بسم الله الرحمن الرحيم
Nigeria ilingia katika zoezi la upigaji kura za kitaifa Jumamosi, 23 Februari 2019 baada ya Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (INEC) kuhairisha tarehe ya awali ya Jumamosi, 16 Februari 2019 saa tano kabla ya muda uliopangiliwa. Baada ya kura za Kitaifa kura za Majimbo zitafuatia mnamo Machi 2019. Kura za kitaifa ziliwavutia wagombea 73 wa urais kukiweko na rekodi kubwa ya wapiga kura waliosajiliwa ya 82,344,107! Wagombea wakuu wakiwa ni raisi aliyekuweko mamlakani Muhammadu Buhari (akiwa na miaka 76) –All Progressive Congress (APC) na Atiku Abubakar (akiwa na miaka 72) –Peoples Democratic Party (PDP). Muhammadu Buhari alimshinda Atiku Abubakar na kuchaguliwa tena kwa hatamu ya pili na kutangazwa mshindi na INEC siku ya Jumatano, 27 Februari 2019. Kwa upande mwingine, Atiku Abubakar alipinga matokeo hayo.
Nigeria ni taifa la kisekula lililo koloniwa na Uingereza kutoka 1800 hadi 1960 na baada ya kupata uhuru bandia ilibakia katika fujo la kuendelea huku tawala za kijeshi zilizoegemea Uingereza na Amerika zikishindana katika kupinduana na kuchukua mamlaka. Mfano mzuri ni ule wa Olusegun Obasanjo kibaraka wa Amerika alichukua mamlaka kama mtawala wa kijeshi wa Nigeria kutoka 13 Februari 1976 hadi 1 Oktoba1979. Muhammadu Buhari kibaraka wa Muingereza alichukua mamlaka kama mtawala wa kijeshi wa Nigeria kutoka 31 Disemba1983 hadi 27 Agosti 1985. Kisha baadaye Olusegun Obasanjo na Atiku Abubakar walichukua mamlaka kwa kuchaguliwa kidemokrasia kwa tiketi ya PDP kama rais na makamu wa rais mtawalia kutoka 29 Mei 1999 hadi 29 Mei 2007. Chama kinachoegemea Marekani cha PDP kilibakia mamlakani wakati wa enzi ya Olusegun Obasanjo (1999 – 2007), Umaru Musa (2007- 2010) na Goodluck Jonathan (2010 – 2015). Muhammadu Buhari (APC) anayeegemea Uingereza akachukua mamlaka kidemokrasia (2015 – 2019) na kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili wa miaka mine kuanzia (2019 – 2013).
Nigeria ni ya 1 Afrika na ya 31 duniani kwa uchumi (GDP) mkubwa wa zaidi ya dola bilioni 397,472 na ikiwa na idadi ya watu zaidi ya milioni 180. Nigeria ni nchi ya 3 duniani yenye watu wachanga baada ya India na Uchina ikiwa na zaidi ya watu wachanga milioni 90 na wengi wao wakiwa chini ya umri wa miaka 18. Wafuasi wengi wa dini ni wa Kiislamu ambao wengi wako kaskazini mwa Nigeria kisha wanafuatiwa na wakristo kutoka kusini mwa Nigeria. Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, Nigeria ni moja kati ya nchi tano duniani ambazo zimechangia kuwepo na watu milioni 368 ambao ni nusu ya watu walio katika umasikini wa kupindukia duniani! Fauka ya hayo, Benki ya Dunia ilitangaza kuwa Nigeria itaipita India na kuwa nchi ya kwanza duniani inayoongoza kwa idadi kubwa ya masikini wa kupindukia! (theeastafrican.co.ke, 06/02/2019) Kinaya, ni kuwa kwa mujibu wa ripoti ya Wealth-X, nchi ambazo zinatarajiwa kutoa mamilionea wapya kwa idadi kubwa ndani ya miaka mitano ijayo ndani ya Afrika ya kwanza ni Nigeria. (africabriefing.org, 22/01/2019)
