Habari kuu kwenye gazeti la The East African (Novemba 9-Novemba 15,2019) ilikuwa chini ya anwani: Janga la madeni la bililioni $100.3 kwa mataifa ya Afrika Mashariki. Kulingana na gazeti hilo, mataifa matano ya Afrika Mashariki yote kwa pamoja yamejirundikizia jumla ya deni la kima cha zaidi ya $100.3 bilioni likiwa ni deni lao la ndani pamoja na la kigeni.Kufikia June 2019, deni jumla la nchi la Kenya lilifikia kima cha $58 bilioni huku lile la Tanzania likifika $22.5. Nchi ya Uganda,deni lake linalotokamana na mikopo nalo likawa limefikia $12. Mwaka jana deni la Rwanda likawa limefikia $5.4. Huku la Burundi nalo likikadiriwa kwa kiasi cha $2.4 Bilioni. Siku ya Alhamisi tarehe 7,2019 baraza la Seneti la Kenya liliipa serikali idhini ya kuongeza kiwango cha mwisho cha serikali kukopa madeni kuwa hadi kima cha Ksh 9 Trilioni.
Katika uchumi wa Kibepari,deni la ndani hujulikana kama kiwango jumla cha deni nchi inalodaiwa na wakopeshaji wa ndani ya nchi. Sambamba na deni la nje linalofafanuliwa kuwa ni lile ambalo nchi inadaiwa na wakopeshaji wa kigeni. Mataifa ya kibepari yamejiwekea kanuni kuruhusu serikali zao kutafuta mikopo. Kwa mfano, kifungo cha 422 cha katiba ya Kenya (Kanuni ya kuchukua mikopo ya Nje) kinaruhusu serikali kukopa au kuchukua mikopo kutoka kwa mtu yoyote yule au serikali yoyote. Shida ya madeni (Debt crisis) hujulikana kama hali ya serikali kukosa uwezo wa kulipa madeni ya mikopo yake. Hali hii vilevile huitwa Public debt overhang ambayo ni hali inayoarifiwa kama kudorora kwa uchumi kwa sababu ya kuzidi kwa kiwango kikubwa cha deni jumla la taifa.
Chini ya kisingizio cha maendeleo na miradi mikuu ya kimiundo mbinu,serikali hukimbilia taasisi za kifedha za kimataifa kama vile Benki ya Dunia na shirika la fedha la kimataifa (IMF) kwa lengo la kupata mikopo inayogeuka kwa laana badali ya kuwa ni maendeleo. Baada ya kufanyika kwa kongamano la Bretton woods mwaka 1944 ambapo ndani yake kukawekwa kanuni za kiulimwengu za kifedha kwa kubuniwa IMF na Benki ya Dunia, ulimwengu ukawanywa pande mbili mataifa ya wakopeshaji na mataifa ya wadeni. Katika miaka ya sabini, benki za kimagharibi zikawa na bidii ya kukopesha “mataifa yanayoendelea” na hapo madeni ya nje katika nchi ziitwazo ulimwengu wa tatu yakaanza kuendelea kukua kwa kiwango cha kutisha. Zikawekwa IMF na Benki ya Dunia kutimika kama zana za mataifa ya kimagharibi kwa lengo la kudhibiti uchumi wa ulimwengu wa tatu. Kupitia mradi ya kimarekebisho ya kimiuondo (Structual adjustment programs- SAPs) iliokuweko tokea mwaka 1980, mabepari wa Kimagharibi huyawekea masharti magumu mataifa yenye madeni ili kuyataka yapange upya uchumi wao kwenda sambamba na sera za mpya za kikoloni za kiliberali kupitia kukata ruzuku na kuthibiti bei na kubinafsisha mashirika ya umma, kuruhusu makampuni ya kigeni kununua mashirika ya umma kupitia mikataba ya serikali na kurudisha faida kwa khiyari. Hivi ndivyo namna ya mataifa ya kigeni yanavyohujumu chumi za mataifa yanayoendelea. Kwa sasa hivi chini ya mwavuli wa mikutano ya kibiashara ya kimataifa kama vile mkutano wa pamoja Marekani na Afrika, kongamano la China kuhusu ushirikiano wake na makongamano ya TICAD ya Japan na Kongamano la pamoja lililomalizika la hivi karibuni Russia na Afrika. Mikataba hiyo itaendelea kuathiri vibaya hali ya kiuchumi kote Afrika
Wanasiasa walioko katika mataifa machanga wanabeba fikra ya kibepari inayowafanya kutojali maslahi ya mwananchi wa kawaida hivyo hali pia imechangia Afrika Mashariki kuwa malimbikizi ya madeni. Kupitia ufisadi,usimamizi mbaya wa pesa za umma, viongozi wa Kiafrika wamekuwa wakipora wenyewe nchi zao. Ripoti ya kiuchunguzi;”The Plunder Route to Panama” (Njia ya uporaji ya Panama) iliotolewa na nyaraka za Panama mwaka 2016, inaangazia jinsi gani viongozi wa Kiafrika wanavyopokea hongo kutoka kwa mashirika ya kigeni na kukwepa ulipaji ushuru. Ripoti ikapata kwamba viongozi hao wanachokifanya ni kuunda taasisi katika utawala zinazoendeshwa na marafiki na jamaa zao kuiba mabilioni ya dollar na kuziweka katika nje ya nchi zao. Jambo hili hupunguza bajeti na kusitisha maendeleo na kuwafanya watu waendelee kuwa masikini.
Kwa hakika suala la kuomba sio kuwa linasababishwa na uhaba wa rasilimali bali linatokomana na ukosefu wa sera madhubuti za kiuchumi juu ya matumizi yake. Fauka ya hayo,viongozi wa Afrika Mashariki hawana maamuzi ya moja kwa moja au uhuru wa kujiamulia na wa kusimamia mambo ya raia wao.Mara nyingi wao hufanya kazi wakishirikiana na Mabeberu wa kikoloni katika kuhudumikia tu maslahi ya pote la warasilimali kupitia uporaji na kuiba rasilimali za nchi kisha baadae kuonekana wakiomba misaada ya kufadhili madaraka yao.
Afrika Mashariki inautajiri wa kutosha wa rasilimali,viongozi wake kwa bahati mbaya wamepora mali hizi na kuamua kuchukua mikopo ili kufadhili serikali zao.Kinachokosekana kwa Afrika Mashariki mfumo wa kiuchumi wa Kiislamu ambao hutilia hima zaidi katika usambazaji na ugavi wa rasilimali wala sio uzalishaji wake na kufungika tu baina kipote cha mabwenyenye wachache. Isitoshe, kwa utaratibu wa kifedha katika mfumo wa uchumi wa Kiislamu uliojengwa juu ya msingi wa dhahabu na fedha mikopo ya riba haina nafasi. Mfumo huu bora wa kiuchumi utatekelezwa chini ya dola ya Khilafah itakayosimamishwa chini ya mfumo wa Bwana Mtume Muhammad (SAAW)
Shabani Mwalimu
Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari Hizb ut-Tahrir Kenya