Serikali ya Kiislamu ya Khilafah husimama kwa misingi ya sheria za Mwenyezi Mungu (swt) yaani kutoka kwa Shari’ah (Qur’an na Sunnah). Serikali hii ipo kwa ajili ya majukumu mawili msingi nayo ni kutekeleza/kutabikisha Shari’ah ndani ya eneo inalotawala na kueneza Da’wah ya Uislamu ulimwenguni kote ili kuwakomboa kutoka katika utumwa wa kumuabudu mwanadamu hadi kumuabudu Muumba wa viumbe vyote chini ya mfumo wenye uadilifu wa Uislamu.
Miongoni mwa nidhamu za Uislamu ni ile ya Kiuchumi. Nidhamu ya kiuchumi humaanisha utaratibu wa mahusiano kati ya watu na mahitaji yao , njia ya kukimu mahitaji hayo pamoja na ufuatiliaji wa njia za kufikia kukidhi mahitaji hayo. Uislamu unatambua kuwa mwanadamu ni mwenye kikomo na hivyo basi mahitaji yake yana kikomo na kuyafunga katika viungo vyake na ghariza zake. Njia (mali) za kushibisha ziko nyingi na zimetapakaa dunia nzima. Ufuatiliaji (usambazaji) wa njia hizo ndio chanzo cha matatizo ya kiuchumi yanayomkumba mwanadamu kutokana na suala la umiliki. Ili tuweze kuyatatua, ni lazima tuirudie fikra inayotokamana na itikadi (mtizamo juu ya maisha). Itikadi ya Uislamu ni Hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa Haki isipokuwa Mwenyezi Mungu na Muhammad ni Mtume wake. Kwa msingi huo nidhamu ya kiuchumi wa Kiislamu imekuja kutatua tatizo la usambazaji wa mali kwa mujibu wa Shari’ah. Kinyume chake ni kuwa itikadi ya Kisekula inayotenganisha dini na maisha; inasema kuwa tatizo la kiuchumi linalomkumba mwanadamu ni uhaba wa bidhaa na huduma haziwezi kukidhi mahitaji mengi ya mwanadamu! Na suluhisho lao la kiuchumi ni warasilimali (wenye viwanda) kuendelea kuzalisha bidhaa na huduma ili ziweze kukidhi mahitaji ya wanadamu!
Sera ya Uchumi wa Kiislamu chini ya Khilafah ipo kuhakikisha kuwa kila binadamu (raia wake) anaweza kukidhi mahitaji yake msingi kwa ukamilifu nayo ni chakula, mavazi na makaazi na kumuewezesha kukidhi mahitaji ya ziada. Mtu anaweza kukidhi mahitaji yake kupitia kufanya kazi. Na ikiwa hawezi kufanya kazi atasimamiwa na msimamizi wake, ikiwa msimamizi wake hawezi; Serikali itamsimamia. Ndani ya Khilafah hakuna utozwaji ushuru/kodi kama inavyoshuhudiwa leo mfano (PAYE, VAT, NHIF, NSSF, Housing Fund n.k). Na hii ina maana Uislamu tayari umedokeza njia za kukusanya mapato yake na jinsi ya usambazaji au matumizi yake. Mapato haya ni kama vile Zaka, Kharaj na Ushru Fai n.k. Ama suala la kutoza ushuru kama ilivyo leo katika mataifa ya kibepari kama Kenya, hakika halipo katika Uislamu ila kwa dharura maalum nayo ikiondoka utozwaji ushuru ni haramu. Hali hii inapelekea maisha kuwa mepesi kwani watu wataweza kumudu bei ya huduma na bidhaa kinyume na ilivyo sasa chini ya dola za kisekula ikiwemo Kenya!
Uislamu umegawanya mali makundi matatu mali; ya mtu binafsi, mali ya ummah na mali ya serikali ya Khilafah. Mali ya mtu binafsi ni anayomiliki na kuitumia kwa njia ya Halali pekee. Mtu binafsi anaweza kupata mali kupitia njia tano: kufanya kazi, kurithi, kupokea matumizi ya kukidhi mahitaji, ruzuku ya Serikali kwa raia wake na Mali anayopata mtu pasi na kutumia fedha au kufanya kazi (kupewa zawadi n.k). Mali ya Ummah ni vitu ambavyo Muumba amevifanya umilikaji wake ni wa Waislamu wote. Na kuwaunganisha katika umilikaji na kuzuia watu binafsi kumiliki mfano vizalishavyo umeme, kawi, viwanda vya gesi, makaa na madini ambayo yako kwa wingi na hayaishi ima yaliyo imara kama dhahabu, chuma au majimaji kama mafuta, gesi mfano gesi ya kawaida, bahari, maziwa, misitu, misikiti vyote hivyo na mfano wake ni Mali ya Ummah inamilikiwa na Waislamu wote, umiliki wa pamoja na ni mapato ya Bait ul Mal ya Waislamu,wakiganyiwa na Khalifah kwa mujibu wa Shari’ah. Mali hii Khalifah haruhusiwi kumpa umilikaji mtu yeyote ima mtu binafsi au kikundi maanake ni ya Waislamu wote kwa pamoja.
الْمُسْلِمُونَ شُرَكَاءُ فِى ثَلاَثٍ الْمَاءِ وَالْكَلإِ وَالنَّارِ
Waislamu ni washirika katika matatu: maji, malisho, moto
[Ahmad na Ibn Maja]
Mali ya Serikali ya Khilafah ni chochote katika ardhi au jengo linalohusiana na haki ya Waislamu wote; inatenganishwa na Mali ya Ummah. Mali ya Serikali inaweza kuwa ardhi, majengo, vitu vya kuhamishika ambavyo vimefungamanishwa na haki ya Waislamu jumla kwa mujibu wa Shari’ah. Khalifah ana mamlaka ya kusimamia, kuichunga na kufanya maamuzi kuhusiana na mali hiyo. Mali hii Khalifah anaruhusiwa kupeana umiliki wake mtu yeyote, kupeana hatimiliki na manufaa au manufaa bila umiliki au kuruhusu waziboreshe na wazimiliki, na anaweza kuitumia katika njia anayoona ni kwa maslahi ya Waislamu. Khalifah ameruhusiwa kupeana umilikaji wa ardhi kwa ambaye hana ardhi ya ukulima, mtu huyo ailime na iwe mali yake.
كَىۡ لَا يَكُونَ دُولَةَۢ بَيۡنَ ٱلۡأَغۡنِيَآءِ مِنكُمۡۚ
ili yasiwe yakizunguka baina ya matajiri tu miongoni mwenu.
[Al-Hashr: 7]
Khalifa hana ruhusa ya kuchukua mali ya mtu binafsi na kisha kumpa mtu mwengine, lakini anweza kupeana kutoka katika Mali ya Serikali na kuwapa masikini na sio matajiri. Mali hizi zimewekwa na Shari’ah hairuhusiwi kubadilisha mpangilio wake, kiasi kwamba Mali ya Ummah kubadilishwa na kuwa Mali ya Mtu Binafsi. Mfano kupeana haki za kutafuta na kuchimba mafuta kwa kampuni binafsi inayoitwa “ubinafsishaji” huku ni kuibadilisha Mali ya Ummah na kuifanya kuwa ya Mtu Binafsi. Vivyo hivyo hairuhusiwi kuhamisha umiliki wa Mali ya Mtu Binafsi na kuifanya kuwa Mali ya Serikali. Mfano kutumia nguvu kuchukua duka la mtu na kulifanya la Serikali inayoitwa “utaifishaji”
Uislamu chini ya kivuli cha Khilafah utahakikisha raia wamo ndani ya mazingira ya uchajimungu na kuwapelekea kuhurumiana baina yao:
Waumini katika kuhurumiana kwao ni kama mwili mmoja. Wakati kiungo kimoja kinaumwa, mwili mzima unashughulishwa kwa kuupelekea kuwa na homa na kukosa usingizi.
[Bukhari na Muslim]
Kuhurumiana huko ni kwa raia jumla chini ya Khilafah kutokana na utekelezaji wa Shari’ah ambao unajumuisha uhalalishaji wa biashara na uharamishaji wa riba, michezo ya bahati nasibu, udanganyifu katika biashara, ukiritimba wa mali na biashara, kufunga bei juu ya bidhaa au huduma n.k. Kutokana na utelekezwaji wa Uislamu kwa ukamilifu wake ndani ya Karne Kumi na Tatu hadi kuangushwa kwake 28 Rajab 1342 Hijria sawia na 3 Machi 1924 Miladi raia chini ya Khilafah waliweza kuona kivitendo namna nidhamu ya kiuchumi ya Uislamu ilivyo wanyanyua binadamu kutoka katika umasikini. Hali hiyo itarudi tena punde tu maisha ya Kiislamu yakataporudi kupitia kusimamishwa kwa Serikali ya Khilafah kwa njia ya Utume.
Kinyume chake ni kuendelea kutaabika ndani ya dola hizi za kisekula za kikoloni. Daima zinawakandamiza raia wake kiuchumi kupitia ushuru na kodi ambazo kiasili zisingestahili kutozwa raia. Huku zikishirikiana na taasisi za kikoloni kama Benki ya Dunia na Taasisi ya Fedha ya Kimataifa, na kuchukua mikopo ya mataifa kama China, Uingereza n.k kuwafunga katika minyororo ya madeni yaliyo na riba! Mali zote ambazo Kenya imeruzukiwa na Mwenyezi Mungu ikiwemo madini, mafuta, ardhi za ukulima n.k; zote zimebinafsishwa na kumilikiwa na watu binafsi ilhali raia jumla wamebakia kudidimia katika umasikini wa kupindukia! Waliobahatika kuajiriwa hulipwa mishahara duni kwa kutegemea makadirio ya matumizi yake kwa kiwango cha chini na kisha kiwango hicho hicho kinatozwa ushuru na kodi zisizoingia akilini! Serikali hizi daima ziko mbioni kupigia debe eti “kulipa ushuru ni kujitegemea!” Na kujitia upofu wakati makampuni ya kikoloni yanaendeleza uporaji wa mali za Ummah na kuyafanyia wepesi katika “uwekezaji wao” kwa kuyaondolea ushuru na kodi!
Shiriki Katika Kampeni yetu Maalumu kwa Mwito: Kuzidi Kwa Gahrama za Maisha: Uislamu Ndio Tiba kwa kufuatilia hashtag hii: #KuzidiKwaGharamaZaMaisha_UislamuNdioTiba napia kwa kuzuru Link zifuatazo
Twitter: twitter.com/HT_KENYA
Ali Nassoro Ali
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya