Habari:
Vyombo vya habari nchini Kenya vimeripoti kwamba Hakimu wa Mahakama Kuu, Teresia Matheka ametangaza kwamba kuwa mke nyumbani lazima izingatiwe kuwa ni kazi kamili yenye kustahili malipo. Hakimu alisema: “Ni rahisi kwa mwanandoa anayefanyakazi mbali na nyumbani na kutumana pesa kudai mali yote iliyonunuliwa na kuendelezwa kwa kutumia pesa alizotuma na mwanandoa anayekaa nyumbani na kuwasimamia watoto na familia. Mwanandoa huyo atasikika akisema kwamba yule mwingine hakuwa ameajiriwa na hakutoa mchango wowote. Kuwalea watoto ni kazi kamili ambayo familia humlipa mtu kufanya pamoja na kupika na kusafisha. Hivyo basi, kwa mwanamke aliyeajiriwa ambaye hulazimika kuwajibikia kubeba mimba na kuilea lazima mchango huu uzingatiwe.”
Maoni:
Matangazo hayo ni natija ya fursa iliyopatikana kwa kujifunga na mfumo wa kirasilimali wa kisekula na nidhamu zake ovu. Ni muhimu kutambua kwamba punde wanadamu wanapokwenda kinyume na njia ya Muumba wao -Mwenyezi Mungu (swt), basi hawaa na matamanio ndiyo yanayowaongoza na kuingia katika maangamivu. Hakika, sera na sheria za kirasilimali za kisekula kama vile Kifungu 45(3) cha Katiba ambacho kimetia ndani ya sheria ya Kenya malengo ya Mkataba wa Kumaliza Ukandamizaji Dhidi ya Wanawake ili kupatikane usawa ndani ya ndoa kwa kuwezesha ‘pande zote katika ndoa kupata haki sawa wakati wa kufunga ndoa, kipindi cha ndoa na kuvunjika kwa ndoa.’ (The Star, 10/10/2021).
Sera na sheria hizo zinachipuza kutoka katika akili finyu za wanadamu ambao wamechukua dori ya kujitungia sheria wenyewe badala ya kujisalimisha kwa maamrisho na makatazo ya Muumba wao. Kwa kuongezea, sera na sheria hizo hupelekea kuchochea chuki zaidi na ushindani duni ndani ya kiungo cha familia ambacho tayari kimesambaratika kwa kuwa misingi yake yenye nyufa imetokamana na nidhamu ya kijamii huria. Nidhamu hatari ya kijamii ambayo inapigia debe aina zote za mahusiano mfano yale yanayoitwa mahusiano ya wazi ambapo mume au mke anaweza kuwa ndani ya ndoa lakini anashiriki vitendo vya ngono na watu wengine! Nidhamu ovu ya kijamii ambayo inawatizama wanachama wa jamii kwa sura ya uzalishaji wa kiuchumi pekee! Hivyo basi, kuifanya taasisi ya ndoa kuwa ni sehemu ya ushindani wa kiuchumi baina ya waliooana.
Sera na sheria za kirasilimali za kisekula zimehalalisha LGBTQ na kuwapa uwezo wa kutafuta ulinzi wa kisheria pale ambapo ‘haki zao’ zinapokiukwa. Takwimu za hivi karibuni zinaashiria kwamba idadi ya LGBTQ inazidi ilhali idadi ya wanaoana inapungua huku viwango vya talaka vikizidi duniani kote. Hatimaye, sera na sheria hizi zipo kwa ajili ya kuzidisha sintofahamu kwa wanachama waliobakia ndani ya taasisi ya ndoa. Kwani mizozo kwa ajili ya mali miongoni mwa wanandoa itaendelea na kuzidi kwa sababu nia msingi ya kuingia katika ndoa ni kwa ajili ya ustawi wa kiuchumi kwa gharama yoyote ile kwa mfano kuwatumia watoto kama ndoano ya kifedha! Na kuwapelekea wanandoa kuwa ni zana za ngono!
Kwa upande mwingine, mfumo wa Kiislamu unaochipuza kutoka kwa Muumba wa ulimwengu, mwanadamu na uhai –Mwenyezi Mungu (swt); unaamrisha ndoa kuwa ni kitendo cha ibada. Kwa hivyo, kama vilivyo vitendo vyote vya ibada lazima vifuatiliwe kwa nia safi ambayo ni kukuza familia makini ambayo itapelekea kuwepo kizazi ambacho kitamuogopa Mwenyezi Mungu (swt) kwa kujifunga na kipimo cha Halali na Haramu katika kupima vitendo vya wanadamu. Katika Uislamu, ndoa ni sehemu ambapo mume na mke/wake hupata faraja, utulivu na upendo. Kwa kuwa ndoa ni fungamano la hiyari baina ya mume (Muislamu) na mke/wake; na hakuna anayelazimishwa juu ya mwingine. Kwa mujibu wa Shari’ah wote mwanamume na mwanamke wako sawa ima wamo katika ndoa au la. Vilevile, Shari’ah imepambanua dori maalumu ambazo kila mmoja anatakiwa kujifunga nazo ndani ya mujtama jumla na katika ngazi ya familia.
Kwa kutamatisha, ripoti nyingi zinazopeperushwa na vyombo vya habari kama vile kuzidi kwa viwango vya talaka, watoto wa mitaani, familia zilizovunjika, kujitoa uhai na mauji katika ndoa n.k. Yote hayo ni sehemu ya kufeli kwa sera na sheria za kirasilimali za kisekula ambazo zinachipuza kutoka katika akili zenye kikomo za wanadamu. Kwa hivyo, vyombo vya habari vilitakiwa viwe vinaangazia chanzo cha majanga haya ya kijamii yasiyohesabika yanayokumba ulimwengu. Badala ya kupeperusha sehemu baadhi ya hukumu ya Mahakama Kuu inayodai kuwalinda washirika katika ndoa kutokamana na ukandamizaji wa kiuchumi. Kwani, ndoa kwa mujibu wa nidhamu ya kijamii huria ni ushirika baina ya watu wazima walioridhiana! Ni chini ya nidhamu ya kijamii ya Kiislamu ndipo wanandoa watakapo shuhudia amani na utulivu. Mwenyezi Mungu (swt) says ﴿وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِّتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُم مَّوَدَّةً وَرَحْمَةً إِنَّ فِي ذَلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ﴾ “Na katika ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokamana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila shaka zipo ishara kwa watu wanao fikiri.” [30. Ar-Rum: 21].
Imeandikwa kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Ali Nassoro Ali
Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir