuweza kutatua dharura iliyopo na pale dharura hiyo ikiondoka basi ushuru huo nao unasitishwa mara moja. Zaidi ya hayo, Uislamu umejifunga na dhahabu na fedha kama sarafu ya matumizi ndani ya mzunguko wake wa kiuchumi na wakati huo huo umeharamisha utozwaji ushuru na riba kwa aina zake zote, upangaji wa bei, uhalifu, uhadaifu na ukiritimba katika biashara na urundikaji wa utajiri miongoni mwa maovu mengineyo. Ndani ya Khilafah inayoendesha sera ya kiuchumi aina hiyo, raia watawezeshwa kufurahia baraka za Muumba wao kwa kuwa riziki zao zitakuwa zimewekwa salama na hivyo kupelekea kupata utulivu, maendeleo na ustawi wa kweli.
Kwa kuhitimisha, Kenya na Afrika kwa ujumla zinatakiwa kuutizama tena mfumo wa Uislamu lakini isiwe kwa sura ambayo inayotokamana na tafsiri ya Uislamu kwa mujibu wa Wamagharibi. Hakuna shaka kuwa mfumo wa Kiislamu ndiyo mfumo mbadala na wenye uwezo wa kutatua matatizo na majanga yaliyo sababishwa na mfumo batili uliofeli wa kisekula wa kirasilimali unaotokana na akili yenye kikomo ya mwanadamu na ukijumuisha na nidhamu yake ya kiuchumi ya kirasilimali, nidhamu ya kidemokrasia na nidhamu ya kijamii ya kiliberali (uhuru) miongoni mwa nyinginezo! Hivyo basi, Kenya na Afrika lazima zikumbatie ulinganizi wa kurudisha tena maisha ya Kiislamu kupitia kusimamisha Serikali ya Kiislamu ya Khilafah kwa njia ya Utume.
Ali Nassoro Ali
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya