بسم الله الرحمن الرحيم
Ijumaa, 9 Machi 2018 Kenya ilishuhudia mahasimu wa kisiasa Rais Uhuru Kenyatta aliyeegemea Uingereza na Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga aliyeegemea Marekani walipokutana Jumba la Harambee, Nairobi na kuzungumza faragha kisha wakatoa taarifa ya pamoja kwa vyombo vya habari. Taarifa iliyoashiria eti “Mwanzo Mpya” uliomakinishwa juu ya msingi wa kuunganisha taifa lote. Mkutano huu ulifanyika takribani saa 5 kabla kuwasili kwa aliyekuwa Waziri wa Kigeni wa Marekani, Rex Tillerson!
Ni wazi kuwa Kenya ni taifa la kisekula linalotawaliwa na mfumo wa kirasilimali iliorithi kutoka kwa mkoloni baada ya kupewa uhuru bandia 1963. Mfumo muovu ulioweka kipaombele maslahi/manufaa katika kupima vitendo vya wanadamu. Jumla ya watawala wa ulimwengu wa tatu ikiwemo Kenya ni vibaraka wa wakoloni. Kwa maana nyingine kila hatua wanazopiga hutegemea maslahi/manufaa yao binafsi na mabwana zao.
Kwa sababu hiyo tumeshuhudia ndani ya mwaka mmoja tokea “Handsheki” kuwa walio nufaika pakubwa na mazungumzo hayo ni Mabwana Wakoloni, Raila, Uhuru na wandani wao wa karibu hususan wanasiasa na wafanyi biashara waliokuwa wanaingia hasara kutokana na sintofahamu zao. Ni wazi kuwa mkutano huo ulikuwa unalenga kuhifadhi maslahi/manufaa ya wachache na kuwatoa kafara wengi kama njia ya kupata ngawira. Kuweka wazi zaidi tutizame yafuatayo:
Kwanza, Utawala wa Jubilee ulipata uhalalishwaji nchini na kiulimwengu na hatimaye kupata pumzi za kuendelea usimamizi wa serikali pasi na mihemko ya kisiasa kutoka kwa upinzani. Marekani ikaipa Kenya zawadi ya kwanza mnamo 30 Mei 2018 kupitia Kitengo cha Kibiashara cha Amerika (AmCham) nchini Kenya kuandaa kwa mara ya kwanza kabisa kikao cha mazungumzo kwa anwani “Kufanya Biashara na Marekani” katika Hoteli ya Movenpick, Nairobi hafla iliyo barikiwa na aliyekuwa balozi wa Marekani nchini Kenya Balozi Robert F. Godec kama Mgeni wa Heshima. Baadaye, ikafuatiwa na kongamano la kibiashara la pande mbili kati ya Marekani na Kenya lililoandaliwa na AmCham Kenya mnamo 28 Juni 2018. Lililoongozwa na Uhuru Kenyatta na Marekani chini ya Waziri wake wa Biashara za Kimataifa Gilbert Kaplan. Utawala wa Marekani ukamzawadia Rais Uhuru Kenyatta kwa kumpa mualiko kwenda ikuluni White House mnamo Jumatatu, Agosti 27, 2018. Zaidi ya hayo, mnamo Jumatatu, 24 Septemba 2018 Marekani ikampa zawadi ya pili Rais Uhuru Kenyatta kupitia chombo chake Umoja wa Mataifa (UN) kwa kumchagua kuwa Mtetezi wa Kiulimwengu wa Ajenda ya Vijana!
