Kuongeza Idadi ya Nafasi zaidi Kwa Wanawake Bungeni na Serikalini Kattu Hakutookoa Mwanamke wa Kawaida Kwenye Makucha ya Ubepari
Habari:
Bunge la Kenya kwa sasa limo kwenye mchakato wa kujadili kupitishwa kwa mswada wa Kijinsia 2018 unaopendekeza marekebisho ya vifungu vya katiba vya 90, 97 na 98, ili kuafikia utekelezwaji wa kanuni ya Kijinsia ya thuluthi mbili katika Bunge la Kitaifa. Kuafikia kwa kanuni hiyo ni kupitia kubuniwa kwa viti maalumu vitakavyo hakikisha utekelezwaji wa kanuni hiyo ndani ya bunge kwa kipindi cha zaidi ya miaka ishirini kutoka kipindi cha kufanyika uchaguzi mkuu. Watetezi na wadhamini wa mswada huu wanashikilia kwamba lengo kuu la kuutaka upitishwe ni kuhakikisha kwamba uwakilishaji bungeni na baraza la Seneti unaenda sambamba na kanuni ya thuluthi mbili ya kijinsia kama ilivyo dokezwa kwenye kifungu cha 81(b) cha katiba ya Kenya.
Maoni:
Mswada huu umesifiwa na wapigiaji debe kama ‘Mswada wenye hatua imara’ unaolenga kuweko na usawa wa kijinsia. Wabunge wanawake pamoja na ”wanaharakati” wa kupigania haki za wanawake wanadai kwamba mswada huu ni chombo muhimu kitakachosaidia kutatua tatizo la mwanya wa kijinsia hivyo ni muhimu sana kwani ni hatua muhimu ya kutoa nafasi sawa za kazi kwa jinsia zote mbili na kuwezesha ushindano sawa katika nyanja zote. Wanaouunga mkono wanashikilia kusema kwamba mswada huu hauwahusu tu wanawake bali unalenga pia kujumuisha uwakilishaji wa jamii zilizotengwa na kupuuzwa kwa muda mrefu miongoni mwao wakiwa walemavu, vijana na kabila zenye idadi ndogo.
Tamko Jinsia lililoko kwenye mswada huu tayari linatoa mtazamo finyo wa kirasilimali wa kufanya jinsia kuwa ndio kigezo cha kutatua matatizo ya watu. Fikra ya usawa wa Kijinsia imekuja na wamagharibi ambao wanahistoria ndefu ya unyanyasaji wa wanawake chini ya mfumo wao muovu wa Kirasilimali. Kupitia Mradi wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa. (UNDP) na wanaharakati wa ukombozi wa wanawake, Warasilimali wakaweka kiashirio kinachojulikana kama Gender Empowerment Measure (GEM), wanachokitumia kupimia ukubwa wa utofauti wa kimapato wa kijinsia ulimwenguni kote. Kipimo hiki huangalia makadario ya uzalishaji wa mapato ya wanawake, kupata kazi na vyeo vya ngazi ya juu serikalini zenye mishahara mikubwa, kuwastawisha kiuchumi na kupata nafasi za uakilishi kwenye mabunge. Kwa Mtazamo huu duni, wamagharibi kimakusudi wanalenga kufuta taswira katika mabongo ya watu wasielewe kwamba Urasilimali kwa miongo mingi umekuwa na dori kubwa katika kupuuza na kubagua jamii kwa miongo mingi. Mfumo huu umesababisha mwanya mkubwa katika kumiliki rasilimali, kukandamiza watu kiuchumi na hili ni kwa kuyapa mataifa makubwa ya kikoloni ya kimagharibi kuleta viongozi waovu wanaojali tu maslahi yao ya kiuchumi- jambo lililowafanya mamilioni ya wanawake kukosa elimu, afya na makaazi.
Hoja kwamba kupitia kuongeza idadi zaidi ya viti vya uwakilishi wa wanawake kwenye mabunge na kuwateua kwa nafasi za kisiasa ni kuwainua kiuchumi na kisiasa ni urongo mtupu. Hii ni kwamba hata mataifa jirani ya Kenya kama vile Tanzania, Rwanda na Uganda licha ya kuwa na idadi kubwa ya wabunge wanawake katika mabunge yao lakini bado maisha ya wanawake katika mataifa hayo ni mabaya mno. Ukweli ni kwamba katika siasa ya Kidemokrasia, uongozi sio amana ya kusimamia na kuchunga maslahi ya umma bali tu ni mradi wa kujitajirisha. Kama yalivyo mataifa ya kidemokrasia, Kenya siasa yake hudhibitiwa na kupelekwa na tabaka maalum la matajiri wakubwa wachache na familia zao ambao kikawaida huwa na mshawasho mkubwa wa kisiasa bali michakato yote ya kisiasa hupelekwa kulingana na maslahi yao. Na la kinaya zaidi wadhamini wa mswada huu na wanaoupigia debe wanaungana na wabunge wenzao kwenye jaribio la tamaa ya fisi kutaka kujiongozea marupurupu makubwa ati waweze ‘kuhudumikia watu vyema’. Hii ni licha ya kuwa wao ni miongoni mwa wabunge wanaopokoea mishahara mikubwa zaidi ulimwenguni. Marupurupu hayo yanajumuisha kupewa nyuma bure, magari ya serikali, pesa za huduma ya afya, gharama za usafiri na mfuko wa kugharamia harakati zao katika maeneo ya bunge wanayowakilisha.
Uislamu kama mfumo kamili wa kimaisha una muundo bora wa kipekee wa serikali (Khilafah) unaodhaminia heshima, haki na ufanisi sio tu kwa wanawake kwa wanadamu wote. Kutekelezwa kwake Uislamu ndani ya serikali yake haki za kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa wanawake zilipatikana kikamilifu. Hivyo Inshaallah kwa kurudi tena Khilafah hivi karibuni wanawake watahamasishwa wawe wanachama wa vyama vya kisiasa, kushiriki katika uchaguzi wa kumchagua Khalifa, kuchaguliwa pia kama wawakilishi kwenye baraza maalumu la ushauri (Majlis Ummah). Hatua hii itawawezesha kutoa malalamishi kwa mahakama maalum iitwayo Mahkamatul Madhaalim inayosikiza kesi dhidi ya watawala. Khilafah bila shaka itakuwa ni dola ambayo mwanamke kuwa na sauti ya kisiasa itakuwa kweli ni suala lenye uzito mkubwa wala sio kama ilivyo leo kuwa sauti zao imekuwa domo kaya.
Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut-Tahrir na
Shabani Mwalimu
Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari Hizb ut Tahrir Kenya