Taarifa kwa Vya Vyombo Vya Habari
Mahakama kuu imeamua kuwa watoto waliozaliwa nje ya ndoa na baba Waislamu wana haki ya kurithi mali ya baba yao, jambo linaloashiria maendeleo makubwa katika tafsiri ya sheria za kibinafsi za Kiislamu nchini Kenya. Hii ni baada ya Mahakama ya Juu Jumatatu tarehe 30 Juni kutupilia mbali rufaa ya Fatuma Athman Abud Faraj, ambaye alitaka kuwatenga watoto wa marehemu mumewe, Salim Juma Hakeem Kitendo, katika mali yake kwa madai kwamba walizaliwa nje ya ndoa inayotambulika ya Kiislamu.
Kwa muktadha huu Hizb ut Tahrir Kenya ingependa kubainisha yafuatayo:-
Kwa kuwa utawala wa Kenya ni wa kisekular (unaofuata itikadi ya kutenganisha Dini na Maisha), uamuzi huu sio wa kushangaza hata kidogo. Hii ni kwamba, usekula – itikadi ya kimagharibi inaamini kwamba Dini na serikali hupaswa kutenganishwa na mwanadamu hupawa uhuru kamili. Kwa muktadha huu, mahakama ya juu sio taasisi ya kuzingatia maadili ya Kidini , badala yake inashikilia mawazo ya kibinidamu. Kuwapa haki ya mirathi watoto waliozaliwa nje ya ndoa, kwa maneno mengine kuhalalisha uzinzi (uovu),yaani kwa ibara nyengine kusawazisha uchafu wa zina na ndoa, hili likiwa ni dhihirisho wazi kuwa itikadi ya kisekula hutukuza uhuru wa mwanadamu na mawazo kuliko maadili na sheria za Dini.
Kutetea na kulinda “haki” za watoto waliozaliwa nje ya ndoa ni sehemu tu ya kampeni kubwa inayoendeshwa na mataifa makuu ya Kimagharibi dhidi ya Uislamu. Hakikisho hili la kikanuni sambamba na propaganda dhidi ya Sheria za Kiislamu yote huenezwa kwa ngazi zote za Jamii kuhalalisha uzinzi na maovu mengine.Hali hii imepelekea kuongezeka idadi ya watoto randaranda mitaani ambao wamekua ni tishio la usalama katika miji mikubwa. Inafahamika wazi kwamba chokoraa nchini Kenya wanakabiliwa na masaibu mengi ikiwa ni pamoja na umaskini, ukosefu wa mahitaji ya kimsingi, matatizo ya afya, na kuathiriwa na aina mbalimbali za unyanyasaji.Hata hivyo, changamoto hizi zinachangiwa zaidi na kushindwa kwa familia katika kutekeleza wajibu wake kamili unaochangiwa na uzembe wa serikali katika kusimamia kusimamia mambo ya watu.
Kinyume chake, Uislamu umefaradhisha na kubaini kwamba asili jukumu la kuchunga mambo ya watoto ni la wanafamilia kisha na serikali. Ama kuhusu mirathi, Uislamu huwapa mirathi watoto waliozaliwa katika ndoa,ama wale waliozaliwa nje ya ndoa na wanaotoka kwenye familia masikini hawastahiki kurithi ingawa ni jukumu la Serikali kuwasimamia: Mtume SAAW amesema:
«أَنَا أَوْلَى بِالْمُؤْمِنِينَ مِنْ أَنْفُسِهِمْ، مَنْ تَرَكَ مَالًا فَلِأَهْلِهِ، وَمَنْ تَرَكَ دَيْنًا أَوْ ضِيَاعًا، فَإِلَيَّ، وَعَلَيَّ
“Mimi niko karibu zaidi na Waumini kuliko nafsi zao, basi atakayekufa (miongoni mwao) na kuacha baadhi ya mirathi, urithi wake utapewa ‘Asaba yake, na atakayekufa akiwa ameacha deni au watoto basi hao ni wangu na juu yangu kuwasaidia,
Hatimaye, tunawaomba Waislamu wasilipuuzile mbali jambo hili kwa vile ni sehemu ya vita vya kimataifa dhidi ya Uislamu. Tuna hisi kuwa uamuzi huu utachukuliwa kama mfano katika taasisi nyingine za kimahakama duniani kote ili kuhujumu sheria ya Kiislamu kuhusu mirathi. Tunatoa mwito kwa Waislamu wote wenye ushawishi nchini Kenya ikiwa ni pamoja na mawakili wa Kiislamu na wale walio katika nyadhifa za kisiasa kupaza sauti zao katika kuutetea Uislamu.
Shabani Mwalimu
Mwakilishi kwa Vyombo Vya Habari Hizb ut-Tahrir Kenya