Pili, Marekani ilimshurutisha Raila Odinga kulegeza msimamo dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta pale alipozuru Marekani. Bwana Odinga aliondoka nchini mnamo 7 Novemba 2017 kwa ziara ya siku 10 nchini Marekani na kuregea mnamo 17 Novemba 2017. Nchini Marekani alifanya msusuru wa mikutano na kamati za bunge la Congress juu ya marudio ya uchaguzi wa uraisi wa Oktoba 26 na sababu za kujiondoa kwake katika kinyang’anyiro. Zaidi ya hayo, alisema, “Nimekutana na viongozi katika Idara ya Serikali, bunge la Congress, na wataalamu wa Kiamerika. Nimewadokeza juu ya hali nchini Kenya, na aina ya changamoto tunazokabiliana nazo kufuatia kuvurugwa wa kura za uraisi.” [Daily Nation, 16/11/2017]. Aliyekuwa Kaimu Waziri Msaidizi wa masuala ya Afrika Donald Yamamoto aliungama kuwa Marekani ilijadili kwa kina na Odinga juu ya haja ya kuwepo maridhiano kwa matayarisho ya ziara ya Waziri wa Kigeni wa Marekani Rex Tillerson. Akizungumza na Jarida la Wallstreet, alithibitisha majadiliano hayo, akisema kuwa “tulimwambia … kwamba uko na fursa kubwa sana ya kihistoria kusukuma kikweli mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi”. [Pulse, 10/03/2018]. Ikapelekea Raila kuwa mwandani wa karibu wa Rais Uhuru Kenyatta na kupelekea washirika wake waliomzunguka kutiwa katika serikali ikiwemo kuwa wanachama wa makampuni ya serikali, mabalozi n.k. Kilele chake ni mnamo Jumamosi 20 Oktoba 2018, pale Muungano wa Afrika (AU) iliyokuwa chini ya Mwenyekiti wake Paul Kagame anayeegemea Marekani, ulimchagua Raila Odinga kuwa Balozi Mkuu wa Maendeleo ya Miundo Mbinu Barani Afrika (africa.cgtn.com, 20/10/2018).
Tatu, Uorodheshwaji katika gazeti rasmi la serikali kwa Jopo Kazi la Utoaji Ushauri wa Kuleta Muungano Baina ya Pande Mbili (serikali na upinzani) mnamo 24 Mei 2018 likiongozwa na Balozi Martin Kimani (Akimwakilisha Kenyatta) na wakili Paul Mwangi (Akimwakilisha Odinga) kama makatibu shirika [The Star, 31/05/2018]. Raila na Uhuru kwa pamoja wanakwenda mbio kwa ushirikiano wa jopo hili kuhakikisha kuwa kunafanyika Kura ya Maoni ili kubadilisha Katiba na kubuni vyeo “vitavyohakikisha hakuna mzozo” tena nchini Kenya kila baada ya uchaguzi.
Ni wazi kuwa waliofaidika na “Handsheki” ni wachache walafi na sio wananchi jumla ambao hivi sasa wanazama ndani ya kashfa za ufisadi wa mabilioni ya fedha katika sekta zote, madeni yamefikia trilioni 1.1, wengi waliouliwa katika mzozo wa uchaguzi wametumika kama ngazi za kuingia au kubakia mamlakani, gharama za maisha zikiendelea kupanda na kuwatia kitanzi raia jumla kiasi kwamba Kenya hivi sasa ina masikini wakupindukia takribani milioni 17.6 kwa mujibu wa ripoti ya hivi majuzi ya Benki ya Dunia! Waislamu wanaendelea kuandamwa na kuhangaishwa kwa kisingizio cha kupambana na misimamo mikali na ugaidi n.k. Kila mtu anakwenda mbio si tajiri si masikini kila mmoja amemaka hajui kesho ataamka vipi!
Kenya ni sawa na jengo lililo na msingi mbovu unaotokana na mfumo batili wa kisekula wa kirasilimali. Kwa hivyo jengo hili Kenya litabakia katika kuyumbayumba hadi pale utawala wake utakapo amua kubadilisha msingi wake kwa kukumbatia ulinganizi wa kurudisha tena maisha ya Kiislamu chini ya Khilafah kwa njia ya Utume. Kwa kuwa Khilafah ni Serikali ya Kiislamu inayosimama juu ya msingi thabiti wa Shari’ah (Qur’an na Sunnah) inayotoka kwa Muumba wa viumbe. Chini ya Khilafah kipaombele ni kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu (swt) na sio maslahi/manufaa kama tunavyoshuhudia hivi sasa! Kwa hivyo “Handsheki” itabakia kuwa mpango wa kikoloni baina ya vibaraka wa wakoloni dhidi ya raia zao vipofu wa kifikra!
(وَيَمۡكُرُونَ وَيَمۡكُرُ ٱللَّهُۖ وَٱللَّهُ خَيۡرُ ٱلۡمَـٰڪِرِينَ)
“Wakapanga mipango yao, na Mwenyezi Mungu akapanga yake. Na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa mipango” [Al-Anfaal: 30]
Ali Nassoro Ali
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya