Mkutano Kati ya Trump na Kenyatta Mnamo 27 Agosti 2018: Mkutano wa Kukaza Kitanzi Shingoni Mwa Koloni ya Kenya
Mnamo 6 Agosti 2018, ikulu ya White House ilitoa taarifa rasmi inayosema, “Raisi Donald J. Trump atampokea Raisi Uhuru Kenyatta wa Kenya ikuluni White House mnamo Agosti 27, 2018. Kenya ni mshirika muhimu wa Amerika, na Raisi Trump anatarajia kujadili njia za kupanua ushirika wa kistratejia uliojengwa juu ya maadili yetu shirika ya kidemokrasia na maslahi ya pamoja. [White House, 06/08/2018]
Msemaji mshikilizi rasmi wa serikali ya Kenya Kanze Dena alithibitisha taarifa hii huku akiwahutubia waandishi wa habari katika ikulu ya Mombasa, mnamo 6 Agosti 2018, na kusema: “Viongozi hawa wawili watajadiliana kuhusu mahusiano mazuri kati ya nchi mbili hizi na mipango ya kuimarisha miongoni mwa sekta nyengine, usalama, biashara na uwekezaji.” Ili kufahamu uhakika nyuma ya mwaliko huu ni wajibu kuangazia kadhia zifuatazo zilizopelekea mwaliko huu:
Kwanza, Uchaguzi mkuu wa Kenya wa 8 Agosti 2017 uliopelekea Raisi Kenyatta – Chama cha Jubilee (mtawala kibaraka wa Uingereza) kutangazwa mshindi dhidi ya aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga – NASA (mtawala kibaraka wa Amerika); lakini Mahakama ya Upeo ya Kenya ilibatilisha ushindi huo mnamo 1 Septemba 2017 na taifa kurudi tena katika uchaguzi wa marudio uliofanyika mnamo 26 Oktoba 2017 lakini ukasusiwa na Raila Odinga aliyedai kuwa sababu zilizotajwa na Mahakama ya Upeo ya Kenya hazikutatuliwa. Kwa upande mwengine, uchaguzi huo wa marudio ulifanyika na Kenyatta kutangazwa mshindi kwa mara ya pili. Kwa upande mwengine mabalozi wa kigeni wakiongozwa na Bob Godec (Amerika) na Nic Hailey (Uingereza) walitoa taarifa kabla na baada ya uchaguzi wa kwanza na wa marudio na ujumbe ulikuwa ni ule ule; matokeo yalikuwa safi licha ya kuwepo baadhi ya dosari. Hii ilimpelekea bwana Odinga kuwa mkali kwa mabalozi hao na kuwatuhumu kujali tu mikataba ya kibiashara badala ya demokrasia na maadili yake! Bwana Odinga aliondoka nchini mnamo 7 Novemba 2017 kwa ziara ya siku 10 nchini Marekani na kuregea mnamo 17 Novemba 2017. Nchini Marekani alifanya msusuru wa mikutano na kamati za bunge la Congress juu ya marudio ya uchaguzi wa uraisi wa Oktoba 26 na sababu za kujiondoa kwake katika kinyang’anyiro. Zaidi ya hayo, alisema, “Nimekutana na viongozi katika Idara ya Serikali, bunge la Congress, na wataalamu wa Kiamerika. Nimewadokeza juu ya hali nchini Kenya, na aina ya changamoto tunazokabiliana nazo kufuatia kuvurugwa wa kura za uraisi.” [Daily Nation, 16/11/2017]. Taarifa yake ilithibitishwa na Donald Yamoto, Kaimu Waziri Msaidizi katika masuala ya Afrika, iliyotajwa katika maongezi ya kongamano na maripota kwamba alikuwa amekutana na bwana Odinga ambapo alisema: “Maongezi hayo – hatuwezi kufafanua zaidi,” akijibu swali kuhusiana na thathmini ya Marekani ya malalamishi ya viongozi wa NASA. [The EastAfrican, 14/11/2017]. Kisha kukafuatiwa na kuapishwa kinyume na katiba kwa bwana Odinga mnamo 30 Januari 2018! Vitendo vyote hivi vya bwana Odinga vilipangwa kimakusudi kuhakikisha kwamba vinatia shinikizo kwa mtawala kibaraka wa Uingereza kujumuisha maslahi ya bwana wake (Marekani) ikizingatiwa kuwa rai jumla ya watu haikuwa pamoja na yeye na hivyo basi ulegezaji msimamo ndio uliokuwa suluhisho pekee!