Hayo yanadhihirisha kuwa Uchaguzi wa 2019 Nigeria ni muendelezo wa mazoezi ya kisanii yanayopigiwa debe na vibaraka watawala wakoloni ili kuyatumia kama upigaji chapa na uhalalishaji wao kuingia mamlakani ili kuhifadhi maslahi yao ya kibinafsi na ya mabwana zao na hatimaye kumakinisha usekula urasilimali kupitia kuwatumia na kuwadanganya watu wasiokuwa makini. WaNigeria wanataabika katika umasikini wa kupindukia, ufisadi, machafuko ya kikabila, vita vyenye msukumo wa kimagharibi vya ugaidi na maovu mengine yanayoendelezwa na mfumo batili unaotawala wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake zinazojumuisha nidhamu ya kiuchumi ya ukandamizaji, nidhamu ya kijamii ya kiliberali na nidhamu ya kidemokrasia. Muhammadu Buhari na Atiku Abubakar wote ni vibaraka wa Magharibi na Waislamu lakini Uislamu wao ni ule unaoambatana na mtizamo wa Kimagharibi juu ya Uislamu kama Uislamu Poa. Hivyo basi, wote ni Waislamu poa ambao ni wavumilivu wa dini nyingine na wanashindana kati yao ili kuhakikisha kuwa wanadhamini uhuru wa kisekula: uhuru wa kuabudu, uhuru wa kumiliki, uhuru wa maoni na uhuru wa kibinafsi ambazo zapigiwa debe na mabwana zao wa Magharibi wakiongozwa na Amerika na washirika wake duniani chini ya kisingizio cha “kuendeleza Demokrasia.” Na ndio maana Nigeria inafahamika duniani kuwa ndio kiigizo cha Demokrasia ndani ya Afrika tokea 29 Mei 1999, siku ambayo Obasanjo alipoingia mamlakani kama rais wa kwanza kwa kuchaguliwa kidemokrasia ndani ya Nigeria baada ya miaka 16 ya utawala wa kijeshi ambayo hivi sasa inaadhimishwa kama Siku ya Demokrasia na siku ya mapunziko ya Umma nchini Nigeria!
Nigeria na Afrika kwa ujumla ni bara lililo barikiwa na rasilimali nyingi mno za madini pamoja na ardhi yenye rutuba, ambazo zilistahili kulinyanyua na kuliweka ngazi za juu zaidi za maendeleo ya kisiasa, kijamii na kiuchumi na ufanisi. Lakini, Nigeria na bara la Afrika limezama katika umasikini na kutegemea misaada ya kigeni kutokana na uongozi mbaya na muovu wa ufujaji unaoendeshwa na ukoloni wa kimagharibi! Wakoloni wamelifanya mateka bara hili hadi wa leo huku wakitumia chaguzi za kujirudiarudia ili kuwapa mamlaka wanadamu ili kutunga sheria kinyume na maamrisho ya Muumba kwa viumbe Wake!.
Hatua ya dharura na msingi ya kuchukuliwa na Nigeria na Afrika kwa ujumla ili kufikia katika Ukombozi wa Afrika wa kweli ni kujiunga na Mradi wa Khilafah kama badala ya ukoloni wa Kimagharibi ambao ndio mzizi wa mateso yake kutokana na utumwa wa kisiasa-kijamii-kiuchumi. Khilafah iliyosimama kwa njia ya Mtume (saw) na yenye kutekeleza kikamilifu Shari’ah (Qur’an na Sunnah) chini ya mtawala muadilifu Khalifah ambaye anakwenda mbio kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu (swt) na sio Wamagharibi na mfumo wao muovu wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake. Chini ya Khilafah, Nigeria na Afrika kwa ujumla, pamoja na rasilimali zake nyingi zitahifadhiwa na kutumiwa kwa ajili ya Afrika na ilhali wakoloni na makampuni yao watafurushwa kikamilifu. Hivyo basi, Khilafah itadhamini amani, utulivu, maendeleo na ustawi kwa wanadamu wanaoishi Nigeria, Afrika na duniani kwa ujumla kwa kutekeleza kivitendo mfumo wa Uislamu na nidhamu zake zinazotokana nao zikijumuisha nidhamu ya Kiislau ya kijamii, nidhamu ya Kiislamu ya kiuchumi, nidhamu ya Kiislamu ya kielimu na nidhamu ya Kiislamu ya utawala miongoni mwa nyinginezo.
Ali Nassoro Ali
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya