Kuzinduliwa kwa Mpango wa Kizazi Kisicho na Mipaka na Kuchaguliwa kwa Uhuru kama Mtetezi wa Vijana wa UN Yathibitisha Kufeli kwa Mfumo Sekula wa Kirasilimali Katika Kudhamini Mustakbali wa Vijana!
Mnamo Jumatatu 24 Septemba 2018, Umoja wa Mataifa (UN) chini ya udhamini wa Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa (UNICEF) ilizindua mpango mpya unaoitwa Kizazi Kisicho na Mipaka unaohusisha ushirika kati ya Mkakati wa Vijana wa Umoja wa Mataifa wa 2030 na Kizazi Kisicho na Mipaka. Lengo la mradi wa Kizazi Kisicho na Mipaka ni kuhakikisha kuwa kila kijana anapata elimu, anasoma, anapata mafunzo au ajira kufikia 2030. Raisi Uhuru Kenyatta wa Kenya alichaguliwa bila kupingwa kama Mtetezi wa Kiulimwengu wa Ajenda ya Vijana!
Ili kuelewa kitendo hiki cha kinafiki cha UN kuzindua mpango mpya na kumchagua Uhuru Kenyatta twahitaji kutaja nukta zifuatazo:
Kwanza: Umoja wa Mataifa ni chombo cha kisiasa kinachomilikiwa na nchi koloni za Kimagharibi hususan Amerika baada ya kuibuka kuwa dola kuu duniani katika Vita vya Pili vya Dunia. Hivyo basi, Amerika imeutia minyororo ulimwengu kupitia sera zake ovu zinazopitia UN. Fauka ya hayo, Amerika huikiuka UN inapotaka kuyafikia maslahi yake kwa haraka. Kwa mfano, Uvamizi wa Iraq licha ya UN kutouidhinisha, Amerika iliendelea na kuivamia Iraq kwa malengo ya kuing’oa serikali ya Saddam Hussein ambaye wakati huo alikuwa mtawala kibaraka wa Uingereza na mnamo 2003, serikali ya Saddam ikaanguka na tangu wakati huo Iraq imekaliwa na Amerika.
Pili: Kwa mujibu wa UN, ili kupatikane usawa wa takwimu katika maeneo yote, hufafanua ‘vijana’, kama watu kati ya umri wa miaka 15 na 24, pasi na mapendeleo kwa taarifu nyenginezo kutoka kwa nchi wanachama. Kufikia 2030 kutakuwa na vijana bilioni 2 wa kike na wa kiume wanaotafuta fursa kwa ajili ya ‘mustakabali angavu’ kote duniani. Shinikizo linaongezeka juu ya UN ikizingatiwa kuwa kila mwaka wakati Kongamano Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) linapokutana, hukabiliwa na changamoto tata zaidi ya mwaka jana na moja ya changamoto hizi ikiwa ni ile ya nishati ya vijana isiyotumika ipasavyo kote duniani.
Tatu: Afrika inaongoza duniani kwani vijana wake walikuwa ni asilimia 19 ya idadi ya vijana duniani mnamo 2015, wakiwa ni milioni 226. Kufikia 2030, inatabiriwa kuwa idadi ya vijana Afrika itakuwa imeongezeka kwa asilimia 42. Idadi jumla ya watu Afrika ni vijana, huku asilimia 60 ya idadi yote ya bara hili ikiwa ni watu chini ya umri wa miaka 25, ikilifanya kuwa bara changa zaidi duniani, kulingana na muundo wa idadi ya watu wake. Nchi zote kumi za kwanza changa duniani zenye umri wa wastani ziko barani Afrika, huku Niger ikishikilia nafasi ya kwanza ikiwa na umri wa wastani wa miaka 15.1. Kufikia 2015, kiwango cha ujinga katika nchi za Afrika zilio chini ya Jangwa la Sahara kilikuwa ni asilimia 35.7 kiwango kikubwa zaidi duniani na ukosefu wa ajira kwa vijana chini ya Jangwa la Sahara ulikuwa katika asilimia 12.88 kufikia 2016!
Nne: Kenya hukadiriwa kuwa kitovu cha Afrika huku kiwango cha elimu cha vijana wake kikiwa asilimia 87 mnamo 2016. Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Miradi ya Maendeleo (UNDP) inasema kuwa karibu watu 4 katika kila Wakenya 10 wenye umri wa kufanya kazi hawana ajira kama kiwango kibaya zaidi cha ukosefu wa ajira eneo hili. Kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira pia kimeiacha Kenya kuwa na mojawapo ya viwango vikubwa vya watu wa kutegemea wengine duniani kwa asilimia 75.4 unaotokana na kuweko kwa idadi kubwa ya vijana katika kila familia.
Tano: Kupasishwa kwa Uhuru Kenyatta ni ujira kutoka kwa serikali ya Amerika hususan sasa ambapo Uhuru yuko katika maelewano mazuri na Raila Odinga rafiki mtiifu wa Amerika. Baada ya uchaguzi mrefu ulokumbwa na ghasia uliomaliziwa kwa kupeana mikono na pia kumpelekea Uhuru Kenyatta kualikwa rasmi katika Ikulu ya White House mnamo 27 Agosti 2018 na kuwa Raisi wa Pili wa Afrika baada ya Muhammadu Buhari wa Nigeria kualikwa na utawala wa Trump. Kupasishwa kwa Uhuru kumelengwa kuendeleza mpango wa Kiamerika ulioundwa na Amerika katika kuminyana na Uingereza nchini Kenya na Afrika kwa jumla ima kwa kupitia kugawanya ngawira nayo au kupitia kuing’oa kutoka katika koloni zake chini ya utabiri wa “upeanaji mikono wa dhahabu” ambao unaongozwa na jopo kazi la ushauri wa Kujenga Daraja za Umoja.
Nukta zilizopo hapo juu zathibitisha waziwazi kuwa kwa hakika UN umefeli vibaya mno kutatua kikweli kadhia za wanadamu hususan vijana. Badala yake, UN inajiingiza katika mabadiliko feki na kuzindua mipango mipya, inayolenga kumakinisha matakwa ya bwana wake chini ya guo la wito wa kiulimwengu kwa tatizo la vijana. Fauka ya hayo, UN kupitia bwana wake inaongoza mipango hatari ya Vita juu ya Ugaidi na Misimamo Mikali inayolenga vijana na Ummah wa Kiislamu kwa jumla wanaojaribu kujifunga kikamilifu na Uislamu na wakati huo huo kufichua maadili ya uhuru yenye sumu yanayo shabikiwa na wakoloni wa Kimagharibi.
Vijana ni waathiriwa wa mfumo sekula wa kirasilimali kupitia akili zao kuchafuliwa na itikadi ya kisekula, mfumo wa kirasilimali na njia yake ya ukoloni ya kuendeleza mfumo huu. Ni wajibu juu ya vijana kuihoji kwa kina hali yao katika jamii huku wakizingatia kuwa mchango wao ni muhimu mno na unaotafutwa kwa dharura katika upande wa ufanisi. Katika kuihoji kwao huko ni lazima waipe kipaumbele kwa kulinganisha baina ya mfumo wa Kiislamu na mfumo wa kisekula wa kirasilimali. Ambapo Uislamu una rekodi iliyo thibitishwa ya takriban karne 14 za utulivu na ufanisi na kwa upande mwengine tuna ghasia na majanga mwaka nenda mwaka rudi bila ya kujali tajiri wala masikini kila mmoja yumo ndani ya hofu katika mfumo sekula wa kirasilimali.
Mwisho, vijana ni lazima waukumbatie ulinganizi wa kusimamisha tena Khilafah kwa njia ya Utume. Chini ya Khilafah vijana na wanadamu kwa jumla watafurahia amani kwa sababu akili zao zitajengwa katika kujifunga na Utambulisho wa Kiislamu (Shakhsiyatul Islam) na nguvu zao zitatumika katika kuendeleza lengo la kutafuta radhi za Allah (swt) kupitia ima kushiriki katika maendeleo ya kieneo au ya kimataifa kupitia sera za ndani na za kigeni za Khilafah. Kinyume na hali za sasa za vijana ambao wanatumiwa na serikali za kiimla za kisekula zinazo watazama vijana kama waraibu wa mihadarati, mashini za kupiga kura wakati wa uchaguzi, magenge ya fujo ya kuajiri kusababisha ghasia dhidi ya mabwenyenye pinzani, maabara ya makampuni ya kirasilimali ya kimataifa nk.
Mustakbali wa vijana umo mikononi mwa Khilafah inayoongozwa na Khalifah mwenye hamu ya kuunganisha nguvu ya vijana chini ya bendera ya Uislamu dhidi ya madhalimu wa wanadamu wakiongozwa na Amerika na washirika wake ambao daima hupanga njama na kuwatumia vijana kwa ajili ya manufaa yao ya kibinafsi. Hadi wakati huo vijana ni lazima wajinasue kutokana na uovu wa mfumo wa kisekula wa kirasilimali na kuuelekea Uislamu kwa moyo wao wote kama badili unaodhamini ukombozi msingi na wa kweli wa wanadamu kutokana na njama za mabwenyenye wachache wa kisekula waliojitolea muhanga kuendesha mambo ya ulimwengu kana kwamba ulimwengu huu ni shamba lao na vijana na wanadamu jumla ni mashamba boi wao!
Ali Nassoro Ali
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya