Mnamo Alhamisi, 3 Disemba 2020, Daily Nation ilichapisha makala kwa kichwa, “Yatani: Jiandaeni kwa siku ngumu.” Kichwa hicho kilitokana na Waziri huyo wa Hazina ya Kitaifa, Ukur Yatani kufika mbele ya Kamati ya Bunge la Kitaifa ya Fedha na Mipango mnamo Jumatano, 2 Disemba 2020. Katika kikao hicho Waziri alinukuliwa akisema, “Nitakuwa sio muaminifu nikisema kuwa kila kitu kiko sawa. Tuko katika hali ambayo haijawahi kushuhudiwa hapo awali. Kupunguwa kwa kasi mapato na uchumi kuzorota kunatupa tumbo joto.” Kwa kuongezea, alisema kuwa madeni ya Kenya yamefikia Shilingi trilioni 7.2 ambayo ni takribani asilimia 71.2 ya GDP! (Daily Nation, 3 Disemba 2020).
Matamshi ya Waziri huyo yamekuja takribani wiki mbili tu baada ya yeye kukemea makala ya Daily Nation kwa kichwa, “Kenya ambayo haina kitu inatafuta njia ya kusimamisha kwa muda ulipaji wa deni lake la Shilingi bilioni 75.” (Daily Nation, 20 Novemba 2020). Waziri aliikashifu makala hiyo na kuitaja kuwa yenye nia mbaya. (treasury.go.ke, 20 Novemba 2020). Sasa imethibitishwa kupitia matamshi mapya ya Waziri huyo kwamba Kenya inakabiliwa na mdororo wa kiuchumi ambao hauwezi kufichika tena!
Lakuvunja moyo ni kwamba mabwenyenye nchini Kenya wanashughulika kukazanisha vitanzi vya kiuchumi katika shingo za raia ambao hawawezi hata kupumua. Covid-19 haikufyeka tu akiba zao bali imesambaratisha amali za kiuchumi na kupelekea kufungwa kwa biashara zao. Wanasiasa walafi wako mbioni wakizunguka nchini kote wakijaribu kuwahadaa raia waliokata tamaa kwa kuwapa uongo zaidi kwamba BBI ndio suluhisho la matatizo yanayoikumba Kenya! Japo wanaoneka mirengo tofauti wengine kupinga na kuunga mkono BBI. Wote ni wa moja.
Mambo yanazidi kuwa mabaya, kwani mnamo Alhamisi 3 Disemba 2020 wazazi na wanafunzi walishtushwa na habari kuwa Hazina, Wakuu wa Vyuo na Wabunge wamepitisha uamuzi wa kuzidisha ada za chuo kikuu kwa kila mwanafunzi kutoka kuwa ni Sh16,000 hadi Sh48,000 kwa mwaka! Hio ikiwa tu ni sehemu ya ongezeko bali jumla ada inakaribia zaidi ya Sh200,000 kwa mwaka kwa mwanafunzi! Uamuzi huo uliotokana na maafisa wakuu kutoka wizara ya fedha na elimu kufika mbele ya Kamati ya Bunge la Kitaifa ya Elimu mnamo Jumatano, 2 Disemba 2020. (The Standard, 3 Disemba 2020). Kwa kuongezea, Hazina itazindua rasmi ushuru wa dijitali wa asilimia 1.5 kwa kila muamala utakaofanyika mtandaoni kuanzia Januari 2021. (The Star, 8 Oktoba 2020).
Pasina shaka tawala za kisekula za kirasilimali zinadai kuwa zinastawi kupitia utaalamu wa kubahatisha katika kusimamia mambo ya watu. Wao ni mabwana katika kuwalaza watu na kutoa suluhisho feki zinazolenga kutibu tu matawi na kuuwacha mzizi ambao ndio chanzo kama ulivyo! Tatizo msingi linaloikumba Kenya ni kujifunga kwake na mfumo wa kisekula wa kirasilimali na kutekeleza kwake nidhamu zenye sumu zinazojumuisha sio tu nidhamu ya kiuchumi ya ukandamizaji kupitia uchukuaji mikopo na utozaji ushuru. Ni mfumo muovu wa kimabavu ambao unatapika moto!
Kwa kadri wanaoitwa ‘wasomi na wajuzi wa kiuchumi’ watakavyoendelea kujifunga na mfumo batili wa kisekula wa kirasilimali basi uchumi utaendelea kuangamia. Hali ni mbaya mno sio tu Kenya bali hata kwa zile zinazojulikana kuwa nchi zenye uchumi mkubwa kama vile Japan ina deni la asilimia 237.54 ya GDP yake, USA ina asilimia 106.7 ya GDP yake, Uchina ina asilimia 55.36 ya GDP yake miongoni mwa wengine. (World Population Review). Kwa kifupi uchumi uko katika janga lakini Covid-19 imetoa fursa ya kunyooshea kidole badala ya kuelekea suala nyeti nalo ni kufeli kwa nidhamu ya kiuchumi ya kisekula ya kirasilimali.
Mbadala ni kuwa mfumo wa Kiislamu unaotoka kwa Muumba na Mpangiliaji wa ulimwengu, mwanadamu na uhai, Allah, umetupa muongozo uliowazi kuhusiana na vyanzo vya mapato na matumizi. Vigawanyo hivyo vimebainishwa na Shari’ah kama mapato kutoka kwa Zakat, Kharaj, Ushr, Fai n.k. Ama kuhusu matumizi Shari’ah imekuwa wazi kama vile vikundi vinane vya wale wanaostahiki kupewa Zakat lakini kwa kuzingatia ijtihadi ya Khalifah.
Kwa kutamatisha, mchakato wa kuandaa bajeti katika Khilafah inayotarajiwa kusimamishwa hivi karibuni kwa njia ya Utume utakuwa sio jambo la kubahatisha. Hivyo basi, hakutakuweko na masuala ya ‘miradi hewa ya ufujaji’ kama inavyoshuhudiwa katika tawala za kisekula za kirasilimali ambazo zimedumu katika mapungufu ya bajeti na ambayo vyanzo vyake vya mapato ni mikopo ya riba na ushuru ilhali matumizi yanategemea hawaa za walioko mamlakani! Hata hivyo, kunapotokea dharura au janga, Khilafah inaweza kwa muda mfupi kutoza ‘kodi’ juu ya wale walio na utajiri wa ziada ili kukidhi hitajio la dharura kama vile ukame n.k. Kwa hiyo ni muhimu kufanya kazi kwa bidi kwa ajili ya Khilafah inayotarajiwa. Kwani ni Khilafah pekee ndio itakayo uondosha mfumo huu wenye kutamausha wa kisekula wa kirasilimali unaosababisha huzuni duniani kote.