Huduma ya Afya ndani ya Khilafah

Kenya imeshuhudia ndani ya mwezi wa Julai 2019 vifo vya watu maarufu, Bob Collymore –Afisa Mkuu Mtendaji wa Safaricom, Ken Okoth –Mbunge wa Kibra na Dkt. Joyce Laboso –Gavana wa Kaunti ya Bomet. Kinachojitokeza kwa waliokufa ni kwamba wote walifariki kwa saratani na kabla hapo  walikwenda ng’ambo kutafuta matibabu. Kwa upande mwingine watu wengine maarufu kama Beth Mugo alipatikaniwa na saratani ya titi na Anyang Nyong’o alipatikaniwa na saratani ya tezidume na wote walitibiwa Marekani. Vyombo vya habari vikuu vilisheeni miito ya kuitaka serikali kutangaza kuwa saratani ni janga la kitaifa na kubuni mipango ya kupambana nayo!

Ukweli ni kwamba wengi wa raia masikini wanaendelea kutaabika na kufa kimya kimya kutokana na saratani na maradhi mengine wakiwa hawana uwezo wa kupata huduma ya afya hapa nchini na nga’ambo. Lakini kwa kuwa sio matajiri, kesi zao hazipati nafasi ya kuangaziwa katika vichwa vikuu vya vyombo vikuu vya habari. Vifo vya kuhusiana na saratani ni sehemu tu ya tatizo kubwa bali ukweli ni thibitisho kwamba huduma ya afya nchini Kenya ni ya hatari na iliyojaa maradhi yanayotishia maisha na yanayoweza kutibika, wagonjwa kuwa na elimu chache juu ya afya, michakato ya tiba ambayo imehakikiwa vibaya kwa kuwa misingi yake haitokani na ushahidi wa kimatibabu, kukosekana kwa mjumuiko wa huduma ya afya kutoka kwa taasisi msingi, upili na za juu, mafunzo duni ya kimatibabu na kukosekana kwa utafiti wa matibabu yanayohusika maradhi ndani ya nchi na mahitaji ya kiafya. Zaidi ya hayo sekta binafsi hivi sasa ndiyo inayo dhibiti nidhamu ya huduma ya afya na kuigeuza kutoka kuwa ni huduma na haki na kuifanya ni biashara na anasa!

Kenya kama ilivyo dola nyingine za kisekula dunia kote utawala wake unapeana kipaumbele manufaa kupitia kushirikiana na makampuni ya bima yanayomilikiwa na kikundi cha matajiri kwa lengo la kuwapora raia mapato yao kupitia sera za ukandamizaji za bima kwa jina la kuwasaidia. Na mpango wa hivi karibuni ni Huduma ya Afya kwa Wote. Vitendo vyao vinadhihirishwa na mfumo wao batili wa kirasilimali unaochipuza kutoka katika akili ya mwanadamu iliyo na kikomo ambao unayatizama maisha ya raia kwa sura ya kiuchumi. Hivyo basi, utawala wa kisekula unatoa huduma za afya kwa lengo la kupata wafanyikazi walio na afya njema ili kuweza kuchangia katika uchumi!

Kinyume chake ni Uislamu, mfumo safi unaochipuza kutoka kwa Muumba wa kila kilichoko unaitizama huduma ya afya kuwa ni hitajio la umma na hivyo ni jukumu la serikali kuwapa raia wote pasina kuzingatia dini au rangi zao. Mtume (saw) alisema: «الإِمَامُ رَاعٍ وَهُوَ وَمَسْؤُولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ»Imamu (mtawala) ni mlinzi, na mwenye majukumu (na ataulizwa) juu ya anaowatawala.” [Bukhari na Muslim] Hivyo basi, Khalifah kama mlinzi lazima asimamie mambo ya watu aliyopewa amana kuwahudumia. Mambo hayo yalijumuisha kuwapa nafasi za kuwawezesha kukidhi mahitaji ya raia waliyopewa na Mwenyezi Mungu (swt). Mtume (saw) alisema:”Mwana wa Adamu hana haki bora zaidi ya kuwa na nyumba ambamo ataishi, kipande cha nguo ambacho ataweza kuhifadhi uchi wake na kipande cha mkate na maji.” [Tirmidhi] na Yeye (saw) alisema: “Yeyote atakayeamka akiwa salama miongoni mwa watu wake, akiwa na afya (kimwili) na akiwa na chakula cha siku hiyo, ni sawa na kama ambaye dunia yote imekusanywa mbele yake.” [Tirmidhi na Ibn Majah]

Hivyo basi, Khalifah amefaradhishiwa na Shari’ah (Qur’an na Sunnah) kutumia kutoka katika Bai ul-Mal ambayo mapato yake ni ya daima na hayatokani na utozaji ushuru kama inavyo shuhudiwa hivi leo. Kwa sababu hiyo Khilafah itatoa huduma ya afya bora kwa kwa wote (Waislamu na wasiokuwa Waislamu). Kwa kuwa nidhamu ya Uislamu inatizama utoaji wa huduma ya afya kwa raia wake kwa sura ya kiubinadamu na sio sura ya kiuchumi. Hii inamaanisha kwamba Khalifah wa Dola ya Kiislamu atakwenda mbio kutoa huduma ya afya ya kutosha na ya kiwango cha juu kwa watu na sio kwa ajili ya kupata wafanyikazi walio na afya njema ili waweze kuchangia katika uchumi bali ni kwa ajili ya kutekeleza jukumu lake la kuwasimamia watu mambo yao kwa kumtii Mwenyezi Mungu (swt)

Kwa kutamatisha, tuungane na kufanya kazi kurudisha maisha ya Kiislamu kupitia kusimamisha Dola ya Kiislamu ya Khilafah kwa njia ya Utume ndani ya taifa la Waislamu. Khilafah itatatua janga la huduma ya afya kwa kuondosha hali hii ya sasa ya kutamausha iliyoko duniani ambayo ni ya kusikitisha kinyume na ilivyokuwa katika enzi ya Khilafah. Khilafah iliwekeza katika sekta ya huduma ya afya kwa umma kwa mujibu wa maamrisho ya Mtume (saw). Kwa mfano wakati wa Ghazwah Khandaq alikutana na wanajeshi waliopata majeraha na yeye (saw) aliagiza kuwa wawekewe hema ili kuwapa huduma za matibabu. Hospitali za Ummah au “Bimiristan” (Nyumba ya Wagonjwa) zilikuwa ni afueni kwa watu. Zilihudumikia watu wote pasina kuzingatia rangi, dini, uraia au jinsia zao. Hospitali ya al-Mansuri iliyoasisiwa Cairo mnamo 1283 ilikuwa na nafasi ya wagonjwa 8,000. Kulikuweko na wauguzi wawili ambao walihudumikia mgonjwa mmoja na ambao walifanya kila kitu kumuwezesha mgonjwa kupata utulivu na furaha na kila mgonjwa alikuwa na kitanda chake, mavazi na vyombo vyake vya kulilia. Hospitali iliwatibu wagonjwa wakulala na wakuondoka kwa kuwapa chakula na dawa za bure. Kulikuwepo na zahanati na kliniki kwa ajili ya huduma za matibabu bora kwa waliokuwa na ulemavu na waliokuwa wakiishi sehemu za mbali. Hakika, ni Khilafah pekee ndio itakayowapa wanadamu lengo la kweli maishani, utulivu na ufanisi wa kweli kwa kutabikisha Uislamu kiukamilifu katika kila nyanja ya maisha kwa kutekeleza nidhamu za Uislamu zinazojumuisha za kiuchumi, kijamii, kisiasa, kielimu na sera ya kigeni.

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya

Makala Na.56: Ijumaa, 01 Dhul-Hijja 1440 | 2019/08/02