Pili, Wakenya mnamo 9 Machi 2018 walipata mshangao pindi walipowatizama Kenyatta na Odinga wakipeana mikono nje ya Jumba la Harambee jijini Nairobi. Hii ni baada ya mkutano wao ambapo waliamua kufanya kazi pamoja na kuunganisha nchi baada ya uchaguzi uliochukua muda mrefu! Hili halikuingia akilini kamwe; lakini lililoingia akilini ni muda uliotengwa kwa ajili ya uamuzi wao, ambao ulichukua takriban saa 5 kabla ya ziara ya Waziri wa Kigeni wa Marekani Rex Tillerson jijini Nairobi. Uamuzi wao na ziara ya balozi mkuu wa kigeni wa Marekani inathibitisha kwamba kwa hakika kulikuwepo na ulegezaji msimamo baina ya Marekani na Uingereza kupitia watawala wao vibaraka. Kaimu Waziri Msaidizi wa masuala ya Afrika Donald Yamamoto aliungama kuwa Marekani ilijadili kwa kina na Odinga juu ya haja ya kuwepo maridhiano kwa matayarisho ya ziara ya Waziri wa Kigeni wa Marekani Rex Tillerson. Akizungumza na Jarida la Wallstreet, alithibitisha majadiliano hayo, akisema kuwa “tulimwambia … kwamba uko na fursa kubwa sana ya kihistoria kusukuma kikweli mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi”. [Pulse, 10/03/2018]
Tatu, Ziara ya Raila ya 24 Mei 2017 kwenda Sudan Kusini kama mjumbe maalumu kuwakilisha Muungano wa Afrika (AU) na kufanya mkutano wa saa 7 na Raisi wa Sudan Kusini Salva Kiir na baadaye kusafiri hadi Afrika Kusini kukutana na aliyekuwa makamu wa raisi wa Sudan Kusini Riek Machar kujadili uwezekano wa suluhisho la mzozo nchini Sudan Kusini [Daily Nation, 27/05/2018]. Hatimaye mahasimu hao wawili walitia saini mkataba wa serikali ya muungano mnamo Jumapili 5 Agosti 2018 jijini Khartoum, uliongozwa na Raisi Omar Bashir (Sudan) pamoja na Raisi Uhuru Kenyatta [The Star, 05/08/2018]. Kisha kufuatiwa na kuorodheshwa katika gazeti rasmi la serikali kwa Jopo Kazi la Utoaji Ushauri wa Kuleta Muungano Baina ya Pande Mbili (serikali na upinzani) mnamo 24 Mei 2018 likiongozwa na Balozi Martin Kimani (Akimwakilisha Kenyatta) na wakili Paul Mwangi (Akimwakilisha Odinga) kama makatibu shirika [The Star, 31/05/2018].
Nne, Mnamo 30 Mei 2018 Kitengo cha Kibiashara cha Amerika (AmCham) nchini Kenya kiliandaa kwa mara ya kwanza kabisa kikao cha mazungumzo kwa anwani “Kufanya Biashara na Marekani” katika Hoteli ya Movenpick, Nairobi hafla iliyo barikiwa na balozi wa Marekani nchini Kenya Balozi Robert F. Godec kama Mgeni wa Heshima. Baadaye, ikafuatiwa na kongamano la kibiashara la pande mbili kati ya Marekani na Kenya lililoandaliwa na AmCham Kenya mnamo 28 Juni 2018. Lililoongozwa na Uhuru Kenyatta na Marekani chini ya Waziri wake wa Biashara za Kimataifa Gilbert Kaplan wakiongoza ujumbe wa zaidi ya viongozi 70 wa kibiashara kujadiliana na serikali na biashara za humu nchini juu ya fursa zilizo pambizoni mwa ajenda Nne Kubwa za Afya kwa wote, viwanda, makaazi ya bei nafuu na usalama wa chakula.
Tano, Utafutaji mkopo wa bilioni 300 kutoka kwa Marekani kufadhili ujenzi wa barabara kuu yenye mikondo sita kuunganisha Mombasa na Nairobi kupitia kampuni kubwa ya ujenzi ya Kiamerika ya Bechtel. Ndege za moja kwa moja zilizopangwa kutoka Nairobi, Kenya kwenda jijini New York, Marekani mnamo Oktoba 2018 zikisubiri kuidhinishwa. Mpango mpya kabisa na sera za kiusalama zinazovizunguka vita vilivyochochewa na wamagharibi juu ya Misimamo Mikali na Ugaidi ikizingatiwa kutokea hivi majuzi kwa mahusiano mazuri kati ya Ethiopia na Eritrea na Eritrea na Somalia. Kufurahishwa na kuwepo kwa Kenya nchini Israel wakati wa kuhamishwa ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi Jerusalem.
Kadhia zote hizo juu zathibitisha kuwa kihakika Marekani imelegeza msimamo na kuamua kufanya kazi na Uingereza ili kupata maslahi yake, ndani ya mwito wake wa “Marekani Kwanza.” Kwa hiyo mualiko huo haulengi kuwanufaisha raia wa Kenya kwa ujumla bali walafi wachache maswahiba wa Raila na Kenyatta waliotambulika kupitia ule unaoitwa “upeanaji mkono”.
Mwamko wa Afrika uko katika kukata mafungamano na dola koloni za kisekula za kimagharibi ambazo ndio mzizi wa kukwama kwake kisiasa, kijamii na kiuchumi kupitia utekelezaji mfumo wao muovu wa kisekula wa kirasilimali unaotokana na akili finyo ya mwanadamu kinyume na mfumo wa Kiislamu unaotoka kwa Muumba wa viumbe. Hadi wakati huo Afrika itaendelea kuteseka kutokana na sera za kimagharibi mpaka ikumbatie mfumo safi wa Kiislamu chini ya uongozi adilifu wa Khilafah inayohukumu kwa Uislamu pekee.
Imeandikwa kwa Ajili ya Radio Rahma
Ali Nassoro Ali
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya
Makala Na.6 Ijumaa, 28 Dhu al-Qi’dah 1439 | 2018/08/10