Chini ya Kisingizio cha Ugaidi Waislamu Wanakumbwa na Idhilali na Mateso

Taarifa kwa Vyombo vya Habari

Umma wa Kiislamu nchini Kenya kwa mara nyengine tena kwa mshtuko mkubwa mnamo Ijumaa, tarehe 16 Februari 2018, ambapo mmoja wao Hania Sagar (mkewe msomi wa Kiislamu aliye uwawa kishahidi, Aboud Rogo) alihukumiwa kifungo cha miaka kumi gerezani katika mahakama moja jijini Mombasa. Kulingana na uamuzi wa hakimu kosa lake lilikuwa ni kupanga njama ya kufanya uhalifu, shambulizi la kigaidi dhidi ya kituo cha Polisi cha Central! Siku iliyofuatia ambayo ni Jumamosi, tarehe 17 Februari 2018 mwengine katika Umma Sheikh Guyo Gorsa alihukumiwa na Mahakama ya Kisheria ya Milimani jijini Nairobi kwa tuhuma za kuwa mwanachama wa kundi la kigaidi la Al-shabab.

Matukio mawili haya ni miongoni mwa mengi ambayo hatukuyaangazia ndiyo matukio mapya zaidi yenye uchungu mwingi yaliyo ukumba Umma wa Kiislamu nchini Kenya na pasi na shaka yanathibitisha kuwa vita dhidi ya ugaidi vimekusudiwa kulenga Uislamu na Waislamu. Katika Vita hivi dhidi ya Ugaidi, Waislamu wanadhalilishwa na kukumbwa na mateso ulimwengu mzima. Ni kwa nini Uislamu na Waislamu wawe ndio walengwa katika vita hivi vya kimagharibi? Uislamu kama mfumo kamili wa maisha uchipuzao kutoka kwa Muumba wa viumbe unaafikiana na umbile la mwanadamu na kutoa suluhisho ya matatizo yote yanayomkabili mwanadamu katika maisha yake yote. Hivyo basi, Uislamu ndio mfumo pekee badili na kamili katika kuchukua mahali pa mfumo batili wa kisekula wa kirasilimali uchipuzao kutokamana na akili finyo ya mwanadamu na ambao unagongana na umbile lake na hivyo ndio kiini cha matatizo yote yanayomkabili mwanadamu leo katika nyanja za maisha ikiwa ni pamoja na kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Tangu kuvunjwa kwa dola ya Kiislamu ya Khilafah mnamo 3 Machi 1924 dola za kimagharibi zinang’ang’ana katika kuuhifadhi na kuusitiri mfumo wao batili wa kisekula wa kirasilimali unaotarajiwa kuanguka wakati wowote. Hivyo basi, zikiongozwa na Amerika wameunda kampeni ya kuuangamiza Uislamu na Waislamu, miongoni mwa nguzo za kampeni hii ni:

  1. Utumiaji wa vyombo vya habari vya kiulimwengu kama silaha hatari vinavyo tawaliwa na Amerika na washirika wake, kulingania miito yake ya (demokrasia, vyama vingi, haki za kibinadamu na uhuru aina nne wa watu (uhuru wa kuabudu, uhuru wa kujieleza, uhuru wa kumiliki na uhuru wa kibinafsi). Kuharibu sura ya Uislamu na kuchochea ulimwengu kuwa dhidi ya wale wanaoshikamana nao, kwa kuwaonyesha kuwa wenye siasa kali, waliovuka mipaka, wenye misimamo mikali na magaidi nk.
  2. Utumiaji watawala vibaraka na mzunguko wa wasaidizi wao, wanafiki, wapatilizaji fursa, na wale walio pagawa na thaqafa huru fisidifu ya kimagharibi na kuvutiwa na mfumo wake wa kimaisha. Mzunguko huu pia unajumuisha wale wanaojifanya kujali Uislamu ima wawe ni mashekhe wa kiserikali au wale wanaowasilishwa kwa watu kama wasomi wa Kiislamu kutoka katika baadhi ya harakati za Kiislamu ambao kiuhalisia si wengine isipokuwa ni walingizi wanaolingania kutenganishwa kwa dini na maisha (masekula).

Kwa nguzo zilotabanniwa kama hizi, Amerika na washirika wake wametangaza vita vya kiulimwengu vya dhahiri kwa Muislamu yeyote atakaye simama na kukiuka miito yao hiyo kwani mtu huyo atakuwa ni tishio kwa hadhara yao ya kimagharibi na hatimaye kwa mfumo wao batili wa kisekula wa kirasilimali. Nchini Kenya mabepari wa kimagharibi wakiongozwa na Amerika wameanzisha mashambulizi rasmi ya kivitendo dhidi ya ugaidi kwa kutumia uvamizi wa jeshi la Kenya almaarufu KDF nchini Somalia mnamo 16 Oktoba 2011. Huku kindani ikishinikiza kauli ya Misimamo Mikali kama lakabu zinazo bandikiwa mtu yeyote atakaye lingania au kuunga mkono kushikamana na Uislamu kiukamilifu.

Serikali ya Kenya kama ilivyo kwa serikali yoyote ya kikoloni utiifu wake kiakili unahitaji kusujudu ili kupata ufadhili wa kifedha kutoka kwa wamagharibi ambao umefungamana na ajenda maalumu ambayo ni fiche inayo jumuisha miongoni mwa mengine kuanzisha vita dhidi ya Uislamu na raia wake Waislamu kama inavyo ongozwa na mpangilio wa sera ya kimagharibi ya Vita dhidi ya Ugaidi. Matukio haya mapya ni sehemu ndogo tu katika makubwa ikilinganishwa na uzito mkubwa wa hivi Vita dhidi ya Ugaidi vilivyo fadhiliwa na dola za kimagharibi dhidi ya Waislamu k.m. nchini Syria, Misri, Tajikistan, Uzbekistan, Urusi nk. Allah (swt) asema:

أَمْ حَسِبْتُمْ أَن تَدْخُلُواْ ٱلْجَنَّةَ وَلَمَّا يَأْتِكُم مَّثَلُ ٱلَّذِينَ خَلَوْاْ مِن قَبْلِكُم مَّسَّتْهُمُ ٱلْبَأْسَآءُ وَٱلضَّرَّآءُ وَزُلْزِلُواْ حَتَّىٰ يَقُولَ ٱلرَّسُولُ وَٱلَّذِينَ آمَنُواْ مَعَهُ مَتَىٰ نَصْرُ ٱللَّهِ أَلاۤ إِنَّ   نَصْرَ ٱللَّهِ قَرِيبٌ

“Mnadhani kuwa mtaingia Peponi, kabla ya kukujieni kama yaliyo wajia walio pita kabla yenu? Iliwapata shida na madhara na wakatikiswa mpaka Mtume na walio amini pamoja naye wakasema: Lini nusra ya Allah itakuja? Jueni kuwa nusra ya Allah iko karibu!” [Al-Baqara: 214]

إن مع العسر يسرا

Hakika, uzito uko pamoja na wepesi [Ash-Sharh: 6]

Shabani Mwalimu

Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari Hizb ut Tahrir Kenya

KUMB: 05 / 1439 AH

Jumapili, 02 Jumada II 1439 H

18/02/2018 M

 

Simu: +254 707458907

Pepe: mediarep@hizb.or.ke