Mwezi wa Rabiul-Awwal utukumbushe sifa ya kimageuzi ya ujumbe wa Mtume (SAAW) katika kuusimamisha Uislamu.

Rabiul-Awwal ni mwezi wa tatu katika kalenda ya Kiislamu ambao  mara kwa mara hukumbukwa ndani yake fadhila kubwa ya MwenyeziMungu (Swt) juu yetu ya kuzaliwa kwa Mtume wa mwisho Muhammad Rehema na Amani za MwenyeziMungu zimshukie yeye. Kikawaida mwezi huu huleta furaha kwa umma wote wa Kiislamu. Kwa unyeti zaidi, Mtume Muhammad SAW hujulikana kuwa ndiye bwana wa mitume wote aliekomboa watu kutokana na giza la ujahilia hadi kwenda katika nuru ya Uislamu. Waislamu walifanywa kuwa ni umma bora kwa sababu wao ni umma wake yeye (SAW) hivyo wanadaraja ya juu zaidi kuliko umma zote. MwenyeziMungu SWT asema:

 

كُنْتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنْكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ

Nyinyi ndio umma bora kuliko umma zote zilizodhihirishiwa watu mnaamrisha mema na kukataza yaliyo maovu  na mnamwamini MwenyeziMungu.

[Al-Imran: 110].

Rai inayoshikiliwa na wanavyuoni wengi wa kitarekh akiwemo Ibn Kathir inatajwa kwamba Mtume Muhammad (Saw) alizaliwa siku ya Jumatatu tarehe 12 Rabiul Awwal (katika mwaka 571 CE). Na katika hadithi sahihi alioipokea Imam Muslim kutoka Abu Qatadah pale Mtume SAAW alipoulizwa kwanini anafunga siku za Jumatatu akajibu kwa kusema:

فِيهِ وُلِدْتُ وَفِيهِ أُنْزِلَ عَلَيَّ

Ndio siku ndani yake nilizaliwa na kuteremshiwa wahyi

Ingawa mwezi huu husheheni mijadala mirefu kuhusiana na usahihi wa kusherehekea siku aliozaliwa Mtume, ni muhimu kueleza kwamba Uislamu una njia maalum ya kutatua masuala yenye ikhtilafu. Muislamu yoyote anayebeba rai ya Kiislamu lazima achukuliwe kama Muislamu maadam rai hiyo anayoibeba ni ya kiislamu na imejengwa juu ya dalili ya Kiislamu. Kuna umuhimu mkubwa sana kila mmoja kuheshimu rai ya mwengine kwani huwa imetokamana na Ijtihadi( Mchakato wa kuvua hukumu kutoka kwa dalili za kisheria) hata kama dalili hiyo sio ya kukatikiwa.(shibhu dalili) Ni makosa makubwa sana kugeuza masuala ya ikhitilafu na kuwa ni ya kivita na fujo. Isitoshe, wanavyuoni wakubwa wa zamani walioishi ndani ya utawala wa Kiislamu waliweza kutatua na kuheshimiana kirai kwenye masuala ya kifiqhi maadamu masuala hayo yametolewa ushahidi wa kidalili. Hii ina maanisha kwamba tofauti zao kattu hazikuweza kuhujumu ummoja wa Waislamu wala kumaliza wakati wao mwingi kushtumiana wao kwa wao. Kubwa zaidi,walilokuwa wakiangazia ni Uislamu ambao uliendelea kubakia kuwa ndio marejeo yao kwa matendo yao yote ya kibinafsi na kijamii.

Kuungazia  mwezi wa Rabiul-Awwal  ni sharti kuwe kwa misingi wa kuwakumbusha Waislamu juu ya maisha na mapambano pamoja na tabia za bwana Mtume SAAW zipaswazo kutia utulivu katika nyoyo zao. Asema

 

ٱلنَّبِيُّ أَوْلَىٰ بِٱلْمُؤْمِنِينَ مِنْ أَنْفُسِهِمْ

Nabii ana haki zaidi kwa Waislamu (waliomfuata) kuliko nafsi zao

(Al-Ahzab: 6)

Maswali ya kutafakari ndani ya mwezi huu mkubwa ni Kitu gani alichotumilizwa nacho Mtume SAAW? Je ni upi ujumbe wake? Je Yeye (SAW) alituletea nini? Maswali haya kwa bahati mbaya hupuuzwa na kusahauliwa kabisa.  Waislamu wakiangalia kwa umakini maisha ya bwana Mtume (SAW) watakuta kwamba jumla ya maisha yote ya bwana Mtume SAW yalikuwa ni yenye kuzunguka kwenye mchakato wa kubadilisha jamii ya Kishirikina iliokita kwenye misingi ya ukabila, ubaguzi, ujaahilia na migawanyiko hadi kuifanya kuwa ni jamii maalumu iliojengeka kwa msingi wa itikadi ya kupwekesha MwenyeziMungu mmoja, jamii ilioshikamana na umoja na yenye nuru. Kuyapata mafanikio haya makubwa, Mtume (SAW) aliulingania Uislamu ili uwewe kutekelezwa kwa lengo la kuunda jamii tulivu, adilifu iliosimama imara katika mji wa Madinatul Munawwara. Maswahaba waongofu wa bwana Mtume SAAW wakachukua jukumu kubwa la kuhifadhi Dini na kuulingania ujumbe wake wakaweza kukomboa mji baada ya mwengine. Kwa bahati mbaya, baada ya historia hii ya kung’ara, hali za Waislamu leo zikabadilika kuwa ni giza lililotanda na kuzagaa chini ya jamii ya kisecular na kiliberali na hii ni baada ya Uingereza lilokuwa dola kuu zama hizo kuuongoza wamagharibi katika kuvunja serikali ya Kiislamu, yaani utawala wa Khilafah uliokuwa dola kuu kwa karne kumi na tatu. Kuondoka kwa Khilafah kukasababisha kugawanywa kwa biladi za Kiislamu, kuporwa utajiri wa umma na mbaya zaidi ni kuacha kuhukumu na sheria za Uislamu. Uislamu wote sasa unashambuliwa na masekular ndani ya mataifa ya Kiislamu ambapo yamebadili kibla kutoka Makka hadi Washington na London. Nao viongozi wa Kiislamu wameruhusu mataifa ya kimagharibi kuhujumu haki za Waislamu chini ya kisingizio cha vita dhidi ya ugaidi.

Ni fikra duni Waislamu wanapoangazia mazazi ya Mtume SAAW kuangazia tu kwenye upande wa tabia zake, matukio ya kimiujiza ambapo miongoni mwake ni kule wanyama kwenda kwa Mtume SAAW kumshatikia , na mapenzi yake aliyokuwa nayo kwa watu, bali kinachotakikana ni kuangazia zaidi kazi kubwa aliokuwa akiifanya Mtume SAW ya kuulingania Uislamu kwa ajili ya kuetekelezwa. Na kwa kuwa hali ya umma leo inatisha, ni muhimu mwezi huu wasiuchukulie tu kuwa ni mwezi wa kufanya dhikri na kumswalia Mtume SAW kwa wingi bali pia wanawajibika kujipinda katika kuubeba ujumbe wa Kiislamu kwa sifa yake ya kimageuzi ili kuweza kuusimamisha Uislamu duniani.

 

Shabani Mwalimu

Mwakilishi kwa vyombo vya Habari

Hizb ut-Tahrir Kenya