Mnamo Jumamosi, 19 Septemba 2020 video ya kutia wasiwasi ilisambaa katika mitandao ya kijamii. Katika video hiyo kulikuwa na mwanamke aliyekuwa na shida kutokana na uchungu wa kuzaa. Lakuvunja moyo ni kwamba alikuwa barabarani nje ya lango la Hospitali ya Pumwani, Kaunti ya Nairobi. Mlinzi aliyekuwa langoni alimkataza kutoingia ndani kwa kuwa madaktari walikuwa wamegoma! Hatimaye, alisaidiwa na wapita njia waliokuwa barabarani kujifungua mtoto wa kike. (The Star, 19/09/2020). Tukio hilo la kutamausha limethibitisha yafuatayo:
Kwanza, tukio hilo sio la kwanza wala la mwisho kutokea nchini Kenya. Tarehe halisi ya tukio hilo ilithibitishwa kuwa ni Jumapili, 13 Septemba 2020 (Nairobi Metropolitan Services, 19/09/2020). Kwa kuongezea, mnamo Jumatatu, 16 Septemba 2019 Mary Otieno alijifungua nje ya Kituo cha Afya cha Dandora, Kaunti ya Nairobi. Mary alikatazwa kuingia kituoni humo kwa kuwa hakuwa na Sh20 ya kujisajili! Sawa na hivyo, mnamo Agosti 2019 mwanamke alizaa katika sakafu ya Hospitali ya Mama Lucy Kibaki, Kaunti ya Nairobi (The Standard, 06/08/2019). Na pia mnamo Aprili 2019 mwanamke alizaa katika sehemu ya mapokezi ya Hospitali ya Shalom Community, Athi River ilhali wauguzi wakiwa wanakunywa chai! (standardmedia.co.ke, 22/04/2019).
Pili, matukio hayo yanafichua kufeli kinidhamu kwa ile inayoitwa nidhamu ya utawala ya demokrasia katika kusimamia mambo ya watu hususan wanawake wetu. Nidhamu hii imechipuza kutoka kwa mfumo batili wa kisekula wa kirasilimali ambao unampa mwanadamu mamlaka ya kutunga sheria kinyume na za Mwenyezi Mungu (swt) Muumba na Mpangiliaji wa ulimwengu, mwanadamu na uhai. Kipimo chake kwa vitendo vya watu ni manufaa na maslahi tu. Hivyo basi, wanaouchukua mfumo wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake za sumu kama muongozo wanataabika na ukosefu wa huruma, ubinafsi na mizozo ya kuendelea kwa uchu wa mali!
Tatu, wale wanaoitwa watawala au viongozi wako mbioni kupora mali za umma ili kufikia maslahi na manufaa yao na ya mabwana zao Wamagharibi. Kwa upande mwingine, raia wameachwa kutaabika katika taasisi za afya zilizopewa mgao mchache na hata huo pia unageuzwa kuwa miradi ghushi ambapo mabilioni yanafujwa katika kashfa kama ile ya Afya House inayohusiana na za kliniki za kuzunguka ambapo inaripotiwa bilioni Sh5.2 zilipotea (The Star, 05/10/2017). Kwa kuongezea, hivi majuzi pesa za afya zilizotengwa kupambana na Covid-19 zimeripotiwa kuporwa ilhali maisha ya raia yanaendelea kusambaratika kutokana na ukali wa janga hilo lililopenya nyanja za kijamii na kiuchumi.
Matukio haya ni matunda ya sifa ya kufeli kwa mfumo wa kisekula wa kirasilimali ambao Kenya imebuniwa juu yake. Kenya ni dola ya kisekula ya kirasilimali na shamba la kikoloni ambalo kiupofu limechukua mfumo wa bwana wake Mmagharibi na hivyo sera zake zinachorwa na bwana wake kwa njia ya moja kwa moja au isiyokuwa ya moja kwa moja. Kwa hivyo, licha ya mji mkuu wa Kenya, Nairobi kuwa ndio kitovu cha kiuchumi cha Afrika Mashariki na Kati bado haiwezi kutimiza mahitaji msingi na ya kijamii kwa raia wake. Hata hivyo, mabwenyenye wako mbioni kuzunguka nchi wakitafuta ima kuingia au kubakia madarakani kwa kupatiliza matatizo yanayowakumba raia ambayo chanzo chake ni kutokana na kikundi hicho kidogo na utekelezaji wake wa mfumo wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake chafu.
Wakati ni sasa wa kuanza kufikiria kuhusu suluhisho la kuwadunisha mama, binti na dada zetu n.k. Hadhi na heshima ambayo inastahili wanawake wetu haiwezi kupatikana kutoka kwa mfumo wa kisekula wa kirasilimali ambao umeifanya jinsia yao kuwa ni chombo cha kushibisha viungo kwa muda! Kwa kuongezea, umama wao unapigwa vita na wale wanaoitwa watetezi wa wanawake wanaodai kuwa umama ni mzigo kwa ustawi wa kiuchumi na kikwazo katika kupanda ngazi ya kijamii na kiuchumi! Badala yake wanawake wetu watapata amani, usalama, utulivu, hadhi na heshima chini ya nidhamu adilifu inayotoka kwa Mwenyezi Mungu (swt) Muumba na Mpangiliaji wa ulimwengu, mwanadamu na uhai. Kwa maana nyingine, nidhamu inayotoka kwa Shari’ah ya Kiislamu (Qur’an, Sunnah, Ijma Sahaba na Qiyas). Nidhamu hiyo si nyingine isipokuwa nidhamu ya Khilafah iliyosimama juu ya njia ya Utume. Nidhamu ya Khilafah inachukua kuwa jukumu msingi la mwanamke ni mke, mama na msimamizi wa nyumba. Nidhamu ambayo inathamini umama kama vile Mtume (saw) aliposema: « الْجَنَّةَ تَحْتَ رِجْلَيْهَا» “Pepo iko chini ya miguu yake (mama)” (Nasai).
Nidhamu ya Khilafah inasimamiwa na kiongozi mwanamume Muislamu, Khalifah ambaye Mtume (saw) amemzungumiza: فَالإِمَامُ رَاعٍ، وَهْوَ مَسْئُولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ “Imam (Khalifah) ni mlinzi wa anaowatala na atahesabiwa kuwahusu” (Bukhari na Muslim). Khalifah atakwenda mbio kutoa fursa kwa anaowatala ili kuwawezesha kutimiza mahitaji yao msingi kama chakula, mavazi na makaazi na mahitaji ya kijamii kama usalama, afya na elimu. Kwani Mtume (saw) alisema: لَيْسَ لاِبْنِ آدَمَ حَقٌّ فِي سِوَى هَذِهِ الْخِصَالِ بَيْتٌ يَسْكُنُهُ وَثَوْبٌ يُوَارِي عَوْرَتَهُ وَجِلْفُ الْخُبْزِ وَالْمَاءِ “Hakuna haki kwa mwanadamu isipokuwa katika haya: Nyumba anamoishi, nguo anazohifadhi uchi wake na Jilf (kipande cha mkate) na maji” [Tirmidhi]. Kwa kuongezea, Mtume (saw) alisema: مَنْ أَصْبَحَ مِنْكُمْ آمِنًا فِي سِرْبِهِ مُعَافًى فِي جَسَدِهِ عِنْدَهُ قُوتُ يَوْمِهِ فَكَأَنَّمَا حِيزَتْ لَهُ الدُّنْيَا “Yeyote anayeamka asubuhi akiwa na: salama sehemu yake ya kulala, afya mwili mwake, chakula cha siku basi ni sawa kama ambaye amekusanyiwa dunia yote” (Tirmidhi na Ibn Majah). Hivyo nidhamu ya Khilafah itaweka hatua na sera zitakazo hakikisha kuwa raia wanahudumikiwa vizuri na kwa wakati na kila wanapokuwa na hitaji. Kwa hakika, wale wanaolingania mabadiliko bandia nchini Kenya sio chochote bali ni wasanii wa kisiasa wanaofanyakazi kubakisha hali iliyoko sasa. Kwa hiyo, tuungane tufanye kazi pamoja #TurudisheKhilafah, mabadiliko ya kweli duniani kote.
Ali Nassoro Ali
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir