Hicho ni kichwa cha habari katika Business Daily mnamo 5 Disemba 2018 kikiashiria serikali iliyochanganyikiwa na iliyouma meno kuhakikisha ina kaza kitanzi shingoni mwa raia wake! Kenya hivi sasa imo ndani ya maumivu ya deni la Trilioni Sh.5.15! “…Kwa mujibu wa Sheria ya Fedha, 2018 ushuru wa kukadiriwa utaanza kulipwa kuanzia Januari 1, 2019. Walipaushuru wote wanaostahili wanashauriwa kulipa ushuru wa kukadiriwa wakati wa malipo ya ada ya kibali au leseni ya biashara,” ilisema KRA katika ilani iliyopeperushwa katika magazeti ya humu nchini. (https://www.businessdailyafrica.com, 05/12/2018).
Serikali ya Kenya kama dola nyengine yoyote ya kisekula ya kirasilimali matakwa ya nidhamu yake ya kiuchumi ya kirasilimali ni kuwa utozaji ushuru na ukopaji ndiyo yawe machimbuko msingi ya mapato ya serikali. Hivyo basi, matumizi yake yanategemea utozaji ushuru na mikopo ya riba. Kinachoshangaza ni kuwa Kenya imebarikiwa na rasilimali nyingi k.m. madini, ardhi ya ukulima, vyanzo vingi vya maji na hivi karibuni kugunduliwa kwa mafuta, titanium nk. ambayo yangeweza kuisukuma Kenya katika ukombozi wa kiuchumi kiulimwengu lau kama yangetumiwa vizuri! Lakini, kwa sasa karibu rasilimali zote hizi zimebinafsishwa na kukabidhiwa kampuni za kimagharibi ambazo hulipa malipo duni kwa serikali ya Kenya. Zaidi ya hayo, kiwango kikubwa cha mapato kikisafirishwa ng’ambo na kunufaisha uchumi wa nchi za kimagharibi kwa gharama ya uchumi wa Kenya! Upande mwingine, raia wanadidimizwa katika maisha ya umasikini zaidi kutokana na mikakati isiyokuwa na huruma ya utozaji ushuru na uchukuwaji mikopo isiyoingia akilini!
Uislamu chini ya Khilafah (Dola ya Kiislamu) iliyosimamishwa kwa njia ya Mtume (saw), utatekelezwa kwa ukamilifu ikiwemo nidhamu ya kiuchumi ya Kiislamu ichipuzayo kutokana nayo. Sera ya kiuchumi ya Kiislamu itakuwa kudhamini ushibishaji wa mahitaji yote msingi ya kila mtu binafsi kikamilifu, na kisha kumwezesha kushibisha mahitaji yake ya ziada kwa kadri awezavyo kama mtu anayeishi katika jamii maalumu iliyo na mfumo fulani wa kimaisha.
Katika Khilafah (Dola ya Kiislamu) Hazina ya Dola (Bait ul-Mal) itajumuisha machimbuko ya mapato yafuatayo: Ngawira (Fai’), Ghanima, Kharaj, Jizya, aina tofauti tofauti za mapato ya mali ya Ummah, mapato ya mali ya Dola, Ushr, Khumus kutokana na Rikaz, madini na pesa za Zakat. Tanbihi: ushuru uliotajwa hapa (Ushuru wa ardhi na Jizya) haupaswi kufahamika kimakosa kama huu unaotozwa leo juu ya watu na serikali za kisekula. Utozaji ushuru na mikopo ya riba imeharamishwa katika Uislamu. Khilafah haitatoza ushuru juu ya raia wake isipokuwa katika baadhi ya hali kama ukame na Jihad. Lakini, ushuru huo, utatozwa juu ya utajiri uliozidi kiwango cha kawaida ambacho mtu hutumia kushibisha mahitaji yake msingi na ya ziada. Hivyo basi, hufikia haki ya thamani ya maisha kwa kila mmoja kibinafsi, na kusahilisha kupatikana kwa mahitaji ya ziada. Wakati huo huo Uislamu umeweka mipaka ambayo mtu aweza kuchuma ili kushibisha mahitaji yake msingi na ya ziada na kupanga mahusiano yake na wengine kwa mujibu wa nidhamu maalumu.
Mwamko wa Kenya na Afrika kwa ujumla uko katika kubadilisha mfumo wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake chafu zitokanazo nao ikiwemo ile ya kijambazi ya demokrasia, nidhamu dhalimu ya kiuchumi na uhuru wa kijamii nk, ambazo ndio chimbuko la mateso na majanga yanayoikumba. Badala yake, kukumbatia mradi wa Khilafah chini ya ulinganizi wa mwamko wa Kiislamu, ambao kwa sasa umeenea ulimwengu mzima na ambayo kusimamishwa kwake tena kwa njia ya Mtume (saw) itaipeleka Kenya na Afrika katika hadhara kuu iliyojaa utulivu, amani na ufanisi ambayo kamwe hayajawahi kushuhudiwa mbeleni katika enzi zote za ukandamizaji wa kisekula wa kikoloni!
Ali Nassoro Ali
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya